Zijue nchi 10 zenye furaha zaidi Afrika mwaka 2026

Kulingana na Ripoti ya Furaha Duniani ya 2026, Mauritius inaendelea kuwa nchi ya Afrika ambapo wakazi wanaripoti kiwango cha juu zaidi cha kuridhika na maisha.

Chanzo cha picha, Ken Welsh/UCG/Universal Images Group via Getty Images

Maelezo ya picha, Kulingana na Ripoti ya Furaha Duniani ya 2026, Mauritius inaendelea kuwa nchi ya Afrika ambapo wakazi wanaripoti kiwango cha juu zaidi cha kuridhika na maisha.
    • Author, Ousmane Badiane
    • Nafasi, Digital Journalist BBC Afrique
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 5

Furaha ya wananchi wa nchi fulani haitegemei ukubwa wa uchumi wake pekee. Hilo ndilo hitimisho la Ripoti ya Furaha Duniani ya 2026 (World Happiness Report 2026), inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa na kupima kiwango cha kuridhika kwa maisha miongoni mwa wakazi wa zaidi ya nchi 140.

Ripoti hiyo hutathmini mambo kadhaa, yakiwemo kipato cha mtu mmoja mmoja, msaada wa kijamii, umri wa kuishi kwa afya njema, uhuru wa kufanya maamuzi binafsi, ukarimu na mtazamo wa wananchi kuhusu rushwa.

Barani Afrika, nchi zilizoongoza zina sifa tofauti.

Baadhi zimefikia nafasi hizo kutokana na uchumi ulio imara kwa kiasi, nyingine kutokana na mshikamano wa kijamii, huku nyingine zikifaidika na huduma bora za umma.

Kimataifa, Finland imeendelea kushika nafasi ya kwanza duniani kwa mwaka wa tisa mfululizo, ikiendeleza ubabe wa mataifa ya Nordic katika viwango vya furaha.

Ripoti ya Dunia ya Furaha 2026 ilichapishwa Machi 19, 2026 na Kituo cha Utafiti wa Ustawi katika Chuo Kikuu cha Oxford kwa ushirikiano na Gallup, Mtandao wa Umoja wa Mataifa wa Suluhisho za Maendeleo Endelevu (SDSN) pamoja na kamati huru ya wanasayansi.

1. Mauritius

Mauritius imeendelea kuwa nchi yenye furaha zaidi Afrika, ikishika nafasi ya 73 duniani.

Kisiwa hicho cha Bahari ya Hindi kinatajwa kuwa na utulivu wa kisiasa, utawala wenye ufanisi kwa kiwango kikubwa na uchumi uliogawanyika katika sekta za utalii, huduma za kifedha, teknolojia na viwanda.

Aidha, kina wastani mrefu wa umri wa kuishi, mfumo wa afya unaofikika na kiwango cha juu cha elimu, mambo yanayochangia hali ya kuridhika kwa wananchi wake.

2. Libya

M

Chanzo cha picha, Getty Images

Libya imeorodheshwa ya pili Afrika na ya 81 duniani.

Licha ya miaka ya migogoro ya kisiasa na kiusalama, ripoti inaonyesha kuwa wananchi wengi bado wanaridhika na maisha yao.

Watafiti wanasema hali hiyo inachangiwa zaidi na mshikamano wa kifamilia, mahusiano ya kijamii na utamaduni wa kusaidiana.

3. Algeria

Algeria inashika nafasi ya tatu Afrika na ya 83 duniani.

Nchi hiyo inanufaika na mfumo mpana wa hifadhi ya jamii, huduma za afya na elimu zinazogharamiwa kwa kiwango kikubwa na serikali pamoja na mapato yatokanayo na mafuta na gesi.

Mahusiano ya karibu ya kifamilia pia yanatajwa kuwa sababu muhimu ya kiwango cha juu cha furaha.

4. Msumbiji

Msumbiji imepanda hadi nafasi ya nne Afrika na ya 93 duniani.

Ingawa bado inakabiliwa na umaskini, majanga ya asili na changamoto za usalama, ripoti inaonyesha kuwa mshikamano wa jamii, kusaidiana na uwezo wa wananchi kukabiliana na changamoto huongeza hali ya kuridhika.

5. Gabon

Gabon inashika nafasi ya tano Afrika na ya 96 duniani.

Utajiri wake wa mafuta umeifanya kuwa miongoni mwa nchi zenye kipato kikubwa kwa mtu barani Afrika.

Pia ina misitu mikubwa, idadi ndogo ya watu na ukuaji wa miji unaodhibitiwa. Hata hivyo, ripoti inaeleza kuwa tofauti kubwa za kipato bado zinawazuia wananchi wengi kunufaika kikamilifu na utajiri huo.

6. Côte d'Ivoire

L

Chanzo cha picha, Getty Images

Côte d'Ivoire imeorodheshwa ya sita Afrika na ya 98 duniani.

Katika kipindi cha muongo mmoja uliopita, imekuwa miongoni mwa uchumi unaokua kwa kasi Afrika Magharibi, ikinufaika na uwekezaji mkubwa katika miundombinu, usafiri na nishati.

Pamoja na maendeleo hayo, gharama ya maisha na pengo la kipato bado ni changamoto kwa wananchi wengi.

7. Cameroon

Cameroon inashika nafasi ya saba Afrika na ya 100 duniani.

Uchumi wake unategemea kilimo, mafuta, madini na huduma mbalimbali.

Kwa mujibu wa ripoti, mshikamano wa kifamilia na kijamii una mchango mkubwa katika kiwango cha kuridhika kwa wananchi licha ya changamoto za kiuchumi na kiusalama katika baadhi ya maeneo.

8. Afrika Kusini

Afrika Kusini imeorodheshwa ya nane Afrika na ya 101 duniani.

Ina uchumi mkubwa zaidi wa viwanda barani Afrika, miundombinu iliyoendelea na vyuo vikuu vinavyotambulika kimataifa.

Hata hivyo, viwango vya juu vya ukosefu wa ajira, tofauti kubwa za kipato na uhalifu vinaendelea kuathiri ubora wa maisha ya wananchi wengi.

9. Niger

D

Chanzo cha picha, Getty Images

Niger imechukua nafasi ya tisa Afrika na ya 103 duniani.

Licha ya kuwa miongoni mwa nchi zenye uchumi mdogo zaidi duniani, watafiti wanasema mshikamano wa kifamilia, uhusiano wa karibu wa kijamii na utamaduni wa kusaidiana huchangia kiwango cha juu cha kuridhika kwa wananchi.

10. Tunisia

Tunisia inafunga orodha ya nchi 10 zenye furaha zaidi Afrika, ikiwa katika nafasi ya 105 duniani.

Nchi hiyo ina mfumo wa elimu ulioendelea, huduma za afya zinazofikika na historia ya uwekezaji katika huduma za umma.

Hata hivyo, ukuaji hafifu wa uchumi, ukosefu wa ajira na hali ya kisiasa vinaendelea kuwa changamoto kwa sehemu ya wananchi.

Kwa nini baadhi ya nchi maskini zinaongoza kwa furaha?

H

Chanzo cha picha, Getty Images

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kwa mtazamo wa kwanza, inaweza kuonekana kuwa jambo la kushangaza kuona nchi kama Msumbiji au Niger zikiorodheshwa mbele ya baadhi ya mataifa yenye uchumi mkubwa.

Sababu ni kwamba ripoti hii haipimi ukubwa wa uchumi wa nchi, bali jinsi wananchi wanavyotathmini maisha yao.

Washiriki huulizwa swali rahisi: Unaridhika kwa kiwango gani na maisha yako kwa alama kati ya sifuri na kumi? Majibu hayo hukusanywa kutoka tafiti za Gallup zilizofanyika kati ya mwaka 2023 na 2025.

Baadaye watafiti huchambua mambo sita yanayoathiri matokeo hayo: kipato cha mtu mmoja mmoja, msaada wa kijamii, afya na umri wa kuishi, uhuru wa kufanya maamuzi, ukarimu na mtazamo kuhusu rushwa.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, nchi inaweza kuwa na uchumi wa kawaida lakini wananchi wake wakaridhika zaidi kutokana na mshikamano wa familia, jamii yenye kusaidiana, taasisi zinazofanya kazi vizuri na matumaini kuhusu maisha yao.

Toleo la mwaka 2026 pia limeangazia ustawi wa vijana, likichunguza athari za matumizi ya mitandao ya kijamii katika kiwango cha furaha na kuridhika kwa maisha.

Kwa mujibu wa watafiti, mbinu hii inaonyesha kuwa maendeleo ya nchi hayawezi kupimwa kwa ukuaji wa uchumi pekee. Ubora wa maisha ya wananchi pia hutegemea mambo ya kijamii, kisiasa na kibinadamu ambayo mara nyingi ni magumu kupimika, lakini yana mchango mkubwa katika ustawi wa watu.