Sababu 8 zinazowafanya vijana kubadili dini

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Isiyaku Muhammed
- Nafasi, BBC News, Abuja
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Mapema wiki hii, kijana mmoja alionekana kwenye video akidai kuacha Uislamu na kufuata Ukristo, tukio lililoibua hasira na mjadala mkali.
Hapo awali, vijana, hasa kutoka kusini mwa Nigeria, pia walitumia mitandao ya kijamii kutangaza kuhama kutoka Ukristo kwenda Uislamu.
Aidha, baadhi ya vijana wanaacha imani yao ya asili, iwe ya Kiislamu au Kikristo, kwa wazi au kwa siri, na kukumbatia mtazamo wa kutokuamini uwepo wa Mungu au kiumbe mkuu, unaojulikana kama atheism.
Ni nini kinachowasukuma vijana kuacha dini waliyozaliwa nayo na kufuata imani au mtazamo mwingine?
Katika mahojiano na BBC, mwandishi wa habari na mtafiti wa masuala ya kijamii na kitamaduni yanayowahusu vijana, Aliyu Samba, alieleza sababu nane zinazoweza kuchangia mabadiliko hayo.
1. Ukosefu wa maarifa ya kina ya kidini
Kwa mujibu wa Samba, namna dini inavyofundishwa kwa watoto na vijana ni jambo muhimu.
Mara nyingi, msisitizo huwekwa katika kukariri mafundisho badala ya kuelewa maana na misingi yake.
"Utakuta vijana wengi wakikua huku wakikariri tu yale wanayofundishwa, bila kupata fursa ya kuuliza hasa ni nini wanachofundishwa," alisema.
Alifafanua kuwa changamoto hii hujitokeza zaidi kijana anapoingia chuo kikuu, kusoma sayansi au falsafa, au anapokutana mtandaoni na maswali mazito kuhusu Mungu, uumbaji wa dunia, mateso, mema, mabaya na hatima ya maisha.
"Ikiwa hawatapata mtu mwenye uwezo wa kujibu maswali haya kwa hekima na uelewa, maswali hayo yanaweza kusababisha kupotea kwa imani," Samba alisema.
2. Ushawishi wa mtandao na upatikanaji wa mawazo mbadala

Chanzo cha picha, Getty Images
Mtandao umebadilisha namna vijana wanavyopata elimu na taarifa.
Hapo awali, wengi walitegemea wazazi, walimu, shule au taasisi za kidini kwa mafunzo ya dini. Leo, ndani ya dakika chache, wanaweza kufuatilia kwa wakati mmoja mhubiri wa dini, mkosoaji wa dini, mwanafalsafa na mwanasayansi.
Samba anasema hali hii si kwamba inawafanya vijana kuacha dini moja kwa moja. Badala yake, inawapa nafasi ya kulinganisha mawazo mbalimbali na kuuliza maswali mengi zaidi.
Utafiti wa mwaka 2026 kuhusu vijana wa Nigeria ulionyesha kuwa mitandao ya kijamii inazidi kuwa njia muhimu ya kukutana na mawazo ya kidini, ikiwemo mijadala kuhusu kuacha au kubadili dini.
3. Kutopata majibu ya maswali magumu
Baadhi ya vijana huanza kuhoji masuala yanayohusu dini, sayansi na falsafa.
Kwa mujibu wa Samba, tatizo si kuuliza swali, bali kushindwa kupata jibu linaloridhisha.
"Kijana akiuliza swali la namna hiyo na asipopata jibu, inasemekana kuwa shetani anapanda mbegu ya shaka akilini mwake," alisema.
Aliongeza kuwa baadhi ya maswali yanahitaji maarifa ya kina ya kifalsafa na hekima ili kumridhisha muulizaji.
Tatizo linaweza kuwa kubwa zaidi pale kijana anapomwona kiongozi wa dini akihubiri maadili mema lakini baadaye akitenda kinyume na mafundisho yake.
4. Ukosefu wa haki na changamoto za maisha
Umaskini, ukosefu wa ajira na ukosefu wa haki vinaweza kuathiri namna vijana wanavyoitazama dini.
Kijana anayepitia hali ngumu anaweza kujiuliza: "Dini ina mchango gani katika tatizo hili? Kwa nini kuna ukosefu wa haki wa namna hii?"
Samba alisema kuwa majibu rahisi yasiyoeleza kwa kina mtazamo wa dini kuhusu changamoto za kijamii yanaweza kutomridhisha kijana anayehitaji ufafanuzi zaidi.
5. Tofauti za mafundisho kati ya viongozi wa dini
Vijana wanaweza kuchanganyikiwa wanaposikia viongozi wa dini wakitoa maelezo yanayokinzana kuhusu suala lilelile.
Mmoja anaweza kusema jambo fulani ni haramu au marufuku, huku mwingine akisema linaruhusiwa.
Samba anasema kuwa bila maarifa ya kutosha kuelewa chanzo cha tofauti hizo, baadhi ya vijana wanaweza kufikia hitimisho kwamba dini yao ina kasoro.
Changamoto huongezeka pale kila upande unapodai kuwa ndio unaoshikilia ukweli pekee.
6. Mbinu za kuhubiri zisizowafikia vijana

Chanzo cha picha, Getty Images
Vijana wa leo wanaishi katika mazingira tofauti na yale ya vizazi vilivyopita.
Wanatumia YouTube, TikTok, podikasti, X, Facebook na majukwaa mengine ya kidijitali kupata taarifa.
Kwa mujibu wa Samba, mafundisho ya dini si lazima yabadilike, lakini namna yanavyowasilishwa inapaswa kuendana na mazingira ya sasa.
Anasema kwamba ikiwa elimu ya dini inabaki katika njia za jadi pekee na haifikishwi kwenye majukwaa yanayotumiwa na vijana, baadhi yao wanaweza kukosa fursa ya kupata majibu ya maswali yao.
7. Mwitikio wa falsafa, sayansi na elimu ya kisasa
Elimu ya juu, sayansi, falsafa na intaneti huwafanya vijana kukutana na mitazamo mipya kuhusu maisha na ulimwengu.
Samba anasisitiza kuwa mambo haya hayamfanyi mtu kuacha dini moja kwa moja. Wakati mwingine yanaweza hata kuimarisha imani.
Hata hivyo, yanaweza kumfanya mtu kuhoji upya imani alizorithi kutoka kwa wazazi au jamii.
Vilevile, uzoefu mbaya unaohusisha wazazi, walimu au mazingira ya taasisi za kidini unaweza kuchangia mabadiliko ya mtazamo wa kijana kuhusu dini.
8. Matendo mabaya yanayofanywa kwa jina la dini
Mojawapo ya sababu zinazoweza kuibua mashaka kwa vijana ni kushuhudia vitendo vya ukatili au uhalifu vinavyofanywa kwa kisingizio cha dini.
Samba alisema kijana aliyefundishwa kuthamini uhai wa binadamu anaweza kushindwa kuelewa kwa nini watu wengine wanafanya vitendo vya vurugu au mauaji kwa jina la Mungu.
Hali hii inaweza kuzua swali la msingi: ikiwa dini inafundisha haki, huruma na amani, kwa nini vitendo vya kikatili vinafanywa kwa jina lake?
Kwa mujibu wake, mgongano huu kati ya mafundisho ya dini na matendo ya baadhi ya wafuasi unaweza kuwasukuma vijana kuhoji misimamo yao ya kidini.
Ni muhimu kutofautisha kati ya kuacha dini, kuhamia dini nyingine, kubadili dhehebu au kutokuwa na dini kabisa. Haya ni mambo tofauti.
Utafiti wa mwaka 2025 wa Kituo cha Utafiti cha Pew kuhusu mabadiliko ya kidini katika nchi 36 ulibaini kuwa kubadili dini miongoni mwa watu wazima nchini Nigeria ni jambo adimu ikilinganishwa na nchi nyingine. Zaidi ya asilimia 95 ya washiriki walisema bado wanafuata dini waliyolelewa nayo.
Kwa mujibu wa Samba, mchakato wa kuondoka katika imani mara nyingi unaweza kufuata hatua hizi:
Swali → shaka → kutafuta jibu → kushindwa kupata jibu → kufadhaika → kujitenga na dini → kutafakari zaidi → kukubali mtazamo mpya.
Hata hivyo, anasisitiza kwamba si kila anayekuwa na maswali huacha dini. Wengine hupata majibu yanayowaondolea mashaka na hata kuimarisha imani yao.
Kwa hiyo, tatizo mara nyingi si kuuliza maswali, bali namna maswali hayo yanavyojibiwa.















