Lissu: “Maneno hayawezi kuwa matendo”

Kesi ya uhaini inayomkabili Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu inaendelea leo ikiwa katika hatua ya majumuisho.
Katika majumuisho yake ya mwisho jana, Tundu Lissu alijikita katika hoja yake; Je, maneno aliyotamka kwenye mkutano wa CHADEMA tarehe 3 Aprili 2025 yanatengeneza kosa la jinai kwa mujibu wa sheria za Tanzania?
Lissu alidai kuwa maneno yanayolalamikiwa ikiwemo “tutazuia uchaguzi”, “tutahamasiha uasi” na “tutakinukisha sana” hayajaainishwa kama kosa katika sheria ya uchaguzi wala hayafikii tafsiri ya kosa la uhaini chini ya Kanuni ya Adhabu. Alisema Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2024 imeorodhesha makosa na adhabu zake, lakini haijaweka kuzuia uchaguzi au kuhamasisha kususia uchaguzi miongoni mwa makosa hayo.
Aliendelea kupinga hoja ya upande wa mashtaka kwamba maneno hayo yalikuwa tishio kwa Serikali kwa sababu uchaguzi unasimamiwa kwa mujibu wa sheria na Katiba. Lissu alisema hata shahidi muhimu wa upande wa mashtaka, PW17, aliyekuwepo kwenye mkutano huo, hakuyataja baadhi ya maneno yanayolalamikiwa katika maelezo yake ya awali na hakusema aliona kosa la uhaini katika mkutano huo.
Kwa upande mwingine, Lissu alisema mashahidi wa upande wa mashtaka walijenga hoja kwamba maneno hayo yalilenga kuitishia Serikali kwa sababu Serikali ndiyo inayosimamia uchaguzi. Alipinga tafsiri hiyo, akisema hakuna mahali katika maneno aliyotamka ambapo alitaja Serikali ya Jamhuri ya Muungano, Rais, Makamu wa Rais au viongozi wengine wa Serikali.
Lissu pia alihamisha hoja kwenye maana ya kisheria ya “nia”, “kitendo” na “uchapishaji”, akisema upande wa mashtaka umejaribu kuyafanya maneno yake yaonekane kama “matendo” ili kujenga kosa la uhaini. Hoja yake ilikuwa kwamba maneno hayawezi kubadilishwa kuwa matendo kwa tafsiri ya upande wa mashtaka bila msingi wa sheria.
Akitumia pia uamuzi wa Mahakama katika kesi ya Freeman Mbowe, Lissu alisema sheria za jinai zinapaswa kuwa wazi ili kumlinda raia dhidi ya matumizi holela ya mamlaka na kulinda haki ya kutoa maoni.
Leo, Lissu anaendelea na majumuisho yake ya mwisho, akitarajiwa kuingia zaidi katika ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande wa mashtaka na utetezi kuhusu nia yake, mkutano wa 3 Aprili 2025 na maana ya maneno yaliyotumika. Upande wa Mashataka nao utapata nafasi ya kufanya majumuisho.












