Nchimbi kufuata nyayo za Maalim Seif au kina Lowassa?

.

Chanzo cha picha, DNews

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Kujiuzulu kwa Emmanuel Nchimbi kutoka nafasi ya Makamu wa Rais wa Tanzania na baadaye kufukuzwa uanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kumemaliza kwa ghafla moja ya safari za kisiasa zilizokuwa zimefika kileleni mwa uongozi wa nchi.

Nchimbi, ambaye kabla ya kuwa Makamu wa Rais alikuwa Katibu Mkuu wa CCM na ameshika nyadhifa mbalimbali serikalini, sasa amejikuta nje ya chama alichokitumikia kwa muda mrefu. Kuondoka kwake kunakuja wakati ambao alikuwa bado hajamaliza mwaka mmoja katika nafasi ya pili kwa ukubwa katika uongozi wa Tanzania.

Kilichoongeza maswali kuhusu hatua yake inayofuata ni kwamba kuondoka kwake serikalini hakukuishia kwenye kujiuzulu. CCM ilitangaza kumfukuza uanachama kwa kile ilichosema ni ukiukaji wa maadili. Hivyo, Nchimbi sasa anakabiliwa na hali ambayo si ya kawaida kwa mwanasiasa aliyekuwa sehemu ya uongozi wa juu wa chama na serikali.

Katika historia ya siasa za Tanzania, wanasiasa waliowahi kuwa na nafasi kubwa ndani ya CCM lakini wakaondoka wamechukua njia tofauti. Wengine waliingia upinzani na kuendelea kuwa na ushawishi, wengine walikaa nje ya chama kwa muda na baadaye wakarejea, huku wengine wakachagua kuachana na siasa.

Kwa Nchimbi, kwa sasa kuna njia tatu zinazoweza kuonekana mbele yake

Kurudi CCM

.

Chanzo cha picha, Dira

Njia ya kwanza ni Nchimbi kuchukua muda, kujiondoa kwenye siasa za wazi na baadaye kutafuta nafasi ya kurejea CCM.

Hii si njia mpya katika siasa za Tanzania.

Historia ya CCM ina mifano ya makada waliowahi kutofautiana na chama, kuondoka au kuvuliwa uanachama, lakini baadaye wakarejea.

Sofia Simba, aliyewahi kuwa mmoja wa viongozi wakuu wa CCM na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, aliwahi kuondolewa katika nafasi za uongozi ndani ya chama na baadaye kurejea katika safu zake.

Bernard Membe, aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na mwanasiasa aliyewahi kutajwa katika kinyang'anyiro cha urais, aliondoka CCM mwaka 2020 na kujiunga na ACT-Wazalendo. Baadaye alirejea CCM.

Edward Lowassa naye ni mfano mkubwa zaidi.

Baada ya kuondoka CCM mwaka 2015 na kujiunga na CHADEMA, Lowassa aliongoza kampeni ya UKAWA katika uchaguzi mkuu wa mwaka huo. Miaka minne baadaye, alirejea CCM.

Mifano hii inaonyesha kwamba kwa mwanasiasa mwenye historia ndefu ndani ya CCM, kuondoka kwenye chama si lazima kuwe mwisho wa uhusiano wake nacho.

Kwa Nchimbi, kurejea kungehitaji yeye kuwa tayari kuomba msamaha au kujenga upya uhusiano na chama, lakini pia CCM kuwa tayari kumpokea tena.

Kwenda upinzani

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Maalim Seif

Njia ya pili ni Nchimbi kuamua kuingia katika siasa za upinzani.

Mfano unaojitokeza hapa ni Maalim Seif Sharif Hamad, ambaye alitoka katika kilele cha uongozi wa CCM Zanzibar na baadaye akawa mmoja wa viongozi wakuu wa upinzani nchini.

Maalim Seif aliwahi kuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar, Waziri wa Elimu, mbunge na mjumbe wa vyombo vya juu vya uongozi wa CCM. Baada ya kuondolewa katika nafasi yake ya Waziri kiongozi ambayo ni kama Waziri Mkuu, alifukuzwa CCM kufuatia mgogoro na viongozi wa chama.

Baada ya mfumo wa vyama vingi kurejea Tanzania, alisaidia kuanzisha CUF na kwa miaka mingi akawa nguzo kuu ya upinzani Zanzibar. Baadaye alijiunga na ACT-Wazalendo na, kuelekea mwisho wa maisha yake ya kisiasa, akawa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar katika Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Tofauti muhimu ni kwamba Maalim Seif aliingia upinzani akiwa na mtandao mkubwa wa kisiasa na wafuasi waliokuwa tayari kusimama naye.

.

Chanzo cha picha, Dailynews

Maelezo ya picha, Lowassa alienda upinzani na kuzoa kura nyingi
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Edward Lowassa pia alionyesha jinsi mwanasiasa mkubwa kutoka CCM anavyoweza kuhamia upinzani na kuleta mabadiliko makubwa. Baada ya kutopitishwa kuwa mgombea urais wa CCM mwaka 2015, alijiunga na CHADEMA na kuwa mgombea wa UKAWA.

Katika uchaguzi huo, Lowassa alipata kura 6,072,848, sawa na asilimia 39.97 ya kura zote, dhidi ya kura 8,882,935, sawa na asilimia 58.46 alizopata John Magufuli wa CCM.

Alipata kura nyingi kuliko mgombea yeyote wa upinzani katika uchaguzi wa urais Tanzania tangu kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi mwaka 1992.

Lakini njia hiyo haikuwa rahisi. Wanasiasa wakuu wa upinzani Tanzania wamekumbana mara kadhaa na kukamatwa, kesi na misukosuko ya kisiasa. Tundu Lissu yuko gerezani akikabiliwa na kesi ya uhaini, huku Freeman Mbowe akiwahi kukaa gerezani kwa miezi 8 akikabiliwa na kesi ya ugaidi kabla ya mashtaka dhidi yake kuondolewa.

Kwa Nchimbi, kuingia upinzani kwa hiyo hakutakuwa tu kubadili chama. Kutakuwa ni kuingia katika mazingira mapya ya kisiasa ambako atalazimika kuthibitisha kama jina, uzoefu na ushawishi alioupata ndani ya CCM vinaweza kugeuka kuwa wafuasi na nguvu ya kisiasa nje ya chama hicho.

Kuachana kabisa na siasa

.

Chanzo cha picha, CCM

Njia ya tatu ni ile ambayo Nchimbi mwenyewe tayari ameionyesha katika barua yake ya kujiuzulu: kustaafu siasa na utumishi wa umma.

Katika barua yake kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Nchimbi alisema si tu anaondoka kwenye nafasi ya Makamu wa Rais, bali pia anastaafu siasa.

Iwapo atashikilia uamuzi huo, anaweza kuchagua maisha nje ya siasa, akijikita katika shughuli binafsi kama kilimo na ufugaji, badala ya kutafuta nafasi nyingine ya kisiasa.

Hii pia si njia ambayo haijawahi kuchukuliwa na viongozi wakubwa nchini Tanzania.

Makamu wa Rais Philip Mpango, kwa mfano, aliwahi kusema katika nyakati mbalimbali kuhusu maisha yake kabla ya kuingia serikalini na umuhimu wa shughuli binafsi, ingawa safari yake ni tofauti na ya Nchimbi.

Kwa Nchimbi, hata hivyo, kuachana kabisa na siasa kunaweza kuwa uamuzi mgumu zaidi kwa kuzingatia umri wake, uzoefu wake na nafasi kubwa alizowahi kushika. Pia alikuwa natajwatajwa kuhusu urais wa mwaka 2030.

Amefanya kazi serikalini, amekuwa mbunge, amewahi kuwa balozi, Katibu Mkuu wa CCM na hatimaye Makamu wa Rais.

Kwa mwanasiasa mwenye historia hiyo, kuondoka kwenye siasa si sawa na kuondoka kwenye kazi ya kawaida. Ni uamuzi wa kuacha mtandao, ushawishi na nafasi ambayo amekuwa akiijenga kwa miongo kadhaa.