Tigray yakana kuanzisha mashambulizi, hofu ya kurejea kwa vita yazuka

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Ubalozi wa Marekani nchini Ethiopia umeituhumu TPLF kwa kuanzisha mashambulizi makubwa ya kijeshi. Katika taarifa iliyotolewa, Septemba 23, 2026, Balozi wa Marekani nchini Ethiopia, Ervin J. Massinga, alisema amesikitishwa kuona uongozi wa TPLF, ambao Marekani iliwekea vikwazo mapema mwaka huu, ukifanya “uamuzi usio sahihi wa kuanzisha mashambulizi makubwa.”
Hata hivyo, uongozi wa eneo la Tigray umekanusha vikali tuhuma hizo. Makamu wa rais wa eneo hilo, Amanuel Assefa, alielezea kauli ya balozi huyo katika chapisho kwenye mitandao ya kijamii kuwa “ya kukatisha tamaa sana,” huku akiishutumu Marekani na wajumbe wa Umoja wa Afrika kwa kupuuza athari za mashambulizi ya ndege zisizo na rubani pamoja na mashambulizi ya mara kwa mara ya anga yanayofanywa na kile alichokiita “utawala wa kidikteta.”
Amesema mashambulizi ya mabomu yamesababisha “vifo vingi vya raia” huko Tigray, akieleza hali ngumu wanayokabili mamia ya maelfu ya watu waliokimbia makazi yao na wanaoishi katika kambi za muda.
“Ni vigumu kuelewa jinsi kuhamishia lawama upande mwingine kwa namna hii kunavyoweza kuchukuliwa kuwa ni haki,” Amanuel aliandika, akiongeza kuwa wasiwasi kuhusu kutokuegemea upande wowote katika diplomasia bado ni “jambo la kutia wasiwasi mkubwa.”
Serikali ya Ethiopia na chama tawala katika eneo la Tigray kaskazini mwa nchi hiyo zimeshutumiana kuhusika na mashambulizi hayo, hali inayozua hofu ya kurejea kwa mapigano makubwa.
Getachew Reda, waziri wa serikali na mshauri wa Waziri Mkuu wa Ethiopia, amesema wapiganaji wa Tigray wamechukua udhibiti wa viwanja vya ndege vinavyodhibitiwa na serikali ya shirikisho huko Tigray, na wameanzisha mashambulizi katika maeneo jirani ya Afar na Amhara.
Awali, mamlaka za Tigray zilisema vikosi vyao vimelazimika kuingia katika “vita vya kujihami.” Kauli hiyo ilitolewa baada ya kuripotiwa mashambulizi ya ndege zisizo na rubani huko Tigray.
Vita vya miaka miwili huko Tigray vilimalizika mwaka 2022, lakini katika miezi ya hivi karibuni pande zote mbili zimekuwa zikishutumiana kwa kukiuka makubaliano ya amani.
Vita hivyo vilikuwa miongoni mwa migogoro iliyosababisha vifo vingi zaidi katika karne hii. Mpatanishi wa Umoja wa Afrika alikadiria kuwa karibu watu 600,000 walifariki katika mzozo huo, uliosababisha eneo hilo kuingia katika hali mbaya ya kibinadamu inayokaribia kuwa janga la njaa.



