Viongozi 10 wa Afrika waliouawa wakiwa madarakani

Chanzo cha picha, Getty Images/BBC
- Author, Abdou Aziz Diédhiou
- Nafasi, BBC News Afrique
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 10
Patrice Lumumba, Thomas Sankara, Anwar Sadat, Melchior Ndadaye... Orodha ya viongozi wa Afrika, wakuu wa nchi au serikali, waliouawa kwa kupigwa risasi wakiwa madarakani ni ndefu.
Baadhi ya mauaji hayo yalivuka mipaka ya mzozo wa ndani wa kisiasa wa kutaka kudhibiti madaraka. Wakati mwingine yalihusisha njama tata zilizowahusisha watu wa ndani na wahusika kutoka nje ya nchi.
Katika makala hii, BBC News Africa inaangazia mauaji 10 ya kisiasa yaliyoacha alama kubwa katika historia ya bara la Afrika.
1. Patrice Lumumba - DRC

Chanzo cha picha, Getty Images Bettmann
Ikiwa kuna mauaji ya kisiasa ambayo yameacha alama kubwa katika historia ya Afrika, ni mauaji ya Patrice Lumumba mwaka 1961 nchini Congo.
Aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu baada ya chama chake, Congolese National Movement (MNC), kushinda uchaguzi wa Mei 1960. Wiki chache baadaye, Lumumba alijitokeza wakati wa sherehe za kutangazwa kwa uhuru wa Congo, Juni 30, 1960.
Siku hiyo, alimjibu kwa ukali Mfalme Baudouin wa Ubelgiji, ambaye alikuwa amesifu kazi ya kikoloni ya babu yake, Mfalme Leopold II.
Lumumba alilaani waziwazi ukatili na ubaguzi aliowahi kukumbana nao yeye na Waafrika wengine wakati wa utawala wa kikoloni.
Hotuba hiyo, iliyotafsiriwa kama ukosoaji wa moja kwa moja wa ukoloni wa Ubelgiji, ilizidisha mvutano kati yake na taifa hilo lililokuwa limetawala Congo.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Akiwa kiongozi wa serikali mpya huru, Lumumba pia alishutumiwa na wapinzani wake kwa kutaka kuiingiza Congo katika kambi ya Umoja wa Kisovieti wakati wa Vita Baridi, jambo lililozitia wasiwasi nchi za Magharibi, hususan Marekani.
Ndani ya nchi, Congo ilikumbwa na machafuko makubwa ya kisiasa, yakiwemo jaribio la kujitenga kwa Katanga. Viongozi wa harakati hiyo walikuwa wakimpinga vikali Lumumba.
Septemba 5, 1960, Rais Joseph Kasa-Vubu aliamua kumuondoa Lumumba katika nafasi ya Waziri Mkuu.
Lumumba aliwekwa katika kifungo cha nyumbani, lakini alifanikiwa kutoroka na kujaribu kufika katika ngome yake ya kisiasa ya Stanleyville. Hata hivyo, alikamatwa na wanajeshi waliokuwa wakiongozwa na Mobutu na kukabidhiwa kwa mamlaka za Katanga.
Januari 17, 1961, aliteswa na kisha kuuawa kwa kupigwa risasi. Mwili wake uliyeyushwa kwa tindikali ili kufuta ushahidi wa mauaji hayo.
Kwa miongo kadhaa, jino moja tu lililokuwa limehifadhiwa na polisi mmoja wa Ubelgiji aliyeshiriki katika kuharibu mwili wake ndilo lililobaki. Jino hilo lilikabidhiwa kwa familia yake na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) miaka kadhaa baadaye.
Ubelgiji na Marekani, hasa kupitia shirika lake la ujasusi CIA, vimehusishwa kwa muda mrefu na mauaji hayo.
2. Sylvanus Olympio - Togo

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Sylvanus Olympio anachukuliwa kuwa baba wa uhuru wa Togo.
Kabla ya kushika wadhifa wa juu zaidi nchini humo, alishikilia nafasi kadhaa za uwaziri na baadaye kuwa Waziri Mkuu kuanzia mwaka 1958.
Baada ya Togo kupata uhuru Aprili 27, 1960, akawa rais wa kwanza wa Jamhuri ya Togo.
Akiwa mkuu wa nchi, alikosolewa na wapinzani wake waliomtuhumu kwa kuendesha serikali kwa njia ya kimabavu. Pia baadhi ya waangalizi walimtaja kuwa alitaka kuitenga Togo na Ufaransa.
Taarifa mbalimbali zinasema alikuwa na azma ya kuanzisha sarafu ya taifa na kujitenga na CFA franc.
Usiku wa Januari 12-13, 1963, kundi la wanajeshi lilivamia vituo vya mamlaka.
Olympio alijaribu kujificha katika ubalozi wa Marekani, uliokuwa karibu na Ikulu. Lakini waasi walimtambua na kumkamata, kabla ya kumuua Januari 13, 1963.
Baada ya mauaji yake, Nicolas Grunitzky, mpinzani wake wa kisiasa na pia shemeji yake, alirejea kutoka uhamishoni na kushika urais.
Hata hivyo, utawala wake ulikuwa mfupi.
Mwaka 1967, alipinduliwa katika mapinduzi yaliyoongozwa na Gnassingbé Eyadéma, ambaye kwa muda mrefu alitajwa kuwa mtu aliyempiga risasi Sylvanus Olympio, ingawa baadaye simulizi hiyo ilipingwa.
Eyadéma alitawala Togo kwa karibu miaka 38 hadi alipofariki Februari 2005.
Tangu wakati huo, mwanawe Faure Gnassingbé amekuwa akiongoza Togo.
3. Murtala Mohammed - Nigeria

Chanzo cha picha, Universal History Archive/Universal Images Group via Getty Images
Kisa cha Murtala Mohammed hakifahamiki sana kwa umma kwa ujumla. Jenerali Murtala Mohammed alikuwa mkuu wa kijeshi wa Nigeria na kiongozi mkuu wa nne wa nchi hiyo.
Akiwa afisa wa jeshi la Nigeria, aliongoza mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 1966 yaliyomuondoa madarakani Johnson Aguiyi-Ironsi. Pia alishiriki kwa kiwango kikubwa katika Vita vya wenyewe kwa wenyewe vya Nigeria kabla ya kushika urais Julai 29, 1975.
Februari 13, 1976, akiwa njiani kuelekea ofisini katika kambi ya kijeshi mjini Lagos, Murtala Mohammed aliuawa katika shambulizi la kuvizia lililoongozwa na Kanali Buka Suka Dimka.
Dimka alikuwa akijaribu kufanya mapinduzi ya kijeshi ambayo hatimaye yalishindwa.
Leo, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Lagos umepewa jina lake. Pia kuna jiwe la kumbukumbu lililowekwa katika eneo alikouawa.
Hata hivyo, wakazi wengi wa Lagos wanaopita kwenye mnara huo hawajui sana historia ya kifo chake.
4. Anwar El-Sadat - Misri

Chanzo cha picha, William Karel/Sygma via Getty Images
Mauaji ya Anwar Sadat yalisababisha baadhi ya watu kusherehekea katika miji mikuu ya nchi za Kiarabu.
Sadat alikuwa kiongozi wa kwanza wa nchi ya Kiarabu kutembelea Israel na kutoa hotuba katika Knesset, bunge la Israel.
Pia alikuwa kiongozi wa Misri wakati wa Vita vya Yom Kippur vya mwaka 1973, ambapo majeshi ya Misri yalifanya mashambulizi dhidi ya wanajeshi wa Israel waliokuwa wameikalia Sinai tangu Vita vya siku sita vya mwaka 1967.
Sadat pia ndiye aliyesaini Mkataba wa Camp David mwaka 1978, ulioweka msingi wa amani kati ya Misri na Israel.
Oktoba 6, 1981, Sadat aliuawa wakati wa gwaride la kijeshi.
Siku hiyo, kundi la wanajeshi lilishuka kutoka kwenye lori katikati ya gwaride, likarusha maguruneti ili kusababisha vurugu na kisha kuanza kuwafyatulia risasi viongozi waliokuwa kwenye jukwaa rasmi.
Sadat alijeruhiwa vibaya na kupelekwa hospitalini, ambako alifariki saa mbili baadaye.
Kundi la Muslim Brotherhood, ambalo mmoja wa watu wake mashuhuri, Omar Abdel Rahman, alikuwa ametoa fatwa ya kutaka kuuawa kwa rais huyo kwa kile wakosoaji wake walichodai kuwa ni kusaliti masuala ya Waarabu na Palestina kwa kusaini mkataba wa amani wa upande mmoja, lilituhumiwa kuhusika katika shambulizi hilo.
Lakini Sadat pia alikuwa na maadui wengi.
Septemba 1981, wiki chache kabla ya kuuawa kwake, alianzisha kampeni kubwa ya kuwakamata na kuwazuia wapinzani wa kisiasa, wakomunisti, Waislamu wenye msimamo mkali, wanachama wa Muslim Brotherhood na wasomi kadhaa.
5- Thomas Sankara - Burkina Faso

Chanzo cha picha, Patrick Durand/Sygma via Getty Images
Kama Lumumba, Thomas Sankara alikuwa kiongozi mwenye uzalendo, aliyekuwa akiunga mkono Pan-Africanism na kupinga ubeberu wa Magharibi nchini Burkina Faso na katika nchi zinazozungumza Kifaransa barani Afrika.
Alishika madaraka mwaka 1983 na kuuawa Oktoba 15, 1987.
Kwa mujibu wa mpangilio wa matukio uliowekwa na waendesha mashtaka wa Burkina Faso wakati wa kesi ya waliohusika na mapinduzi hayo ya umwagaji damu, yaliyofanyika kati ya Oktoba 2021 na Aprili 2022, Sankara alielekea katika Baraza la Entente, makao makuu ya National Revolutionary Council, majira ya saa 10:20 jioni Oktoba 15, 1987.
Alipoingia katika chumba cha mkutano, watu waliokuja kumuua walikuwa tayari wamefika.
Kundi lililotumwa kumuua liliwapiga risasi walinzi wake, kisha likawagawa watu waliokuwamo humo katika makundi mawili.
Sankara na washirika wake waliamriwa kutoka nje ya chumba hicho na wakapigwa risasi mmoja baada ya mwingine.
Dunia ilipata habari za mapinduzi hayo siku hiyo hiyo na baadaye ikabaini kwamba aliyekuwa nyuma ya tukio hilo alikuwa Blaise Compaoré, aliyekuwa rafiki na mshirika wa karibu wa Sankara.
Kifo cha Sankara kilibadili mwelekeo wa kisiasa na kiuchumi wa Burkina Faso. Hata hivyo, jina lake limeendelea kuwa sehemu muhimu ya historia ya nchi hiyo.
Hadi leo, Sankara anaendelea kuheshimiwa na sehemu kubwa ya vijana barani Afrika wanaojitambulisha na mapambano yake dhidi ya ubeberu wa Magharibi.
6- Mohamed Boudiaf - Algeria

Chanzo cha picha, Daniel SIMON/Gamma-Rapho via Getty Images
Mohamed Boudiaf alikuwa rais wa High State Committee ya Algeria, serikali ya mpito iliyokuwa ikitekeleza majukumu ya mkuu wa nchi.
Alishika madaraka Januari 1992, baada ya jeshi kusitisha mchakato wa uchaguzi nchini humo.
Katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa bunge wa vyama vingi uliofanyika Desemba 1991, Islamic Salvation Front (FIS) iliongoza kwa kiasi kikubwa dhidi ya vyama vingine.
Kutokana na uwezekano mkubwa wa chama hicho kushinda duru ya pili iliyopangwa kufanyika Januari 16, 1992, jeshi lilisitisha mchakato wa uchaguzi na kuunda serikali ya mpito ya miaka miwili ili kuongoza nchi na kuzuia kile lilichodai kuwa ni hatari ya nchi kutawaliwa na wanamgambo wa Kiislamu.
Mohamed Boudiaf alikubali kuongoza serikali hiyo na kupewa mamlaka ya muda Januari 16, 1992.
Miezi michache baadaye, alitembelea Annaba ambako alipanga kutoa hotuba muhimu.
Akiwa mbele ya kamera za televisheni, hotuba yake ilikatizwa na mlipuko wa bomu na kisha milio ya risasi.
Mmoja wa viongozi wa jeshi , ambaye alielezwa kuwa Mwislamu mwenye msimamo mkali, alimfyatulia rais risasi kwa bunduki aina ya submachine gun.
Mshambuliaji huyo alikamatwa mara moja, lakini hakutoa taarifa kuhusu sababu za shambulizi hilo au mtu aliyeliagiza.
Mohamed Boudiaf hakunusurika. Alipteza maisha
7- Melchior Ndadaye - Burundi

Chanzo cha picha, DABROWSKI/AFP via Getty Images
Melchior Ndadaye alihudumu kama rais wa Burundi kwa siku 102 tu.
Julai 1993, alichaguliwa kuwa rais wa kwanza wa Burundi kwa njia ya kidemokrasia, baada ya kupata zaidi ya asilimia 64 ya kura.
Mpinzani wake mkuu, rais aliyekuwa madarakani Pierre Buyoya, alipata asilimia 32.47.
Saa chache kabla ya kuuawa Oktoba 21, 1993, tetesi za mapinduzi ya kijeshi zilisambaa mjini Bujumbura hadi kuwafikia maafisa wa rais, ambao walijaribu bila mafanikio kuthibitisha ukweli wa taarifa hizo.
Oktoba 20, 1993, mkuu wa ujasusi wa jeshi la gendarmerie aliwafahamisha wakubwa wake kuhusu hali ya mvutano iliyokuwa ikiongezeka mjini Bujumbura. Tetesi za mapinduzi zilizidi kusambaa.
Usiku wa Oktoba 20-21, vikosi vya jeshi vilianzisha mapinduzi na kuzingira Ikulu ya rais mjini Bujumbura.
Melchior Ndadaye, familia yake na baadhi ya wafuasi wake waliondolewa na walinzi wake na kupelekwa katika kambi ya kijeshi.
Lakini viongozi wa mapinduzi waliwafuatilia na hatimaye wakawapata.
Ndadaye, ambaye baadaye alijulikana kama "shujaa wa demokrasia", pamoja na baadhi ya washirika wake wa karibu, waliuawa kikatili Oktoba 21 mwaka huo.
8- Ibrahim Baré Maïnassara - Niger

Chanzo cha picha, ISSOUF SANOGO / AFP via Getty Images
Aprili 9, 1999, Rais wa Niger Ibrahim Baré Maïnassara alipigwa risasi na kuuawa.
Zaidi ya miongo miwili baadaye, mazingira kamili ya mauaji yake bado hayajaeleweka.
Kinachojulikana kwa uhakika ni kwamba risasi zilizomuua zilitoka sehemu ya walinzi wake.
Wakati huo walinzi hao walikuwa wakiongozwa na Daouda Mallam Wanké, ambaye alichukua madaraka baada ya mapinduzi.
Kwa mujibu wa baadhi ya taarifa, Maïnassara alivamiwa na kuuawa na wanajeshi waliokuwa wameasi wakati akijaribu kuondoka nchini.
Mamlaka za kijeshi zilisema kifo chake kilikuwa "ajali ya kusikitisha".
Katika kujibu ripoti ya Amnesty International iliyokuwa ikihoji mazingira ya mauaji hayo, Daouda Mallam Wanké, ambaye wakati huo alikuwa mkuu wa utawala wa kijeshi, alisema jeshi lilikuwa na nia "si kumuua, bali kumkamata Rais Baré."
Wanké alifariki mwaka 2004, akiwa madarakani kutoa msamaha kwa waliohusika na mapinduzi hayo.
9- Laurent Désiré Kabila - RDC

Chanzo cha picha, ODD ANDERSEN/AFP via Getty Images
Mtu aliyempindua Mobutu Sese Seko, Laurent-Désiré Kabila, aliuawa Januari 16, 2001.
Hadi leo, maswali mengi bado hayajajibiwa kuhusu kifo chake.
Hata hivyo, inajulikana kwamba Kabila alipigwa risasi na kuuawa ofisini kwake katika ikulu na mmoja wa walinzi wake wa karibu.
Mshambuliaji huyo, Rachidi Mizele, alikuwa mwanajeshi kijana aliyejiunga na Alliance of Democratic Forces for the Liberation of Congo-Zaire (AFDL), kundi la waasi lililomuingiza Kabila madarakani baada ya kuliteka jiji la Kinshasa na kuumaliza utawala wa Mobutu Sese Seko wa miongo kadhaa.
Rachidi Mizele baadaye aliuawa na Eddy Kapend, kanali aliyekuwa karibu na rais.
Wakati tetesi kuhusu kifo cha Kabila zikienea, mamlaka zilijaribu kuweka hali ya sintofahamu kabla ya kutangaza rasmi Januari 18 kwamba "Mzee", kama alivyokuwa akijulikana, amefariki.
Tume ya kimataifa ya uchunguzi ilihitimisha kwamba kulikuwa na njama iliyohusisha nchi jirani za DRC pamoja na watu waliokuwa karibu na kiongozi huyo wa zamani wa waasi.
Makumi ya watu walipatikana na hatia ya kushiriki katika njama hiyo katika kesi ambayo, hata hivyo, haikuondoa kabisa maswali kuhusu mauaji hayo ya kisiasa.
10- Joao Bernardo ''Nino'' Vieira - Guinée Bissau

Chanzo cha picha, (Photo by SEYLLOU DIALLO/AFP via Getty Images)
João Bernardo "Nino" Vieira alikuwa rais wa Guinea-Bissau na wakati huo alikuwa na umri wa miaka 69.
Akiwa mwanajeshi wa zamani wa msituni, alishiriki kwa kiasi kikubwa katika harakati za nchi hiyo za kupata uhuru na alishikilia urais kwa vipindi tofauti kwa karibu miaka 23.
Alipinduliwa katika mapinduzi ya mwaka 1998 na kwenda uhamishoni nchini Ureno hadi mwaka 2005.
Baadaye alirejea madarakani baada ya kuondolewa kwa mrithi wake, Kumba Yala, ambaye alikuwa amechaguliwa kidemokrasia lakini baadaye akapinduliwa katika mapinduzi.
Wakati huo, hali ya kisiasa nchini humo ilikuwa na ushindani mkubwa kati ya Rais Vieira na Mkuu wa Majeshi, Jenerali Batista Tagme Na Waie.
Mvutano huo ulihusishwa pia na vita dhidi ya magenge ya dawa za kulevya yaliyokuwa yakitumia Guinea-Bissau kama njia ya kusafirisha dawa hizo.
Machi 1, 2009, Jenerali Batista Tagme Na Waie aliuawa katika mlipuko wa bomu kwenye makao makuu ya jeshi.
Saa chache baadaye, wanajeshi waliokuwa watiifu kwa Mkuu huyo wa Majeshi walivamia makazi ya rais mapema Machi 2.
Nino Vieira, ambaye alikuwa amebaki katika makazi yake huku mke na watoto wake wakikimbilia katika ubalozi wa Angola, alishambuliwa kwa mapanga kabla ya kupigwa risasi na kuuawa.
Baadaye jeshi lilisema mauaji yake yalifanywa na kundi la wanajeshi waliokuwa wakitenda kwa hiari yao wenyewe.














