Je, Iran inaweza kutega mabomu katika mlango bahari wa Hormuz?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, Reza Thabeti
- Nafasi, Mwandishi
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 7
Awamu ya karibuni ya mvutano kati ya Iran na Marekani ilianzia katika Kisiwa cha Larak, eneo lililo karibu na Lango la Bahari la Hormuz, mojawapo ya njia muhimu zaidi za usafirishaji wa mafuta duniani.
Baada ya kipindi cha takriban mwezi mmoja bila mashambulizi ya moja kwa moja ya Marekani dhidi ya Iran, Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) ilisema imefanya mashambulizi yaliyolenga mifumo miwili ya Kikosi cha Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC) katika kisiwa hicho tarehe 30 Agosti.
Kwa mujibu wa msemaji wa CENTCOM, Kapteni Tim Hawkins, wanajeshi wa IRGC walionekana wakijiandaa kurusha makombora yaliyobeba migodi ya majini kuelekea Lango la Hormuz. Marekani ilisema hatua hiyo ilitafsiriwa kuwa tishio kwa usalama wa usafiri wa baharini katika eneo hilo.
Iran ilijibu kwa kurusha makombora dhidi ya kituo cha kijeshi kinachotumiwa na vikosi vya Marekani nchini Jordan, hatua iliyochochea kurejea kwa makabiliano ya moja kwa moja kati ya pande hizo mbili baada ya kipindi cha utulivu wa kiasi.
Kilichovutia wachambuzi wengi wa masuala ya kijeshi ni mbinu iliyodaiwa kutumiwa na Iran ya kutega mabomu ya majini. Tofauti na njia za kawaida, ambapo mabomu hutegwa baharini kwa kutumia meli au boti, safari hii ilidaiwa kuwa mabomu hayo yangerushwa kwa kutumia makombora kutoka pwani.
Walinzi wa Mapinduzi wa Iran wamewahi kuonyesha kile ambacho vyombo vya habari vya serikali vilisema ni uwezo wa kutumia teknolojia hiyo wakati wa mazoezi ya kijeshi katika miaka ya hivi karibuni. Hata hivyo, tukio la Kisiwa cha Larak linaonekana kuwa mara ya kwanza ambapo mfumo huo umetajwa kuhusishwa na hali halisi ya mapambano kati ya Iran na Marekani.
Wataalamu wa usalama wa baharini wanasema matumizi ya makombora kubeba mabomu yanaweza kufanya iwe vigumu zaidi kutambua na kuzuia vitisho dhidi ya meli zinazopita katika Lango la Hormuz, njia ambayo sehemu kubwa ya mafuta ya dunia hupitishwa kila siku.
Mvutano huo mpya unaongeza wasiwasi kuhusu usalama wa eneo la Ghuba na hatari ya kuongezeka kwa mzozo ambao unaweza kuathiri biashara ya kimataifa na usambazaji wa nishati duniani.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Muda wa tukio hilo ulikuwa wa umuhimu mkubwa. Siku mbili tu kabla ya shambulio la Kisiwa cha Larak, Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) ilikuwa imetangaza kuwa mabomu yaliyokuwa yametegwa kando ya njia za kimataifa za usafiri wa meli katika Lango la Bahari la Hormuz yalikuwa yameondolewa.
Kwa mujibu wa gazeti la Financial Times, operesheni hiyo ya kuondoa mabomu ilidumu kwa muda wa miezi minne na ilitekelezwa kwa kiwango kikubwa yakati za usiku ili kupunguza hatari za kiusalama. Operesheni hiyo ilihusisha wapiga mbizi wa Jeshi la Wanamaji la Marekani, boti zinazoendeshwa kutoka mbali pamoja na maboti yasio na muelekezi yanayofanya kazi chini ya maji.
Shirika la Kimataifa la Baharini lilikadiria mwezi Juni kwamba kulikuwa na takriban mabomu 80 yaliyotegwa karibu na njia muhimu za meli katika eneo hilo. Uwepo wa mabomu hayo ulizua hofu kuhusu usalama wa usafirishaji wa kimataifa kupitia Hormuz, njia inayobeba sehemu kubwa ya mafuta na bidhaa za nishati duniani.
Mwishoni mwa Agosti, Rais wa Marekani Donald Trump alisema mabomu yote yaliyokuwa katika njia za kimataifa za usafiri wa majini yalikuwa yameondolewa au kuharibiwa. Hata hivyo, licha ya tangazo hilo, huduma mbalimbali za ufuatiliaji wa usalama wa baharini ziliendelea kutoa tahadhari kuhusu uwezekano wa kuwepo kwa mabomu yanayoelea au yale ambayo hayakuwa yameainishwa kwenye ramani rasmi.
Katika mazingira hayo, madai ya Marekani kwamba wanachama wa Walinzi wa Mapinduzi ya Iran walikuwa wakijiandaa kurusha makombora yaliyobeba migodi ya majini kutoka Kisiwa cha Larak yalionekana kama tishio jipya kwa juhudi zilizokuwa zimefanyika kusafisha njia za usafiri wa meli. Tukio hilo liliibua hofu kwamba hata baada ya operesheni ndefu ya kuondoa mabomu, njia za baharini za Hormuz zinaweza kuendelea kubaki katika hatari kutokana na mbinu mpya za vita vya majini.
Kwa wachambuzi wa usalama, matukio hayo yanaonyesha jinsi ushindani kati ya Iran na Marekani unavyozidi kuhamia katika mbinu zisizo za kawaida, huku udhibiti wa usalama wa njia za baharini ukiendelea kuwa moja ya maeneo nyeti zaidi katika mzozo huo.
Scott Savitz, mhandisi mwandamizi katika Shirika la RAND, aliambia BBC Idhaa ya Kiajemi kwamba kutega mabomu hayo kunahitaji rasilimali chache sana ikilinganishwa na kuiondoa, na kunaweza kufanyika kwa haraka zaidi.
Aliongeza: "Kutengeneza eneo lenye mabomu kunaweza kuchukua saa chache,lakini kufungua njia salama kupitia eneo hilo kunaweza kuchukua siku au wiki kadhaa."
Wazo lililofichuliwa wakati wa mazoezi ya Walinzi wa Mapinduzi
Mfumo huo, unaoonekana kuwa mtangulizi wa ule uliotajwa na Marekani katika tukio la Kisiwa cha Larak, uliwasilishwa hadharani wakati wa zoezi la kijeshi la Great Prophet 19 lililoendeshwa na Jeshi la Wanamaji la Walinzi wa Mapinduzi ya Iran (IRGC) mwezi Januari 2025.
Picha na video zilizorushwa na vyombo vya habari vya Iran zilionyesha makombora kadhaa yakirushwa kutoka kwenye mifumo ya kurushia iliyowekwa juu ya malori. Baada ya kurushwa, video hizo zilionyesha vitu vyenye umbo la koni vikitua majini na kuelea juu ya bahari, vikielezwa kuwa ni mabomu ya majini.
Shirika la habari la Defa Press, ambalo lina uhusiano na taasisi za kijeshi za Iran, lilisema mabomu hayo huwekwa ndani ya chombo maalumu kinachofanana na makombora ya Fajr-5 kabla ya kurushwa kutoka pwani kuelekea maeneo yaliyolengwa baharini.
Kwa mujibu wa maelezo hayo, mfumo huo unaipa Iran uwezo wa kutega mabomu katika maeneo tofauti baharini kutoka nchi kavu, badala ya kutegemea meli au boti za kijeshi. Wachambuzi wa masuala ya ulinzi wanasema mbinu hiyo inaweza kupunguza hatari kwa vikosi vinavyotega maomu hayo na kuongeza kasi ya utekelezaji wa operesheni hizo.
Maonyesho ya mfumo huo katika mazoezi ya kijeshi yalivutia wataalamu wa usalama wa baharini, lakini hadi tukio la hivi karibuni la Kisiwa cha Larak hakukuwa na ushahidi wazi wa kuhusishwa kwake na makabiliano halisi ya kijeshi. Hilo ndilo lililofanya madai ya Marekani kuhusu maandalizi ya kurusha mabomu kwa kutumia mifumo ya kurusha makombora kuelekea Lango la Bahari la Hormuz kuvuta hisia za jumuiya ya kimataifa.
Ikiwa mfumo huo ndio uliokuwa ukitumiwa katika kisiwa hicho, ungeashiria hatua mpya katika mbinu za Iran za kuzuia au kutishia usafiri wa meli katika mojawapo ya njia muhimu zaidi za biashara ya mafuta duniani. Mfumo huo pia unaonyesha jinsi teknolojia mpya zinavyoendelea kubadilisha mbinu za vita vya baharini katika eneo la Ghuba.
Kwa nini mfumo wa makombora wa "Fajr-5" umevuta hisia nyingi?

Chanzo cha picha, Tasnim News
Mfumo wa makombora wa Fajr-5 umeibuka kuwa kitovu cha mjadala katika mzozo wa hivi karibuni kati ya Iran na Marekani kutokana na madai kwamba unaweza kutumika kurusha mabomu ya majini kutoka nchi kavu na kuyapeleka baharini. Mbinu hiyo, iwapo itatumika kwa kiwango kikubwa, inaweza kubadilisha namna vitisho vya usalama wa baharini vinavyotekelezwa katika Lango la Bahari la Hormuz.
Tofauti na njia za kawaida za kutega mabomu ya majini kwa kutumia meli, boti au ndege, Fajr-5 inadaiwa kuwa inaweza kurusha mabomu hayo kwa kutumia makombora kutoka pwani. Hatua hiyo inaweza kuipa Iran uwezo wa kuweka mabomu katika maeneo ya bahari bila kupeleka vyombo vyake majini, jambo ambalo lingeifanya operesheni hiyo kuwa ngumu zaidi kugunduliwa au kuzuiwa.
Mjadala kuhusu Fajr-5 uliongezeka baada ya jeshi la Marekani kusema kuwa lililenga vifaa vya Walinzi wa Mapinduzi wa Iran katika Kisiwa cha Larak, kufuatia madai kwamba kulikuwa na maandalizi ya kurusha makombora yaliyobeba mabomu ya majini. Tukio hilo liliufanya mfumo huo wa silaha kuwa sehemu muhimu ya mvutano mpya kati ya Tehran na Washington.
Fajr-5 si silaha mpya. Mfumo huo ulitengenezwa nchini Iran katika miaka ya 1990 kama mfumo wa kurusha makombora mengi kwa wakati mmoja. Makombora yake yana uwezo wa kufikia umbali wa takriban kilomita 75, huku baadhi ya matoleo mapya yakitajwa kuwa na uwezo wa kufika mbali zaidi.
Wachambuzi wa masuala ya kijeshi wanasema umuhimu wa Fajr-5 kwa sasa haupo katika uwezo wake wa kawaida wa kushambulia malengo ya ardhini, bali katika madai ya kugeuzwa kuwa mfumo wa kutawanya mabomu ya majini kwa haraka katika maeneo muhimu ya usafiri wa meli. Ikiwa uwezo huo utathibitishwa, unaweza kuongeza changamoto kwa juhudi za kulinda usalama wa njia za baharini katika Ghuba ya Uajemi.
Kwa kifupi, sababu ya Fajr-5 kuzungumziwa sana ni kwamba imehusishwa na mbinu mpya inayoweza kubadili mwenendo wa vita vya majini katika lango la Hormuz, mojawapo ya njia muhimu zaidi za biashara na usafirishaji wa nishati duniani.

Chanzo cha picha, IRIB
Wataalamu wa masuala ya kijeshi wametilia shaka uwezo wa mfumo wa Fajr-5 kutumika kurusha mabomu ya majini, wakisema kuwa kuna changamoto kubwa za kiufundi zinazoweza kuathiri ufanisi wa mbinu hiyo.
Akizungumza na BBC Persian, mchambuzi wa masuala ya ulinzi, Savitz, alisema kuwa mabomu ya majini kwa kawaida hutegwa kwa meli za juu ya maji, nyambizi au ndege. Mabomu yanayodondoshwa kutoka angani mara nyingi hutumia parachuti ili kupunguza kasi wakati wa kushuka na kuzuia uharibifu.
"Kwa ujumla, mabomu ya majini hayarushwi kwa makombora," alisema. "Badala yake, hudondoshwa kutoka kwenye meli, nyambizi au ndege."
Kwa mujibu wake, moja ya changamoto kuu ni namna ya kuunganisha kombora na bomu la majini bila kulisababishia uharibifu mkubwa wakati wa kurushwa au linapoingia majini.
"Ni vigumu kufikiria mfumo unaounganisha kombora na bomu la majini kwa namna ambayo bomu hilo halitaharibiwa vibaya wakati wa kurushwa au linapoingia majini, au katika hatua zote mbili," alisema. "Kimsingi jambo hilo linawezekana kinadharia, lakini kwa upande wa matumizi ya vitendo linaonekana kuwa gumu sana."
Wataalamu wanasema bomu lolote la majini linalobebwa na kombora lingelazimika kuhimili nguvu kubwa za kurushwa na baadaye kuingia majini bila kuharibu kifaa chake cha kulipua au vipengele vingine nyeti vinavyohitajika ili liweze kufanya kazi ipasavyo.
Mtazamo huo pia umeungwa mkono na Harlan Ullman, afisa wa zamani wa ngazi ya juu wa Jeshi la Wanamaji la Marekani. Katika mahojiano na Al Jazeera, alisema nguvu ya mgongano wakati bomu linaingia majini inaweza kusababisha uharibifu mkubwa kwa kifaa hicho na kuathiri uwezo wake wa kufanya kazi.
Aidha, Ullman alibainisha kuwa Iran tayari ina njia nyingine mbalimbali za kuweka mabomu ya majini, hali inayozua maswali kuhusu faida halisi ya kutumia mfumo wa makombora kutekeleza jukumu hilo.
Savitz pia alieleza changamoto nyingine inayohusiana na usiri wa operesheni hiyo. Alisema kwamba njia inayofuatwa na kombora pamoja na eneo ambalo mzigo wake unaingia majini vinaweza kuonekana kwa urahisi kupitia mifumo ya ufuatiliaji, jambo ambalo lingesaidia vikosi vya kuondoa mabomu kubaini haraka eneo la kufanya upekuzi.
"Kutega mabomu kutoka kwenye meli kunaweza kufanyika kwa usiri zaidi," alisema. "Hata kama meli inaweza kufuatiliwa, mara nyingi ni vigumu kujua mahali hasa mabomu yametegwa. Bomu linapodondoshwa kutoka kwenye meli husababisha tu mtawanyiko wa maji, jambo ambalo ni rahisi zaidi kuficha kuliko kurusha kombora."
Kkutokana na hilo, baadhi ya wachambuzi wanaamini kuwa ingawa matumizi ya Fajr-5 kutega mabomu ya majini yanaweza kuwa hatua ya ubunifu wa kijeshi, bado kuna maswali mengi kuhusu ufanisi wa utekelezaji wake katika mazingira halisi ya mapigano.















