Siri ya mwanamke mwenye umri mkubwa zaidi duniani

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Mfahamu mtu mwenye umri mkubwa zaidi duniani aliye hai na wengine waliowahi kushikilia rekodi hiyo.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Sista André, mtawa wa Kifaransa, aliyefariki mwaka 2023 akiwa na miaka 118.

Mtu mwenye umri mkubwa zaidi kuwahi kuthibitishwa duniani ni Jeanne Louise Calment, ambaye aliishi hadi umri wa miaka 122 na siku 164.

Ni jambo la kushangaza kufikiria mambo ambayo Calment na watu wengine waliofikisha umri wa miaka 110 au zaidi wameyashuhudia katika maisha yao. Hebu fikiria jinsi ilivyokuwa kuwa kijana katika miaka ya 1920, kuishi wakati wa Vita vya Dunia vya Kwanza na vya Pili, kushuhudia kutua kwa binadamu mwezini ukiwa na miaka ya 50 au 60, na kisha kuendelea kuishi hadi mwanzoni mwa karne ya 21 na kushuhudia maendeleo ya haraka na makubwa katika sayansi na teknolojia.

Kwa sasa, mtu mwenye umri mkubwa zaidi duniani, hadi Septemba 2026, ni Ethel Caterham wa Uingereza. Hivi karibuni ametimiza miaka 117, umri ambao ni mkubwa zaidi ya wastani wa umri wa kuishi wa binadamu.

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Mfalme Charles III apolikwenda kumtembelea Ethel Caterham mwenye umri wa miaka 117 hivi sasa

Nchini Uingereza, wastani wa umri wa kuishi kwa mwanaume ni miaka 79.1, huku wanawake wakitarajiwa kuishi wastani wa miaka 83, kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (ONS). Nchini Marekani, wastani huo ni mdogo kidogo, ambapo wanaume wanatarajiwa kuishi miaka 76.5, na wanawake miaka 81.4.

Kwa sababu mbalimbali za kitamaduni, kiafya, usafi na maendeleo ya kisayansi, wastani wa umri wa kuishi hutofautiana duniani kote kulingana na nchi unayoishi na hata eneo unaloishi ndani ya nchi hiyo.

Umoja wa Mataifa ulikadiria mwaka 2024 kwamba wastani wa umri wa kuishi duniani ni miaka 73.3 — takribani miaka minane zaidi ikilinganishwa na mwaka 1995.

Nani ndiye mtu mwenye umri mkubwa zaidi aliye hai duniani?

Mtu mwenye umri mkubwa zaidi aliye hai hadi Septemba 2026 ni Ethel Caterham, mwenye umri wa miaka 117.

Alizaliwa tarehe 21 Agosti 1909 huko Hampshire, Uingereza, wakati wa utawala wa Mfalme Edward VII. Kwa sasa anaishi katika nyumba ya wazee huko Lightwater, Surrey.

Kwa mujibu wa Guinness World Records, alikuwa mtoto wa pili kati ya watoto wanane. Kwa kushangaza, dada yake mkubwa, Gladys Babilas, naye aliishi zaidi ya miaka 100, akifariki akiwa na miaka 104 na siku 78.

Mume wake, ambaye alikutana naye kwa mara ya kwanza mwaka 1931, alifariki mwaka 1976 na kuacha gari lake aina ya Triumph Dolomite, ambalo Ethel aliendelea kuliendesha hadi alipofikisha umri wa miaka 97.

Kwa masikitiko, Ethel pia aliishi muda mrefu kuliko watoto wake wote wawili.

Waliowahi kushikilia rekodi hiyo

Jeanne Louise Calment – Mtu aliyeishi muda mrefu zaidi kuwahi kuthibitishwa

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Jeanne Louise Calment mwenye miaka 120 akiwa nyumbani

Jeanne Louise Calment ndiye mtu mwenye umri mkubwa zaidi kuwahi kuishi na kuthibitishwa rasmi. Mwanamke huyo kutoka Ufaransa aliishi hadi umri wa miaka 122 na siku 164.

Alizaliwa tarehe 21 Februari 1875 na alifariki tarehe 4 Agosti 1997, akiwa na miaka 122.

Kwa mujibu wa Guinness World Records, Calment alikula karibu kilo moja ya chokoleti kila wiki na alianza kuvuta sigara akiwa na miaka 21, tabia aliyoiacha alipofikisha miaka 117.

Pia aliwahi kusema kwamba aliuza turubai za kuchorea kwa Vincent van Gogh, ambaye alimtaja kuwa mtu mwenye sura mbaya, hasira kali na aliyenuka pombe.

Jiroemon Kimura – Mwanaume aliyeishi muda mrefu zaidi

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Jiroemon Kimura aliishi hadi miaka 116 na siku 54.

Mwanamume huyo kutoka Japan alizaliwa tarehe 19 Aprili 1897 na alifariki tarehe 12 Juni 2013.

Guinness World Records inamnukuu akisema: "Kula kidogo ili kuishi muda mrefu." Pia aliendelea kujishughulisha na kilimo hadi alipofikisha umri wa miaka 90.

Lucile Randon – Miaka 118

Mfaransa mwingine, Lucile Randon, aliishi hadi miaka 118 na siku 340.

Alizaliwa tarehe 11 Februari 1904 na alifariki tarehe 17 Januari 2023.

Kane Tanaka – Miaka 119

Kane Tanaka alizaliwa tarehe 2 Januari 1903 na alifariki tarehe 19 Aprili 2022.

Mwanamke huyo kutoka Japan aliishi hadi umri wa miaka 119 na siku 107.

Chiyo Miyako – Miaka 117

Mwingine kutoka Japan, Chiyo Miyako, alizaliwa tarehe 2 Mei 1901 na alifariki tarehe 22 Julai 2018.

Aliishi hadi umri wa miaka 117 na siku 81.

Nabi Tajima – Miaka 117

.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Maelezo ya picha, Nabi Tajima mwenye umri wa miaka 117

Mwanamke mwingine kutoka Japan, Nabi Tajima, aliishi hadi miaka 117 na siku 260.

Alizaliwa tarehe 4 Agosti 1900 na alifariki tarehe 21 Aprili 2018.

Violet Brown – Miaka 117

Tukielekea Jamaica, tunampata Violet Brown, ambaye aliishi hadi miaka 117 na siku 189.

Alizaliwa tarehe 10 Machi 1900 na alifariki tarehe 15 Septemba 2017.

Emma Martina Luigia Morano – Miaka 117

.

Chanzo cha picha, OLIVIER MORIN/AFP via Getty Images

Maelezo ya picha, Emma Morano in 2016

Emma Martina Luigia Morano kutoka Italia pia aliishi hadi umri wa miaka 117 na siku 137.

Alizaliwa tarehe 29 Novemba 1899 na alifariki tarehe 15 Aprili 2017.

María Branyas Morera – Miaka 117

María Branyas Morera alifariki akiwa na umri wa miaka 117 na siku 168 mwezi Agosti 2024. Wakati wa kifo chake, alikuwa mtu wa nane mwenye umri mkubwa zaidi kuwahi kuthibitishwa katika historia.

Alizaliwa tarehe 4 Machi 1907 huko San Francisco, California, na aliishi Texas na New Orleans kabla ya familia yake ya Kihispania kurejea Catalonia wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia.

Kwa mujibu wa Guinness World Records, aliwahi kueleza kwamba aliishi "maisha yenye utaratibu na yenye mahusiano mazuri kijamii... maisha mazuri, bila kupitiliza."

Susannah Mushatt Jones – Miaka 116

Susannah Mushatt Jones kutoka Marekani aliishi hadi miaka 116 na siku 311.

Alizaliwa tarehe 6 Julai 1899 na alifariki tarehe 12 Mei 2016.

Jeralean Talley – Miaka 116

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Jeralean Talley mwaka 2015

Mwisho katika orodha hii ni Jeralean Talley, ambaye pia alikuwa anatokea Marekani.

Aliishi hadi miaka 116 na siku 25. Alizaliwa tarehe 23 Mei 1899 na alifariki tarehe 17 Juni 2015.