Iran na Marekani zimebadili mbinu za kivita?

Chanzo cha picha, Getty Images
Siku moja ya mashambulizi, siku moja ya amani; mzunguko ambao umerudiwa mara nyingi katika mvutano kati ya Iran na Marekani katika miezi iliyofuata makubaliano ya Islamabad.
Jeshi la Marekani limelenga meli kadhaa za mafuta za Iran katika wiki za hivi karibuni, mashambulizi ambayo CENTCOM inasema yalikuwa ni majibu kwa makombora ya jeshi la Iran (IRGC) yaliyorushwa dhidi ya meli za Marekani.
IRGC pia imetangaza mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya meli za Marekani na kituo cha kijeshi cha Marekani nchini Jordan.
Kadiri mvutano unavyoongezeka, bei ya mafuta imevuka tena dola 100 kwa kila pipa. Hatua za kijeshi za Wahouthi na kuingia kwao katika mlingano wa kikanda kumezidisha ugumu wa hali hiyo.
Wakati huohuo, vitisho vya Rais wa Marekani Donald Trump, ikiwa ni pamoja na tishio la kukikalia kisiwa cha Kharg, vimeongeza wasiwasi kuhusu kuenea kwa mzozo huo.
Kwa nini Washington inaongeza mashambulizi ya kijeshi kuelekea uchaguzi wa katikati ya muhula, pamoja na mzingiro ambao umeathiri uchumi wa Iran, na hatua hizi zimebadilishaje hesabu za pande zote mbili?
Mashambulizi dhidi ya Meli za Mafuta
Katika kueleza mashambulizi dhidi ya meli hizo za mafuta, CENTCOM imezitaja kuwa sehemu ya mtandao wa ufadhili wa IRGC na makundi yanayoshirikiana nayo.
Baada ya duru ya kwanza, kamanda wa CENTCOM Brad Cooper alisema kuwa Marekani imeweka gharama kubwa zaidi za kiuchumi kwa kuzishambulia meli tatu za Iran ikiwa ni kisasi baada ya kurushwa kwa makombora dhidi ya meli zake mbili. Siku tatu baadaye, meli nyingine tano za mafuta zililengwa.
Mashambulizi hayo yameibua maswali miongoni mwa wachambuzi kuhusu kama Marekani inatafuta aina fulani ya mabadiliko ya sera kuelekea Iran.
Hamidreza Azizi, mchambuzi mkuu wa Iran katika taasisis ya International Crisis Group, aliiambia BBC: "Sidhani kama kuna mabadiliko ya sera. Kwa kweli, upande ambao umebadilisha sera yake ni Iran."
Anaamini kwamba katika hatua hii Marekani inataka kudumisha mzingiro wa majini, na kwamba Iran inajaribu kubadilisha hali hiyo kwa kutumia mkakati mkali zaidi.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Meli ambazo Iran imekuwa ikijaribu kuzilenga zina jukumu katika kutekeleza mzingiro huu. Bw. Azizi anaeleza kwamba kwa kuongeza gharama ya kushambulia vikosi hivi, Marekani inataka kujenga kizuizi katika hatua ya kufanya maamuzi na kuwakatisha tamaa maafisa wa Iran kuamuru shambulio jingine.
Katika hesabu hii, kuzuia mashambulizi ya Iran kunaruhusu shinikizo la kiuchumi kuendelea, ambalo Washington inatumaini litaifanya Tehran ikubali matakwa yake.
Mwanzoni mwa mzingiro huo, waangalizi walidai kwamba shinikizo la kijeshi dhidi ya uchumi wa Iran lingekuwa njia ya kuilazimisha serikali kujisalimisha.
Hata hivyo, hadi sasa, mkakati huu haujafikia malengo ya Marekani.
Brandt Kassler, profesa wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha James Madison, pia anaamini kwamba inawezekana lengo la mashambulizi haya ni kuiweka Iran katika hali dhaifu na huenda kuirudisha kwenye meza ya mazungumzo.
Wakati huohuo, ana mashaka kuhusu ufanisi wa sera hii, akisema katika mahojiano na BBC: "Sioni mkakati ulio wazi katika hatua za serikali ya Marekani, na sidhani kwamba sera hii ina ufanisi mkubwa.
Kuendelea kwa mashambulizi ya kulipiza kisasi, angalau hadi sasa, kunaonesha kwamba gharama iliyowekwa bado haijawa kubwa vya kutosha kuizuia Tehran kurudia mashambulizi hayo."
Hesabu za Iran wakati wa kipindi cha uchaguzi wa Marekani
Katika wiki za hivi karibuni, kufuatia kuendelea kwa shinikizo la kiuchumi na mzingiro wa majini wa Marekani dhidi ya Iran, maafisa wa kijeshi katika Jamhuri ya Kiislamu wameendelea kusisitiza mara kwa mara umuhimu wa kutathmini upya sera yao katika mzozo huu, na wamezungumzia uwezekano wa kufuata sera ya uchokozi zaidi.
Sehemu ya hesabu za maafisa wa Iran inategemea matumaini kwamba kupanda kwa bei ya mafuta, kwa kufanya nishati kuwa ghali zaidi nchini Marekani, kutaongeza shinikizo la ndani kwa utawala wa Trump.
Mashambulizi ya hivi karibuni ya Wahouthi dhidi ya Saudi Arabia na tishio kwa Mlango bahari wa Bab al-Mandab pia yanaweza kuongeza wasiwasi kuhusu upatikanaji wa nishati na hivyo kusaidia mkakati wa Tehran.
Ingawa waangalizi hawakubaliani kwamba shinikizo hili litakuwa kubwa vya kutosha kumfanya Donald Trump kutathmini upya au kurekebisha mkakati wake kuelekea Iran, angalau maafisa wa Iran wanatumaini kwamba kutekeleza sera hizi za uchokozi hatimaye kutamfanya Trump kufikia hitimisho hilo.

Chanzo cha picha, Getty Images
Hamidreza Azizi anaona mabadiliko katika sera za Iran kuwa matokeo ya hali hii, akisema: "Kuzingatia kauli za makamanda wa kijeshi wa Iran katika wiki za hivi karibuni kunaonesha kwamba walikuwa wamezungumzia kuhusu kuchukua msimamo mkali zaidi, na sasa msimamo huo unatekelezwa.
Ukweli ni kwamba shinikizo la kiuchumi, likiambatana na mzingiro wa majini, limeongeza utayari wa Iran kuchukua hatua ya hatari, na kuongezeka kwa bei ya mafuta, ambako hasa kunatathminiwa kuwa ni matokeo ya hatua za Wahouthi, kumewahimiza maafisa wa Iran kuendelea na njia hii na kuongeza kujiamini kwao."
Katika kauli zake za hivi karibuni, Hossein Mohebbi, msemaji wa Walinzi wa jesho la Mapinduzi la Iran, amezungumzia masharti mapya ya Iran ya kumaliza vita.
Afisa huyo mwandamizi ametaja masharti sita ya kumaliza vita: kusitishwa kabisa kwa uhasama, kukomeshwa kwa vitisho, Israel kujiondoa nchini Lebanon, kumalizika kwa mzingiro wa Yemen, kuachiliwa kwa dola bilioni 24, mali za Iran zilizozuiwa, na hatimaye, kukomeshwa kwa kile Bw. Mohebbi alichokiita "kuingilia kwa Marekani katika uwezo wa Iran wa makombora na nyuklia."
Sera hizo zinaonekana kulenga kuilazimisha Marekani kubeba gharama kubwa kupitia hatua zinazochukuliwa na Iran na washirika wake katika muda mfupi uliosalia kabla ya uchaguzi wa katikati ya muhula wa Marekani.
Hatua hizo ni zile ambazo upande wa Iran unatumaini kwamba ama zitadhoofisha Chama cha Republican au zitamshawishi Bw. Trump kutathmini upya matakwa yake na kukubaliana na Tehran.
Uchaguzi katika hesabu za Washington
Donald Trump, katika matamshi yake ya tarehe 9 Septemba, pia alihusisha kumalizika kwa vita na uchaguzi, akitabiri kwamba mzozo huo ungemalizika mara tu baada ya upigaji kura.
Alidai kwamba Iran itapinga ili kuathiri uchaguzi, lakini isingeweza tena kustahimili shinikizo la kiuchumi.
Kutokana na kauli hii, inaweza kuonekana kwamba Bw. Trump bado anatumaini kuvuka kipindi hiki kwa kudumisha shinikizo na kuilazimisha Tehran kulegeza msimamo wake, hata kama mashambulizi ya kulipiza kisasi yataendelea hadi uchaguzi.
Seneta wa Republican Ted Cruz alitumia neno "mzozo wa kijeshi" katika mahojiano ya hivi karibuni na CNN, kauli ambayo Brandt Cussler anaifasiri kuwa sehemu ya juhudi za Republican kupunguza uzito wa vita kabla ya uchaguzi, akisema: "Mashambulizi yanapoendelea, kwa kawaida hakuna mtu anayeweza kuamini kwamba vita vimekwisha."
Anaamini kwamba, wakati Democrats wanasisitiza gharama ya vita na kupanda kwa bei ya petroli, mpiga kura anayehisi gharama hiyo anapojaza mafuta hataliona tu mzozo huo kama tukio la mbali lisilohusiana na maisha yake.
Iran inategemea athari za kuongezeka kwa bei ya nishati kwenye uchaguzi, lakini haijulikani ni kwa kiwango gani shinikizo hili litaathiri uamuzi wa Bw. Trump.
Ikiwa hesabu hii haitafanikiwa kufikia wakati wa upigaji kura, Tehran inaweza kukabiliwa na uchumi dhaifu zaidi na fursa chache za kutumia wasiwasi wa Republican kuhusu uchaguzi.
Katika hali hiyo, Bw. Trump pia atakabiliwa na vikwazo vichache vya kukabiliana na Iran na kufuata msimamo mkali zaidi.
Matarajio ya mzozo unaodhoofisha taratibu
Katika siku ambazo IRGC inapendekeza masharti mapya ya kumaliza vita, Trump anaendelea kuzungumzia athari za shinikizo la kiuchumi katika kuilazimisha Iran kulegeza msimamo wake, na bado hakuna ishara ya wazi katika misimamo iliyotangazwa na pande zote mbili kwamba masharti yao ya kufikia makubaliano yanakaribiana.
Brandt Kassler anaamini kwamba licha ya kauli ambazo pande hizo hutoa mara kwa mara kuhusu makubaliano, bado hakuna utayari wa dhati wa kufanya diplomasia huko Tehran na Washington.
Profesa huyo wa Chuo Kikuu cha James Madison anaendelea kusema: "Nadhani kuna imani hatari kwa pande zote mbili kwamba ikiwa hawatajibu shambulio lolote au kuchukua hatua ya kulipiza kisasi, itaonekana kama ishara ya udhaifu.
Kwa hiyo, sidhani kama upande wa Iran au upande wa Marekani uko tayari kwa dhati kuelekea kwenye diplomasia, ingawa huenda kukawa na kauli zinazoashiria hivyo, lakini sizichukulii kwa uzito mkubwa."
Brandt Kassler anasema kwamba huenda Iran inataka kuivuta Marekani katika mzozo mrefu na wa kudumu, hali inayofanana na "vita visivyoisha" ambavyo wanasiasa wa Marekani wameanza kuviogopa kutokana na uzoefu wa Afghanistan na Iraq.
Pia anasisitiza kwamba gharama ya njia kama hiyo itakuwa kubwa sana kwa raia na kwa uchumi wa Iran, ambao tayari ulikuwa ukikabiliwa na changamoto kabla ya vita.



































