'Wizi wa nyeti': Jinsi mitandao ya kijamii ilivyochochea uvumi uliogeuka mauaji

Chanzo cha picha, Alfred Lasteck / BBC
- Author, Mungai Ngige
- Nafasi, BBC Global Disinformation Unit
- Author, Alfred Lasteck
- Nafasi, BBC Africa
- Akiripoti kutoka, Tunduma
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Zaidi ya watu 80 wameuawa kati ya Oktoba 2025 na Julai 2026 kutokana na madai ya uongo ya kile kinachoitwa "wizi wa sehemu za siri", kulingana na uchunguzi wa Kitengo cha BBC cha Kushughulikia Taarifa Potofu Duniani (BBC Global Disinformation Unit) uliotumia takwimu za polisi kutoka nchi sita za Afrika.
Mauaji hayo yamechochewa na uvumi unaodai kuwa kuguswa tu na mtu asiyejulikana kunaweza kusababisha sehemu za siri za mwanaume kusinyaa au kutoweka. Taarifa hizo potofu zimeenea kwa kasi kupitia mitandao ya kijamii, zikisababisha hofu, vurugu na mashambulizi ya umati.
"Walikuwa wakipiga kelele kwamba tumeiba sehemu za siri za mtu na hatukuwa na njia ya kutoroka kwa sababu kulikuwa na umati mkubwa wa watu," anasema Boniface Mgala, fundi mitambo kutoka Tanzania aliyeshambuliwa mwezi Aprili baada ya kutuhumiwa kuwa mwizi wa sehemu za siri.
Maelezo yake yanafanana na matukio mengine kadhaa yaliyonaswa katika video zilizochunguzwa na BBC, ambapo wanaume hudai sehemu zao za siri zimetoweka au kusinyaa baada ya kukutana na watu wasiowafahamu, kabla ya umati kuwashambulia wanaotuhumiwa.
Madai hayo yanatokana na hofu na imani za muda mrefu zinazohusishwa na ushirikina katika baadhi ya jamii za Afrika. Hata hivyo, watafiti wanasema mitandao ya kijamii imeongeza kasi ya kusambaa kwa uvumi huo.

Wimbi la hivi karibuni la uvumi huu linaonekana kuanzia mwaka jana nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambako madai kama hayo yaliripotiwa pia mwaka 2008.
Kadiri miezi ilivyopita, uvumi huo ulienea katika nchi zingine za eneo hilo, zikiwemo Burundi, Zambia na Tanzania, pamoja na Msumbiji, Angola, Malawi na Kenya.
Nchini Zambia, madai ya kupotea kwa sehemu za siri yalianza kuenea kwa kasi mwezi Machi baada ya mwanamke mmoja kuuawa na umati wenye hasira. Tukio hilo lilizidisha hofu na uvumi huo kuvuka mpaka hadi Tanzania.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Akiwa nyumbani kwake Mpemba, karibu na mji wa biashara wa Tunduma mpakani mwa Tanzania na Zambia, Boniface Mgala anapapasa kovu lenye umbo la mundu upande wa kulia wa kichwa chake huku akisimulia yaliyompata.
"Kama ningejua kifo kilikuwa kinanikodolea macho siku hiyo, nisingeingia kwenye mgahawa ule kula. Tatizo ni kwamba hatujui kifo kiko karibu kiasi gani," anasema fundi huyo wa magari.
Mgala na rafiki yake walikuwa wamefika Tunduma tarehe 1 Aprili kwa ajili ya kukutana na mteja kuhusu uuzaji wa gari. Kabla ya mkutano huo waliamua kula chakula cha mchana katika mgahawa mmoja.
Hata hivyo, muda mfupi baadaye walivutwa nje na kundi la watu wenye hasira.
Makovu mawili madogo kwenye kidevu chake na jino lililong'oka ni baadhi ya alama za shambulio hilo. Wakati akipigwa, alipoteza fahamu na kuja kuzinduka hospitalini siku mbili baadaye, ambako alielezwa kuwa rafiki yake alikuwa ameuawa.
Sasa akiwa nyumbani na mke wake pamoja na watoto wao wanne, Mgala anatembea kwa kuchechemea na anasema husumbuliwa na maumivu ya kichwa ya mara kwa mara.
Bado hajarejea kwenye karakana yake ya magari. Anasema majirani na marafiki wamekuwa wakimsaidia kununua dawa anazohitaji wakati akiendelea kuuguza kovu lake.
Siku ambayo Mgala na rafiki yake walishambuliwa, mpiga picha na mwanabiashara Michael Silavwe anasema alishuhudia tukio jingine la aina hiyo huko Tunduma. Anasema hofu ilikuwa imeanza kutanda katika eneo hilo baada ya video zinazodai watu kuibiwa sehemu za siri kuanza kusambaa kwenye TikTok.
Akiwa nje ya duka lake, Silavwe anasema aliona watu wakikimbia huku na kule. Baadaye alibaini kuwa mwanaume mmoja alikuwa ametuhumiwa mahali karibu na hapo na alikuwa akipigwa na umati wa watu kabla ya kuchomwa moto.
"Baada ya kumchoma moto, polisi walifika eneo la tukio ndipo kila mmoja akakimbia," kijana huyoaliye na umri wa miaka 23 aliiambia BBC.
Katika video ya shambulio hilo iliyothibitishwa na Kitengo cha BBC cha Kushughulikia Taarifa Potofu Duniani, na ambayo imetazamwa zaidi ya mara 100,000 kwenye mitandao ya TikTok na Facebook, kundi la watu linaonekana likimpiga mwanaume huku likimtaka arejeshe sehemu za siri alizodaiwa kuziiba.
Silavwe anasema matukio kama hayo yaliendelea kuongezeka huku watu zaidi wakishambuliwa kutokana na tuhuma hizo.
"Matukio hayo yaliendelea kushika kasi huku watu wakiendelea kupigwa," anasema, akiongeza kuwa wakati huo yeye na vijana wengine walikuwa na hofu, lakini sasa anaelewa kuwa uvumi huo hauna msingi wowote.
I came to realise it was not true"
Asha Steven Mwakilasa, fundi cherehani na mbunifu wa mitindo mwenye umri wa miaka 50 kutoka Tunduma wilayani Momba, anakubaliana na hilo.
"Nilikuja kugundua kuwa haikuwa kweli," anasema.
Hata hivyo, hilo halijaondoa kabisa hofu yake, hasa mumewe au wanawe wasipokuwa nyumbani. Anasema anafarijika kuona kwamba polisi sasa wanafanya doria mara kwa mara.
Mkuu wa Wilaya ya Momba, Elias Daniel Mwandobo, aliiambia BBC kuwa uchunguzi uliofanywa katika eneo hilo ulionyesha kuwa baadhi ya matukio hayo yalihusisha nia ya makusudi ya kihalifu.
"Watu walipanga njama za kutenda uhalifu na kuzua hofu kwa umma ili kujinufaisha wenyewe," alisema.
Video nyingine iliyorekodiwa katika jiji la Dar es Salaam inaonyesha umati wa watu ukimsukuma mwanaume kwenye barabara yenye vumbi katika eneo la soko. Watu hao wanaonekana wakimsukuma, kumshika na kumpiga huku wakimtaka arejeshe sehemu za siri alizodaiwa kuziiba, wakati yeye akiendelea kusisitiza kuwa hana hatia.
Kitengo cha BBC cha Kushughulikia Taarifa Potofu Duniani (BBC Global Disinformation Unit) pia kilithibitisha video nyingine zinazofanana na hizo kutoka Msumbiji na Kenya.
Video za vurugu za umati, simulizi zinazodaiwa kutoka kwa wahusika, maonyo kuhusu matukio yanayodaiwa kutokea, pamoja na maoni na video zinazowasilishwa kama taarifa za matukio katika maeneo mbalimbali, zimeendelea kusambaa kwenye TikTok na Facebook.
Nyingi ya video hizo zilizochambuliwa na BBC, zikiwemo zinazoonyesha mashambulizi ya umati, bado zinapatikana mtandaoni.
"Tunapitia maudhui yaliyoshirikishwa nasi na tutachukua hatua dhidi ya yale yatakayobainika kukiuka sera zetu," msemaji wa Meta aliiambia BBC.
TikTok haikujibu ombi la BBC la kutoa maoni.
Kwa baadhi ya watengenezaji wa maudhui kwenye mitandao ya kijamii wanaowatahadharisha watazamaji kuwa waangalifu, mara nyingi si rahisi kufahamu kama wanaamini madai hayo au kama wanajaribu tu kuongeza ushiriki wa wafuasi wao.
Wakati huo huo, baadhi ya watumiaji wa mitandao ya kijamii hutangaza hirizi wanazodai zinaweza kulinda dhidi ya wizi wa sehemu za siri, huku wachekeshaji wakitumia madai hayo kama nyenzo ya vichekesho.
Mwandishi Julien Bonhomme anasema simu janja na mitandao ya kijamii vimeufanya uvumi kusambaa kwa kasi zaidi, kuwafikia watu wengi zaidi na kuwa mgumu kudhibiti mara unapoanza kuenea.
Katika kitabu chake The Sex Thieves: The Anthropology of a Rumor, Bonhomme anachunguza namna uvumi kuhusu "wezi wa sehemu za siri" unavyosambaa na sababu zinazowafanya watu kuuamini.
Anasema watu husikii tu madai kwamba mtu amepoteza sehemu zake za siri. Badala yake, huwaona wanaume walioko katika hali ya msongo wakidai jambo hilo limewapata, au hushuhudia umati wa watu ukiitikia tuhuma hizo.
Kwa mujibu wake, video zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii zinaweza kufanya madai ambayo hayajathibitishwa yaonekane kuwa ya kuaminika zaidi kwa sababu ya namna zinavyowasilisha matukio kwa wakati halisi, jambo analolitaja kuwa "moja ya tofauti kubwa zaidi" kati ya mazingira ya sasa ya kidijitali na milipuko ya awali ya uvumi huo.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Nchi iliyoathirika zaidi na wimbi hili la uvumi ni Msumbiji, ambapo polisi walisema mwezi Mei kuwa watu 55 waliuawa ndani ya kipindi cha wiki sita, miongoni mwao akiwa afisa wa polisi, wahudumu wawili wa afya na watumishi wengine wa umma.
Rais wa Msumbiji, Daniel Chapo, alikemea hadharani uvumi huo na vifo vilivyosababishwa nao, akisema madai hayo hayakuwa na msingi wa ukweli na kwamba serikali haikupata ushahidi wowote wa kitabibu unaoonyesha kuwa mtu yeyote alikuwa amepoteza sehemu ya mwili wake.
Wahudumu hao wawili wa afya waliuawa mwezi Aprili waliposhambuliwa majumbani na katika maeneo yao ya kazi katika jimbo la Cabo Delgado, eneo la kaskazini mwa Msumbiji linalopakana na Tanzania na ambalo limekumbwa na uasi wa wanamgambo wa Kiislamu kwa karibu muongo mmoja.
Kutokana na hali hiyo, vituo vya afya katika baadhi ya maeneo vilifungwa kwa wiki kadhaa huku mamlaka zikianzisha kampeni za uhamasishaji wa umma kupinga madai hayo.
Kama sehemu ya kampeni hiyo, serikali ilisema baadhi ya hofu hizo zinaweza kuhusishwa na ugonjwa unaojulikana kama Koro syndrome, tatizo la afya ya akili ambalo humfanya mtu kuamini kuwa sehemu zake za siri zinapungua au zitatoweka.
Matukio mengine ya hivi karibuni ya vurugu yaliripotiwa nchini Kenya, ambako watu watano waliuawa na makundi ya wananchi wenye hasira katika kaunti za pwani za Kwale na Mombasa.
Baada ya matukio ya kwanza kuripotiwa mwezi Julai, Kamishna wa Kaunti ya Mombasa, Mohamed Noor, aliwalaumu baadhi ya watengenezaji wa maudhui mtandaoni kwa kusambaza madai hayo ili kuongeza ushiriki wa watumiaji.
"Taarifa potofu kama hizo zinaweza kusababisha vifo kwa urahisi," Noor aliiambia BBC.
Alisema polisi walifanikiwa kudhibiti vurugu hizo na kuwakamata watu kadhaa. Miongoni mwao walikuwa baba na mwanawe ambao walihukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela baada ya kukiri kosa la kumshambulia mwanamke waliyemtuhumu kusababisha kupotea kwa sehemu za siri za wanaume.
Nchini Malawi, madai kama hayo pia yalichochea mashambulizi ya makundi ya watu na kusababisha vifo vya watu wanane.
Huko Tunduma, Tanzania, Boniface Mgala anaendelea kuuguza majeraha aliyopata wakati wa shambulio lililomkumba. Lakini anasema maumivu ya kihisia bado hayajapungua.
"Bado naumia sana ninapokumbuka jinsi rafiki yangu alivyouawa kikatili na bila sababu, hadi wa leo sijawahi kuelewa kilichotokea," alisema.
"Unajikuta ghafla ukipigwa mawe bila sababu yoyote. Yaani unauawa bure?"












