Wanawake 6 wenye ushawishi mkubwa zaidi Afrika

Chanzo cha picha, Business Insider
Jarida la Forbes limetoa orodha ya wanawake 100 wenye nguvu na ushawishi mkubwa zaidi duniani, ikiangazia jinsi wanawake hao walivyokabiliana na changamoto katika mwaka ambao jarida hilo lilieleza kuwa "ulijawa na vikwazo katika sekta ya ajira za wanawake na fursa za kupanda ngazi katika sehemu zao za kazi."
Ripoti hiyo inaelezea kuwa makampuni mengi yamepunguza kuwaunga mkono wanawake katika taaluma yao ikilinganishwa na miaka minne iliyopita.
Kulingana na McKinsey na Lean In, ni asilimia 54 pekee ya kampuni zimeweka kipaumbele ya kuwasaidia wafanyakazi wanawake kupanda ngazi za uongozi, ikilinganishwa na asilimia 90 miaka minne iliyopita.
Wanawake wa Umoja wa Mataifa (UN Women) wametoa tahadhari kuhusu ongezeko la ubaguzi wa kijinsia mtandaoni. Shirika hilo limesema kwamba kuongezeka kwa uchochezi katika kile kinachojulikana kama "manosphere" inayohusishwa na mitazamo potofu dhidi ya wanawake imeanza kukithiri katika sehemu za kazi.
Hata hivyo, wanawake duniani kote wamekataa kukata tamaa au kubaki nyuma.

Chanzo cha picha, Business Insider
Mary Vilakazi (Afrika Kusini)
Mary Vilakazi, alizaliwa mwezi Agosti mwaka wa 1977, ni mhasibu kutoka Afrika Kusini ambaye amekuwa miongoni mwa watu mashuhuri na wenye ushawishi mkubwa katika sekta ya fedha nchini humo.
Kazi yake ilianza katika kampuni ya ukaguzi wa hesabu ya PwC, ambako alipanda ngazi kwa kasi na kuwa mmoja wa washirika wachanga zaidi wa kampuni hiyo akiwa na umri wa miaka 27. Alibobea katika ukaguzi wa hesabu za taasisi za huduma za kifedha.
Baadaye, alishikilia nyadhifa mbalimbali za juu, ikiwemo kuwa Afisa Mkuu wa Fedha wa Mineral Services Group kabla ya kujiunga na MMI Holdings, ambako alipanda hadi kuwa Naibu Afisa Mkuu Mtendaji.
Mwaka wa 2018, Vilakazi alijiunga na FirstRand kama Afisa Mkuu wa Uendeshaji wa Kundi hilo.
Mwezi Aprili, 2024, aliandikisha historia kwa kuwa mwanamke wa kwanza, na mwanamke wa kwanza mweusi, kuongoza FirstRand Group katika historia yake ya miaka 185.
FirstRand ni kampuni kubwa zaidi ya huduma za kifedha nchini Afrika Kusini kwa kuzingatia thamani yake ya soko.

Chanzo cha picha, Business Insider
Judith Suminwa Tuluka (DRC)
Judith Suminwa Tuluka ni mwanasiasa na mwanauchumi kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambaye mwezi Juni 2024 aliweka historia kwa kuwa mwanamke wa kwanza kuwa Waziri Mkuu wa DRC.
Tuluka alianza kazi katika sekta ya fedha kabla ya kushika nyadhifa mbalimbali za ngazi ya juu serikalini, na baadaye alijiunga na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP).
Ana uzoefu pia katika usimamizi wa fedha za umma, tathmini ya programu, udhibiti wa bajeti na uratibu wa shughuli za serikali.
Mwezi Machi 2023, utawala uliokuwa madarakani wakati huo ulimteua kuwa Waziri wa Nchi anayeshughulikia Mipango.
Tarehe 1 Aprili 2024, aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa kwanza mwanamke katika historia ya DRC. Aliapishwa rasmi tarehe 12 mwezi Juni 2024, baada ya uteuzi wake kuidhinishwa na bunge.

Chanzo cha picha, Business Insider
Netumbo Nandi-Ndaitwah (Namibia)
Netumbo Nandi-Ndaitwah ni mwanasiasa na mwanadiplomasia kutoka Namibia ambaye tarehe 21 mwezi Machi mwaka wa 2025 aliandikisha historia ya kuwa mwanamke wa kwanza kuwa Rais wa Namibia.
Ametumikia serikali ya Namimbia kwa miongo kadhaa kupitia chama tawala cha SWAPO, akiwa mwanachama wa chama hicho tangu kipindi cha mapambano ya ukombozi. Katika safari yake ya kisiasa na serikalini, amewahi kushika nyadhifa mbalimbali, kuanzia Waziri wa Mambo ya Kigeni, Naibu Waziri Mkuu hadi Makamu wa Rais.

Chanzo cha picha, Business Insider
Mpumi Madisa (Afrika Kusini)
Mpumi Madisa alianza kazi yake katika kampuni ya bima kabla ya kujiunga na Bidvest mwaka wa 2003. Huko alipanda ngazi mbalimbali na kushika nyadhifa kadhaa, zikiwemo Meneja wa Mahusiano na Wateja, Mkurugenzi wa Masuala ya Kampuni, Mkurugenzi wa Mauzo na Masoko, pamoja na Meneja Mkuu wa Maendeleo ya Biashara.
Mnamo Machi 2019, aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Bidvest, na hivyo kuwa mwanamke wa kwanza mweusi kuongoza kampuni iliyoorodheshwa katika orodha ya kampuni 40 kubwa zaidi kwenye Soko la Hisa la Johannesburg.
Chini ya uongozi wake, Bidvest imeendelea kukua kwa kiasi kikubwa. Kampuni hiyo sasa inasimamia wafanyakazi wapatao 130,000, imepanua shughuli zake kimataifa, imeongoza vitengo mbalimbali vya biashara na kurejesha kampuni hiyo katika hali ya kupata faida baada ya kupata hasara katika miaka ya awali.

Chanzo cha picha, Getty Images
Ngozi Okonjo-Iweala (Nigeria)
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Ngozi Okonjo-Iweala amebaki kuwa miongoni mwa wachumi na watunga sera mashuhuri zaidi duniani.
Mwaka 2010, alisimamia kampeni ya Benki ya Dunia ya kuchangisha fedha, na kufanikisha kupatikana kwa dola za Marekani bilioni 49.3 katika misaada na mikopo yenye riba nafuu kwa nchi maskini zaidi duniani.
Baada ya kipindi chake serikalini, aliendelea kushiriki kikamilifu katika masuala ya kimataifa, akiongoza mashirika kama Gavi ambao Muungano wa Chanjo kuanzia mwaka 2016 hadi 2020. Pia alikuwa mwenyekiti mwenza wa Global Commission on the Economy and Climate, na alishiriki katika juhudi za kimataifa zinazohusu milipuko ya magonjwa na mabadiliko ya tabianchi.
Tarehe 1 mwezi Machi 2021, aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Biashara Duniani (WTO), na kuwa mwanamke wa kwanza na Mwafrika wa kwanza kushikilia nafasi hiyo.
Uongozi wake umemwezesha kupata muhula wa pili kama Mkurugenzi Mkuu wa WTO. Mwishoni mwa mwaka 2024, nchi wanachama zilimchagua tena kwa wingi mkubwa, jambo linaloonyesha imani kubwa waliyonayo katika uongozi wake.

Chanzo cha picha, Getty Images
Mo Abudu (Nigeria)
Mo Abudu ni mjasiriamali wa vyombo vya habari na mtu mashuhuri katika sekta ya utamaduni nchini Nigeria, ambaye anabadilisha namna simulizi za Afrika zinavyowasilishwa kupitia maono yake makubwa na miradi inayolenga hadhira ya kimataifa.
Kama mwanzilishi na Mkurugenzi Mkuu wa EbonyLife Media, inayojulikana pia kama EbonyLife Group, anaongoza himaya ya vyombo vya habari inayojumuisha televisheni, utengenezaji wa filamu, huduma za utiririshaji wa maudhui mtandaoni pamoja na miradi ya mtindo wa maisha.
Ushawishi wa Mo Abudu umeendelea kukua katika miaka ya hivi karibuni kutokana na kuanzisha miradi mipya yenye malengo makubwa. Mwaka 2025, jarida la TIME lilimtaja miongoni mwa "Watu 100 Wenye Ushawishi Mkubwa Duniani", kutokana na mchango wake katika kuinua simulizi za Afrika na kuhamasisha wabunifu barani Afrika na diaspora.
Pia alitangaza mipango mikubwa kadhaa kupitia EbonyLife, ikiwemo Afro Film Fund, mfuko wa dola za Marekani milioni 50 kwa ajili ya kugharamia utengenezaji wa filamu na tamthilia zinazotokana na simulizi za Afrika kwa hadhira ya kimataifa, pamoja na EbonyLife Place London.















