Moja kwa moja, Trump athibitisha mazungumzo ya Marekani na Iran ya kumaliza vita

Shirika la habari la serikali ya Iran limethibitisha kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, alikutana na mjumbe maalum wa Marekani, Steve Witkoff.

Muhtasari

Trump athibitisha mazungumzo ya Marekani na Iran ya kumaliza vita

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Ufaransa yaandaa azimio kuhusu kufunguliwa kwa Mlango Bahari wa Hormuz

    s

    Chanzo cha picha, Reuters

    Taarifa kutoka katika mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa zinaeleza kuwa Ufaransa, kwa ushirikiano na Marekani, imeanza kuandaa azimio litakalowasilishwa kwa Baraza hilo.

    Maafisa wa kidiplomasia wamesema Jumanne kuwa azimio hilo linalenga kuanzisha operesheni ya kimataifa ya kurejesha usafirishaji wa meli katika Mlango Bahari wa Hormuz.

    Hatua hiyo inakuja baada ya juhudi za awali za Ufaransa za kuandaa azimio kama hilo kushindikana.

    Mpango huo mpya umefuatia mazungumzo kati ya Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Rais wa Marekani Donald Trump yaliyofanyika Jumatatu jioni, wakati viongozi hao walipokuwa mjini New York kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa.

    Baada ya mkutano huo, Macron alisema:

    “Chaguzi kadhaa zilijadiliwa. Katika saa zijazo, tutafanya kazi kutafuta suluhisho za kidiplomasia ambazo zinaweza kuruhusu meli nyingi zaidi za mizigo na mafuta kupita, hata kama makubaliano kamili hayatapatikana.”

    Baadhi ya maafisa wa ujumbe wa Ufaransa wamesema Macron anatarajia kuwasilisha rasimu ya azimio hilo kwa wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa hivi karibuni.

    Soma Zaidi:

  2. Trump athibitisha mazungumzo ya Marekani na Iran ya kumaliza vita

    r

    Chanzo cha picha, Reuters

    Rais wa Marekani Donald Trump amesema Jumanne kwamba wawakilishi maalum wa Marekani, Steve Witkoff na Jared Kushner, wamekutana na wapatanishi kujadili uwezekano wa makubaliano ya kumaliza vita kati ya Marekani na Iran.

    Wakati huo huo, Shirika la Utangazaji la Iran limeripoti kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araghchi, alikutana na Steve Witkoff pembezoni mwa Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa unaoendelea mjini New York.

    Kwa mujibu wa shirika hilo, lengo kuu la mkutano huo lilikuwa kuwasilisha masharti ya Iran ya kufunguliwa tena kwa Mlango Bahari wa Hormuz.

    Iran imetaja kuondolewa mara moja kwa kizuizi cha majini, kuachiliwa kwa mali zake zote zilizogandishwa na kusitishwa kwa mapigano katika maeneo yote yanayohusisha makundi yanayoiunga mkono, kuwa miongoni mwa masharti yake.

    Viongozi mbalimbali wa nchi wako mjini New York kuhudhuria Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa ulioanza leo.

    Pakistan na Qatar ndizo nchi mbili zinazohusika katika juhudi za upatanishi kati ya Iran na Marekani.

    Maelezo zaidi:

  3. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya 23/09/2026.