Je, kuna viumbe kwenye sayari nyingine?

Chanzo cha picha, Aaron Foster
Iwe ni meli kubwa za anga za kivita, viumbe wa kijani wenye umbo la binadamu kutoka sayari ya Mirihi, au viumbe wa kutisha wanaotambaa kwenye sayari zisizojulikana, fasihi ya hadithi za kisayansi imejenga taswira mahususi kabisa kuhusu viumbe wa kutoka sayari nyingine isiyo ya dunia.
Wanasayansi wengi mashuhuri pia wanaamini kwamba huenda kuna uhai wa aina hiyo.
Katika utafiti wa hivi karibuni, asilimia 86.6 ya wataalamu wa astrobiolojia walisema wanakubaliana kuwa huenda kuna uhai nje ya dunia mahali fulani katika ulimwengu.
Walipoulizwa swali hilo hilo kuhusu uwepo wa viumbe wenye maisha changamano au wenye akili, asilimia ya waliokubaliana ilishuka hadi asilimia 58.2 pekee.
Hii ina maana kwamba wanaoamini kuwa viumbe hao wapo ni wengi kuliko wale wasioamini.
Kwa hivyo, wanasayansi hawa wanajua nini ambacho sisi hatujui? Na kwa nini wana uhakika kiasi kwamba hatuko peke yetu katika ulimwengu huu?
Kwa nini huenda viumbe wa nje ya dunia wapo
Hakuna kitu cha kipekee kuhusu dunia au binadamu. Haya si maoni yetu, bali ni wazo kuu linalojulikana kama kanuni ya Copernicus.
Hii ni dhana kwamba, ingawa mara nyingi tunaiona dunia kuwa ya kipekee au bora, kwa hakika si ya kipekee kuliko sayari nyingine yoyote.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Lakini jambo hilo linahusianaje na viumbe walio nje ya dunia?
Wanasayansi wengi wanaochunguza uhai wa nje ya dunia wanaamini kwamba hali ya dunia inayowezesha uhai, pamoja na maendeleo ya viumbe mbalimbali wenye akili, ni ishara kwamba huenda jambo kama hilo linawezekana pia katika maeneo mengine.
Na kutokana na ukubwa wa ulimwengu, baadhi ya wanasayansi wanasema swali si kama viumbe wa nje ya dunia wapo, bali ni wapi wanapatikana.
Kwa mfano, galaksi yetu ina kati ya nyota bilioni 100 na 400. Wanaastronomia tayari wamethibitisha uwepo wa takribani sayari 4,000 zinazozunguka nyota na hiyo ni katika galaksi yetu pekee.
Milky Way( jua,nyota na sayari) yenyewe ni sehemu ndogo sana ya ulimwengu unaoweza kuonekana, ikiwa ni takribani sehemu moja kati ya milioni moja ya ulimwengu huo.
Ukiongeza ukubwa huo, unapata takribani nyota sextilioni 100 (100,000,000,000,000,000,000,000) na kila moja inaweza kuwa na sayari zinazoizunguka.
Hiyo ni idadi kubwa isiyoweza kufikiriwa kwa urahisi. Kwa mfano, si kwamba kuna uwezekano wa kuwa na sayari nyingi zaidi katika Ulimwengu kuliko chembe za mchanga duniani, bali huenda zikawa nyingi mara bilioni 13.33 zaidi. Kwa uwezekano kama huo, inaonekana kuwa ni jambo lisiloepukika kwamba angalau sayari moja kati ya hizo inaweza kuwa na viumbe hai na wenye akili nje ya dunia.
"Kwa sasa tunajua kwamba nyota nyingi zina mfumo wa sayari. Hii ina maana kwamba kuna maeneo mengi ambako uhai unaweza kutokea," anasema Mike Garrett, mwenyekiti wa taaluma ya unajimu katika Chuo Kikuu cha Manchester.

Chanzo cha picha, Shawn PNW
Na si idadi kubwa ya sayari pekee inayofanya uwepo wa viumbe wa nje ya dunia uonekane kuwa jambo linalowezekana , bali pia ni vitu vinavyounda sayari hizo.
Viambata vya msingi vinavyohitajika kwa uhai vinapatikana kwa wingi kuliko unavyoweza kufikiria.
Kaboni, hidrojeni, oksijeni na nitrojeni ambazo ni elementi zinazounda viumbe hai duniani zote zimegunduliwa kwenye kometi, asteroidi na sayari za mbali.
Wanaastronomia pia wamegundua sayari nyingi ambako kuna maji, ambayo ni kiambata kingine muhimu kwa uhai.
Chukua mfano wa KOI-5715.01, sayari iliyo nje ya mfumo wetu wa jua, iliyoko takribani miaka 3,000 ya mwanga kutoka kwetu. Huenda jina lake lisivutie, lakini sayari hii ni miongoni mwa zile zinazofanana zaidi na dunia ambazo tumewahi kugundua.
Ina ukubwa unaokaribiana na wa dunia, iko katika eneo lenye halijoto inayoweza kuruhusu uhai, na ina dalili za kuwepo kwa maji jambo linaloifanya kuwa miongoni mwa sayari zinazochunguzwa kwa karibu katika utafutaji wa viumbe wa nje ya dunia.
Tunaweza pia kuangalia dunia kama ushahidi kwamba uhai unaweza kustawi katika maeneo ambayo hapo awali yalionekana kuwa hayawezi kuhimili uhai.
Kuanzia chemchemi za maji moto zenye tindikali hadi matundu ya maji moto kwenye kina kirefu cha bahari na maeneo yaliyoganda ya Antaktika, aina mbalimbali za viumbe wanaojulikana kama 'extremophiles' zimegunduliwa hivi karibuni, zikionyesha kwamba viumbe hai wanaweza kuzoea mazingira magumu zaidi kuliko yale ya sayari yenye hali ya wastani inayofanana na dunia.
Kwa mfano, minyoo wakubwa wenye umbo la mirija hustawi katika giza totoro la kina kirefu cha bahari, wakikusanyika kuzunguka matundu ya maji moto yanayotoa maji yenye joto kali na madini mengi, yenye halijoto ya hadi nyuzi joto 350.
Licha ya joto hilo kali, shinikizo kubwa na kutokuwepo kabisa kwa mwanga wa jua, minyoo hao huunda makundi makubwa na hutegemea bakteria wanaoishi nao kwa ushirikiano ili kubadilisha kemikali kutoka kwenye matundu hayo kuwa nishati.

Chanzo cha picha, GETTY
"Dunia ilipotokea miaka bilioni 4.5 iliyopita, mwanzoni uso wake ulikuwa na joto kali sana. Bahari za magma iliyokuwa ikitiririka zilifunika uso wa dunia, na kuifanya kuwa mazingira yasiyofaa kabisa kwa uhai. Hata hivyo, uhai ulitokea mara tu mazingira yalipopoa," anasema Douglas Vakoch, mwandishi na mwanzilishi wa METI (Messaging to Extra-Terrestrial Intelligence), shirika linalofanya utafiti kuhusu mawasiliano na viumbe wa nje ya dunia.
Hata kama viumbe wa nje ya dunia wapo, changamoto mojawapo ni kuwapata. Kwa mfano, iwapo kila mwanadamu angepewa jukumu la kutafuta viumbe hao, kila mtu angelazimika kuchunguza sayari 13,000.
Ingawa hilo limekuwa changamoto kwa miaka mingi, wanasayansi wanaamini kwamba sasa inazidi kuwa rahisi kugundua dalili zinazoonyesha kwamba sayari nyingine ina viumbe hai.
"Tuko katika nafasi nzuri zaidi ya kugundua uhai wa nje ya dunia sasa kuliko tulivyokuwa miaka mitano iliyopita. Kila kitu kinaelekea katika mwelekeo mzuri katika suala la ugunduzi," anasema Garrett.
"Maendeleo katika teknolojia ya kompyuta, matumizi ya teknolojia za kidijitali na akili unde (AI) yanamaanisha kwamba tunasonga kwa kasi kuelekea kugundua viumbe wa nje ya dunia, kwa sababu teknolojia inaboreshwa kwa kasi kubwa sana sasa."
Vakoch anakubaliana na mtazamo huo. "Katika miaka 20 ijayo, tutakuwa na darubini zitakazoweza kuchanganua angahewa za sayari zinazozunguka nyota nyingine tunapotafuta dalili za uhai," anasema.
Kwa nini huenda tuko peke yetu
Ikiwa kuna uwezekano mkubwa wa viumbe wa nje ya dunia kuwepo, kwa nini bado hatujawagundua? Na kwa nini hatujawahi kupokea wageni kutoka nje ya dunia?
Karibu kwenye kile kinachojulikana kama Kitendawili cha Fermi (Fermi Paradox).
Wakati wa chakula cha mchana mwaka wa 1950, mwanafizikia Enrico Fermi aliwauliza wenzake swali la kuvutia kuhusu viumbe wa nje ya dunia: "Wako wapi?" Fermi alitoa hoja kwamba ikiwa viumbe wenye akili wanapatikana kwa wingi katika galaksi, basi dunia ingekuwa tayari imetembelewa mara nyingi.
Lilikuwa swali lililolenga moja kwa moja kiini cha mjadala huo na ambalo wanasayansi bado wanajaribu kulijibu hadi leo. Maktaba nzima za nadharia zimeandikwa kujaribu kulieleza, lakini baadhi ya wanasayansi wanaamini kwamba jibu halisi huenda likawa rahisi na la kushangaza. Ulimwengu wenye ukubwa wa kutosha kuweza kuwa na uhai pia una ukubwa wa kutosha kuuficha.
Kwa maneno mengine, ikiwa kweli kuna uhai sehemu nyingine, huenda tusifanikiwe kuugundua kamwe. Binadamu wameishi duniani kwa takribani miaka laki mbili, kipindi ambacho ni kifupi sana ukilinganisha na historia ya Ulimwengu.
Tumekuwepo kwa takribani asilimia 0.000002 tu ya historia yote ya Ulimwengu.
Huenda ustaarabu mwingine wenye akili uliibuka na kutoweka, au bado uko katika hatua za mwanzo za maendeleo. Ili tugundue uhai nje ya Dunia, matukio mengi yanahitaji kutokea kwa wakati mmoja

Chanzo cha picha, GETTY
"Sayansi kwa asili ina mashaka. Inahitaji ushahidi na hadi sasa, hakuna ushahidi wa moja kwa moja wa kuwepo kwa uhai nje ya dunia," anasema Vakoch. "Lakini miongo michache iliyopita, hali ilikuwa hivyo hivyo kuhusu sayari zinazozunguka nyota nyingine. Tulidhani huenda zilikuwepo, lakini hatukuweza kuziona."
Hilo lilibadilika katika miaka ya 1990, wakati sayari za kwanza zilizo nje ya mfumo wetu wa jua zilipothibitishwa. Leo, wanaastronomia wamegundua maelfu ya sayari hizo, na kuthibitisha kwamba ulimwengu mwingine si jambo linalowezekana tu, bali ni nyingi.
"Wanaastronomia walilazimika kwanza kuamini kwamba sayari hizo zilikuwepo ili wazigundue," anaongeza Vakoch. "Kisha wakafanya kazi kubwa ya kuzitafuta na kuzithibitisha."
Kwa watafiti wengi, uhai wa viumbe wa nje ya dunia unaonekana kuwa katika hatua ileile ambayo sayari za nje ya mfumo wetu wa jua zilikuwa hapo awali: unashukiwa kuwepo, lakini bado haujaonekana. Zana za kuugundua zinaendelea kuboreshwa, lakini ugunduzi mkubwa unaweza kuchukua miongo kadhaa au hata zaidi.
Lakini nani anajua? Huenda mahali fulani mabilioni ya miaka ya mwanga, kwenye sayari ya mbali sana, kuna kiumbe mwenye akili anayeketi na kutafakari swali hili hili: "Je, tuko peke yetu katika Ulimwengu?"



































