Moja kwa moja, Bunge la Marekani laidhinisha mswada wa vikwazo dhidi ya Iran na Urusi

Mswada huo, unaofahamika kama Sheria ya Lindsay O. Graham ya Vikwazo dhidi ya Urusi na Iran, ulipitishwa Jumatano kwa kura 262 dhidi ya 159.

Moja kwa moja

Na Ambia Hirsi

  1. Muisrael ahukumiwa miaka 13 Jela kwa ujasusi wa Iran

    Mahakama nchini Israel imemhukumu kifungo cha miaka 13 jela mwanaume mwenye umri wa miaka 30 baada ya kupatikana na hatia ya kufanya ujasusi kwa niaba ya Iran.

    Mwendesha mashtaka alieleza kuwa mtuhumiwa Alexander Granevsky alihusika katika shughuli za kukusanya na kusambaza taarifa kwa mawakala wa Iran, jambo ambalo mahakama ilitaja kuwa lilihatarisha usalama wa taifa la Israel

    Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Israel, hukumu hiyo ni miongoni mwa adhabu kali zaidi kuwahi kutolewa nchini humo katika kesi zinazohusiana na shughuli za ujasusi kwa niaba ya Iran.

    Waendesha mashtaka walisema Granevsky alitekeleza misheni kadhaa baada ya kuwasiliana na mtu aliyedaiwa kuwa wakala wa Iran kupitia programu ya Telegram, akiahidiwa malipo ya fedha kwa kazi alizopewa.

    Mahakama ilimpata na hatia ya kuandika kaulimbiu za kupinga serikali katika maeneo mbalimbali kwa kutumia rangi ya dawa ya kupuliza, kuchoma moto magari tisa, pamoja na kufuatilia eneo la makazi la Benny Gantz, aliyewahi kuwa Mkuu wa Majeshi ya Israel na Waziri wa Ulinzi.

    Pia alihukumiwa kwa kupiga picha za maeneo nyeti, yakiwemo miundombinu ya kuzalisha umeme, na kuwasilisha taarifa hizo kwa mawasiliano yake wa Iran.

    Mamlaka za Israel zimekuwa zikitahadharisha kuhusu kile zinachodai ni juhudi za Iran za kuwatumia raia wa Israel kukusanya taarifa za kiintelijensia na kutekeleza vitendo vya hujuma ndani ya nchi.

    Hukumu ya Granevsky inaonekana kuashiria msimamo mkali wa Israel dhidi ya vitendo vinavyohusisha ushirikiano na mataifa yanayoonekana kuwa tishio kwa usalama wa taifa.

  2. Bunge la Marekani laidhinisha mswada wa vikwazo dhidi ya Iran na Urusi.

    .

    Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock

    Bunge la Wawakilishi la Marekani limepitisha mswada mpya unaopanua wigo wa vikwazo dhidi ya Urusi na Iran, hatua inayolenga kuongeza shinikizo kwa mataifa hayo kutokana na shughuli zake za kiuchumi na kijeshi.

    Mswada huo, unaofahamika kama Sheria ya Lindsay O. Graham ya Vikwazo dhidi ya Urusi na Iran, ulipitishwa Jumatano kwa kura 262 dhidi ya 159, baada ya awali kupitishwa na Seneti mwezi Agosti kwa kura 86 dhidi ya 11. Sasa unasubiri kutiwa saini na Rais wa Marekani, Donald Trump, ili kuwa sheria.

    Chini ya sheria hiyo, Marekani itaweza kuweka vikwazo dhidi ya maafisa wa Urusi, taasisi za kifedha, benki pamoja na sekta za nishati na ulinzi za nchi hiyo.

    Aidha, mswada huo unalenga kile kinachoitwa “shadow fleet” au meli zinazotumiwa kusafirisha mafuta ya Urusi kwa lengo la kukwepa vikwazo vya kimataifa.

    Sheria hiyo pia itampa Rais wa Marekani mamlaka ya kuweka ushuru wa hadi asilimia 100 kwa nchi zinazotambuliwa kuwa wanunuzi wakubwa wa mafuta na gesi kutoka Urusi.

    Kwa upande wa Iran, mswada huo unapanua vikwazo vinavyohusiana na ushirikiano wake na Urusi, hususan katika maeneo ya kijeshi.

    Vilevile, sheria hiyo itaongeza muda wa uhalali wa Sheria ya Vikwazo dhidi ya Iran ya mwaka 1996 kwa kipindi cha miaka mitano zaidi, kuanzia mwaka 2026 hadi 2031. Hatua hiyo inalenga kuendelea kudumisha mfumo wa kisheria wa vikwazo uliopo.

    Hata hivyo, mswada huo haujaweka orodha mpya ya watu binafsi au makampuni yatakayowekewa vikwazo. Badala yake, unatoa msingi wa kuchukuliwa hatua dhidi ya taasisi na makampuni ya Iran yatakayobainika kushiriki katika ushirikiano wa kijeshi na Urusi.

  3. Karibu kwa matangazo ya moja kwa moja.