Rais wa zamani wa Kosovo ahukumiwa miaka 25 jela

Chanzo cha picha, Getty Images
Aliyekuwa Rais wa Kosovo Hashim Thaçi amehukumiwa kifungo cha miaka 25 jela kwa uhalifu wa kivita.
Thaçi aliongoza Jeshi la Ukombozi wa Kosovo (KLA) wakati wa harakati za Kosovo za kujitenga na Serbia.
Mahakama hiyo pia ilimhukumu Yakup Krasniqi, aliyekuwa kiongozi wa KLA aliyeshtakiwa pamoja na Thaçi, kifungo cha miaka 25 jela.
Kadri Veseli amehukumiwa miaka 18, huku Recep Selimi akihukumiwa miaka 13 jela.
Mahakama Maalum ya Kosovo mjini The Hague imesema Thaçi, ambaye upande wa mashtaka uliomba ahukumiwe kifungo cha miaka 45, anawajibika kwa uhalifu wa kivita uliofanyika Kosovo katika miaka ya 1990, ukiwemo mauaji, mateso na kuwazuilia watu kinyume cha sheria.
Mahakama hiyo imeamua kumhukumu miaka 25 jela.
Thaçi mwenye umri wa miaka 58 alikutwa na hatia ya kuhusika na mauaji ya wapinzani 96 wa kisiasa, pamoja na mateso na kutendewa vibaya kwa mamia ya watu waliotuhumiwa kushirikiana na Waserbia.
Thaçi alisikiliza hukumu hiyo akiwa amesimama. Hapo awali alikuwa amekanusha mashtaka dhidi yake.
Kabla ya kusomwa kwa hukumu hiyo mjini The Hague, Uholanzi, idadi kubwa ya Waalbania wa Kosovo waliandamana kuonyesha kumuunga mkono Thaçi na wenzake.
Wafuasi wake walionekana kusikitishwa na hukumu hiyo.






































