Je, unajua ulaji wako unaweza kuathiri hali yako ya kihisia?

Canjeero

Chanzo cha picha, SOCIAL

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 3

Lishe si jibu kwa matatizo yote ya afya ya akili. Hata hivyo, tafiti zinaonyesha kuwa lishe inaweza kuwa na athari kubwa kuliko inavyotarajiwa kwenye hisia na msongo wa mawazo, kupitia mambo mbalimbali kama vile kupunguza kiwango cha sukari kwenye damu na kuboresha afya ya utumbo.

Wataalamu wanaeleza mabadiliko manne rahisi na yenye ufanisi katika lishe ambayo yanaweza kusaidia kuimarisha afya yako ya akili.

Je, chakula kinaweza kutibu msongo wa mawazo?

Linapokuja suala la msongo wa mawazo, kuboresha lishe yako hakuwezi kuchukua nafasi ya msaada na matibabu kutoka kwa wataalamu wa afya, lakini bado kunaweza kuwa sehemu muhimu ya matibabu ya kina.

Profesa Felice Jacka kutoka Chuo Kikuu cha Deakin amekuwa akifanya utafiti kuhusu uhusiano kati ya lishe na msongo wa mawazo kwa miaka kadhaa.

"Utafiti mkubwa na unaoendelea kuonyesha matokeo yanayofanana unaonyesha kuwa kula lishe bora humsaidia mtu kukabiliana na msongo wa mawazo."

Hii inahusu lishe inayofanana na lishe ya Mediterania, ambayo ina virutubisho vingi, ikiwa ni pamoja na:

Nafaka zisizokobolewa

  • Mboga
  • Matunda
  • Samaki
  • Mafuta ya zeituni

Aliongeza:

"Lishe bora na yenye uwiano huupa ubongo virutubisho unavyohitaji ili kusaidia hali nzuri ya hisia, na huboresha miunganiko na mawasiliano kati ya seli za ubongo, jambo ambalo ni muhimu kwa utendaji wa ubongo."

Utafiti wa SMILES uliofanywa na Jacka ulionyesha kuwa kubadili kwenda kwenye lishe inayofanana na lishe ya Mediterania kunaweza kusaidia kupunguza dalili za msongo wa mawazo.

Sasa, anaunga mkono juhudi za kuendeleza mfumo wa afya wa Australia ili watu wenye msongo wa mawazo waweze kupata msaada wa lishe na mazoezi kama sehemu ya matibabu yao.

Hizi ni njia nne ambazo lishe inaweza kusaidia kuboresha hali yako ya hisia:

1. Kula chakula kwa wakati

Kula chakula kwa wakati husaidia mwili kudumisha kiwango cha sukari kwenye damu kilicho sawia.

Kiwango cha sukari kwenye damu kinaposhuka, tunaweza kujisikia tumechoka na kukosa utulivu.

Kupanda kwa kiwango cha sukari kwenye damu baada ya kula pia kumehusishwa na matatizo ya hisia, yakiwemo msongo wa mawazo na wasiwasi.

Mtaalamu wa lishe na saikolojia, Dkt. Sonal Shah, alisema:

"Ikiwa unahisi njaa mara kwa mara siku nzima na hali hiyo inaathiri hisia, umakini na viwango vyako vya nguvu, ni muhimu kula kwa vipindi vya kawaida."

Shah anapendekeza kula kila baada ya saa tatu hadi nne ili kudumisha viwango vya nguvu.

Hata hivyo, alisisitiza kuwa hii haimaanishi mtu anapaswa kula vitafunwa kila wakati, kwa sababu kufanya hivyo "hakuruhusu mwili kudhibiti ipasavyo hamu ya kula na homoni za insulini."

2. Kunywa maji ya kutosha

Unapokuwa na kiu, inaweza kuwa vigumu kufikiri vizuri na kuzingatia kile unachotaka kufanya.

Kwa mujibu wa Shah, ubongo unahitaji maji.

Hii inaeleza kwa nini mtu anaweza kuwa katika hatari zaidi ya kupata msongo wa mawazo wakati mwili umepungukiwa na maji.

"Maji husaidia mtiririko wa damu. Wakati hakuna maji ya kutosha kusaidia mwili kuondoa sumu, unahisi udhaifu," alisema.

Kwa mujibu wa Shah, upungufu wa maji mwilini unaweza pia kuongeza hamu ya kula vyakula visivyo na afya, kama vile chipsi na vyakula vyenye wanga uliosindikwa.

Kwa ujumla, maji ndiyo chaguo bora kwa ajili ya kuupa mwili maji, lakini vinywaji vingine pia vinaweza kusaidia kupata maji yanayohitajika.

Hata hivyo, jaribu kuepuka vinywaji vyenye sukari nyingi.

3. Punguza utegemezi wa vyakula vilivyosindikwa sana

Hii inamaanisha kupunguza matumizi ya vyakula vilivyosindikwa, kama vile chipsi, biskuti, peremende na vyakula vyenye sukari, chumvi au mafuta mengi.

Badala yake, ni bora kuchagua vyakula vya asili vyenye virutubisho.

4. Zingatia kula zaidi vyakula vya asili

Utumbo ni sehemu muhimu katika kukabiliana na msongo wa mawazo, na tafiti zinaonyesha kuwa kile tunachokula kinaweza kusaidia afya ya utumbo.

"Lishe ni miongoni mwa mambo muhimu zaidi yanayoathiri afya ya utumbo na bakteria waliomo ndani yake."

"Sasa tunajua kuwa bakteria wa utumbo, wanaojulikana kama mikrobiota, wana jukumu muhimu katika afya ya mfumo wa kinga, umetaboli, utendaji wa vinasaba, pamoja na afya ya ubongo na mfumo wa neva."

Watafiti wanashauri kwamba kula aina mbalimbali za vyakula vinavyotokana na mimea kunaweza kusaidia utumbo kukuza aina nyingi zaidi za bakteria wenye afya.

Hii inaweza kuwa na athari kubwa kwa afya yetu kwa ujumla, ikiwa ni pamoja na afya ya akili.