Ndege za kivita za NATO zaangusha ndege isiyo na rubani iliyoingia katika anga ya Lithuania

Chanzo cha picha, AFP Via Getty
Marubani wa ndege za kivita za NATO wameidungua ndege isiyo na rubani (drone) iliyoingia katika anga ya Lithuania usiku kucha, Rais wa Lithuania amesema.
Mamlaka zimesema kuwa ndege hiyo huenda iliingia kusini mwa Lithuania, karibu na jiji la pili kwa ukubwa la Kaunas, ikitokea nchi jirani ya Belarus muda mfupi baada ya saa sita usiku siku ya Jumanne.
Rais wa Lithuania, Gitanas Nausėda, aliandika katika taarifa kwenye mtandao wa X: "Ndege isiyo na rubani iliyoingia katika anga ya Lithuania imeangamizwa na ndege za kivita za NATO."
Chanzo cha ndege hiyo bado hakijajulikana, msemaji wa kituo cha kitaifa cha usimamizi wa dharura cha Lithuania alisema.
Tahadhari kuhusu ndege hiyo zilisikika katika mji mkuu wa Vilnius na maeneo ya jirani mapema siku ya Jumanne.
Jeshi la Lithuania na marubani wa Italia wanaohudumu katika Operesheni ya NATO ya Ulinzi wa Anga "walionyesha mwitikio wa haraka na wa uwajibikaji" dhidi ya kuingia kwa ndege hiyo, Wizara ya Ulinzi ya Lithuania ilisema.
Ujumbe wa Nausėda kwenye mitandao ya kijamii uliongeza: "Wakati Urusi ikiongeza uchokozi wake dhidi ya Ukraine, utayari wa namna hii ni muhimu sana kwa eneo letu. Kwa kushirikiana na washirika wetu wa NATO, Lithuania italinda anga yake."
Moscow haijatoa maoni yoyote kuhusu tukio hilo.


