Je, imekuwa vigumu zaidi kuliko wakati mwingine wowote kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza?

- Author, James Landale
- Nafasi, Diplomatic correspondent
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 11
Historia ya siasa za Uingereza katika miaka ya karibuni inaweza kuelezwa kwa takwimu chache tu. Ndani ya kipindi cha miaka saba, nchi hiyo imekuwa na mawaziri wakuu watano, na hakuna hata mmoja aliyemaliza muhula kamili wa bunge. Katika kipindi hicho hicho, kumekuwa na mawaziri saba wa mambo ya nje, mawaziri sita wa fedha na makatibu wakuu wanne wa serikali.
Ni simulizi ya kukosekana kwa uthabiti wa kisiasa na mwendelezo wa sera. Hali hiyo imeingia katika sura mpya baada ya Waziri Mkuu wa Uingereza wa sasa Sir Keir Starmer, kujiuzul , ambaye licha ya kuwa na wingi mkubwa wa wabunge bungeni kuliko ule uliomsaidia Clement Attlee kuleta mageuzi makubwa mwaka 1945, kushindwa kuhimili joto la kisiasa kama watangulizi wake.
Ni nini kinachosababisha hali hii? Kwa nini Uingereza inaonekana kubadilisha viongozi wake kwa kasi ambayo zamani ilihusishwa zaidi na Italia? Kwa nini wapiga kura na wabunge wanaonekana kutoa na kuondoa uungwaji mkono wao kwa urahisi mkubwa? Na je, Uingereza inaelekea kuwa nchi ngumu kutawalika?
Kwa Sir Keir Starmer, jibu ni wazi. Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mwezi jana, alisema: "Hapana, sidhani kwamba Uingereza haitawaliki."

Chanzo cha picha, Getty Images
Kiongozi wa Chama cha Conservative, Kemi Badenoch, pia alikubaliana na mtazamo huo alipoliambia Bunge la Commons kwamba: "Uingereza si nchi isiyotawalika."
Hata hivyo, viongozi hao wawili wanaongoza wabunge ambao katika miaka ya karibuni wameonyesha utayari wa kuwaondoa viongozi wao madarakani. Aidha, wanapaswa kuongoza serikali ndani ya mfumo tata wa kiutawala, kisheria na kidhibiti ambao mara nyingi hufanya utekelezaji wa sera kuwa mgumu. Wakati huo huo, wanakabiliwa na wapiga kura wanaozidi kukosa subira na kutaka matokeo ya haraka.
Je, huu ni wakati wa misukosuko ya kipekee katika historia ya Uingereza ambao umewaacha viongozi wakikumbwa na mawimbi ya matukio yasiyoweza kudhibitiwa? Au je, mivutano na misukosuko inayoendelea Westminster inaakisi matatizo ya kina na ya kimfumo ndani ya siasa za Uingereza?
Nyakati ngumu kwa viongozi wa kisiasa
Wachambuzi wengi wanaamini kuwa changamoto zinazowakabili viongozi wa leo ni matokeo ya matukio makubwa yaliyotikisa dunia katika kipindi cha hivi karibuni.
Miongoni mwao ni mdororo wa kifedha wa mwaka 2008, mgogoro wa Brexit, athari za janga la Covid 19, vita vya Ukraine na msukosuko wa nishati uliosababishwa na mzozo huo, pamoja na athari za kisiasa na kiuchumi zinazohusishwa na Rais wa Marekani Donald Trump.
Changamoto hizi si za Uingereza pekee. Serikali nyingi barani Ulaya zimejikuta zikikabiliwa na uchumi dhaifu na wapiga kura wanaotaka matokeo ya haraka.

Chanzo cha picha, EPA - EFE/REX/Shutterstock
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Hannah White, Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Serikali (Institute for Government), anaamini kuwa tatizo si kwamba Uingereza haitawaliki, bali ni kwamba vyama vya siasa vimekuwa vikitoa viongozi ambao hawana baadhi ya ujuzi muhimu wa uongozi katika kipindi ambacho migogoro imekuwa ikitokea kwa mfululizo.
Kwa upande wake, Profesa Anand Menon wa taasisi ya UK in a Changing Europe anasema mfumo wa kisiasa wa Uingereza bado unampa waziri mkuu mwenye wingi wa wabunge mamlaka makubwa ya kutekeleza mabadiliko. Kwa maoni yake, kushindwa kutumia mamlaka hayo ni tatizo la uongozi zaidi kuliko dosari ya mfumo.
Sir Anthony Seldon, mwanahistoria na mwandishi wa wasifu wa mawaziri wakuu kadhaa wa Uingereza, anaamini kuwa baadhi ya viongozi wa hivi karibuni, akiwemo Boris Johnson, Liz Truss na Sir Keir Starmer, hawakuwa na uwezo wa kisiasa unaohitajika kwa nafasi hiyo wala unyenyekevu wa kutafuta msaada wanapouhitaji.
"Hawakuwa na ujuzi unaohitajika na pia hawakuwa tayari kuwashirikisha watu wengine wenye uwezo," anasema.
Anaongeza kuwa mawaziri wakuu wa zamani walikuwa na washauri na walezi wa kisiasa waliowasaidia katika maamuzi yao. "Hata Margaret Thatcher alikuwa na Willie Whitelaw," anasema.
Mfumo wa serikali unazuia mabadiliko?
Baadhi ya viongozi wa kisiasa wanaamini kuwa changamoto nyingine ipo ndani ya mfumo wa utumishi wa umma.
Sir Keir Starmer mwenyewe alikiri mbele ya kamati ya bunge mwaka jana kuwa mara nyingi amekuwa akikatishwa tamaa na ugumu wa kutekeleza maamuzi ya serikali.
Alisema kuwa ''kila ninapojaribu kusukuma sera mbele, ninakutana na kanuni nyingi, mashauriano marefu na taasisi mbalimbali zinazochelewesha utekelezaji''.
Kwa upande mwingine, baadhi ya watumishi wa umma wanadai kuwa mara nyingi mawaziri hushindwa kutoa maelekezo ya wazi kuhusu kile wanachotaka kutekeleza.

Chanzo cha picha, Reuters
Lord Hill, aliyekuwa katibu wa masuala ya kisiasa wa Waziri Mkuu John Major katika miaka ya 1990, anasema "Kukusanywa kwa mamlaka katika Ofisi ya Waziri Mkuu na Ofisi ya Baraza la Mawaziri, pamoja na kujikita kupita kiasi katika usimamizi wa habari, kumepunguza umuhimu na ushawishi wa mawaziri. Ni jambo la kushangaza kwamba bado kuna watu wanaotaka kuingia katika siasa na kuwa mawaziri."
Hata hivyo, swali linaendelea kubaki: Je, matukio ya sasa, udhaifu wa uongozi na changamoto ndani ya utumishi wa umma vinatosha kueleza mkwamo unaoshuhudiwa katika siasa za Uingereza leo?
Mitandao ya kijamii na siasa za haraka
Wachambuzi wengine wanaamini kuwa mitandao ya kijamii imebadilisha kabisa namna siasa zinavyofanyika.
Theo Bertram, mshauri wa zamani wa mawaziri wakuu Tony Blair na Gordon Brown, anasema tatizo kubwa ni kwamba masuala mengi yanayohitaji kutatuliwa nchini Uingereza yanahitaji miaka mingi ili kuzaa matunda.
Lakini katika zama za mitandao ya kijamii, viongozi wa kisiasa hukabiliwa na shinikizo la kutoa matokeo ya haraka.
Mitandao hiyo pia imefanya iwe rahisi kwa wabunge kuandaa upinzani dhidi ya viongozi wao kwa muda mfupi sana, hali inayodhoofisha nidhamu ya vyama vya siasa.
Baadhi ya wachambuzi wanaamini kuwa vyombo vya habari navyo vina mchango katika hali hiyo kwa sababu ya kuzingatia zaidi migogoro na drama za kisiasa kuliko mijadala ya sera.
Steve Baker, aliyekuwa mbunge wa Chama cha Conservative na mmoja wa wahamasishaji wakuu wa Brexit, amesema kuwa mitandao ya kijamii imebadilisha kwa kiasi kikubwa namna siasa zinavyoendeshwa.
Aliandika:
"Wasimamizi wa nidhamu ya chama na mawaziri hujikuta wamechelewa kuingia katika mjadala ambao tayari umeshahitimishwa kwenye mitandao ya kijamii saa moja iliyopita."
Aliongeza kuwa hali hiyo sasa inaonekana pia ndani ya Chama cha Labour, ambapo makundi madogo ya ushawishi yanaundwa kupitia orodha za mawasiliano za WhatsApp na huanza kupanga mikakati dhidi ya kiongozi wao kwa muda wa siku chache tu badala ya miezi kadhaa kama ilivyokuwa hapo awali.
Kwa maneno mengine, Baker anaamini kuwa teknolojia na mitandao ya kijamii imeongeza kasi ya siasa za ndani ya vyama, na kufanya uasi dhidi ya viongozi kuwa rahisi zaidi kuandaliwa na kutekelezwa.

Chanzo cha picha, Bloomberg via Getty Images
Wengine wanaamini kuwa vyombo vya habari navyo vina mchango katika hali hii. Nick Bryant, mchambuzi wa masuala ya kisiasa na mwandishi wa zamani wa BBC, anaona kwamba "msisimko uliopitiliza wa waandishi wa habari" ni sehemu ya tatizo.
Anasema kuwa "utamaduni wa kupenda drama miongoni mwa wanasiasa na waandishi wa habari wanaowaripoti huchochea mzunguko usioisha wa sintofahamu na misukosuko ya kisiasa, hali ambayo inazidi kudhoofisha misingi ya demokrasia."
Kwa hakika, siasa za Brexit zilikuwa za mgawanyiko mkubwa kiasi kwamba baadhi ya wachambuzi wanaamini ziliacha athari za kudumu katika siasa za Uingereza. Mvutano huo ulijenga utamaduni wa migogoro ya mara kwa mara na uasi ndani ya vyama vya siasa.
Wabunge wa Chama cha Conservative walizoea kuwaondoa viongozi wao mara kwa mara. Hivyo basi, swali linaloulizwa ni kama kizazi cha sasa cha wabunge wa Labour kimejifunza na kuiga utamaduni huo, na kuanza kuona jambo hilo kuwa la kawaida, ilhali kihistoria halikuwa sehemu ya kawaida ya siasa za Uingereza.

Chanzo cha picha, Getty Images
Je, vyama vikuu vinapoteza ushawishi?
Lakini je, hiyo ndiyo picha kamili ya tatizo? Baadhi ya wachambuzi wanaamini kwamba hali ya sasa haiwezi kuelezwa kwa sababu hizo pekee. Wanasema kwamba asili na mwenendo wa siasa za Uingereza wenyewe vinabadilika, jambo linalobadili namna mamlaka yanavyopatikana, kuendesha serikali na kudumisha uungwaji mkono wa kisiasa.
Kuongezeka kwa ushawishi wa vyama vidogo kama Reform UK na Green Party kumepunguza nguvu za jadi za Labour na Conservative.
Ingawa Labour ina wingi mkubwa wa wabunge bungeni, baadhi ya wachambuzi wanaona kuwa idadi ya kura ilizopata haikutoa mamlaka makubwa ya kisiasa kama ilivyokuwa zamani.
Aidha, migawanyiko ya ndani ya vyama vikuu imezifanya serikali kuwa dhaifu zaidi.
Kwa mujibu wa Lord Wood, mshauri wa zamani wa Gordon Brown, Chama cha Conservative kilidorora kutokana na mgawanyiko uliochochewa na Brexit, huku Labour ikikosa dira ya pamoja ya kuongoza nchi licha ya ushindi wake mkubwa wa uchaguzi wa mwaka 2024.

Chanzo cha picha, Getty Images
Baadhi ya wachambuzi wanaamini kuwa tatizo ni la kina zaidi kuliko inavyoonekana. Kwa mtazamo wao, kudhoofika kwa mipaka ya jadi kati ya vyama vya siasa kunaonyesha kushindwa kwa tabaka la viongozi wa kisiasa kukabiliana ipasavyo na changamoto kubwa zinazoikabili Uingereza.
Miongoni mwa changamoto hizo ni udhaifu wa kimuundo wa uchumi, viwango vya juu vya uhamiaji vinavyoendelea kuwepo, kudhoofika kwa mahusiano na washirika wa jadi barani Ulaya na nchini Marekani, pamoja na utegemezi mkubwa wa nishati kutoka Mashariki ya Kati, eneo ambalo mara nyingi hukumbwa na misukosuko ya kisiasa na kiusalama.
Tatizo la matarajio ya wananchi
Wachambuzi wengi wanaamini kuwa changamoto kubwa zaidi ni pengo kati ya matarajio ya wananchi na uwezo wa serikali kuyatimiza.
Kwa miaka mingi, serikali ziliweza kutatua matatizo kwa kuongeza matumizi ya umma au kupunguza kodi. Hata hivyo, hali ya sasa ya uchumi imepunguza uwezo huo.
Uingereza inakabiliwa na ukuaji hafifu wa uchumi, deni kubwa la taifa na kupungua kwa uwezo wa wananchi kumudu gharama za maisha.
Wakati chama cha Conservative kiliahidi mafanikio makubwa ya Brexit, Labour nayo iliahidi kukuza uchumi. Hadi sasa, ahadi hizo hazijatoa matokeo yaliyotarajiwa na wananchi wengi wameanza kupoteza imani kwa wanasiasa.
Sir John Major, aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, anasema wapiga kura wanazidi kutaka majibu ya haraka kwa matatizo magumu.
Anahoji kuwa sehemu ya jukumu la viongozi wa kisiasa ni kuwaambia wananchi ukweli hata pale ambapo ukweli huo haupendwi.
Kwa mtazamo huo, huenda tatizo kubwa si kwamba Uingereza haitawaliki, bali ni kwamba matarajio ya wananchi yamekuwa makubwa kuliko uwezo wa serikali kuyatimiza katika mazingira ya sasa ya kiuchumi na kisiasa.
Lord Hill anasema wengi katika Westminster wameisahau dhima halisi ya siasa, ambayo ni kuamua unachotaka kufanya, kujenga hoja ya kukitetea na kuwashawishi wananchi wengi iwezekanavyo kukiunga mkono katika uchaguzi mkuu.
Kwa mujibu wake, wanasiasa wengi wa sasa wanaonekana kuamini kuwa kazi yao ni kubaini matakwa ya makundi mbalimbali ya watu, kusawazisha maslahi hayo tofauti na kukusanya kura za kutosha ili kushinda uchaguzi.
"Badala ya kuwa chombo cha kuongoza na kuelekeza sera, serikali na bunge zimegeuka kuwa taasisi zinazopokea na kujibu matakwa ya makundi mbalimbali, kana kwamba ni mashine kubwa ya ushawishi wa kisiasa," anasema.
Naye Theo Bertram wa taasisi ya Social Market Foundation anaongeza kuwa mojawapo ya sifa ambazo zimeonekana kupungua kwa mawaziri wakuu wa hivi karibuni ni uwezo wa kukabiliana na upinzani kutoka kwa wabunge wa chama chao wenyewe, pamoja na kuwaeleza wananchi ukweli kuhusu masuala magumu.
"Mojawapo ya mambo ambayo hatujaona sana kwa mawaziri wakuu wa hivi karibuni ni uwezo wa kukabiliana na wabunge wao wa nyuma ya viti vya mbele, kukabiliana na maoni ya umma na kuwaambia wananchi mambo magumu ambayo wanahitaji kuyasikia," anasema.

Chanzo cha picha, Andrea Deans/Glyn KIRK / AFP via Getty Images
Baadhi ya wachambuzi wanaamini kuwa wanasiasa bado hawajawa waaminifu kikamilifu kwa wapiga kura kuhusu hatua ngumu zinazohitajika ili kukabiliana na changamoto za nchi. Hatua hizo ni pamoja na kupunguza matumizi ya ustawi wa jamii, kuongeza bajeti ya ulinzi, kufanya mageuzi katika mfumo wa huduma ya afya wa NHS na kuufanya uchumi kuwa na tija zaidi.
Hatua kama hizo zinaweza kusababisha maumivu ya muda mfupi kwa wananchi na, kwa mtazamo wa baadhi ya wataalamu, zingehitaji pia kubadilisha namna serikali inavyogawa rasilimali zake kutoka kwa kizazi cha wazee kwenda kwa vijana.
Siasa ni sanaa ya kushawishi, na wakati mwingine hata ya kuvutia uungwaji mkono. Hata hivyo, inaonekana baadhi ya mawaziri wakuu wa hivi karibuni wamesahau kuwa kazi hiyo inahitaji juhudi za kila wakati za kuwashawishi wapiga kura, wabunge na watumishi wa umma ili waendelee kuunga mkono ajenda za serikali.
Lakini je, wapiga kura wenyewe wamekuwa na papara zaidi? Katika enzi ambayo bidhaa zinazonunuliwa mtandaoni huwasilishwa nyumbani ndani ya saa chache, je, wananchi wameanza kutarajia matokeo ya kisiasa kwa kasi ambayo hakuna serikali inayoweza kuyafikia?
Kuongezeka kwa uungwaji mkono kwa vyama vinavyopinga mfumo wa kisiasa uliopo, kama Reform UK na Green Party, kunaonekana kuwa ishara ya kukatishwa tamaa kwa wapiga kura na vyama vikuu vya kisiasa. Wengi wao wanaamini kuwa vyama hivyo vimeshindwa kutatua matatizo yanayoikabili Uingereza.
Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Sir John Major, alikubaliana na mtangazaji Matt Chorley wa BBC Radio 5 Live kwamba wapiga kura wanatafuta majibu ya haraka na rahisi kwa matatizo ambayo kwa asili ni magumu.
"Nina hofu kwamba ni kweli tunafanya hivyo, na sababu ni kwamba hakuna anayetuambia wazi kuwa hatuwezi kupata kila tunachotaka," alisema. "Inaonekana serikali zimepoteza uwezo wa kusema hapana. Na sehemu ya kazi ya siasa ni kujua wakati wa kusema hapana."
Huenda hapa ndipo kiini cha tatizo kilipo: pengo kati ya matarajio ya wananchi na uwezo wa viongozi kuyatimiza.
End of Soma Zaidi:
Hapo zamani, mawaziri wakuu mara nyingi waliweza kujinasua katika matatizo kwa kuongeza matumizi ya serikali. Viongozi wa mrengo wa kulia wangeweza kupunguza kodi, huku wale wa mrengo wa kushoto wakiongeza matumizi ya ustawi wa jamii. Leo, chaguo zote mbili zimekuwa ngumu zaidi kutekeleza.
Ahadi za Chama cha Conservative za kupunguza kodi bila kubainisha vyanzo vya fedha, pamoja na dalili kutoka Labour za kulegeza masharti ya matumizi ya serikali kwa lengo la kukopa zaidi, zimekuwa zikizua wasiwasi sawa katika masoko ya fedha.
Wakati huo huo, uchumi wa Uingereza unaonekana kukwama katika mzunguko wa ukuaji hafifu, madeni makubwa na mapato halisi yasiyoongezeka. Wananchi wengi wanaendelea kuhisi makali ya gharama kubwa za maisha.
Hannah White wa Taasisi ya Serikali (Institute for Government, IFG) anasema shinikizo kwa huduma za umma linaendelea kuongezeka.
"Matumaini na matarajio ya wananchi ni makubwa, lakini uwezo wa serikali kuchukua hatua ni mdogo," anasema.
Anaeleza kuwa wananchi wengi hawajazoea kukabiliana na uchaguzi mgumu wa sera na matumizi ya fedha za umma. Badala yake, wamezoea kuona serikali ikiingilia kati kwa kiwango kikubwa, kama ilivyofanya wakati wa janga la Covid 19 na mgogoro wa nishati uliosababishwa na vita vya Ukraine.
Kwa sababu hiyo, wananchi wengi wanashindwa kuelewa kwa nini serikali haijaweza kudhibiti kikamilifu ongezeko la gharama za maisha linaloendelea kuwakabili.
"Hata hivyo, ukosefu wa fedha unaweka vikwazo vikubwa kwa chaguo za sera ambazo serikali inaweza kutekeleza," anasema White.
Ukweli mchungu
Hivyo basi, njia ipi inaweza kusaidia kuvunja mzunguko huu wa misukosuko ya kisiasa?
Kwa mujibu wa Lord Wood, viongozi wa kisiasa wanapaswa kuwa tayari kuwaambia wananchi ukweli mgumu kuhusu hali halisi ya nchi, hasa katika masuala ya fedha za umma, ulinzi na usalama wa taifa. Pia wanapaswa kuwa tayari kuiongoza nchi kupitia hatua ngumu na maumivu ya muda mfupi yanayoweza kuhitajika ili kukabiliana na changamoto hizo.
Aidha, anasema viongozi wanapaswa kujenga ajenda ya kisiasa inayotokana na uelewa wa wazi wa dunia ya sasa, inayozingatia maadili yanayotambulika na inayotoa matumaini ya kweli kuhusu mustakabali wa nchi.
Kwa kufanya hivyo, wanaweza kuviunganisha vyama vyao, kurejesha imani ya wapiga kura na kuwapa wananchi sababu mpya ya kuamini katika uongozi wa kisiasa.

Chanzo cha picha, EPA/Shutterstock
Lakini hilo linaweza kuhitaji wapiga kura walio tayari kukubali maamuzi magumu na kutoa muda wa kutosha kwa wanasiasa kuyatekeleza. Pia linaweza kuhitaji vyama vya siasa vilivyo tayari kukabiliana na ukweli mgumu na kuwashawishi wananchi kuuunga mkono.
Zaidi ya yote, mafanikio hayo yangetegemea uwepo wa viongozi wenye uwezo na mawaziri wakuu wanaodumu madarakani kwa muda wa kutosha kutekeleza ahadi walizowapa wapiga kura.
Kwa sasa, huenda mkazi aliyedumu kwa muda mrefu zaidi katika makazi ya Waziri Mkuu wa Uingereza, Downing Street, ni paka anayeitwa Larry the Cat. Na hilo ni tatizo linalowahusu si panya pekee, bali ''Waingereza wote''.
End of Soma Zaidi:
Imetafsiriwa na Mariam Mjahid













