Kazungu: Kada wa CCM azungumza na BBC alivyotekwa na kuteswa

Chanzo cha picha, Kazungu Bakari
- Author, Sammy Awami
- Nafasi, BBC Swahili, Dar es Salaam
- Akiripoti kutoka, Dar es Salaam
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 3
Kada wa Chama Cha Mapinduzi Kazungu Bakari Kazungu amesema anaendelea kupatiwa matibabu akiwa eneo la siri, akihofia watesi wake kurudi na kumuumiza tena.
Kazungu amesema hayo alipozungumza na BBC kuelezea maendeleo ya afya yake akisema kwamba bado ana maumivu makali hasa maeneo ya usoni alipopigwa mateke na kukanyagwa, mikononi alipofungwa pingu, mgongoni, eneo la makalio na miguuni ambapo alichapwa na kitu ambacho hana uhakika ni kitu gani.
Kazungu alitekwa tarehe 04 Agosti akiwa nyumbani kwake akijiandaa kuoga, ambapo watekaji walimchukua kwa nguvu, kumuingiza katika gari aina ya Land Cruizer na kuzunguka naye kwa masaa mengi, kwa mwendo wa kasi huku akiwa amefungwa kitambaa cheusi usoni na pingu mikononi.
"Nilikuwa napigwa kila mara, na mangumi na mirungu. Mimi nilikuwa sioni kitu, mimi ninachohisi ni kipigo na kusikia sauti zao wakiongea, na matusi. Zaidi walikuwa wanamtukana matusi mama yangu mzazi," alisema Kazungu.

Chanzo cha picha, Kazungu Bakari
Tukio hili la kutekwa kwa Kazungu linakuja wakati ambapo kumekuwa na taarifa za watu kadhaa wakiripoti kutekwa, baadhi wakipatikana wakiwa wameumizwa huku wengine wakiwa bado hawajapatikana wala watuhumiwa wa matukio hayo kutiwa nguvuni.
Mwezi Mei 2026, Msaidizi wa Mwenyekiti wa Kitaifa wa Chadema (Tundu Lissu) David Joseph Jumbe alinusurika jaribio la kutekwa na watu wasiojulikana. Jumbe alifanikiwa kuwatoroka watekaji baada ya waendesha bodaboda kushuhudia tukio hilo na kujaribu kuingilia kati kumnusuru Jumbe.
Mwezi mmoja kabla ya tukio hilo, Mwenyekiti wa Tume ya Kuchunguza Mauwaji ya Oktoba 29 Jaji Othman Chande alilitaja suala la upoteaji na kutekwa kwa watu kuwa ni changamoto kubwa inayowaikabili jamii nchini Tanzania.
Chande alisema kati ya mwaka 2003-2005 watu 758 walipotea, kutekwa na kujiteka huku zaidi ya watu 440 kati yao hawajapatikana. Akinukuu ripoti rasmi za polisi, Jaji Chande alisema moja ya sababu kuu za watu kujiteka ni mapenzi, Imani za ushirikina, kutekwa na wahalifu kwa lengo la kujipatia mali, matukio ya kulipizana kisasi na waliojiteka wao wenyewe.

Chanzo cha picha, Kazungu Bakari
Hata hivyo, katika mazungumzo yaliyochapishwa tarehe 16 Agosti na mtandao wa The Jenerali Ulimwengu Post, Makamu wa Rais Mstaafu Jaji Joseph Sinde Warioba amesema sababu moja ambayo Jaji Chande hakuitaja ni sababu ya kisiasa, akiongeza kwamba wananchi wengi wanaogopa kuzungumza masuala ya kisiasa wakihofia kutekwa.
"Sasa hivi, Watanzania wanaishi kwa woga, sio kama ilivyokuwa wakati ule. Wanaishi kwa uwoga, wanaogopa kutekwa, kupotea. Kwahivyo unakuta hata kwa haya yote tunayoyafanya hupati maoni ya wananchi, wanavyoona, kwasababu wanaogopa kupotea na kutekwa" alisema Jaji Warioba akizungumza na mwanahabari mkongwe wa The Jenerali Ulimwengu.

Chanzo cha picha, Kazungu Bakari
Kazungu anasema watekaji wake walikuwa wakimuuliza zaidi juu ya video zake anazoweka katika mitandao yake ya kijamii ambazo anaonekana akimtetea Makamu wa Rais Dr. Emmanuel Nchimbi, Mwenyekiti wa Chadema Tundu Lissu na kupotea kwa aliyekua balozi wa Cuba Humphrey Polepole.
"Swali lao kubwa ni kwa nini unamtetea Makamu wa Rais, Dr. Emmanuel Nchimbi? Kwa nini unamtetea? Wewe ni kama nani? Una mamlaka gani nchini ya kumtetea Nchimbi? Hilo ndio swali lao kubwa sana," alisema Kazungu.
Anaongeza kwamba watekaji pia walimuuliza kuwa kwanini anamtete mwenyekiti wa chadema Tundu Lissu?
Kuhusu tukio la kutekwa kwa Kazungu, Polisi Mkoa wa Tanga wamethibitisha kutokea, na kumuhoji Kazungu na kwamba uchunguzi wa kina wa tukio hilo unaendelea.
Hata hivyo BBC pia ilimtafuta kiongozi wa polisi mkoani Tanga lakini hakupatikana na wala kujibu ujumbe.
















