Mambo matano muhimu katika hotuba ya Mfalme wa Uingereza kwa Bunge la Marekani

,k

Chanzo cha picha, Reuters

Maelezo ya picha, Makamu wa Rais wa Marekani JD Vance na Spika wa Baraza la Wawakilishi Mike Johnson,, wakimtazama Mfalme Charles III wa Uingereza akiwahutubia wajumbe wa Bunge la Marekani jijini Washington Aprili 28, 2026.
    • Author, Anthony Zurcher
    • Nafasi, BBC
  • Muda wa kusoma: Dakika 6

Ziara ya Mfalme Charles III wa Uingereza, nchini Marekani imekusudiwa kuwa ni sherehe ya maadhimisho ya miaka 250 ya uhuru wa Marekani, na uhusiano wa kudumu na maalumu kati ya Uingereza na Marekani. Lakini pia imetajwa kuwa ziara ya kuweka mambo sawa.

Hali ya sasa ya uhusiano wa Marekani na Uingereza imezorota – kutokana na Uingereza kutounga mkono vita vya Marekani na Israeli dhidi ya Iran. Kwa hivyo lengo la Mfalme ni kupunguza mvutano huo, hasa kwa hotuba yake katika Bunge siku ya Jumanne alasiri.

Mfalme alizungumzia "upatanisho na kuanza upya” kutokana na karne nyingi za mwingiliano kati ya mataifa hayo mawili, mada aliyoirudia baadaye kwenye karamu ya serikali ya Ikulu ya White House.

Ilikuwa ni hotuba ya kwanza ya kifalme kwa Bunge la Marekani tangu Malkia Elizabeth II alipozungumza katika Majengo ya Bunge ya Capitol mwaka 1991.

Kukiri kuwepo kwa mvutano

Kukubali kwamba kuna tatizo ni hatua ya kwanza ya kuondoa tatizo. Mfalme Charles alianza hotuba yake kwa kuzama moja kwa moja katika "nyakati za mivutano" zinazoikabili Marekani na Uingereza.

Amezungumzia migogoro ya Mashariki ya Kati na Ulaya - vyanzo vya mzozo wa hivi karibuni kati ya Marekani na Uingereza - huku pia akibainisha tishio kwa demokrasia lililosababishwa na aina ya vurugu za kisiasa zilizotokea wakati wa Chakula cha Jioni cha Waandishi wa Habari katika Ikulu ya Marekani Jumamosi usiku.

Kuanzia hapo, Mfalme alianza kuzungumzia ukweli kwamba Marekani na Uingereza hazina misimamo sawa muda wote.

"Tukikumbuka siku ya uhuru wa Marekani," amesema, "tunaweza kukubaliana kwamba hatukubaliani kila wakati".

Hitimisho lake ni kwamba mataifa hayo mawili, yanapokuwa katika mpangilio mmoja, yanaweza kufanya mambo makubwa "sio kwa faida ya watu wetu, bali pia kwa watu wote."

Onyo kuhusu nguvu za madaraka

b

Chanzo cha picha, New York TImes

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Mfalme Charles amebainisha kwamba nguvu za utendaji "zinategemea mizani" kama ilivyo desturi ya sheria za Uingereza, kama iliyoainishwa katika mkataba wa Magna Carta, ambao ndio msingi wa Katiba ya Marekani. Kwa kauli hiyo alipokea makofi mengi ya kusimama - na msisimko.

Shangwe zilianza upande wa chama cha Democratic, kabla ya kuenea katika chumba kizima.

Wakosoaji wa Donald Trump wamekuwa wakimkosoa rais mara kwa mara kwa kile wanachokiona kama matumizi mabaya ya madaraka.

Hisia kwamba rais anapaswa kuwa na mizania ya madaraka ni mojawapo ya hisia zilizochochea maandamano ya "hakuna wafalme" ambayo yamevutia maelfu ya watu kote nchini katika mwaka uliopita.

Baadaye, Mfalme alipomaliza hotuba yake, moja ya mistari yake ya mwisho ilisababisha baadhi ya manung'uniko - ya kukubali na wasiwasi - kutoka upande wa Democratic.

"Tangu uhuru, kauli za Marekani zina uzito na maana," Mfalme alisema. "Matendo ya taifa hili kubwa yana umuhimu zaidi."

Wa-Democratic wamekuwa wakosoaji mara kwa mara wa maneno ya Trump, na jinsi anavyoyatoa, pamoja na matendo yake.

Wafuasi wa uliberali miongoni mwa hadhira huenda walimwona Mfalme kama akitoa ujumbe wa onyo kwa taifa - huku wakiwapa nafasi ya kuelezea hisia zao za "hakuna wafalme."

Kuunga mkono Nato na muungano wa Ulaya

,k

Chanzo cha picha, New York Times

Maelezo ya picha, Ni mfalme wa kwanza wa Uingereza kuhutubia Bunge hilo tangu mama yake, Malkia Elizabeth II, mwaka 1991.

Akimnukuu Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Marekani Henry Kissinger, Mfalme alizungumzia ushirikiano wa Marekani na Ulaya na akasema – haikuwa mara ya kwanza miongoni mwa washirika wa Marekani barani Ulaya - kwamba wakati pekee ambao Nato ilijipanga kuilinda moja ya nchi wanachama ilikuwa baada ya mashambulizi ya kigaidi ya 9/11 yaliyofanywa na al-Qaeda.

Trump amelidhihaki Jeshi la Wanamaji la Uingereza, ambalo kwa muda mrefu ni jeshi la kujivunia la ufalme. Aliziita meli zao "vinyago" na akasema meli zao za kubeba ndege "hazifanyi kazi".

Mfalme Charles, ambaye alihudumu kwa miaka mitano katika Jeshi la Wanamaji la Uingereza, aliutaja muda wake katika jeshi hilo – na kisha kuzungumzia faida za uhusiano wa usalama na ujasusi kati ya mataifa hayo mawili - na kati ya Amerika na Ulaya.

Pia alitaja mabadiliko ya hali ya hewa, suala ambalo limekuwa likimsumbua kwa muda mrefu.

"Kuanzia kina cha bahari ya Atlantiki hadi kwenye barafu inayoyeyuka ya Aktiki, kujitolea na utaalamu wa Vikosi vya Jeshi vya Marekani na washirika wake uko katikati ya Nato, tukiahidiana ulinzi, tukiwalinda raia na maslahi yetu, tukiwaweka Wamarekani na watu wa Ulaya salama kutokana na maadui zetu," alisema.

Hakuwataja waathiriwa wa Epstein

Ukiacha masuala ya siasa za kimataifa, moja ya maswali makubwa yaliyohusu ziara ya Mfalme Charles, yalihusu ikiwa atamtaja mhalifu wa ngono Jeffrey Epstein katika hotuba zake au kuwataja waathiriwa wake.

Hakufanya hivyo.

Jambo la karibu zaidi alilolizungumzia ni kuhusu hitaji la "kuwasaidia waathiriwa wa baadhi ya matatizo ambayo, kwa kusikitisha, yapo katika nchi zetu zote mbili leo."

Kwa wale waliomtaka Mfalme akutane na manusura wa Epstein akiwa Marekani, maoni hayo pekee yanaweza kuonekana – kama kauli dhaifu.

Mwaka jana, kutokana na pingamizi za utawala wa Trump, Bunge lilipitisha sheria inayoagiza kutolewa kwa faili zilizoshikiliwa na serikali ya Marekani zinazohusiana na uchunguzi wa Epstein.

Faili hizo zilisababisha ufichuzi mpya kuhusu uhusiano kati ya Epstein na matajiri na watu wenye nguvu, akiwemo balozi wa zamani wa Uingereza nchini Marekani Peter Mandelson na kaka yake Mfalme, Andrew Mountbatten-Windsor.

Kwa sasa, sakata ya Epstein limekuwa na athari kubwa zaidi nchini Uingereza ikilinganishwa na Marekani, ambako ni watu wachache sana katika nafasi za madaraka ya kisiasa wamekabiliwa na matokeo mabaya.

Hata kama mada hiyo haikujitokeza wakati wa hotuba, suala hilo halijafifia kutoka kwenye vichwa vya habari - na habari kamili huko Marekani kuhusu suala hilo inaweza kuwa bado haijaibuka.

Ucheshi wa kifalme

k

Chanzo cha picha, New York Times

Kwa kuzingatia malengo ya Mfalme – juu ya mustakabali wa uhusiano wa Marekani na Uingereza - hotuba yake, wakati mwingine, ilikuwa ya uchezi.

Alianza hotuba yake kwa maneno yanayonukuliwa mara kwa mara - na kunukuliwa vibaya - kutoka kwa Oscar Wilde kuhusu Marekani na Uingereza kuwa zinafanana kila kitu "isipokuwa lugha moja."

Alitania kuhusu mbunge wa bunge la Uingereza ambaye hushikiliwa kama "mateka" wakati Mfalme anapozungumza huko Westminster - na akauliza kama kuna mtu yeyote katika Bunge la Marekani aliyejitolea kwa kazi kama hiyo leo.

Pia alisema kuhusu jinsi uhuru wa Marekani ulivyo wa muda mrefu kama wa Uingereza na hakuja Marekani kama "hatua ya ujanja" ili kurejesha utawala wa Uingereza.

Huenda kukawa na mvutano kati ya Marekani na Uingereza kwa sasa, lakini siku ya Jumanne, Mfalme anaonekana kufanikiwa kupunguza mvutano.