Kwa nini kufikiria kifo chako kunaweza kuwa na faida?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 2

Kila aliye hai leo wewe, marafiki zako na familia yako siku moja hatakuwepo. Ni ukweli usioepukika, lakini mara nyingi tunajitahidi sana kuupuuza au kutokubali ukweli huo. Jules Howard anaeleza kwa nini huenda kufanya hivyo si jambo zuri.

Kwa mujibu wa data kutoka kampuni ya Statista, ni asilimia 11 pekee ya watu wanaofikiria kuhusu kifo katika maisha yao ya kila siku. Wengi wetu tumejikita zaidi katika mambo ya maisha, kiasi kwamba huenda tukafikiria kuhusu kifo mara tatu au nne tu kwa mwaka.

Sisi katika nchi za Magharibi, kwa maneno ya mwanasaikolojia wa kijamii Sheldon Solomon, ni mabingwa wa "kuzika hofu na wasiwasi wa kuwepo chini ya mlima wa viazi vya kukaanga."

Lakini hilo linaeleweka, sivyo? Kifo ni jambo la kutisha. Tunaishi. Tunakufa. Na hapo ndipo kila kitu kinaishia. Kwa hiyo, kuna sababu gani ya kufikiria zaidi kuhusu kifo?

Na zaidi ya yote, viazi vya kukaanga ni vitamu.

Hata hivyo, kwa mujibu wa baadhi ya wanasayansi, kuna faida za kufikiria zaidi kuhusu kifo. Wanasaikolojia, hasa, wanaelekeza kwenye tafiti kadhaa zinazoonyesha kuwa kufikiria kuhusu kifo au "ufahamu wa kufa" kunaweza kuongeza hali ya mtu ya kujithamini, kuwafanya watu wasizingatie sana masuala ya pesa, na hata kuwafanya wawe wachangamfu na wenye ucheshi zaidi.

Kwa kuhamasishwa na tafiti kama hizi, kumeibuka harakati za kijamii kama vile Death Cafés na kundi la Death Salon, ambazo huwapa watu nafasi ya kukutana na kuzungumza kwa uwazi kuhusu kifo.

Kwa namna nyingi, makundi haya yanafanana na falsafa za Mashariki ambazo kwa karne nyingi zimewahimiza watu kutafakari kuhusu kifo na udhaifu wa maisha ya mwanadamu.

Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Kwa mfano, Buddha alikuwa akihimiza kile kinachojulikana kama "kutafakari maiti", ambapo watu hutazama miili ya watu waliokufa katika hatua mbalimbali za kuoza.

Andiko moja linasema: "Mwili huu pia… ndivyo ulivyo katika asili yake, ndivyo utakavyokuwa hatimaye, na hivyo ndivyo hatima yake isiyoweza kuepukika."

Na hata dhana yenyewe ya "yin na yang" wazo la vitu viwili vinavyopingana kama "mwanga na giza", "moto na maji" na "maisha na kifo" inaonekana kuwafanya watu katika jamii zisizo za Magharibi kuthamini zaidi mambo ya kawaida ya kila siku kuliko watu wa jamii za Magharibi.

Kwa hiyo, je, sisi katika nchi za Magharibi tunafikiria kuhusu kifo kwa njia isiyo sahihi? Ningesema, hapana. Kwa sababu hakuna njia "isiyo sahihi" ya kufikiria kuhusu kifo.

Lakini bila shaka, tunaweza kufikiria zaidi kuhusu kifo. Si lazima sana, bali kiasi ambacho kila mmoja wetu anaona kinafaa. Kwa kufanya hivyo, mtazamo wetu kuhusu matukio ya kila siku unaweza kuboreka, hata kama kwa namna isiyoonekana sana.

Kwa maana, kwa wale wanaotambua kwamba maisha hayadumu milele, viazi vya kukaanga havijawahi kuwa vitamu zaidi.