WARIDI WA BBC: 'Nina miaka 23 na nywele zangu zinanyonyoka'

- Author, Na Asha Juma
- Nafasi, BBC Nairobi
- Akiripoti kutoka, Nairobi
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 4
Alopecia, kama linavyojulikana kwa lugha ya Kiingereza ni tatizo la kung'oka au kunyoyoka nywele na linakadiriwa kuwaathiri watu milioni 160 duniani kote. Lakini kwa hali ya kawaida, ungelishirikisha na watu wenye umri wa makamo au mkubwa.
Hali ni tofauti kwa Sharon Chepkoech maarufu kama 'Kechi', 23, ambaye aligundua kuwa na tatizo hili mwaka jana. Je limemuathiri vipi hasa katika maisha yake kama kijana. Mwanahabari wa BBC Asha Juma alipata wasaa wa kuzungumza naye.
"Nilijua kuwa nina tatizo hili mwishoni mwa mwaka 2024, baada ya kuona kuwa kila nakifungua nywele, za katikati zilikuwa zinanyonyoka na hatimaye zikaanza kuwa kidogo kisha nikaanza kuzisikia ni nyepesi kuliko upande mwingine," Kechi anakumbuka.
"Hapo ndio nilijua nina tatizo na nikaamuza kuanza kulishughulikia."
Anasema mara ya kwanza alifikiria nywele zake zinanyonyoka kwa sababu zimekazwa sana wakati anasukwa.
"Niliamua niache kusuka kwa muda fulani huku msusi wangu akipendekeza nipake mafuta kama ya Rosemary na mengine ya kujipaka ili zianze kukua tena," anasema Kechi.
Lakini nilipoona hakuna mabadiliko, nikaamua kumuona daktari.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Asha alitaka kujua kama tatizo hili ni lake peke yako ama ni kitu ambacho kimekuwa kwenye familia?
"Familia yetu, kuwa na upara ni upande wa wanaume pekee. Hakuna wanamke wala msichana ambaye ananyonyoka nywele. Wote wana nywele zao vizuri. Wanaume pekee ndio wanaanza upara na hili huwa linaonekana kuwa jambo la kawaida katika jamii," Kechi anasema.
Kechi anasema ingawa akitafakiri nyuma tatizo lilianza zamani, mwaka jana ndio alijua kuwa ana upara ingawa hakuwa bado anakubali.
"Hali ilikuwa inaendelea kudodora, nikaamua kwenda kumuona daktari. Wakati huo bado nilikua sitaki kunyoa nywele zangu hasa ukizingatia kuwa mimi ni msichana mwenye umri mdogo. Nataka kusonga na kuwa na nywele nyingi kama wenzangu, nataka tu kuwa na nywele," Kechi anasema.
"Mwaka huu ndiyo nimesema, liwe liwalo itakavyokuwa nitakubali," Kechi anaongeza.
Kwa mtazamo wa binti huyu nywele zimefanywa kuwa kama msingi wa urembo, hivyo basi, hilo limemfanya yeye pia kutaka kuwa na nazo.
"Sikuwa nataka kuacha kusuka na kwa sababu hiyo niliendelea tu. Nilichokuwa nikiwaambia wasusi ni kuwa musuke kando kando lakini hapo katikati mupaache, msikuguse kabisa, Kechi anasema.
Nywele zinaweza kukua tena?

Chanzo cha picha, Sharon Chepkoech
"Kila kitu nilichopimwa na daktari kilikuwa sawa. Na pia nimekubali kuwa itachukua muda kabla ya kupata suluhisho na sitaki hilo liniathiri kwa namna yoyote," anasema Kechi.
Wasichana wengi wenye tatizo hili, wanaficha hali zao, Kechi anasema.
"Nataka wenye tatizo kama mimi wasitengwe, badala yake wakubaliwe jinsi walivyo. Wengi wanajificha kwa kuvaa nywele bandia," anaendelea kusema Kechi.
"Nywele zangu ni dhaifu sana na huwa zinanyonyoka taratibu. Tatizo ni kwamba iking'oka, inatoka na mizizi yake. Hii inamaanisha hata nikipaka dawa, haiwezi tena kukua, anasema Kechi.
Kechi amekuwa na panda shuka zake, kuna wakati alikuwa anatumia dawa akaamua kucha hasa baada ya kuona hakuna mabadiliko lakini kwa sasa amerudi tena kuanza kutumia dawa. Lakini je, kuna uwezekano wa nywele kukua tena wakati mizizi imeng'oka?
Kulingana na Kechi, njia ziko lakini sio sawa kwa kila mtu kwa sababu chanzo ni tofauti.
"Unaweza kutumia tiba ya kuchoma sindano kichwani kuchochea nywele kukua tena ama ukafanyiwa matibabu ya kupandikiza nywele," Kechi anasema.
'Niliacha kwenda saluni'

Chanzo cha picha, Sharon Chepkoech
Kwa Kechi, urembo kila mtu anaweza kuufafanua kwa namna yake na ingawa amekuwa na changamoto hii, haijaathiri mahusiano yake.
Lakini hili halimaanishi kuwa hajapitia misukosuko yake.
Kitambo nilikuwa nikienda saluni kutengenezwa nywele lakini siku hizi niliacha.
"Kilichosababisha niache watu walikuwa wakiniona wanaanza kuniuliza maswali mengi na kutoa ushauri kwa kuzingatia dhana walizonazo.
"Wengine wanasema ni uchafu, hujatunza nywele zako vizuri ndio maana zinanyonyoka. Wengine wanasema ni saratani, kurogwa na hata uchawi," anasema Kechi.
Licha, ya yote anayopitia na umri wake mdogo, Kechi anashukuru familia yake ambayo imetembea na yeye.
"Nimekuwa na familia ambayo inatembea na mimi katika safari hii," Kechi anasema.
"Lakini pia, mimi mwenyewe nilianza kujikubali na mtu kutoka nje hawezi kunifanya nijihisi vibaya. Ninajua kuwa nina kipara na maneno mabaya ambayo mtu atasema, hayawezi kuniathiri, Kechi anasema.
Anasema kuwa kitu kimoja ambacho hawezi kuruhusu kimtokee ni kuacha kujiamini kwa sababu ya kukosa nywele.
Hukumu za jamii
Yote tisa, kumi anachoomba Kechi kwa sasa, jamii ikubali kila mtu jinsi alivyo na kulingana na yeye kila mtu atengeneze nywele zake alizo nazo.
"Sikubaliani na dhana kwamba msichana au mwanamke ni nywele, na iwapo nitakubaliana nayo, kila mtu akubaliwe na nywele alizonazo. Usilazimishwe uwe na nyewele kama ilivyozoeleka.
"Watu wanafikiria unafaa kuwa na nywele ndefu kama msichana. Wengine wanasema msichana hufai kuwa na kipara kama wanaume kama mimi sasa, msichana hufai kuwa na hili… hapana, mambo mengine kama haya, hatuna uwezo wa kufanya nywele zikue. Mengine yanatupata tu," Kechi anasimulia.
"Unaweza kupata mtu anapitia changamoto za kinga ya mwili na hata afanye nini, si makosa yake, nywele hazitakua. Je, inamaanisha kuwa tutamtenga? Tutamtoa kwenye jamii, hapana. Itabidi tukubali kila mtu na nywele zake zilivyo. Na tusitumie nywele peke yake kutathmini urembo wa mtu," Kechi anasema.
Kulingana na yeye, yeyote ambaye ananyonyoka nywele itakuwa bora apate matibabu kwanza badala ya kuanza kutumia dawa moja kwa moja bila ushauri wa daktari.
Matumaini ya Kechi ni kwamba siku moja nywele zake zitakua tena na kusuka anachotaka.
"Ninapenda sana kusuka tangu utotoni", Kechi anasema.











