Kwa nini Tanzania inawashirikisha majaji wa nje kuchunguza ghasia za Oktoba 29?

.

Chanzo cha picha, Mwananchi

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 4

Baada ya uchaguzi mkuu wa Tanzania wa Oktoba 29, 2025, ghasia na ukiukwaji wa sheria uliotokea wakati na baada ya uchaguzi uliibua maswali kuhusu chanzo cha vurugu hizo na waliohusika.

Sasa, karibu mwaka mmoja baadaye, Rais Samia Suluhu Hassan ameunda na kuzindua Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Wahusika wa Ghasia na Ukiukwaji wa Sheria katika matukio hayo.

Tume hiyo ina jukumu la kwenda hatua zaidi ya kuchunguza matukio yenyewe, ikiwemo kubaini waliohusika, waliochochea na, kwa mujibu wa Rais Samia, hata waliotoa fedha ili ghasia hizo zitokee.

Lakini uamuzi wa kuunda tume hiyo umeibua swali jingine: Kwa nini Tanzania imeamua kuwashirikisha majaji kutoka nje ya nchi, na je, tume hiyo inaweza kupata majibu ambayo tume iliyotangulia haikupata?

Kwa nini majaji kutoka Uganda na Namibia?

.

Chanzo cha picha, Fullshangwe

Maelezo ya picha, Makamishna wa nje kwenye Tume hiyo ni ni Petrus Tileinge Damaseb, Naibu Jaji Mkuu wa Namibia, na Cheborion Barishaki, Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Uganda.

Tume hiyo ina makamishna sita, wakiwemo majaji kutoka Tanzania, Uganda na Namibia.

Rais Samia amesema uamuzi wa kuwashirikisha majaji kutoka Uganda na Namibia ulilenga kuipa tume hiyo mtazamo mpana zaidi na kufanya uchunguzi wa kina.

"Tumeamua kuwashirikisha wenzetu (Namibia, Uganda) ili kupata muono mpana na kwamba tume hii inakwenda kuingia kwa undani zaidi, kutafuta nani hasa waliochochea, waliohusika, waliotoa fedha ili mambo yale (ghasia) yatokee ndani ya nchi yetu," alisema Rais Samia wakati wa uzinduzi wa tume hiyo Ikulu jijini Dar es Salaam.

Miongoni mwa makamishna hao ni Petrus Tileinge Damaseb, Naibu Jaji Mkuu wa Namibia, na Cheborion Barishaki, Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Uganda.

Lakini ushiriki wa Damaseb tayari umepingwa na vyama vya upinzani nchini Namibia, ambavyo vinahoji athari zake kwa uhuru na taswira ya mahakama ya nchi hiyo.

Vyama vya Affirmative Repositioning (AR) na Independent Patriots for Change (IPC) vimesema uteuzi huo unaweza kuibua maswali kuhusu uhuru wa mahakama ya Namibia na nafasi ya nchi hiyo katika mjadala kuhusu haki za binadamu nchini Tanzania.

Nchini Tanzania, chama kikuu cha upinzani, CHADEMA pia imepinga tume hiyo, kwa hoja ya tofauti.

CHADEMA ina mashaka gani?

Makamu Mwenyekiti wa CHADEMA, John Heche, amehoji kama tume hiyo mpya inaweza kupata majibu tofauti na yale yaliyotolewa na tume iliyotangulia.

Akitoa mfano, amesema:

"Ukijenga msingi wa tope halafu ukachukua nyumba ya ghorofa ukaweka juu, itasimama hapo?"

Heche ameendelea kuhoji ufanisi wa tume hiyo mpya akisema:

"Kama Tume ya Jaji Chande ilishasema kwamba watu wanatekwa kwa sababu ya mapenzi, hii tume ya sasa (Jaji Lila) itapata ukweli?"

Hoja ya CHADEMA, kwa msingi huo, ni kwamba suala si tu kuunda tume nyingine au kuongeza makamishna kutoka nje ya nchi, bali ni kama mazingira na msingi wa uchunguzi mpya utaiwezesha tume kupata ukweli ambao chama hicho kinaamini haukujitokeza katika uchunguzi uliopita.

Tume hii inatofautiana vipi na ya Jaji Chande?

.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Wajumbe wa Tume ya Jaji Chande wakiwa na Rais Samia
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Hili ndilo jambo muhimu katika kuelewa kwa nini tume mpya imeundwa.

Tume iliyoongozwa na Jaji Mstaafu Mohamed Chande Othman ilichunguza matukio ya vurugu yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025 na kutoa mapendekezo.

Tume mpya, inayoongozwa na Jaji wa Mahakama ya Rufani Shabani Lila, imepewa jukumu la kuchunguza wahusika wa ghasia na ukiukwaji wa sheria na kutoa mapendekezo kuhusu hatua zinazoweza kuchukuliwa.

Kwa hiyo, kwa mujibu wa mamlaka yake, tume mpya inalenga kwenda hatua nyingine: si tu kueleza kilichotokea, bali kutafuta nani alihusika na kwa namna gani.

Rais Samia ameunda tume hiyo akitumia mamlaka aliyopewa chini ya Sheria ya Tume za Uchunguzi, Sura ya 32.

Tume hiyo imepewa muda wa miezi mitano kukamilisha kazi yake. Rais amesema iwapo kutakuwa na ombi la kuongeza muda, suala hilo litaangaliwa baadaye.

Hivyo, kisheria, kuundwa kwa tume hiyo ni utekelezaji wa mamlaka ya Rais chini ya sheria hiyo, lakini mjadala wa kisiasa unaendelea kuhusu uhuru, uaminifu na uwezo wa tume hiyo kupata ukweli kuhusu matukio ya Oktoba 2025.

Je, majaji wa nje wanaweza kuongeza uaminifu?

Kwa upande wa serikali, ushiriki wa majaji kutoka Uganda na Namibia unaweza kuonekana kama njia ya kuleta mtazamo wa nje na kuongeza upeo wa uchunguzi.

Lakini kwa wakosoaji, swali ni kama uwepo wa majaji wa kigeni pekee unaweza kutatua changamoto zinazohusu mchakato huo.

Huko Namibia, vyama vya upinzani vimepinga ushiriki wa Jaji Damaseb, huku CHADEMA nchini Tanzania ikipinga tume yenyewe.

Ingawa upinzani Tanzania awali ulitaka jumuia za kimataifa kuja kufanya uchunguzi wa matukio hayo ya Oktoba 29, kwa sababu ya kutokuwa na imani na wajumbe wa ndani watakaokuwa sehemu ya tume.

Kwa hiyo, wakati tume mpya ikianza kazi yake, changamoto yake kubwa haitakuwa tu kubaini waliohusika na ghasia za Oktoba 2025, bali pia kujenga imani kwamba uchunguzi wake unaweza kutoa majibu yanayoaminika na yanayokubalika kwa sehemu pana ya jamii.

Ingawa kwa upande wa mamlaka za Tanzania msingi wa tume hii ni sheria na mamlaka iliyopewa pamoja na majukumu iliyoundwa kuyatekeleza, CHADEMA inaendelea kuhoji kama mchakato huo utaweza kufikia ukweli ambao chama hicho kinaamini haukupatikana katika uchunguzi uliotangulia.

Kwa upande wake, serikali inasema tume mpya imepewa jukumu la kwenda kwa undani zaidi, ikiwemo kubaini waliochochea, waliohusika na waliotoa fedha kwa ajili ya ghasia hizo.

Hivyo, wakati tume ikianza kazi yake, swali litakalopimwa si tu uwezo wake wa kubaini wahusika, bali pia kama matokeo ya uchunguzi wake yataweza kujenga imani miongoni mwa pande zinazotofautiana kuhusu matukio ya Oktoba 2025.