Barabara 10 hatari zaidi duniani 2026

Chanzo cha picha, Alamy
Ukiwa kwenye safari ya barabarani mara nyingi utaona msongamano fulani wa magari, ujenzi wa barabara au alama zinazokutaka upunguze mwendo. Lakini kuna mambo hatari zaidi ya hayo kwenye barabara.
Fikiria gari kupishana kwenye njia iliyo juu ya mlima, ambapo kosa dogo tu linaweza kusababisha maafa.
Huo ndio ukweli katika maeneo fulani duniani, ambapo chaguo pekee la kutoka sehemu A hadi B ni kuhatarisha maisha yako.
Kwa hivyo funga mkanda na ujiandae kwa safari ya kutisha tunaposafiri katika baadhi ya barabara hatari zaidi duniani.
Barabara ya Keylong Kishtwar, India

Chanzo cha picha, Getty Images
Ni kilomita 235 za njia ya udongo na gari moja katika milimani, barabara ya Keylong hadi Kishwar nchini India ni hatari sana.
Hakuna vizuizi vya usalama pembeni ya barabara ambako kuna bonde. Ongeza tishio la maporomoko ya ardhi na hali ya hewa inayobadilika.
Eneo moja la Barabara linalojulikana kama 'Cliff Hanger', ni jembamba na kuna uwezekano wa kumomonyoka ikiwa utakaribia sana ukingoni.
Ibarska Magistrala, Serbia

Chanzo cha picha, BrankaVV/Wikipedia Commons
Inajulikana kama 'Barabara Nyeusi', Barabara ya Jimbo 22 au 'Barabara Kuu ya Ibar' ni mojawapo ya barabara hatari barani Ulaya, na pia ni mojawapo ya barabara zenye shughuli nyingi zaidi nchini.
Barabara hii inaunganisha Belgrade na manispaa zingine kubwa ndani ya Serbia na nchi jirani kama vile Montenegro.
Ni barabara yenye kona hatari ambazo husababisha matukio mengi ya ajali, hasa usiku. Nyingi kati ya hizi husababishwa na mwendo kasi au madereva kuendesha gari wakiwa wamelewa.
Transfăgărășsan, Romania

Chanzo cha picha, getty mages
Romania ina baadhi ya barabara mbaya barani Ulaya. Lakini barabara yao maarufu na hatari zaidi ni Barabara Kuu ya Transfăgărășan.
Barabara hii ya milimani inayopinda inafikia juu zaidi ya mita 2,000 na inaonyesha mandhari ya kuvutia katika urefu wake wa kilomita 150.
Inajumuisha kona kali, handaki na miinuko mikubwa, na kuifanya iwe changamoto kubwa kwa watalii wanaoendesha magari katika barabara hii.
Hatari nyingine kuu unayoweza kukutana nayo kwenye barabara hii ni makundi makubwa ya kondoo katikati ya barabara. Wachungaji pia hutumia njia hiyo kuhamisha kondoo wao kati ya malisho.
Barabara ya Skippers Canyon, New Zealand

Chanzo cha picha, Bernard Spragg/Wikipedia Commons
Korongo la Skippers ni korongo huko New Zealand linalofuata njia ya Mto Shotover. 1862, dhahabu iligunduliwa katika eneo hili, jambo lililohitaji ujenzi wa barabara kupitia korongo hilo.
Barabara ilichongwa kwenye miamba na wachimbaji madini kwa kutumia vifaa vya mkono na vilipuzi. Kwa sababu ya mwamba, barabara hii huteleza wakati wa mvua na kupasuka inapokauka.
Ina mikunjo mingi na ina upana wa kutosha tu kwa gari moja katika urefu wake wa kilomita 22. Kwa sababu ya asili yake hatari, bima ya kukodisha gari haihesabiwi katika sehemu hii ya barabara.
Barabara ya James Dalton, Marekani

Chanzo cha picha, Alamy
Barabara Kuu ya James Dalton, iliyojipatia umaarufu katika kipindi cha televisheni cha 'Ice Road Truckers', ni barabara ndefu inayounganisha jiji la Fairbanks na jamii ya kaskazini ya Deadhorse, juu ya Mzingo wa Aktiki.
Barabara hii ya kilomita 666 imepewa jina la mhandisi wa Alaska na hutumika kama njia kuu ya malori yanayosafirisha mafuta na vifaa kwa wafanyakazi wa mafuta. Theluthi moja tu ya barabara imetengenezwa kwa lami, sehemu iliyobaki ikiwa na changarawe na mawe.
Hali mbaya ya hewa kama vile theluji na barafu ndio hatari kuu ambazo watu hukutana nazo kwenye barabara hii. Hata hivyo, hatari nyingine ni uwepo wa dubu njiani.
Zojila Pass, India

Chanzo cha picha, Getty Images
Njia ya Zojila ni barabara muhimu inayounganisha eneo la Ladakh na Bonde la Kashmir. Kwa sababu ipo katika milima ya Himalaya, barabara hii hupigwa na theluji na barafu na mara nyingi hufungwa kwa miezi kadhaa.
Ina upana wa kutosha gari moja. Bila vizuizi vya usalama vilivyowekwa, kuna maeneo mengi ambapo hakuna kitu kati yako na sehemu ya kushuka kwenye bonde. Kwa kifupi, si njia kwa watu wenye mioyo dhaifu.
Kuna handaki jipya linajengwa ili kuilinda kutokana na hali mbaya ya hewa ya baridi kali, na kusaidia kuiweka barabara wazi mwaka mzima. Lakini bado haijabainika ikiwa hii itafanya barabara hiyo kuwa salama.
Barabara ya Fairy Meadows, Pakistani

Chanzo cha picha, Alamy
Barabara hii ya kutisha hupitia milima ya Pakistani juu katika urefu wa zaidi ya mita 3,000 usawa wa bahari katika sehemu fulani na ina upana wa kutosha gari moja kwa wakati mmoja.
Kwa mara nyingine tena, hakuna vizuizi vya usalama vya kukuzuia usitumbukie kwenye mabonde yaliyo chini.
Ni Barabara ya kilomita 16 inaunganisha Barabara Kuu ya Karakoram na kijiji kidogo cha Tato katika Hifadhi ya Kitaifa ya Fairy Meadows.
Kwa sababu ni hatari sana, barabara hiyo inaruhusiwa kuendeshwa na wenyeji pekee.
Barabara ya Yungas, Bolivia

Chanzo cha picha, getty imags
Barabara ya North Yungas ni mojawapo ya barabara hatari duniani.
Barabara hii ya kilomita 64 inaunganisha jiji la La Paz na eneo la Yungas la Bolivia na inakadiriwa ilikuwa ikiondoka na wastani wa maisha ya watu kati ya 200 na 300 kila mwaka, hadi barabara kuu mpya ilipofunguliwa ili kutoa njia mbadala salama zaidi.
Barabara hii ya kutisha ni ya changarawe na inapita milimani. Changamoto zake kuu ni ukungu na mvua zinazozuia kutoona mbele na utelezi.
Barabara ya Sichuan-Tibet, China

Chanzo cha picha, Getty Images
Barabara Kuu ya Sichuan-Tibet ni mojawapo ya barabara za juu zaidi duniani, ambayo ina changamoto zake. Kuanzia theluji na maporomoko ya ardhi. Kuna sehemu zenye njia moja kwenye miinuko mirefu bila vizuizi.
Hii pia ni barabara yenye shughuli nyingi sana ukizingatia asili yake. Msongamano wa magari na kukwama mara kwa mara kunamaanisha kwamba kusafiri barabara nzima wakati mwingine kunaweza kuchukua siku 15, na ugomvi hutokea kati ya madereva wakati mambo yanapokuwa magumu.
Ukiwa jasiri kusafiri katika barabara hii basi utazawadiwa mandhari nzuri yenye milima iliyofunikwa na theluji na korongo zenye kina kirefu za kuvutia.
Bayburt D915, Uturuki

Chanzo cha picha, Alamy
Barabara ya D915 inayopinda mara kwa mara huitwa moja ya barabara za kutisha zaidi duniani kutokana na mikunjo yake mingi inayopita katika milima.
Inaunganisha Bahari Nyeusi kwenye pwani ya kaskazini na jiji la Bayburt - ambalo hapo awali lilikuwa sehemu ya njia ya biashara ya zamani ya Barabara ya Hariri kati ya China na Ulaya.
Barabara ni njia muhimu kwa safari za ndani, lakini mara nyingi hali ya hewa mbaya na hatari inahitaji uangalifu na uvumilivu mwingi ili kuisafiri bila kujeruhiwa.














