Roboti zinaweza kuwa wanajeshi wa vita vijavyo?

Chanzo cha picha, Getty Images
Kutana na ndege zisizo na rubani, magari ya ardhini yanayodhibitiwa kwa mbali na roboti wa miguu minne wanaobadilisha taswira nzima ya vita duniani
Wanajeshi wa Urusi hawakusikia hata roboti zilizowaua. Kikosi cha wanajeshi watano kilikuwa kimeingia kwa siri nchini Ukraine na kujificha katika majengo madogo kaskazini mwa Dobropillya, katika mkoa wa Donetsk.
Walikuwa nyuma ya mistari ya adui na walikuwa na uhakika kwamba vikosi vya Ukraine havikujua walikokuwa. Ikiwa wanajeshi wa Ukraine wangegundua uwepo wao, wangetarajia shambulio la kushtukiza, ambalo lingeambatana na milio ya risasi kutoka kwa wanajeshi waliokuwa karibu.
Lakini hakukuwa na haja ya kutuma wanajeshi kukabiliana na tishio hilo. Badala yake, Warusi hao waliuawa na waendeshaji wa ndege tatu zisizo na rubani (UAVs) na magari mawili ya ardhini yasiyo na rubani (UGVs), yaliyokuwa yamewekewa bunduki za mashine za kiwango kikubwa.
Vita vinavyowezeshwa na satelaiti
Ingawa mashambulizi kwa kutumia ndege zisizo na rubani yamekuwa jambo la kawaida tangu Urusi kuivamia Ukraine Februari 2022, matumizi ya magari ya ardhini yasiyo na rubani kushikilia na kutwaa tena maeneo yameongezeka kwa kasi katika kipindi cha miezi sita iliyopita.
Uwezo wa UGVs katika operesheni za kujilinda na kushambulia umeonekana kuwa mkubwa kiasi kwamba jeshi la Ukraine hivi karibuni lilianzisha mashindano ya kutafuta miundo mipya ya roboti hizo.
Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotangaza mashindano hayo, (ambayo iliambatana na picha iliyotengenezwa kwa kutumia akili bandia ikionyesha roboti zinazofanana na Terminator zikirusha risasi kuelekea kwenye midoli zenye umbo la binadamu), lengo kuu ni "kuongeza kiwango cha matumizi ya mifumo ya kiotomatiki katika mstari wa mbele na kupunguza hatari kwa wanajeshi."
Hilo ndilo limekuwa lengo la UGVs tangu awali, anasema Robert Tollast, mtafiti katika kitengo cha vita vya ardhini cha Taasisi ya Royal United Services Institute (RUSI).
Ingawa historia ina mifano mingi ya magari ya ardhini yenye silaha yanayodhibitiwa kwa mbali – kama vile Schneider Crocodile iliyotumiwa na jeshi la Ufaransa wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia – nchini Ukraine, roboti hizo zilianza kupata umaarufu zaidi kama njia ya kupeleka vifaa katika maeneo ya mbele yaliyotengwa na kuwaokoa wanajeshi waliojeruhiwa.
Urusi na Ukraine zote hutumia mara kwa mara UGVs hizi, ambazo nyingi zinafanana na mikokoteni bapa yenye mikanda ya kutambaa badala ya magurudumu. Lakini maendeleo katika teknolojia ya mawasiliano yamewezesha vifaa hivyo kubadilika kutoka kuwa zana za kuwaokoa wanajeshi hadi kuwa silaha za kupigana.

Chanzo cha picha, Getty Images, Devdroid
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Kuongezeka kwa matumizi ya intaneti ya satelaiti ya Starlink katika jeshi la Ukraine kumewezesha waendeshaji binadamu kudumisha mawasiliano ya kuaminika na UGVs kwa muda mrefu zaidi kuliko mifumo ya kawaida ya mawasiliano kwa redio, ambayo pia inaweza kuzuiwa.
Ingawa mfumo wa Starlink "hauwezi kuzuia kabisa" changamoto hizo, Tollast anasema uwezo wake wa kubadilisha kwa haraka masafa ya juu ya mawimbi umewezesha operesheni kama ile iliyofanyika nje ya Dobropillya.
Ukraine imekuwa na faida dhidi ya Urusi katika eneo hili tangu Februari 2026, wakati Starlink ilipozuia matumizi ya vituo vyake na jeshi la Urusi, ingawa Tollast anaonya kwamba hali hiyo inaweza kubadilika.
Urusi inashirikiana na China kutafuta njia za kuzuia huduma hiyo bila kutegemea vifaa vyake vya gharama kubwa vya kuzuia mawasiliano, ambavyo vina ukubwa wa lori na ambavyo waendeshaji wa ndege zisizo na rubani wa Ukraine wamekuwa wakiviharibu mara kwa mara katika miezi ya hivi karibuni.
Wakati huo huo, Ukraine imekuwa ikitafuta njia mpya za kutumia idadi inayoongezeka ya UGVs zake, ambazo sasa zinafikia maelfu kadhaa.
Tishio la roboti wenye miguu minne
Matumizi moja ya wazi ya roboti hao ni katika operesheni za mashambulizi. Mwezi Julai, jeshi la Ukraine lilifanikiwa kupeleka roboti aina ya ARK-1 iliyokuwa na bunduki ya mashine katika Kinburn Spit, eneo dogo linalogombaniwa na linalokaliwa na Urusi kusini mwa Mykolaiv.
Ingawa matokeo ya shambulio hilo bado hayajawekwa wazi, Tollast anatabiri kwamba Ukraine itafanya operesheni zaidi za aina hiyo katika miezi ijayo.
Je, roboti wenye umbo la binadamu wanaweza kuonekana hivi karibuni katika mstari wa mbele?
Tollast haamini hivyo, na jeshi la Ukraine linakubaliana naye. Linasema roboti hao ni wazito, ni ghali na mara nyingi huanguka.

Chanzo cha picha, Getty Images / Morris MacMatzen
Badala yake, roboti wenye miguu minne wana uwezekano mkubwa zaidi wa kutumika, anasema Tollast. Kinadharia, roboti hao wanaweza kusonga katika uwanja wa vita kwa urahisi zaidi – hali iliyowahi kuonyeshwa kwa kutisha katika kipindi cha Metalhead cha mwaka 2017 kutoka kwenye tamthiliya ya Black Mirror.
Mizinga isiyo na rubani pia ni uwezekano mwingine, anasema Tollast. Lakini maendeleo ya Ukraine katika kutengeneza UGVs yanaweza kuendelea kwa mafanikio ikiwa tu mawasiliano ya kuaminika yataendelea kuwepo kati ya waendeshaji binadamu na roboti walio uwanjani.
Iwapo China na Urusi watafanikiwa kupata njia za bei nafuu za kuzuia Starlink, basi kila kitu kinaweza kubadilika.
Suluhisho mojawapo linaweza kuwa kuifanya mitambo hiyo iwe na uwezo wa kufanya kazi kikamilifu bila kuongozwa na binadamu, kama inavyozidi kufanyika kwa baadhi ya UAVs zinazotumiwa na pande zote mbili katika vita hivi.
"Natarajia kwamba Ukraine itakuwa ikifanya kazi kwa bidii katika hili," anasema Tollast, "na huenda wakafanikiwa kutatua tatizo hilo kwa kiwango kikubwa."
Hata hivyo, hilo linaweza kuchukua muda. Ingawa gharama ya vihisio (sensors) vinavyohitajika kwa uongozaji wa kiotomatiki inapungua, lakini pia ndege zisizo na rubani zinazotumia mifumo ya kisasa zaidi ya kuona kwa kutumia mashine bado zinapata ugumu kupita katika maeneo yenye ardhi iliyochimbuliwa na kuharibiwa sana katika eneo lisilo na wanajeshi kati ya pande zinazopigana nchini Ukraine.
Kwa hiyo, huenda tukasubiri kwa muda kabla roboti hazijachukua nafasi ya wanajeshi vitani.
Tukitumaini kwamba njia pekee nyingine ya kufikia hilo si kuendelea kwa vita.














