Je, dunia kupoteza nguvu yake ya mvuto kwa sekunde saba?

Chanzo cha picha, Getty Images
Je, una mipango gani kwa ajili ya tarehe 12 Agosti, 2026? Ikiwa machapisho fulani ya mitandao ya kijamii yanaaminika, huenda ukahitaji kushikilia kitu kizito ili kuzuia siku yako kuharibika.
Nadharia ya siri inaenea mtandaoni ikidai kuwa siku hiyo, nguvu ya uvutano wa Dunia "itashindwa kufanya kazi" kwa sekunde saba kutokana na shughuli zinazohusiana na mashimo meusi (black holes).
Uvumi huo unahusishwa na madai kuhusu mpango wa siri wa NASA unaoitwa "Project Anchor" na maonyo kuhusu matokeo mabaya. Hata hivyo, NASA inasema madai haya si ya kweli.
Machapisho mengine yanadai kuwa ndani ya mfumo wa mpango huu, karibu dola bilioni 90 zimetumika kuzuia matatizo makubwa yanayoweza kusababishwa na kupotea kwa muda kwa nguvu ya uvutano au mvuto.
Ni nini kingetokea iwapo Dunia ingepoteza nguvu hizi?
Kulingana na tovuti ya How Stuff Works, iwapo nguvu ya uvutano ingetoweka, hata kwa muda mfupi tu, hakungekuwa na nguvu ya kushikilia watu, majengo, na hata hewa pamoja na maji juu ya uso wa Dunia.
Aidha, uharibifu na majeraha yangejitokeza, hasa wakati nguvu ya uvutano ingerejea na kila kitu kushuka tena chini dunian na yangekuwa ya kudumu na yasiyoweza kurekebishika kwa muda mrefu.
Je, Dunia itapoteza mvutano wake kwa sekunde saba?
Hakuna ushahidi wowote unaoonyesha kuwa Dunia itapoteza mvutano wake mnamo tarehe 12 Agosti. Pia, hakuna rekodi yoyote ya umma inayothibitisha kuwa NASA inafanyia kazi mpango unaoitwa "Project Anchor."
Huu ni mfano wa upotoshaji wa makusudi unaosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kwa lengo la kueneza habari za uongo.
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Inawezekana kuna mtu anajaribu kuharibu sifa ya NASA kwa kusambaza taarifa zisizo za kweli kuhusu shirika hilo.
Machapisho ya watu walioamini madai hayo na kuyasambaza wenyewe ni mfano wa upotoshaji unaoenea bila nia ya awali; yaani, usambazaji wa habari za uongo unaotokana na kutokujua ukweli.
Ili kufahamu zaidi kuhusu uhusiano wa Dunia na nguvu ya uvutano, BBC iliwasiliana na Kituo cha Uangalizi wa Anga cha Jodrell Bank huko Cheshire, ambacho ni maarufu kwa darubini yake kubwa ya mawimbi ya redio.
"Vitu huwa na nguvu ya uvutano kwa sababu vina masi," alieleza Lexie Southern, afisa elimu wa kituo hicho. "Kadiri kitu kinavyokuwa na masi kubwa, ndivyo nguvu yake ya uvutano inavyokuwa kubwa zaidi."
"Nguvu ya uvutano ya Jua ndiyo inayotawala mfumo wa jua na kuwezesha sayari kusalia katika njia zake za kuzunguka, kwa sababu Jua lina masi kubwa zaidi kuliko kitu kingine chochote katika mfumo wa jua."
"Nguvu ya uvutano inayohisiwa pia hutegemea umbali; kadiri unavyokuwa karibu na kitu, ndivyo unavyohisi nguvu kubwa zaidi ya uvutano. Hii ndiyo sababu nguvu ya uvutano kati ya Dunia na Mwezi huufanya Mwezi usalie katika njia yake ya kuzunguka Dunia, na nguvu ya uvutano ya Mwezi pia huathiri mawimbi ya bahari."
"Ili 'kuondoa' nguvu ya uvutano, ingebidi kuifanya Dunia na kila kitu kilichomo ndani yake visiwe na masi, na jambo hilo haliwezekani," alisema.

Chanzo cha picha, Getty Images
Ni nini hasa kitakachotokea tarehe 12 Agosti 2026?
Tukio la kiastronomia litatokea katika tarehe hii, lakini halihusiani hata kidogo na nguvu ya uvutano. Kupatwa kwa jua kwa ukamilifu kunatarajiwa kuonekana kutoka Bahari ya Aktiki, Greenland, Iceland, Bahari ya Atlantiki, Ureno na kaskazini mwa Uhispania.
Hakuna uhusiano wowote kati ya tukio hili la kupatwa kwa jua na madai kwamba nguvu ya uvutano itatoweka.
NASA ilieleza hivi: "Kupatwa kwa jua kwa ukamilifu hakuna athari yoyote isiyo ya kawaida kwa nguvu ya uvutano ya Dunia.
Nguvu ya uvutano ya Jua na Mwezi juu ya Dunia, ambayo haiathiri nguvu ya jumla ya uvutano wa Dunia bali huathiri nguvu zinazosababisha kupwa na kujaa kwa maji baharini, inajulikana vyema na inaweza kutabiriwa miongo kadhaa kabla."















