Njia tano ambazo wanaume wanaweza kutumia kuboresha uzazi wao

Chanzo cha picha, Getty Images
Ikija katika suala la kupanga kizazi, wengi huhusisha suala hilo la wanawake.
Wao huchukuliwa kama kupanga uzazi ni jukumu lao, na njia nyingi za kupanga uzazi hutumika na wanawake.
Ila wataalam wa afya wanadokeza kuwa kupanga uzazi pia kunahusisha wanaume ambao wanamchango mkubwa wa kuhakikisha wanawake hawapati ujauzito kwa kufuatanisha.
"Kupanga uzazi husaidia kulinda afya ya mama na mtoto, huku pia kukiwezesha familia kuwahudumia watoto wao kwa uangalifu na ubora zaidi," anaeleza Farida Abdullahi, muuguzi katika hospitali binafsi jijini Abuja, Nigeria.
Kulingana naye, ingawa njia nyingi za kupanga uzazi zimekusudiwa wanawake, wanaume pia wana chaguo zao na, muhimu zaidi, wanaweza kushiriki kikamilifu katika kufanya maamuzi kuhusu afya ya uzazi.
Muuguzi huyo anaelezea njia tano ambazo wanaume wanaweza kutumia katika upangaji uzazi.
Kumwaga mbegu za kiume

Farida Abdullahi anaeleza kuwa mojawapo ya njia zinazotumiwa na baadhi ya wanaume katika kupanga uzazi ni kutoa uume wao nje ya uke kabla ya kumwaga mbegu za kiume.
Kulingana naye, mbinu hii huhitaji kiwango kikubwa cha kujidhibiti na uwezo mzuri wa kutambua mapema wakati wa kumwaga mbegu za kiume.
Hata hivyo, anaeleza kuwa hii si njia ya kuaminika ikilinganishwa na njia nyingine za kupanga uzazi, kwa sababu ujauzito unaweza kutokea hata kama mwanaume atajitoa kabla ya kumwaga mbegu za kiume. Hii ni kutokana na uwezekano wa kuwapo kwa mbegu za kiume kwenye majimaji yanayotoka kabla ya kumwaga manii.
"Endapo mwanaume hawezi kujidhibiti kwa usahihi wakati wa kumwaga mbegu za kiume, kuna uwezekano mwanamke akapata ujauzito,"
Mpira za kondomu

Chanzo cha picha, Getty Images
Muuguzi huyo anaeleza kuwa matumizi ya kondomu ni miongoni mwa njia rahisi na zinazotumiwa kwa wingi zaidi na wanaume.
Anafafanua kwamba kondomu ikitumiwa kwa usahihi, huzuia mbegu za kiume kufika kwenye mfuko wa uzazi, hivyo kupunguza uwezekano wa kutokea kwa ujauzito.
Mbali na kuzuia ujauzito, kondomu pia zina mchango muhimu katika kuzuia maambukizi ya magonjwa mbalimbali ya zinaa.
Kutumia kalenda ya hedhi

Chanzo cha picha, Getty Images
Farida Abdullahi anaeleza kuwa njia ya kalenda ni mojawapo ya mbinu zinazotumiwa kupanga uzazi, lakini mafanikio yake hutegemea ushirikiano wa karibu kati ya wenzi wote wawili.
Njia hii inahusisha kufuatilia mzunguko wa hedhi wa mwanamke ili kubaini siku ambazo mayai yanarutubishwa na kipindi ambacho uwezekano wa kupata ujauzito huwa mkubwa zaidi. Katika kipindi hicho, wapenzi wanaweza kujizuia kufanya ngono au kutumia njia nyingine ya kujikinga, kama vile kondomu.
"Njia hii inamhitaji mwanamke kufuatilia kwa makini mzunguko wake wa hedhi, na huwa na ufanisi zaidi kwa wanawake wenye mizunguko ya hedhi iliyo ya kawaida," anaelezea.
Hata hivyo, mbinu hii inahitaji nidhamu, maelewano, na uvumilivu kutoka kwa wenzi wote wawili ili iweze kuwa na ufanisi wa kweli.
Kuhasi

Chanzo cha picha, Getty Images
Njia ya vasektomi au kuhasi uume, ni upasuaji mdogo unaofanywa kwa wanaume katika sehemu yao ya uzazi.
Baada ya upasuaji huo, mwanaume huendelea kumwaga manii kama kawaida wakati wa kujamiiana, lakini haziwezi kusababisha ujauzito.
Kinyume na imani potofu iliyoenea, vasektomi si lazima iwe ya kudumu katika kila hali. Katika baadhi ya visa, upasuaji wa kurekebisha mirija ya mbegu za kiume unaweza kufanyika ikiwa mwanaume anataka kurejesha uwezo wake wa kupata watoto.
"Vasektomi ni njia yenye ufanisi mkubwa katika kuzuia ujauzito, na kuna taratibu za kitabibu zinazoweza kuunganisha tena mirija ya mbegu za kiume endapo itahitajika," anaeleza.
Hata hivyo,Farida anaonya kuwa mafanikio ya upasuaji wa kurejesha uwezo wa kupata watoto hutofautiana kati ya mgonjwa mmoja na mwingine.
Kujizuia kushiriki ngono

Chanzo cha picha, Getty Images
Baadhi ya wenzi pia huchagua kujizuia kwa muda kufanya ngono ili kupanga uzazi.
Njia hii inahusisha kujiepusha na kujamiiana kwa kipindi maalumu ili kuzuia ujauzito. Haihitaji matumizi ya dawa wala kifaa chochote maalumu, bali hutegemea zaidi nidhamu na kujidhibiti kwa wenzi wote wawili.
Hata hivyo, njia hii inahitaji kuaminiana kwa kiwango kikubwa na kujitolea kwa pande zote mbili ili iweze kutekelezwa kwa ufanisi na kudumu.
Farida Abdullahi anaeleza kuwa kupanga uzazi na kuweka nafasi kati muda wa kupata ujauzito, si jukumu la wanawake pekee.
Kulingana naye, kushiriki kwa wanaume katika majadiliano na maamuzi yanayohusu uzazi wa mpango huchangia kuongeza uelewano na kufanya maamuzi ya pamoja ndani ya familia.
Upangaji uzazi ni muhimu kwa afya ya mama na mtoto, hasa katika kupunguza hatari ya matatizo yanayoweza kutokana na mimba zinazofuatana kwa karibu au kujifungua kabla ya wakati, huku pia ukiwezesha familia kuhakikisha ustawi bora wa watoto wao.













