Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Moja kwa moja, Marekani yaishambulia tena Iran, Tehran yajibu
Marekani imedai kuzuia mashambulizi ya Iran baada ya kudungua makombora ya balistiki na ndege zisizo na rubani zilizokuwa zikielekea Mlango wa Hormuz pamoja na nchi jirani za Ghuba ya Uajemi.
Muhtasari
- Iran yasema Marekani haina nia ya kumaliza vita
- Wanajeshi watatu wa Lebanon wauawa na Israel
- Ukraine yaishambulia mji wa St Petersburg nchini Urusi
- DRC yateua gavana mpya wa Ituri
- UAE yapiga marufuku wasafiri kutoka Uganda, DRC, Sudan Kusini kwa hofu ya Ebola
- Mlipuko wa Ebola huenda ukawa mkubwa kuliko ule uliotokea Afrika Magharibi mwongo mmoja uliopita
- DRC yatetea hatua yake ya kuwapokea wahamiaji kutoka Marekani
- Iran yakanusha kuitumia Lebanon kama ajenda kuu cha mazungumzo na Marekani
- Timu ya soka ya Iran yapokea viza za kuingia Marekani
- Putin akataa kukutana ana kwa ana na Zelensky
- Petro aishutumu Marekani kwa kuingilia uchaguzi wa nchi hiyo
- Iran ni nchi yenye kiburi- Trump
- Marekani yaishambulia tena Iran, Tehran yajibu
Moja kwa moja
Na Beldeen Waliaula
Iran yasema Marekani haina nia ya kumaliza vita
Wizara ya Mambo ya Kigeni ya Iran imelaani vikali mashambulizi ya Marekani dhidi ya "vituo vya rada katika eneo la Sirik na Kisiwa cha Qeshm," ikiyataja kuwa ni "ukiukaji wa usitishaji mapigano yaliyoafikiwa mwezi Aprili tarehe 10.”
Iran pia imetaja shambulio la Marekani kuwa “uchokozi.”
Taarifa ya wizara hiyo inasema kuwa “mashambulizi ya Marekani ni ishara kuwa taifa hilo limepuuza sheria za kimataifa na inamaanisha kuwa nchi hiyo haina nia ya kumaliza vita wala kuruhusu amani kurejea”
Iran imesisitiza ina haki ya kujilinda dhidi ya uchokozi wowote na kutaka mataifa Jirani za eneo hilo kuzingatia kanuni za ujirani mwema, na kutoruhusu adui kutumia ardhi yao kutekeleza mashambulizi.
Aidha, Kuwait na Bahrain zimeshtumu mashambulizi ya Iran yaliyolenga kambi za Marekani katika mataifa hayo.
Pia unaweza kusoma:
Wanajeshi watatu wa Lebanon wauawa na Israel
Jeshi la Israel IDF, limesema limeanzisha uchunguzi, baada ya kukiri kutekeleza shambulizi linalosemekana kuwauwa wanajeshi watatu wa Lebanon mapema leo asubuhi.
Jeshi la Lebanon limesema maafisa wawili wa polisi na mwanajeshi mmoja waliuawa katika shambulio lililolenga gari walimokuwa ndani.
Lebanon imetaja shambulio hilo kuwa “la kikatili”
Jeshi la IDF limesema kuwa gari hilo lilikuwa linaendeshwa llikielekea walikokuwa vikosi vya Israel kwa njia ya kutia shaka, na kuwalazimu vikosi hivyo kuwafyatulia risasi.
Israel na kundi la Hezbollah wamekuwa wakipigana kuanzia mwezi Machi kusini mwa Lebanon.
Pia unaweza kusoma:
Ukraine yaishambulia mji wa St Petersburg nchini Urusi
Mamlaka za Urusi zimesema Ukraine imetekeleza mashambulizi nchini humo kwa kulenga mji wa St Petersburg, kipindi ambacho mji huo ni mwenyeji wa mkutano wa kila mwaka wa uchumi.
Ndege zisizo na rubani zaidi ya 140 zimedunguliwa katika eneo la Leningrad, huku gavana wa mji wa St Petersburg akiwataka wakaazi wa mji huo kusalia majumbani.
Hii ni mara ya kwanza mji huo unapokea mashambulizi makali kutoka Ukraine tangu vita hivyo kuanza.
Mashambulizi haya yanajiri siku moja tu baada ya rais wa Urusi kusema kuwa haoni maana ya kukutana ana kwa ana na rais wa Ukraine kufanya mazungumzo.
Rais wa Urusi amesema wamelenga kambi za kijeshi na maghala za kuhifadhi silaha za Urusi.
Pia unaweza kusoma:
DRC yateua gavana mpya wa Ituri
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imemtua gavana mpya wa kijeshi kuongoza wilaya ya Ituri, mashariki mwa taifa hilo.
Wilaya ya Ituri kwa sasa ni kitovu cha mlipuko wa ugonjwa wa Ebola na pia inakumbana na utovu wa usalama.
Rais Felix Tshisekedi amemteua Meja Jenerali Kasongo Mulumba Batoka Gaby kuwa gavana wa Ituri na kumrithi Luteni Jenerali Johnny Luboya Nkashama.
Mabadiliko hayo yalitangazwa mapema leo katika televisheni ya kitaifa ya taifa hilo.
Jenerali Luboya amekuwa akiongoza wilaya ya Ituri kuanzia mwaka wa 2021, alipotumwa kudhibiti makundi yaliyojihami ambayo yalikuwa yanawahangaisha wakazi eneo hilo.
Gavana huyo mpya wa Ituri anachukua madaraka kipindi ambacho eneo hilo linapambana na mlipuko wa ugonjwa wa Ebola.
Kati ya visa 452 vya Ebola vilivyothibitishwa nchini DRC, 94% ya visa hivi vimetokea eneo la Ituri, huku watu 82 wakiripotiwa kufariki katika wilaya ya Ituri,Kivu kusini na Kivu Kaskazini.
Watu nane wameripotiwa kupona kutokana na ugonjwa huo
Pia unaweza kusoma:
UAE yapiga marufuku wasafiri kutoka Uganda, DRC, Sudan Kusini kwa hofu ya Ebola
Kulingana na taarifa ya pamoja ya Mamlaka ya Kitaifa ya Kukabiliana na Dharura na Majanga ya UAE (NCEMA) na Mamlaka ya Shirikisho ya Vitambulisho, Uraia, Forodha na Usalama wa Bandari (ICP), maagizo hayo yataanza kutekelezwa siku ya Jumamosi, Juni 6, 2026.
Kusitishwa kwa usafiri huu kutaathiri viza zote mpya, ikiwa ni pamoja na viza za kutembelea, na itaathiri Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Sudan Kusini, na Uganda.
"Hatua hizo ni sehemu ya jitihada ya UAE ya kuimarisha utayari wa kitaifa wa kukabiliana na virusi vya Ebola," mamlaka ya UAE ilisema, na kuongeza kuwa uamuzi huo unaweza kuongezewa muda.
Chini ya miongozo hiyo mipya, wasafiri wanaofika moja kwa moja kutoka mataifa matatu yaliyoorodheshwa, au wale ambao wamepitia mataifa hayo , watakataliwa kuingia UAE.
wale watakaoruhusiwa kuingia UAE ni ambao wametumia zaidi ya siku 21, nje a nchi zilizoathiriwa kabla ya kuwasili kwao.
Hata hivyo, shughuli za usafiri wa ndege kupitia UAE na safari za ndege za mizigo zitaendelea bila kukatizwa.
Mamlaka ya UAE ilibainisha kuwa wanafanya kazi na washirika wa kimataifa kufuatilia hali hiyo na watarekebisha vikwazo kulingana na tathmini zinazoendelea za hatari.
Pia unaweza kusoma:
Mlipuko wa Ebola huenda ukawa mkubwa kuliko ule uliotokea Afrika Magharibi mwongo mmoja uliopita
Shirika la Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) limesema kuwa kupitia utafiti wa kisayansi, iwapo hatua madhubuti hazitachukuliwa kwa haraka, mlipuko wa sasa wa Ebola aina ya Bundibugyo, unaweza kuenea na kuwa mkubwa kama,au hata kuzidi ule uliotokea Afrika Magharibi mwaka wa 2014 hadi 2016
Katika jarida lake la kila wiki la ‘Morbidity and Mortality Report’, CDC ilichapisha taarifa ikitoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kuwekeza rasilimali zaidi kudhibiti mlipuko huo.
Pia unaweza kusoma:
DRC yatetea hatua yake ya kuwapokea wahamiaji kutoka Marekani
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imesema kuwa mpango wake wa kupokea raia waliofurushwa kutoka Marekani kwa muda bado unaendelea, huku zaidi ya nusu ya waliowasili nchini humo tayari wameondoka na kurejea katika mataifa yao ya asili.
Katika taarifa iliyotolewa hii leo, serikali ya DRC imesema mpango huo wa kuwapokea wahamiaji ni wa muda mfupi, ikisisitiza kuwa unatekelezwa kwa mujibu wa sheria za nchi hiyo
Wizara ya Habari na Mawasiliano nchini DRC imesema kuwa kati ya wahamiaji 15 waliofika mjini Kinshasa tarehe 17 mwezi Aprili, wengi tayari wamerudi katika nchi zao za asili, na wengine wanatarajiwa kuondoka hivi karibuni.
Wahamiaji waliowasili Kinshasa waliripotiwa kutoka Colombia, Peru na Ecuador.
Kuwasili kwa wahamiaji hao mapema mwaka huu nchini DRC kulizua maandamano katika mji mkuu wa Kinshasa, huku vyama vya upinzani vikihoji kuhusu uwazi, usalama na uhuru wa taifa hilo.
Chama cha Ensemble pour la République kilikuwa miongoni mwa vilivyokosoa hatua hiyo, kikisema,“Serikali isiyoweza kudhibiti mipaka yake au kuwalinda raia wake ghafla inaweza kusimamia vituo vya kuwahifadhi raia wa kigeni."
Mnamo 2026, baadhi ya nchi za Afrika, zikiwemo Uganda, Ghana, Rwanda, Sudan Kusini na Eswatini, zilipokea au kukubali kupokea wahamiaji wasio na hati waliorejeshwa kutoka Marekani.
Pia unaweza kusoma:
Iran yakanusha kuitumia Lebanon kama ajenda kikuu ya mazungumzo na Marekani
Rais wa Lebanon Joseph Aoun amesema Iran inatumia taifa lake kama kigezo au kipengele cha majadiliano kati yao na Marekani.
Aoun amesema kwa sasa wanafanyia kazi sera itakayoitenga Lebanon na vita vyoyote vinavyoendelea eneo hilo la Mashariki ya Kati.
Rais huyo alisema “raia wa Lebanon ndiyo wanalipia gharama kubwa ya maslahi ya Iran, na tumechoka na vita kati ya Israel na Hezbollah”
Aoun alitoa onyo kwa Iran kutoingilia taifa lake na kuiambia Hezbollah kuwa njia pekee ya kumaliza vita na Israel ni kupitia diplomasia.
Rais huyo wa Lebanon aliiambia jeshi la Iran IRGC kuwa “hili si taifa lenu, ni letu, siyo jukumu lenu kuingilia taifa letu”
Akijibu mahojiano hayo ambayo rais wa Lebanon alifanya na shirika la habari la CNN, Waziri wa mambo ya kigeni wa Iran, Abbas Araghchi aliandika kwenye mtandao wa X kuwa,
“Kulingana na Aoun ni Iran imekalia kimabavu maeneo ya Lebanon,kuwahamisha robo ya raia wa taifa hilo na kutekeleza mashambulizi, Rais, ikomboe Lebanon kutoka kwa adui wake halisi”
Waziri huyo wa Iran alimwambia rais wa Lebanon kuwa iwapo Iran ingekuwa inaitumia taifa lake kama kipengele kikuu cha majadiliano basi wangekuwa tayari wameafikia makubaliano na Marekani.
Pia unaweza kusoma:
Timu ya soka ya Iran yapokea viza za kuingia Marekani
Timu ya taifa ya soka ya Iran imepokea viza za kuingia Marekani kabla ya mashindano ya Kombe la Dunia yatakayoanza wiki Ijayo
Vibali hivyo vimetolewa siku 10 tu kabla ya mechi yao ya kwanza dhidi ya New Zealand, inayotarajiwa kuchezwa Los Angeles tarehe 15 mwezi Juni.
Taarifa iliyotolewa na maafisa inasema “Viza zimetolewa kwa Iran kushiriki Kombe la Dunia, ikijumuisha wanamichezo na wasaidizi wao”
Taarifa hiyo iliongeza kuwa “Marekani haitaruhusu timu ya Iran kutumia mfumo huu kuingiza magaidi nchini Marekani kwa kisingizio cha uongo.”
Shirikisho la soka la Iran bado halijatoa taarifa rasmi kuhusu kupokea viza hizo.
Mashindano ya Kombe la Dunia 2026 yanatarajiwa kuanza tarehe 11 mwezi Juni, wenyeji wa mechi hizo wakiwa Marekani, Canada na Mexico.
Pia unaweza kusoma:
Putin akataa kukutana ana kwa ana na Zelensky
Rais wa Urusi, Vladimir Putin amesema haoni haja ya kukutana na rais wa Ukraine VlodymyrZelesnky, baada ya kiongozi huyo wa Ukraine kutaka kufanya mazungumzo ya ana kwa ana, ili kumaliza vita kati ya mataifa hayo mawili.
Zelensky alikuwa ameandika barua siku ya Alhamisi akitaka kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Putin akisema “ni vibaya kusubiria” vita hivi vilivyoanza na Urusi kuvamia Ukraine mwaka wa 2022 kuangaziwa ten ana Marekani.
Rais wa Ukraine pia alitaka kuwepo na usitishaji mapigano.
Putin alijibu barua hiyo akisema ni ya “kifedhuli” na kukataa kufanya mazungumzo ya ana kwa ana na Zelensky na kusisitiza kuwa mazungumzo lazima yafanyike kabla ya usitishaji mapigano.
“Sioni maana ya mkutano huo” Alijibu Putin alipoulizwa iwapo atakubali mwaliko wa Zelensky
Baada ya kuskia jibu la Putin, Zelensky alisema “Putin amechagua vita tena, hataki kumaliza vita, na dunia imesikitishwa na jibu lake”
Pia unaweza kusoma:
Rais wa Colombia, Petro aishutumu Marekani kwa kuingilia uchaguzi wa nchi hiyo
Rais anayemaliza muda wake nchini Colombia, Gustavo Petro, ameishutumu Marekani kwa kuingilia uchaguzi wa nchi hiyo baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kumuunga mkono mgombea wa mrengo wa kulia Abelardo de la Espriella.
Akizungumza na CBS News, Petro alisema uungwaji mkono huo kutoka kwa Trump ni kitendo cha kuingilia masuala ya ndani ya Colombia, wakati taifa hilo likijiandaa kwa duru ya pili ya uchaguzi wa urais, itakayofanyika wiki mbili zijazo.
Trump alionyesha wazi kumuunga mkono Abelardo de la Espriella kupitia mitandao ya kijamii na kusema matokeo ya uchaguzi huo ni muhimu kwa mustakabali wa Colombia na uhusiano wake na Marekani.
Petro amesema tofauti kati ya serikali yake na Washington zinatokana na misimamo ya kisiasa, akidai Marekani imekuwa ikiipinga serikali yake kwa sababu ni ya mrengo wa kushoto.
Kauli hizo zinakuja huku ushindani mkali ukiendelea kati ya mgombea huyo wa mrengo wa kulia na seneta wa mrengo wa kushoto, Iván Cepeda, kuelekea uchaguzi wa marudio nchini Colombia.
Iran ni nchi yenye kiburi- Trump
Rais wa Marekani, Donald Trump, amesema Iran bado haijakubali makubaliano yaliyopendekezwa na Washington kwa sababu ni nchi yenye “nguvu” na “kiburi” na ndiyo maana sio rahisi kwao kukubali matakwa ya Marekani.
Trump alisema hayo akijibu maswali ya wanhabari.
Aidha kiongozi huyo aliongezea kuwa Iran imebakisha takriban 22% ya akiba yake ya makombora, na Marekani inaufahamu wa maeneo yaliyoko makombora hayo yaliyosalia pamoja na ndege zisizo na rubani.
Rais huyo wa Marekani alisema vituo vingi vya kutengeneza makombora, na maeneo ya kurushia silaha nchini Iran vimeharibiwa, ingawa Iran bado ina idadi fulani ya makombora na ndege zisizo na rubani.
Trump alikiri kuwa kuafikia makubaliano na Iran imekuwa jambo gumu ila bado anamatumaini la hilo kutokea.
Pia unaweza kusoma:
Marekani yaishambulia tena Iran, Tehran yajibu
Jeshi la Marekani limesema limedungua ndege nne zisizo na rubani za Iran zilizokuwa zikielekea Mlango bahari wa Hormuz, na kudai kuwa yalikuwa tishio la moja kwa moja kwa usafiri wa majini eneo hilo na mataifa mengine ya Ghuba ya Uajemi.
Kituo kikuu cha kuendesha oparesheni za Marekani za Kijeshi (CENTCOM) imesema kuwa baada ya kudungua ndege hizo, vikosi vya Marekani vilishambulia vituo vya rada za ufuatiliaji vya Iran katika eneo la Goruk na Kisiwa cha Qeshm ili kuzuia mashambulizi zaidi.
Iran ilijibu hatua ya Marekani kwa kurusha makombora ya balistiki na kulenga kambi za kijeshi za Marekani zilizoko Kuwait na Bahrain.
CENTCOM imesema kati ya makombora saba ya Iran yaliyolenga nchi hizo mbili za Ghuba, sita yalidunguliwa huku moja haikufikia lengo lake.
Pia unaweza kusoma:
Hujambo na karibu katika matangazo yetu ya moja kwa moja