Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Kutoka kivuli hadi alama ya nguvu duniani, Putin alijengaje taswira yake?
Katika miaka yake yote akiwa Rais wa Urusi, Vladimir Putin amekuwa akitambua daima nguvu ya taswira na picha katika vyombo vya habari.
Mara ya kwanza nilipomhoji mwaka 2001, muda mfupi kabla kamera hazijaanza kurekodi, mmoja wa wasaidizi wake alisogea ghafla mbele na kuondoa bilauri ndogo za maji zilizokuwa mezani mbele yetu.
Nilimuuliza, "Kwa nini umefanya hivyo?"
Akanijibu:
"Hatutaki mtu yeyote afikirie kwamba kulikuwa na vodka ndani yake. Na hatuwezi kuhatarisha bilauri kumwagika mezani wakati wa matangazo ya moja kwa moja. Televisheni ni kama bomu la nyuklia kwa upande wa utangazaji na athari zake."
"Kila mtu nchini Urusi, na hasa Putin, alielewa kwamba televisheni ndiyo ilikuwa ufunguo wa kuimarisha mamlaka," anasema Peter Pomerantsev, mwandishi na mchambuzi wa masuala ya kisiasa.
Kwa miaka mingi, Vladimir Putin ameibadilisha Urusi kutoka taifa lenye demokrasia changa na dhaifu kuwa dola yenye mfumo wa kiutawala wa kimabavu ambao kwa kiasi kikubwa umejengwa kumzunguka yeye kama rais. Wakati huo huo, amejibadilisha pia kwa namna kubwa na ya kuvutia.
Picha za utotoni na ujana wake zinaonesha alikuwa mwembamba, mwenye haya, na asiyeipenda sana kamera. Lakini ni kwa namna gani mtoto huyu aliyeonekana mtulivu na mwenye kujitenga, pamoja na kuwa mtumishi wa kawaida wa serikali, alikuja kuwa rais anayependa sana kuwa katikati ya uangalizi wa Umma na vyombo vya habari?
Zao la televisheni
Mapenzi yake kwa nguvu ya taswira na picha yaliibuka muda mrefu kabla hajafika madarakani. Kama vijana wengi wa miaka ya 1960 na 1970, Vladimir Putin alikuwa mtoto wa enzi ya televisheni.
Watu aliowaona kama mifano ya kuigwa walikuwa majasusi waliokuwa wahusika wa vipindi maarufu vya televisheni na filamu za Kisovieti.
Kwa mujibu wa maelezo yake mwenyewe, mawakala hao wa siri waliokuwa watulivu lakini wenye nguvu, waliopambana dhidi ya maadui wa dola ya Kisovieti, walimhamasisha kujiunga na KGB, shirika la ujasusi la Umoja wa Kisovieti.
Aliepuka kuwa kitovu cha uangalizi wa umma wakati wa utumishi wake katika KGB na baadaye alipokuwa mtendaji wa chama aliyekuwa na nidhamu na mwaminifu.
Lakini alipokuwa rais wa mpito ghafla mwaka 1999 na kisha kuchaguliwa rasmi kuwa rais miezi michache baadaye, yeye na washauri wake wa kampeni walionesha wazi kwamba walielewa vizuri umuhimu wa taswira katika kujenga sura ya kisiasa ya rais.
Sehemu ya mchakato huo wa kujenga taswira ilikuwa kuondoa chochote ambacho kingeweza kumharibia sifa au kumletea taswira hasi. Ndiyo maana Vladimir Putin alionekana kana kwamba hanywi pombe kabisa.
Katika mikutano ya kila mwaka ya Valdai Discussion Club, ambapo wageni walihudumiwa divai za hali ya juu, kwa kawaida yeye alitosheka na kikombe cha chai chenye asali.
Kila mara alipokunywa pombe, watu waliokuwa karibu naye walijitahidi kuficha jambo hilo.
Wakati mmoja nilikutana na msimamizi wa jumba la makumbusho ambaye aliniambia kwamba yeye na rais walikula blini (aina ya chapati nyembamba za Kirusi), zikiwa zimeongezewa kiasi kidogo cha vodka ili kuongeza ladha.
"Lakini usimwambie mtu yeyote," alinisihi. "Walikuwa makini sana kuhusu mambo kama haya. Yangeweza kuniletea matatizo makubwa."
Sehemu nyingine ya kampeni hiyo ya kujenga taswira ilikuwa kusambaza mara kwa mara ujumbe kwamba Vladimir Putin hakuwa kabisa kama mtangulizi wake, Boris Yeltsin.
Yeltsin alikuwa mwanasiasa ambaye tabia zake za hadharani akiwa amelewa ziliwashtua na kuwaaibisha Warusi wengi. Hivyo, taswira ya Putin iliundwa kwa makusudi ili kumwonesha kama kiongozi mwenye nidhamu, mwenye kujidhibiti, na tofauti kabisa na mtangulizi wake.
Vladimir Putin alipiga picha akiwa ameketi kwenye sehemu ya kuongozea ndege ya kivita huku akiwa amevaa kofia ya rubani, na pia akaonesha ustadi wake wa mchezo wa judo. Yote haya yalilenga kuwasilisha ujumbe kwamba yeye ni mtu mwenye nguvu, afya njema na uwezo wa vitendo, si mgonjwa au mraibu wa pombe.
Labda mfano maarufu zaidi ulikuwa mfululizo wa picha zilizoanza kutolewa mwaka 2007, zikimuonesha akiwa hana shati, akiendesha farasi kama toleo la Kirusi la "Marlboro Man", au akivua samaki mtoni, au akionesha misuli yake alipokuwa akiogelea kwa mtindo wa kipepeo.
Je, picha hizi zilikuwa za kuchukuliwa kwa uzito? Au kulikuwa na aina fulani ya ucheshi wa makusudi ndani yake?
Peter Pomerantsev anaamini kwamba watu waliokuwa wakisimamia kampeni ya kujenga taswira yake walijua vizuri kabisa walichokuwa wakifanya.
"Kwa kundi moja la watazamaji, picha hizi zilionekana za juu juu na hata za kukera, lakini ziliwasilishwa kwa namna ya kejeli ili ziwe na mvuto fulani," anasema.
"Kwa kundi jingine, ujumbe ulikuwa kwamba Urusi inapaswa kuongozwa na shujaa wa jadi na mtu mwenye nguvu."
Putin alikuwa akicheza nafasi ya jadi sana ya kiongozi wa Kisovieti, lakini alikuwa akiifanya katika enzi ya vipindi vya reality show na MTV," anaongeza.
"Putin ni mtu anayebuni na kuanzisha mitindo," anasema Fiona Hill, mtaalamu wa masuala ya Urusi na mshauri wa marais wa Marekani. "Ameunda taswira ya rais wa kwanza wa mrengo wa umaarufu wa kisiasa (populist) na mtu wa kwanza mwenye nguvu aliyepata kuabudiwa katika karne ya 21."
Bila shaka, Vladimir Putin alikuwa akituma ujumbe tofauti kwa hadhira tofauti. Kwa ulimwengu wa nje, lengo lilikuwa kuonesha kwamba Urusi haikuwa tena taifa dhaifu, bali ni nguvu ambayo lazima ichukuliwe kwa uzito au kama alivyowahi kusema, dubu mwenye meno makali na makucha makubwa.
Maonesho mengine ya kuvutia yalikuwa ya ajabu zaidi, labda yakionesha yule mvulana wa shule wa Leningrad aliyepata nafasi ya kutimiza ndoto zake za utotoni: kuzama katika Bahari Nyeusi ili "kugundua" vitu vya kihistoria ambavyo tayari vilikuwa vimewekwa huko, kuruka kwa glider yenye injini pamoja na ndege korongo walio katika hatari ya kutoweka, au kucheza na mtoto wa simbamarara wa Siberia.
Putin mwenyewe alidai kwamba madhumuni ya shughuli hizo yalikuwa kuongeza uelewa wa umma kuhusu masuala ya mazingira na sayansi.
Lakini je, alijua kwamba maonesho hayo wakati mwingine yalikaribia kuwa ya kujifanyia mzaha mwenyewe?
Au labda hakuna mtu aliyekuwa karibu naye aliyethubutu tena kumwambia jambo kama hilo?
Au huenda hakujali tena maoni ya watu wengine kumhusu?
Kuendelea kujijenga
Picha za awali za Vladimir Putin, ikiwa ni pamoja na ile iliyoko kwenye kitambulisho chake cha Stasi mwaka 1985, zinaonesha kwamba nyuma ya uso huo baridi usio na hisia kulikuwa na azma thabiti ya chuma; ukimya wa makusudi na kujizuia ambao bila shaka ulifaa kwa wakala wa KGB, na ambao uliimarishwa zaidi kupitia mafunzo yake ndani ya shirika hilo.
Baada ya kuanguka kwa Umoja wa Kisovieti mwishoni mwa mwaka 1991, Vladimir Putin alijijenga upya kama afisa wa umma mwenye sifa ya uaminifu na ufanisi, akianza kama naibu meya wa St. Petersburg na baadaye, baada ya kuhamia Moscow, katika serikali ya Boris Yeltsin.
Katika picha za kipindi hicho, kwa kawaida huonekana akiwa pembezoni mwa picha au mwisho wake; akiwa haangalii kamera wala si kiini cha uangalizi.
Nina Khrushcheva, ambaye ni mzao wa kiongozi wa zamani wa Kisovieti Nikita Khrushchev, anasema aliambiwa katika miaka ya 1990 kwamba ndani ya duru za KGB, Putin alikuwa akiitwa jina la utani "Willow", mtu ambaye aliweza kujificha popote, mtu wa kivuli.
Lakini alipokuwa rais, hadithi hiyo ilibadilika kabisa na akaonekana kukaribisha nafasi ya kufanya majukumu tofauti.
Miaka michache baadaye, alipopigwa picha kwa ajili ya jarida la Time katika "Mtu wa Mwaka" wa 2007, alijiegemeza nyuma kwenye kiti chake kwa hisia za asili na kumtazama moja kwa moja mpiga picha, kama mfalme (tsar) aliyeketi kwenye kiti cha enzi au mkuu wa genge la kihalifu.
"Alikuwa akionesha nguvu kwangu," anasema mpiga picha wa Time aliyepiga picha hiyo, Platon. "Kwa kadiri ninavyojua, Putin anapenda picha hizi. Wafuasi wake wengi pia wanazipenda. Zinamuonesha kama mzalendo thabiti."
Mtu aliyevaa kinyago
Picha maarufu za Vladimir Putin akiwa hana shati mara nyingi zimefasiriwa kama ishara ya kujiamini kwake. Hata hivyo, huenda pia zinaonesha wasiwasi wake, na hamu ya kuwahakikishia wengine na hata yeye mwenyewe, kwamba bado ndiye mtu aliye madarakani, mwenye nguvu na uwezo kama zamani.
Baada ya kuachia urais kwa miaka minne mwaka 2008 na kuwa waziri mkuu, picha hizo za hadhi ya juu pia zilikuwa zikituma ujumbe kwamba nguvu halisi ya nchi bado ilikuwa mikononi mwake, si mikononi mwa rais wa wakati huo, Dmitry Medvedev.
Mwaka 2011, mabadiliko makubwa ya muonekano wake yalitokea, ambayo pia yaliashiria mabadiliko katika safari yake ya kisiasa.
Vladimir Putin alijitokeza hadharani akiwa na uso uliojaa zaidi, wenye uvimbe na usiosogea kwa urahisi, mabadiliko yaliyowaacha wengi wakiwa na maswali.
Je, uvimbe huo ulikuwa ishara ya matumizi ya dawa za cortisone kwa ajili ya hali fulani ya afya? Au alikuwa akitumia Botox kupambana na kuzeeka na kulegea kwa ngozi ya uso?
Miezi michache baadaye, aligombea urais tena. Matokeo ya uchaguzi yalikuwa karibu yamekwisha kujulikana, lakini katika mkutano wa kusherehekea ushindi wake, machozi yalimtoka usoni mwake, uso mpya uliokuwa umebadilika.
Niliona kwamba hiki kilikuwa kilio cha kweli. Sauti yake pia ilikuwa imejaa hisia. Alionekana amepata nafuu kwamba kila kitu kilienda kama kilivyopangwa, baada ya maandamano makubwa yaliyotokea kabla ya uchaguzi, ambapo waandamanaji walikuwa wakipiga kelele za kumkosoa kwa ujasiri ambao haujawahi kuonekana hapo awali.
Hata hivyo, baadhi ya wachambuzi wanaamini kwamba huenda hii ilikuwa mojawapo ya maonesho yake yaliyopangwa kwa makusudi; jaribio la kuibua taswira ya kidini ya sanamu takatifu zinazotoa machozi na kuingiza hisia kwamba yeye ni mwokozi mtakatifu wa Urusi.
Chochote kilichokuwa, ule wakati ulikuwa wa kihistoria na muhimu sana. Kwa miaka mingi, udhibiti wake juu ya nchi ulikuwa ukiongezeka taratibu. Kuanzia hapo, upinzani wa hadharani haukuwa tu unakatishwa tamaa, bali ulikuwa karibu kuwa haramu kabisa. Vladimir Putin alizidi kuwa kiongozi wa kimabavu, na Urusi ikawa na uvumilivu mdogo zaidi kwa sauti za upinzani.
Nadezhda Tolokonnikova, mwanachama wa kikundi cha kifeministi cha Pussy Riot ambaye alifungwa gerezani kwa maandamano yake na baadaye kutajwa kama "wakala wa kigeni," anaeleza mabadiliko hayo:
"Putin alizama katika wazo la kutaka kuacha jina lake katika historia kama mwokozi, si tu wa Urusi bali wa dunia nzima. Na huo ndio ulikuwa mabadiliko muhimu yaliyomgeuza kuwa Putin tunayemfahamu leo."
Sasa akiwa na umri wa miaka 73, Vladimir Putin yuko karibu na wakati wa kukabidhi madaraka kuliko alivyokuwa mwaka 1999, lakini uwepo wake wa hadharani umepungua.
Wengi wanaamini kwamba katika miaka ya hivi karibuni, hasa baada ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine na janga la COVID-19, Vladimir Putin amezidi kuwa na mashaka na wasiwasi. Sasa kila anapoonekana kwenye kamera, kila kitu hupangwa kwa uangalifu na kudhibitiwa, kana kwamba anataka kudumisha umbali wake na ulimwengu wa nje.
"Ni wazi kwamba anataka kuwa makini ili wengine wasiweze kumfuatilia kwa urahisi," anasema Fiona Hill. "Tabia hii inaonesha mtu aliyekuwa nyeti na mwenye mashaka kuhusu usalama wake binafsi, iwe ni kutokana na vijidudu au hofu ya jaribio la kumuua."
Vita nchini Ukraine sasa viko katikati ya utambulisho wake wa kisiasa. "Tukirudi kipindi cha mwaka 2012, Putin aliporudi Kremlin, bado hakujua hasa yeye ni nani au jukumu lake ni nini," anasema Mikhail Fishman. "Lakini sasa anaamini hatimaye amepata jukumu lake; na jukumu hilo ni vita."
Hata hivyo, zaidi ya miaka minne baada ya kuanza kwa vita dhidi ya Ukraine, vita hivyo pia vimekuwa mzigo. Kuendeleza vita kunazidi kuwa vigumu, na kukimaliza kunahusisha hatari kubwa. Vladimir Putin ameunda mashine ya vita ya kiuchumi na kijeshi, pamoja na mfumo wa ukandamizaji wa ndani, ambao hawezi kuusimamisha au kuubadilisha bila kuhatarisha nafasi yake mwenyewe.
Sasa, robo karne baada ya kuingia madarakani, anaonekana kuwa mbali na asiyeweza kubadilika, kana kwamba amenaswa katika mtego alioujenga mwenyewe.
Taswira hii iko mbali kabisa na ile ya mwanariadha mwenye nguvu na shujaa wa matukio aliyewahi kutamani iwe ndiyo inayomfafanua.