Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Je, vita vya Iran viliimarisha vipi Ukraine?
Wakati Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, akiwa na sura ya kijasiri ndani ya mavazi meusi, akitembea kwenye zulia la rangi ya nyekundu nchini Saudi Arabia mwezi Machi, tukio hilo liligeuka kuwa la maana katika vita kati ya Marekani na Israel dhidi ya Iran jambo ambalo halikutarajiwa kwa kiasi fulani.
Aliandika katika ujumbe kwenye X-Net kwamba lengo la safari hiyo ni "kuimarisha ulinzi wa maisha ya binadamu."
Bw. Zelensky, ambaye amelemewa na vita kati ya nchi yake dhidi ya Urusi, alitumia fursa hiyo kusafiri kwenda nchi za Ghuba ya Uajemi, akionyesha hadharani thamani ya kimataifa ya Ukraine na uwezo wake wa kutoa uzoefu wa kijeshi katika uwanja wa vita, hasa katika matumizi ya ndege zisokuwa na rubani.
Ukraine inasema imesaini makubaliano na Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu na Qatar nchi ambazo zimekuwa zikilengwa na makombora kutoka Iran katika wiki za hivi karibuni ili kushirikiana utaalamu na teknolojia ya ndege zisizokuwa na rubani.
Hatua hiyo itasaidia kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na pia kuwa na faida za kibiashara. Kyiv ina matumaini kuwa hatua hii itasababisha mikataba zaidi ya ulinzi na washirika matajiri wa Marekani.
"Tunahitaji kuwasaidia [mataifa ya Ghuba] kujilinda, na tutaendelea kujenga ushirikiano wa aina hii na nchi nyingine," alisema Bw. Zelensky.
Mwanzoni, athari za mgogoro wa Iran kwa Ukraine zilionekana kuwa hasi kwa kiasi kikubwa. Kulikuwa na hofu kwamba vita hiyo ingemfanya Donald Trump kupunguza umakini wake kwa Ukraine.
Bw. Trump mwenyewe alikuwa akisita kujaribu kupatanisha kati ya Moscow na Kyiv, huku tishio jingine likiwa ni kupanda kwa bei ya mafuta kungeathiri zaidi katika vita dhidi ya Urusi.
Moscow imeweza kuuza mafuta zaidi kwa nchi nyingi kwa bei ya juu zaidi, kwa sababu meli zinazobeba mafuta kutoka Mashariki ya Kati haziwezi tena kupita katika Mlango wa Hormuz, unaopakana na Iran, ili kufikia masoko ya dunia.
Bw. Trump pia ameongeza muda wa msamaha unaoruhusu nchi kununua mafuta ya Urusi yaliyo chini ya vikwazo, hata wakati gharama duniani kote zimekuwa zikiongezeka kwa kasi.
Kadiri Urusi inavyopata fedha zaidi, ndivyo vita nchini Ukraine vinaweza kuendelea kwa muda mrefu zaidi na, kinadharia, kuwa vikali zaidi.
Lakini Kyiv imekuwa ikipinga mara kwa mara utabiri wa kimataifa tangu uvamizi wa Urusi mwezi Februari 2022.
Na sasa imefanya hivyo tena: kwa kutumia busara ili kukabili athari za vita ya Iran ziwe kwa faida yake, huku ikijaribu kujiweka katika nafasi imara zaidi iwezekanavyo kabla ya mazungumzo ya amani yanayoweza kufanyika na Urusi.
Donald Trump hivi karibuni alisema kwamba ana imani kuwa "suluhisho" kuhusu Ukraine litapatikana "kwa muda mfupi" baada ya mazungumzo "mazuri sana" na Vladimir Putin. "Nadhani baadhi ya watu wamemfanya iwe vigumu kwake," aliongeza.
Hii si mara ya kwanza kwa Donald Trump kutoa kauli chanya kuhusu Bw. Putin, hata wakati ambapo kwa njia ya wazi au ya ishara amekuwa akimkosoa kiongozi wa Ukraine kwa kukataa kukubali usitishaji wa mapigano.
Hata hivyo, bado hakuna "suluhisho" lililofikiwa.
Wakati huo huo, Volodymyr Zelensky ameendelea kuangazia kuimarisha nafasi ya Ukraine. Ujanja wa kisiasa unaweza kuchukuliwa kama moja ya silaha zake kuu.
Alisema Saudi Arabia, ambayo aliitembelea tena mwezi Aprili, inakabiliwa na aina ile ile ya mashambulizi ya makombora ya balistiki na ndege zisizokuwa na rubani kutoka Iran, sawa na yale ambayo Urusi inafanya dhidi ya Ukraine.
Moja ya silaha muhimu za Moscow ni mashambulizi ya masafa marefu, ya gharama nafuu aina ya Shahed-136 iliyotengenezwa na Iran.
Nchi hiyo pia ina toleo lake lililoboreshwa na la gharama kubwa zaidi la Urusi.
Wakati kila shambulizi moja la aina hiyo linagharimu kati ya dola 80,000 na 130,000, Bw. Zelensky anasema inaweza kudunguliwa kwa kutumia mifumo inayogharimu takribani dola 10,000 tu, ambayo ni nafuu sana ukilinganisha na makombora ya kawaida ya ulinzi wa anga yanayogharimu mamilioni ya dola.
Mwezi Aprili, Ukraine ilisaini mikataba miwili mikubwa ya ushirikiano wa ulinzi na washirika wake wa Ulaya: mmoja na Norway wenye thamani ya dola bilioni 8.6 kama sehemu ya mpango wa msaada wa dola bilioni 28 hadi mwaka 2030, na mwingine na Ujerumani, ukihusisha "aina mbalimbali za ndege zisizokuwa na rubani, makombora, programu za kompyuta, na mifumo ya kisasa ya ulinzi" wenye thamani ya dola bilioni 4.7.
Bw. Zelensky pia alieleza matumaini yake kuwa nchi za Ghuba zitasaidia kulinda Ukraine dhidi ya Urusi.Hasa kwa kuwa kwa sasa Marekani ina silaha chache za kuuza Ulaya ili kusaidia Ukraine kutokana na kutumia rasilimali zake huko Mashariki ya Kati.
Alipoulizwa kuhusu kuelekeza upya usafirishaji wa silaha, Bw. Trump alisema: "Tunafanya hivyo mara kwa mara. Wakati mwingine tunachukua kutoka sehemu moja na kutumia sehemu nyingine."
"Tunataka pia nchi za Mashariki ya Kati zitupatie nafasi ya kuimarisha uwezo wetu. Wana makombora ya ulinzi wa anga ambayo sisi hatuna ya kutosha. Lengo letu ni kufikia makubaliano kama hayo," Bw. Zelensky aliliambia gazeti la Ufaransa Le Monde.
Mashambulizi dhidi ya miundombinu
Ukraine pia imejifunza somo muhimu kutoka vita vya Iran: athari kubwa ya kushambulia miundombinu ya uuzaji wa mafuta ya adui.
Miundombinu ya nishati ya Urusi sasa imekuwa lengo kuu, na Ukraine inatumia ndege zisizokuwa na rubani za masafa marefu zinazotengenezwa nchini humo kushambulia maeneo hayo.
Kwa mujibu wa Bw. Zelensky, Urusi imepata "hasara kubwa muhimu" zenye thamani ya mabilioni ya dola katika sekta yake ya nishati, licha ya kupanda kwa bei ya mafuta duniani hivi karibuni.
Takwimu za mauzo ya mafuta zinaonyesha kuwa kupanda kwa bei pamoja na kulegezwa kwa vikwazo vya Marekani dhidi ya wanunuzi wa mafuta ya Urusi kulifanya mapato ya Moscow katika wiki ya tatu ya vita vya Iran kuwa mara 2.3 zaidi ya kiwango cha Desemba hadi Februari.
Hata hivyo, katika wiki ya nne, mashambulizi ya ndege zisokuwa na rubani ya Ukraine dhidi ya miundombinu ya nishati ya Urusi yalipunguza mapato ya nchi hiyo kwa dola bilioni 1, na kufuta takribani theluthi mbili ya faida iliyopatikana wiki iliyotangulia.
Je ni ishara ya kutoheshimu?
Lakini hali ya mazungumzo ya kuanzisha usitishaji wa mapigano wa kudumu ipo vipi? Urusi na Ukraine zote zimetangaza kwamba zitazingatia usitishaji wa mapigano tofauti na wa upande mmoja katika siku zijazo.
Kabla ya Krismasi, utawala wa Bw. Trump ulikuwa ukizungumzia sana mazungumzo haya. Bw. Trump alirudia mara kwa mara kabla ya kuchaguliwa kwake tena kwamba angeweza kumaliza vita vya Ukraine ndani ya saa 24. Hata hivyo, sasa akiwa madarakani, hali halisi haijaendana na ahadi zake.
Dalili muhimu ni mienendo ya wajumbe wake wa amani, Jared Kushner, mkwe wake, na Steve Witkoff, ambaye ni mfanyabiashara wa zamani wa mali isiyohamishika. Ziara yao kwenda Kiev imekuwa ikiahirishwa mara kwa mara na kwa sasa wameelekeza zaidi nguvu zao katika Mashariki ya Kati.
Bw. Zelensky ameuita kutofika kwao kuwa ni "kutoheshimu." Anasema mazungumzo ya amani yanaendelea katika ngazi ya "kiufundi," lakini ana wasiwasi kwamba maendeleo ya kweli hayatapatikana hadi vita vya Iran vitakapomalizika.
Ni muhimu kutambua kuwa Kushner na Witkoff hawajawahi kutembelea Kiev kwa uwezo rasmi wa kiserikali. Walikwenda Moscow mwishoni mwa mwaka uliopita wakati mazungumzo ya usitishaji vita vya Ukraine yalipoanza kupata msukumo, na tena mwezi Januari. Witkoff ametembelea Moscow mara nane; awali amefanya shughuli kubwa za kibiashara nchini Urusi bila rasmi na amekutana na Vladimir Putin mara kadhaa.
Utawala wa Trump umekanusha kuwepo kwa upendeleo wowote kwa Urusi.
Hata hivyo, Ukraine na nchi nyingine za Ulaya zilishangazwa na kutolewa kwa Mkakati wa Usalama wa Taifa wa Marekani mwishoni mwa mwaka uliopita. Hati hiyo haikutaja wazi Urusi kama tishio la kiusalama, tofauti kubwa na mtazamo wa washirika wa Ulaya wa NATO kuhusu Moscow.
Mkakati huo wa Marekani unasisitiza umuhimu wa kumaliza vita vya Ukraine, lakini lengo lake si kuleta amani ya kudumu kwa Kiev. Badala yake, lengo lililotajwa ni kuhakikisha "utulivu wa kimkakati" na hata uwezekano wa kushirikiana na Urusi, ili Marekani iweze kuelekeza rasilimali zake kwenye vipaumbele vingine.
Mwelekeo huu wa utawala wa Trump umepokelewa kwa furaha na Kremlin. Msemaji wa Kremlin, Dmitry Peskov, alisema wakati wa kutolewa kwa hati hiyo kwamba mkakati wa usalama wa Marekani "kwa kiasi kikubwa unaendana na mitazamo ya Moscow."
Chini ya Trump, Marekani imeshindwa kuweka au kudumisha vikwazo vikali vya kiuchumi dhidi ya Urusi ambavyo vingebadilisha hali na kuilazimisha Kremlin kufika mezani pa mazungumzo bila masharti ambayo Kiev au washirika wake wa Ulaya hawakubaliani nayo.
Zaidi ya hayo, msaada wa kijeshi na kiuchumi wa Marekani kwa Ukraine umepunguzwa karibu hadi kiwango cha chini sana. Badala yake, nchi za Ulaya zimekuwa zikinunua vifaa vya kijeshi kutoka Marekani ili kuvituma Kiev. Hata hivyo, njia hii ya usambazaji sasa iko hatarini kukatwa kufuatia mzozo wa Iran.
Mashaka ya Ukraine
Wakati Kiev ikiendelea kusubiri ushiriki wa moja kwa moja wa Marekani, maafisa wengi wa Ukraine kwa faragha wanatilia shaka kama Marekani chini ya Rais Donald Trump itawahi kuchukua hatua wanazotarajia kuhakikisha amani, au hata ikiwa usitishaji mapigano utapatikana, kama itaweza kutoa dhamana thabiti na za kuaminika za usalama ambazo zingezuia Urusi kurejea tena siku zijazo.
"Ni vigumu sana kufikiria aina ya dhamana za usalama ambazo Waukraine wataziona za kuaminika kiasi cha kutosha kusaini makubaliano ya amani, na ambazo Urusi, Marekani, na Ulaya zote zitakubali," alisema Mark Kansian, mshauri mkuu katika Kituo cha Mafunzo ya Kimkakati na Kimataifa.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Tom Keating, mkurugenzi wa Kituo cha Fedha na Usalama cha Taasisi ya Royal United Services, viongozi wa Ulaya ambao kwa kiasi kikubwa wanaamini kwamba ushindi wa Urusi nchini Ukraine baadaye ungekuwa tishio kubwa sana kwa usalama wa bara zima, "hawana muda wa kupoteza."
Tom Keating anasema kwamba licha ya vita vya Mashariki ya Kati, Trump ambaye anajulikana kwa kutokuwa na subira, anaweza kuacha ghafla kuangazia suala la Iran wakati wowote ikiwa kufikia makubaliano na Tehran kutakuwa kugumu.
Hapo basi anaweza kurudi haraka kwenye suala la vita vya Urusi na Ukraine. Ndiyo maana Keating anasisitiza kuwa Ulaya inapaswa kuchukua hatua madhubuti zaidi kuhusu Ukraine sasa kuliko ilivyofanya hadi sasa.
Wakosoaji kwa muda mrefu wamekuwa wakiwashutumu viongozi wa Ulaya kwa "kusimamia" tu vita badala ya kufuatilia kwa dhati amani ya Ukraine, kwa kurudia kauli ya "kadri inavyohitajika" katika msaada wao kwa Ukraine.
Licha ya hotuba zote, safari zote kwenda Kiev na fedha zote zilizotumika kununua silaha kwa Ukraine, inapofika hatua ya kuchukua msimamo mkali kweli—hasa kuweka vikwazo vya kiuchumi vinavyoweza kuwa na athari kubwa—"Wazungu wanasimama pembeni na kusubiri Wamarekani," alisema Bw. Keating. "Wako waangalifu sana, ilhali Umoja wa Ulaya ni eneo kubwa la biashara."
Brussels sasa inafanya kazi kwenye kifurushi chake cha 21 cha vikwazo dhidi ya Urusi. Lakini je, kuhusu euro bilioni 210 za mali za Benki Kuu ya Urusi zilizogandishwa ambazo EU inashikilia, hasa nchini Ubelgiji?
Viongozi wa EU, wakitaja changamoto za kisheria na za mikopo, wamekataa kutumia fedha hizo kusaidia Ukraine, badala yake wakatengeneza mkopo wa euro bilioni 90 unaotegemea walipa kodi wa Ulaya. Bw. Keating anasema viongozi wa Ulaya wangeweza kufanya zaidi kwa ufanisi dhidi ya Urusi. "Lakini ama hawako tayari au hawajaungana vya kutosha kuingia kikamilifu (kushinikiza kwa nguvu zote) kumaliza vita."
Viongozi wa Ulaya kwa dhati wanataka mwisho wa mateso nchini Ukraine na amani ya haki na ya kudumu katika mipaka yao, lakini wakati huo huo ukweli ni kwamba usitishaji mapigano nchini Ukraine utaibua maamuzi magumu yasiyo rahisi.
Nchi chache za Ulaya zinaunga mkono uanachama wa haraka wa Ukraine katika Umoja wa Ulaya kuliko inavyodhaniwa.
Katika kesi ya kile kinachoitwa "Muungano wa Wanaotaka," unaoongozwa na Ufaransa na Uingereza, ambao umeahidi kuwa "nguvu ya ulinzi" nchini Ukraine iwapo mapigano yatakoma, swali ni ni nchi zipi hasa zilizo tayari kutuma wanajeshi wa ardhini na kwa muda gani, hasa kama vikosi hivyo havitakuwa na msaada wa anga wa Marekani.
Wiki iliyopita, Donald Trump alielezea kile alichokiita uhasama kati ya Putin na Zelensky kuwa "kichekesho." Washington pia imepunguza umuhimu wa juhudi za Ukraine za kuuza teknolojia yake ya droni kwa nchi za Ghuba. Pia ofa ya wazi ya Zelensky kushirikisha ujuzi wa droni wa Kiev na serikali ya Marekani imepokelewa kwa tahadhari, angalau hadharani.
Hata hivyo, kiongozi huyo wa Ukraine anayejulikana kwa mavazi meusi anaonekana kutojali maelezo haya. Maadamu jina lake linaendelea kuonekana kwenye vyombo vya habari, anatumai kwamba Ukraine haitasahaulika na kwamba Washington itarudi tena hivi karibuni kuelekeza macho yake katika eneo hili la dunia.