Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mashambulizi ya makombora na 'hatari inayowakabili viongozi wa Iran'
"Tunafikia makubaliano kupitia makombora sio mazungumzo. Kwenye meza ya mazungumzo tunakuja kujadili kilichotokea. "Kauli hii ya kutisha ni mojawapo ya machapisho ya hivi punde zaidi ya mpatanishi mkuu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Mohammad Bagher Ghalibaf, kwenye mtandao wa kijamii wa X.
Siku za hivi karibuni lugha ya makabiliano na vitisho imeonekana kushamiri katika taarifa za maafisa wa Iran kuliko kuzingatia diplomasia na ''mazungumzo".
Uchunguzi wa matamshi ya maafisa wa kisiasa na kijeshi unaonyesha kuwa wanazidi kusisitiza hatua za kijeshi na makabiliano. Mohsen Rezaei, kamanda wa zamani wa IRGC na mshauri wa kijeshi wa Amiri Jeshi Mkuu, pia mara kwa mara amezungumzia uwezekano wa hatua ya tahadhari ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, na, kwa mujibu wa Mohammad Baqer Qalibaf: "Tutavunja kizuizi cha majini ima kwa mazungumzo au hatua ya moja kwa moja."
"Mazungumzo" ni mojawapo ya maneno yanayotumiwa mara kwa mara kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, sambamba na vita na usitishaji mapigano. Neno hilo limekuwa likitumika sana kiasi kwamba kwa baadhi ya watu limeibua neno duru nyingine ya mazungumzo kati ya Iran na mataifa ya Magharibi ambayo wakosoaji wameyataja kuwa ya matamshi yasiyo na tija.
Katika miaka iliyopita wakati Saeed Jalili alipokuwa mpatanishi mkuu wa nyuklia wa Iran chini ya Rais Mahmoud Ahmadinejad, maafisa wa Iran mara kwa mara walizungumzia kuhusu hatua zilizopigwa katika mazungumzo hayo, lakini mchakato huo wakati mwingine ulikwama na hata mara nyingine kufikia mkwamo.
Sasa, baada ya zaidi ya miongo miwili ya mazungumzo na kufuatia mizozo miwili ya kijeshi katika mwaka uliopita, majadiliano ya vita na mazungumzo yamekuwa yakizingatiwa zaidi kuliko hapo awali. Kiasi kwamba siku moja, uvumi kuhusu makubaliano na kuanza tena kwa mazungumzo yanafufuliwa, na saa kadhaa baadaye, maafisa kutoka pande zinazozozana wanazungumzia uwezekano wa ukiukaji wa makubaliano ya usitishaji mapigano, utayari wa kijeshi, na uwezekano wa mapigano kuzuka upya.
Masoko pia yanaonekana kunganyika na taarifa zinazojirudia kuhusu mazungumzo. Ingawa kauli za maafisa wakuu, akiwemo Donald Trump, bado zinaweza kuathiri soko la mafuta, thamani ya sarafu na bei ya dhahabu, kwani huathiriwa na taarifa kama vile "makubaliano yanakaribi kufikiwa". Hata hivyo, matukio yasiyotarajiwa au taarifa muhimu za maafisa wakuu bado zinaweza kusababisha mabadiliko makubwa.
Mazungumzo hayo yamekuwa na heka heka zake tangu kuafikiwa kwa makubaliano ya usitishaji vita wa wiki mbili Aprili 9. Lakini pengine muhimu zaidi kuliko mazungumzo yenyewe ni masimulizi yanayotofautiana na mitazamo tofauti ikiwa ni pamoja na: nani atatoa uamuzi wa mwisho, lengo halisi la mazungumzo hayo ni nini, na ni kwa kiasi gani Jamhuri ya Kiislamu ya Iran itakuwa tayari kuafikiana au kubadili misimamo yake.
Mazungumzo au "mapambano ya kimkakati''
Kile ambacho kimekuwa kikiendelea katika vyombo vya habari vya Iran na mitandao ya kijamii katika wiki za hivi karibuni kimetafsiriwa na baadhi ya waangalizi kama mfano wa "mapambano ya kimkakati." Katika wakati huu, vyombo vya habari vilivyo karibu na serikali na baadhi ya maafisa katika serikali ya Iran vimesisitiza kwamba Tehran haiko tayari kwa maelewano, bali iko katika nafasi ambayo inaweza kuwasilisha masharti yake yenyewe katika mazungumzo.
Ebrahim Azizi, Mkuu wa Kamati ya Usalama ya Kitaifa ya Bunge, aliandika kwenye Mtandao wa X mnamo Juni 29: "Trump anapaswa kujua kwamba Iran, kama mshindi na ataamua masharti (ya mazungumzo). Fedha za fedha, mkopo kwa mkopo, bila kwa bila.
Kipengee kingine muhimu kuhusu mazungumzo ni kuzingatiwa kwa "masharti ya uongozi", mistari nyekundu iliyowekwa na Mojtaba Khamenei. Hii inaashiria kuwa, sehemu kubwa ya matukio yanayoangaziwa katika vyombo vya habari ni ya kusistiza msimamo wa uongozi wa nchi kwamba ukiukaji wowote wa kile kilichofikiwa kwenye makubaliano unaweza kutafsiriwa kama "uvunjifu wa makubaliano" au "kuvuka mistari mwekundu."
Mahmoud Naboyan, mbunge wa kihafidhina na naibu mwenyekiti wa Tume ya Usalama ya Kitaifa, amekuwa mmoja wa watu walioweka bayana misimamo ya kuhusu suala hili. Ingawa maudhui ya mazungumzo hayo hayajatolewa rasmi, aliandika Juni 25 akijibu baadhi ya ripoti kuhusu mchakato wa mazungumzo: "Mkataba huu ni batili," na kuzingatia makubaliano yanayoweza kuwa kinyume na maslahi ya kitaifa ya Iran kutokana na "utata wa uondoaji wa vikwazo," "kushindwa kubainisha fidia," "masharti ya matumizi ya amani ya nyuklia," na "ukiukaji wa masharti ya uongozi."
Hisia hizi ziliongezeka baada ya baadhi ya vyombo vya habari kuchapisha orodha ya masharti yaliyohusishwa na Mojtaba Khamenei. Kulingana na ripoti hizi, alielezea matakwa ya serikali kabla ya kufikia makubaliano yoyote na Marekani na kwamba mazungumzo yanapaswa kujikita kwenye masuala hayo. Masharti yaliyotajwa ni pamoja na "kukubali urutubishaji" na "kuondolewa kabisa kwa vikwazo dhidi ya Iran," "kuondolewa kwa vikosi vya kijeshi vya Marekani kwenye eneo la ghuba," "kugharamia uharibifu wa miundombinu ya Iran," na "kusitishwa kwa vita pande zote, ikiwa ni pamoja na dhidi ya Hezbollah nchini Lebanon."
Baada ya ujumbe wa Iran unaoongozwa na Mohammad Baqer Qalibaf kuzuru Islamabad tarehe 11 Aprili na kufanya mazungumzo, baadhi ya wabunge na vyombo vya habari vilivyo karibu na Mrengo huo walidai kuwa, kinyume na "masharti" iyaliyowekwa katika kikao na wawakilishi wa Marekani, suala la nyuklia pia lilishughulikiwa. Tangu wakati huo, ukosoaji dhidi timu ya mazungumzo na watu kama Mohammad Baqer Qalibaf umeongezeka katika baadhi ya vyombo vya habari na ulingo wa kisiasa.
Majadiliano, vyombo vya habari na maoni ya umma
Tathmini ya vyombo vya habari vilivyo karibu na serikali inaonyesha kuwa vyombo hivyo vimeunga mkono kwa kiasi kikubwa mchakato wa mazungumzo na kuwasilisha taarifa zinazowiana na misimamo rasmi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Wakati huo huo, upinzani dhidi ya mchakato wa mazungumzo pia umeandaliwa haswa ndani ya mfumo wa masharti yaliyohusishwa na Mojtaba Khamenei na dhana kama vile "kukataa mfumo wa kutawala" na imejikita kidogo katika kurekebisha au kuboresha uhusiano na Marekani.
Kutokana na hilo katika wiki za hivi karibuni, vyombo vya habari, vimekuwa vikiwanukuu maafisa wa serikali, ikiwa ni pamoja na katika ujumbe mpya unaohusishwa na Mojtaba Khamenei siku ya Ijumaa, Juni 29, vikionya mara kwa mara dhidi ya "tofauti za kipuuzi za kisiasa," kuzua mgawanyiko," na "kudhoofisha uwiano wa kitaifa." Misimamo hii, pamoja na msisitizo wa kudumisha uwiano wa ndani, imeathiri wigo wa majadiliano ya umma kuhusu mazungumzo na Marekani. Katika hali hiyo, utangazaji wa mitazamo tofauti juu ya kuendelea kwa mivutano au njia ya mazungumzo katika vyombo vya habari ndani ya Iran inaonekana kuwa na mipaka zaidi.
Udhibiti wa vyombo vya habari na nafasi ya kisiasa pia umefanya kuwa vigumu kutathmini maoni ya umma. Kwa sababu hiyo, data huru na inayoweza kuthibitishwa kuhusu nia ya umma kujadiliana, kufikia makubaliano, au kutatua mizozo kati ya Iran na Marekani ni ndogo. Sehemu kubwa ya tafiti zilizochapishwa pia zimefanywa na taasisi zilizo karibu na serikali, na mara nyingi, maelezo kuhusu idadi ya watu walioshiriki, mbinu ya sampuli, na mbinu ya utafiti haijachapishwa kikamilifu.
Sampuli ya hivi punde zaidi ya tafiti hizi ilichapishwa tarehe 26 Juni na "Taasisi ya Mafunzo na Utafiti ya Chuo Kikuu cha Mapinduzi ya Kiislamu." Katika uchunguzi huu, ambao uliripotiwa kufanywa Mei mwaka huu, asilimia 48 ya waliohojiwa walipinga mazungumzo na Marekani, asilimia 36 waliunga mkono mazungumzo, na asilimia 12 "haikuunga mkono wala kupinga." Kulingana na matokeo yaliyochapishwa, idadi ya wale wanaopinga mazungumzo iliripotiwa kuwa juu kuliko wale wanaopendelea.
Wiki chache zilizopita, katika siku ya mwisho ya Farvardin, kanali ya Ofogh ya Shirika la Utangazaji la Iran pia ilitangaza katika kipindi cha televisheni kwamba "asilimia 87 ya Wairan wanataka vita viendelee." Hata hivyo, mwenyeji wa programu hakueleza ni shirika gani lililofanya uchunguzi huo au mbinu kufikia hilo ilikuwa ipi. Kauli hiyo iliibua mjadala kwenye mitandao ya kijamii, huku baadhi ya watumiaji wakitoa tafsiri tofauti.
Mnamo Mei 26, shirika la habari la serikali la IRNA pia lilichapisha matokeo ya kura ya maoni ya Kituo cha Utafiti cha Majlis, ambayo ilionyesha zaidi ya asilimia 67 ya waliohojiwa waliichukulia Iran kuwa "upande ulioshinda" vita. Asilimia 1.6 waliona Marekani na Israel kuwa washindi, na asilimia 26 walisema kwamba hakuna upande wowote ambao uliyokuwa mshindI.
Ripoti ya IRNA, kama tafiti zingine rasmi, haikuchapisha maelezo ya kina kuhusu idadi ya watu walioshiriki na maelezo ya sampuli, kwasababu ilitaja kwamba utafiti huo ulifanywa kwa simu na nchi nzima.
Utata uliozunguka ukusanyaji wa data, pamoja na ufikiaji mdogo wa data huru, umefanya kuwa vigumu zaidi kutathmini maoni ya umma kuhusu suala la mazungumzo na Marekani. Hili ni muhimu hasa katika kadhia kama vile uhusiano wa Iran na Marekani, ambao umekuwa miongoni mwa masuala nyeti zaidi ya sera za ndani na nje za Jamhuri hiyo ya Kiislamu kwa miaka mingi.
Hata hivyo, hata ndani ya nafasi hii ndogo, maelezo tofauti yanaangaziwa katika magazeti ya Iran. Uhakiki wa nyenzo zilizochapishwa unaonyesha kwamba hakuna maafikiano kamili ndani ya muundo wa kisiasa wa Jamhuri ya Kiislamu kuhusu jinsi ya kushughulikia mazungumzo hayo.
Mnamo tarehe 4 Juni, magazeti muhimu zaidi kote Iran yalielekeza vichwa vyao kuu vya habari kwenye mazungumzo na uwezekano wa kufikiwa kwa makubaliano, lakini simulizi zao kuhusu suala hilo zilitofautiana sana.
Magazeti ya Kayhan na Asr Iranian yaliyo karibu na mirengo yenye misimamo mikali, yamesisitiza kuwa "makubaliano yanayokidhi masharti ya Kiongozi wa Jamhuri ya Kiislamu ndiyo yanayokubalika"; makala na vichwa vya habari vya magazeti haya pia vilisisitiza haja ya kuepuka jaribio lolote la kushulikia siala hilo nje ya mfumo huu.
Kwa ujumla, tathmini ya vyombo vya habari vya Iran inaonyesha kwamba sehemu kubwa ya majadiliano yanayozunguka mazungumzo hayo yamelenga jinsi ya kufafanua "ushindi," "kujiondoa," na "makubaliano yanayokubalika."