Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Iwapo Iran na Marekani wataafikia makubaliano, Israel itakuwa na chaguo gani?
Juhudi za kufikia makubaliano kati ya Marekani na Iran bado zinaendelea, huku Israel ikijadili uwezekano wa makubaliano kuafikiwa na athari zake.
Swali kuu si iwapo makubaliano yataafikiwa, ni nini Israel itafanya iwapo Tehran na Washington wataafikia makubaliano?
Vyombo vya habari na wataalam wa usalama wameacha kuhoji kuhusu makubaliano hayo, na sasa wanataka Israel ijiandae kukabiliana na matokeo ya Marekani kukubaliana na Iran, haswa kuhusu uhuru wa jeshi la Israel na mpango wa nyuklia wa Iran.
Israel inahofia nini?
Israel inahofia kuwa makubaliano yatakayoafikiwa ni sawa na ile ya JCPOA, ambayo itadhibiti mpango wa nyuklia, lakini itatoa uhuru wa kuendelea na mpango wa makombora na ndege zisizo na rubani.
Gazeti moja la Israel lilichapisha taarifa na kusema kuwa makubaliano yatakayoafikiwa hayatakuwa yameafikia malengo hitajika ya kulemaza nguvu za kijeshi za Tehran, mfumo wake na washirika wake wa karibu.
Kulingana na gazeti hilo, Israel haina haja na ushindi kamili dhidi ya Iran, bali wanataka hakikisho kutoka Washington kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran na Hezbolllah.
Ila Israel bado hawajakubaliana jinsi ya kukabiliana na changamoto hii na inasemekana kuwa inamsumbua akili Waziri mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.
Danny Citrinovich mtafiti wa masuala ya ulinzi ambaye awamehi kuhudumu katika idara ya ujasusi ya Israel,anasema kuwa,iwapo makubaliano hayataafikiwa haraka, utawala wa Trump utaanza kuchoka, na hali huenda ikawa kama ya awali ambapo hakuna vikwazo kuhusu nyuklia ya Iran, au hatua yoyote itakayochukuliwa na Marekani, na baadaye ushawishi wa Tehran utakuwa katika eneo hilo.
Watu wengi Israel wanaona kuwa mkataba wowote utakaoafikiwa utakuwa mbaya, kwani vita hivyo bado havijaafikia malengo ya Tel Aviv na Washington
Tofauti hii ya maoni inaonyesha mgawanyiko uliopo katika wataalam wa usalama na wachambuzi wa Israel. Makubaliano yanaweza yasiwe ya kuifaa Israel, lakini kushindwa kabisa kwa mazungumzo hayo kunaweza pia kusababisha hali hatari zaidi, kulingana na baadhi ya wachambuzi
Katika mazingira kama hayo, Israel inakabiliwa na njia mbalimbali za kuchukua hatua.
Chaguo la Kwanza: kufanya makubaliano yawe magumu zaidi kuafikiwa
Mojawapo ya hatua ambazo Israel inaweza kuchukua ni kujaribu kuvuruga maandishi ya mwisho ya mkataba wa makubaliano.
Mshauri wa zamani wa usalama wa taifa wa Israel, Yaakov Amidror, alinukuliwa akisema kwamba matakwa makuu ya Israel katika makubaliano yoyote na Iran yanapaswa kuwa, kusitishwa kwa urutubishaji wa urani na kuwekwa vikwazo kwenye mpango wa makombora wa Iran.
Kulingana na matakwa haya, Israel inaweza kufanya makubaliano kati ya Marekani na Iran kuwa magumu zaidi na yenye gharama kubwa kwa Tehran.
Baadhi ya wachambuzi wanasema pengo kati ya matakwa ya Israel na kile ambacho utawala wa Trump unaweza kukubali imeongezeka.
Kurudia mkataba wa JCPOA na kujaribu kupinga makubaliano
Chaguo jingine ambalo maafisa wa Israel huenda wakalifuata, kwa kurejelea historia, ni makubaliano ya nyuklia ya mwaka wa 2015 yanayojulikana kama JCPOA.
Israel inaweza kuzuia mkataba huo kutumika tena.
Wakati wa mazungumzo ya nyuklia ya 2015, serikali ya Benjamin Netanyahu ilitofautiana waziwazi na ile ya Barack Obama. Mnamo Machi mwaka huo, Netanyahu alihutubia Bunge la Marekani kwa mwaliko wa chama cha Republican, bila uratibu wa Ikulu ya Marekani, na akafafanua makubaliano yaliyoafikiwa na Iran kama "tishio kwa Israel."
Hotuba hiyo, ilitolewa wakati wa kilele cha mvutano kati ya Obama na Netanyahu.
Baadhi ya wachambuzi wa Israel wana wasiwasi kwamba makubaliano mapya yanaweza kuwa mabaya zaidi kwa nchi hiyo kuliko JCPOA, kwa sababu Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, kwa sasa imefika mezani pa mazungumzo wakijua kuwa Israel na Marekani hawajaafikia malengo yao katika vita hivyo.
Chaguo la Pili: Kudumisha uhuru wa kuchukua hatua za kijeshi
Chaguo lingine ambalo Israel huenda ikajaribu kulihifadhi licha ya makubaliano yoyote ni kile maafisa wa usalama mjini Tel Aviv wanakiita "uhuru wa kuchukua hatua", kumaanisha kuwa na uwezo wa kufanya mashambulizi au operesheni za kijeshi dhidi ya malengo ndani ya Iran na kanda hiyo hata kama makubaliano yatafikiwa kati ya Tehran na Washington.
Chaguo la Tatu: Kurudi Vitani
Ikiwa makubaliano mapya yatapunguza uwezo wa Israel kuchukua hatua za kijeshi moja kwa moja, Tel Aviv inaweza kurudi kwenye mtindo wa "vita kati ya vita," yaani mfululizo wa operesheni za kimtandao, hujuma, mauaji ya siri, na shinikizo la kijasusi ambazo zimekuwa sehemu ya mkakati wa Israel dhidi ya Iran kwa miaka kadhaa.
Tovuti ya Ynet, inayohusishwa na kundi la vyombo vya habari la Yedioth Ahronoth, ilifichua katika ripoti ya mwezi Machi kuwa mkuu wa Mossad, David Barnea, alimpa Waziri Mkuu Netanyahu tathmini kabla ya vita, kuwa Israel inaweza kuchochea machafuko ya ndani nchini Iran,ila licha ya mashambulizi na uchochezi, machafuko ya kiwango kikubwa hayajashuhudiwa. Ila Israel inaweza kutumia wazo hili kuvuruga Iran.
Chaguo la Nne: Hezbollah na makundi mengine eneo hilo
Kando na suala la nyuklia, wasiwasi mkubwa wa Israel ni ushawishi wa Iran katika kanda hiyo, kuanzia Hezbollah ya Lebanon hadi makundi yenye silaha yaliyo karibu na Iran Iraq, Syria, na Yemen.
Maafisa wa Iran wamesisitiza umuhimu wa kujumuisha mazungumzo kuhusu Lebanon katika makubaliano yoyote yatakayoafikiwa.
Hii itapunguza uwezo wa Israel kuwalenga washirika wa Iran eneo hilo, lakini wakati huohuo, hakuna anayejua utayari wa serikali ya Netanyahu kukubaliana na hilo.
Baadhi ya wachambuzi wanasema kwamba katika mazingira kama hayo, Lebanon na Hezbollah huenda zikawa kisa cha mvutano kati ya Washington na Tel Aviv.
Vikwazo vya Israel
Licha ya chaguo zote zinazozingatiwa nchini Israel, Tel Aviv inakabiliwa na vikwazo vikubwa.
Vita vya hivi karibuni vimekuwa na gharama kubwa za kijeshi na kiuchumi, na utegemezi wa Israel kwa msaada wa Marekani kuhusu silaha na uungwaji mkono umeongezeka.
Gazeti la Uingereza The Guardian liliripoti tarehe 25 Mei kwamba Israel kwa sasa "inategemea kikamilifu maamuzi ya rais wa Marekani ambaye hatabiriki na anayebadilika badilika."
Katika mitazamo tofauti kutoka Israel ni kwamba hata kama makubaliano yatafikiwa kati ya Tehran na Washington, mgogoro hautaisha kikamilifu
Taasisi ya Israel Institute for National Security Studies, katika uchambuzi wenye mada "Vita vya Israel na Iran: Vimeisha lakini Havijatatuliwa," inasema kwamba mashambulizi ya Israel na Marekani yanaweza kuwa yalitoa jibu la muda kwa changamoto ya silaha za nyuklia za Iran, lakini si suluhisho la kina kwa aina zote za vitisho vinavyotokana na Iran.
Ikiwa mazungumzo yatagonga mwamba, Israel huenda italazimika kutegemea kampeni ya muda mrefu inayohusisha operesheni za kijeshi na za siri ili kuzuia Iran kupata silaha za nyuklia.
Hata hivyo, kuna mtazamo mwingine nchini Israel, kwamba Tel Aviv licha ya kutoridhika kwake, itakubali makubaliano kati ya Marekani na Iran.