Jinsi abiria 'alivyojaribu kufungua mlango wa ndege' kabla ya kutua Lagos

Chanzo cha picha, CLARENS SIFFROY/AFP kupitia Getty Images, @the_neene/Instagram
Shirika la Ndege la Kenya Airways limethibitisha kifo cha abiria aliyekuwa kwenye ndege yake kutoka Nairobi hadi Lagos muda mfupi kabla ya kutua katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Murtala Muhammed.
Katika taarifa iliyochapishwa kwenye ukurasa wake wa X Jumatano, kampuni hiyo ilisema tukio hilo lilitokea Oktoba 6, 2026, yapata saa 9:20 usiku kwa saa za Nigeria.
Kampuni hiyo ilisema abiria huyo alipoteza fahamu takriban dakika 20 kabla ya ndege hiyo kupangwa kutua, na wafanyakazi walimpa msaada wa matibabu ya dharura na kufuata taratibu zote muhimu ili kukabiliana na hali kama hizo.
Hata hivyo, baadhi ya ripoti zilizochapishwa kwenye mitandao ya kijamii na abiria waliokuwa kwenye ndege hiyo zilisema kwamba mtu huyo alijaribu kufungua mlango wa ndege hiyo ilipokuwa hewani.
Mwanamke mmoja wa Nigeria aliyekuwa ndani ya ndege, Adekunbi Ewaola, alifichua kwenye ukurasa wake wa Instagram kwamba abiria walimfunga haraka mwanamume huyo ili kumzuia kufungua mlango wa ndege.
Abiria mwingine alidai kwamba mwanamume huyo alianza kuonyesha tabia ya ukali hata kabla ya kupanda ndege.
BBC iliwasiliana na Kenya Airways kwa taarifa zaidi kuhusu tukio hilo na chanzo cha kifo cha mtu huyo, lakini shirika la ndege halikujibu kabla ya kutoa taarifa yake. Taarifa hiyo pia haikuzungumzia madai yaliyotolewa na abiria.
Kampuni hiyo ilisema kwamba baada ya ndege hiyo kutua Lagos, maafisa wa matibabu katika uwanja wa ndege walithibitisha kwamba abiria huyo alikuwa amefariki.
Unaweza pia kusoma:
































