Mfahamu rubani Smit Machhar, aliyeinusuru ndege ya Dubai kuelekea Israel

Chanzo cha picha, @IsraelMFA
Rubani wa ndege ya Flydubai, Kapteni Smit Machhar, ameibua gumzo duniani kutokana na 'ujasiri' aliouonyesha wakati wa safari ya ndege kati ya Dubai na Israel.
Machhar, raia wa India, amepongezwa na viongozi mbalimbali duniani, akiwemo Rais wa Marekani Donald Trump na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi.
Kwa mujibu wa taarifa, Kapteni Machhar alishambuliwa kwa kisu ndani ya ndege ya Flydubai nambari FZ1073. Inadaiwa kuwa alifanikiwa kufungua mlango wa chumba cha marubani kabla ya kupoteza fahamu kutokana na majeraha aliyoyapata katika shambulio hilo.
Inaripotiwa kuwa ajali ya ndege iliepukika kutokana na hatua zao za tahadhari katika mazingira magumu sana.
Yaniv Hayun, abiria raia wa Israel aliyekuwa kwenye safari hiyo, alitoa taarifa hizo wakati akizungumza na Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu katika Uwanja wa Ndege wa Ben Gurion siku ya Jumatano (Septemba 30).
Hayun alimwambia Netanyahu kuwa mlango wa chumba cha marubani ulikuwa wazi, lakini rubani alikuwa karibu sana na mlango huo kiasi kwamba ilikuwa vigumu kuufungua.
"Hitimisho langu ni kwamba alitufungulia mlango kwa tahadhari na kisha akapoteza fahamu," alisema Hyeon.
Baadaye, Waziri Mkuuj wa Israel Benjamin Netanyahu alizungumzia tukio hilo katika taarifa kwenye mtandao wa 'X' na kusifu ushujaa wa Smith.
"Licha ya kujeruhiwa vibaya katika shambulio la kisu, alichukua hatua, akamkabili mshambuliaji, akafungua mlango wa chumba cha marubani, na kuwatahadharisha abiria pamoja na wahudumu ili kumdhibiti mshambuliaji huyo.
Matokeo yake, janga kubwa la anga lilizuiwa," aliandika Waziri Mkuu wa Israel.
Netanyahu alisema kuwa Smith aliokoa maisha ya watu 174, wakiwemo raia wa Israel na raia wa nchi nyingine.

Chanzo cha picha, Getty Images
Narendra Modi asifu ushajaa wa rubani
Akizungumzia matukio haya, Waziri Mkuu wa India Narendra Modi aliandika kwenye Twitter, "Kapteni Smit Machhar ni 'shujaa'. Licha ya kukabiliwa na hatari kubwa na yeye mwenyewe kujeruhiwa vibaya, alionyesha ujasiri mkubwa na azimio thabiti la kuokoa maisha ya watu wengine."
"Ujasiri wake uliokoa mamia ya maisha na kuzuia janga kubwa. India inajivunia rubani Machhar. Ninaomba apone haraka, apate nguvu mpya, na aendelee kuwa na afya njema," aliongeza.
Smit alifanya nini wakati wa shambulio la kisu?
Smit Machhar pia anapokea sifa nyingi kwenye mitandao ya kijamii. Mwanamke mmoja raia wa Iran aliandika kwenye ukurasa wake wa Instagram, "Mume wangu ni rubani. Aliniambia kuwa kuna swichi katika chumba cha kuendeshea ndege (cockpit) ambayo hufungua mlango wa chumba hicho kutoka ndani. Hivyo, huenda Kapteni Smit Machhar hakupiga tu simu kuomba msaada, bali pia alibonyeza swichi hiyo kabla ya kupoteza fahamu, jambo lililowezesha wahudumu wa ndege na abiria kuingia ndani ya chumba hicho. Hii ndiyo hali inayowezekana zaidi kutokea."
Kama mlango wa chumba cha kuendeshea ndege ungeendelea kufungwa, hakuna mtu ambaye angeweza kuingia na kusaidia kuokoa ndege hiyo. Hongera kwao. Uamuzi huo mmoja ulichukua nafasi muhimu katika kuokoa maisha ya watu wote waliokuwemo ndani ya ndege.

Chanzo cha picha, Getty Images
Kulingana na tovuti ya habari ya Israel ya 'Jerusalem Post', abiria kadhaa walimpa huduma ya kwanza Smit Machhar, ambaye alikuwa amejeruhiwa.
Miongoni mwao alikuwepo daktari wa meno kutoka Israel, Shota Musayev. Baada ya ndege hiyo kutua kwa dharura katika Uwanja wa Ndege wa Tabuk, Smit Machhar alilazwa hospitalini nchini Saudi Arabia.
Musayev aliambia vyombo vya habari vya Israel kwamba Smit Machhar alikuwa amejeruhiwa vibaya na alikuwa akivuja damu nyingi kutoka kichwani na mikononi mwake. Alisaidia kusimamisha uvujaji huo wa damu. Alisema kuwa hali ya Smit Machhar ilitengemaa baada ya hapo. Hata hivyo, hali yake ilizorota tena wakati ndege hiyo ilipokuwa ikitua.
Musayev pia alisema kuwa Machhar alikuwa na uwezo wa kuzungumza kiasi cha kusema kuwa rubani mwenzake alikuwa amemshambulia kwa kisu.
Smit Machhar ni rubani mwenye uzoefu na pia amewahi kuwafunza marubani wapya.
Je, 'mbu wanaotabasamu' ni akina nani?
Kulingana na wasifu wake wa LinkedIn, kabla ya kujiunga na Flydubai, alifanya kazi katika shirika la ndege la India la SpiceJet kwa zaidi ya muongo mmoja, ambapo alihudumu kama nahodha wa mafunzo na mshauri kwa marubani wapya.
Kulingana na wasifu wake, amefanya safari za ndege kwa takriban saa 9,750 akitumia ndege aina ya Boeing 737-800 na 737 Max 8 na 9.
Wasifu huo wa LinkedIn pia unaonyesha kuwa Smit Machhar ameoa na ana watoto.
Ubalozi wa India nchini Saudi Arabia umesema kuwa Smit Machhar amelazwa katika hospitali iliyoko katika mji wa Tabuk, kaskazini-magharibi mwa Saudi Arabia, na anapatiwa matibabu yanayohitajika.
Taarifa kamili kuhusu hali ya rubani Smit Machhar bado hazijapatikana. Hata hivyo, ubalozi umearifu kuwa hali yake ni shwari. Maafisa wa ubalozi pia walisema kuwa wanawasiliana na familia ya Smit Machhar.
Trump pia alimsifu Smit
Rais wa Marekani Donald Trump amemtaja rubani wa Flydubai, Smit Machhar, kuwa 'shujaa'. Alisema rubani huyo alimzuia rubani mwenzake aliyemshambulia kwa kisu, akafungua mlango wa chumba cha kuendeshea ndege na kuomba msaada, hatua iliyosaidia kukwamisha jaribio la makusudi la kuangusha ndege hiyo.
Akizungumza na waandishi wa habari katika Ofisi ya Oval, Trump alisema alizungumza na Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu.
Kwa mujibu wa Trump, Netanyahu alimweleza kuwa fundi bomba ambaye hakuwahi kuendesha ndege alichukua nafasi muhimu katika kutatua tukio hilo la ndege, ambayo ilikuwa ikisafiri kutoka Dubai kwenda Tel Aviv. Hatimaye ndege hiyo ilitua nchini Saudi Arabia.
"Hali ya rubani huyo ilikuwa mbaya sana. Nadhani bado iko hivyo. Lakini hatua alizochukua katika mazingira hayo zilikuwa za kushangaza kweli; kwa namna fulani, alikuwa shujaa," Trump alisema pia.

Chanzo cha picha, Getty Images
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Trump alisema rubani aliweza kufungua mlango wa chumba cha kuendeshea ndege na kupiga kelele kuomba msaada.
"Inaonekana kuwa rubani msaidizi alikuwa gaidi au mtu mwenye matatizo ya akili na alimshambulia mwenzake kwa kisu," Rais huyo wa Marekani alisema.
Kisha Trump alielezea dhima "isiyo ya kawaida" ya abiria raia wa Israel, ambaye alijitambulisha kama fundi bomba.
Kulingana na Trump, abiria ambaye hakuwahi kuendesha ndege aliingia kwenye chumba cha kuendeshea ndege, akamvuta rubani msaidizi kutoka kwenye kiti chake na kumsukuma nyuma. Kisha alidhibitiwa na abiria wengine.
Trump alisema kuwa baadaye abiria huyo alieleza kuwa alijifunza misingi kadhaa ya kuendesha ndege kwa kutazama kipindi cha televisheni cha 'Air Disasters'.
"Alisema hutazama kipindi hiki mara kwa mara na hapo ndipo alipojifunza kuendesha ndege, kwa kiasi fulani," Trump alisema.
Kulingana na Trump, marubani wengine na maafisa wa usalama waliokuwepo sehemu ya nyuma ya ndege walifika kwenye chumba cha kuendeshea ndege na kuchukua udhibiti wa ndege hiyo.
"Nadhani ni hadithi ya kushangaza sana," aliongeza.
Hata hivyo, Trump pia alifafanua kuwa alikuwa akitoa tu taarifa alizokuwa amezipokea na hakuwa amethibitisha ukweli wa mambo hayo.


































