Ebola ni nini na kwa nini kuzuia mlipuko huu ni vigumu sana?

Chanzo cha picha, Getty Images
- Author, James Gallagher
- Nafasi, Health and science correspondent
- Author, Emery Makumeno
- Nafasi, BBC Africa
- Akiripoti kutoka, Kinshasa
- Author, Hafsa Khalil
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 5
Mlipuko wa ugonjwa wa Ebola nchini DRC umetangazwa kuwa dharura ya afya ya umma ya kimataifa na WHO.
Kukabiliana na mlipuko huu ni jambo gumu kwa sababu Inahusisha aina adimu ya virusi ambayo haina chanjo, na visa vya ugonjwa huo vimegunduliwa katika eneo lililoathiriwa na migogoro.
Ebola ni nini na dalili zake ni zipi?
Ebola ni ugonjwa adimu lakini hatari unaosababishwa na virusi.
Virusi vya Ebola kwa kawaida huambukiza wanyama, hasa popo wa matunda, lakini milipuko kwa binadamu wakati mwingine huanza pale watu wanapokula au kushika wanyama walioambukizwa.
Huchukua siku mbili hadi 21 kwa dalili kujitokeza. Dalili huanza ghafla na kufanana na mafua, kama vile homa, maumivu ya kichwa, na uchovu.
Kadiri ugonjwa unavyoendelea, mgonjwa hutapika na kuharisha, na hali inaweza kusababisha viungo vya mwili kushindwa kufanya kazi.
Baadhi ya wagonjwa, lakini si wote, hutokwa damu ndani ya mwili na nje ya mwili.
Virusi hivyo huenea kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine kupitia kugusana na majimaji ya mwili yaliyoambukizwa kama damu au matapishi.
Kwa nini mlipuko huu wa Ebola ni tofauti na je, kuna chanjo?
Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.
Bonyeza hapa kujiunga
Mwisho wa Whatsapp
Mlipuko huu unasababishwa na aina ya Ebola inayojulikana kama Bundibugyo, ambayo haikuwa imeonekana kwa zaidi ya muongo mmoja.
Aina ya Bundibugyo imesababisha milipuko miwili tu hapo awali, ambapo iliua takribani theluthi moja ya watu walioambukizwa.
Aina hii adimu ya Ebola inaleta changamoto nyingi.
Vipimo vya awali vya damu vya Ebola vilionesha matokeo hasi kwa sababu vipimo hivyo hutambua zaidi aina za kawaida za virusi hivyo.
Hakuna chanjo iliyoidhinishwa kwa Ebola ya Bundibugyo, lakini chanjo za majaribio zinaendelea kutengenezwa.
Inawezekana kwamba chanjo ya aina nyingine ya Ebola inayoitwa Zaire inaweza kutoa kinga fulani.
Pia hakuna dawa zilizotengenezwa mahsusi kutibu Bundibugyo, jambo ambalo linafanya matibabu kuwa magumu zaidi.
Changamoto nyingine ni kwamba mlipuko huu unatokea katika eneo lenye migogoro, ambapo karibu watu laki mbili na hamsini wamekimbia makazi yao, na watu wengi wanavuka mipaka isiyodhibitiwa kuelekea nchi jirani.
Hata hivyo, tangazo la WHO kwamba huu ni dharura ya afya ya umma ya kimataifa halimaanishi kuwa dunia iko katika hatua za mwanzo za janga kama la COVID-19. Hatari ya Ebola kuenea nje ya Afrika Mashariki ni ndogo sana.
Mlipuko huu wa ugonjwa ulianzaje?
Kisa cha kwanza kilichojulikana kilikuwa cha muuguzi aliyepata dalili tarehe 24 Aprili, jambo linaloonesha kwamba virusi vilikuwa vinaenea bila kugunduliwa kwa wiki kadhaa.
Hii ina maana kwamba ukubwa halisi wa mlipuko huo haujulikani, na kazi ya kuwatafuta wagonjwa walioambukizwa pamoja na watu ambao huenda waliwaambukiza wengine imekuwa ngumu zaidi.
Muuguzi huyo alifariki mjini Bunia, mji mkuu wa jimbo la Ituri mashariki mwa DRC, kulingana na waziri wa afya wa nchi hiyo, Samuel Roger Kamba.
Mwili wa muuguzi huyo ulirejeshwa Mongwalu, mojawapo ya miji miwili ya uchimbaji dhahabu ambapo visa vingi vimeripotiwa.
Kamba alisema moja ya sababu zilizofanya virusi kuenea haraka ni idadi kubwa ya watu waliogusana wakati wa mazishi.
Mkurugenzi wa Africa Centres for Disease Control and Prevention, Jean Kaseya, alikiambia kipindi cha Newsday cha BBC World Service kwamba mazishi yalikuwa jambo la kutia wasiwasi mkubwa, kama ilivyokuwa katika milipuko iliyopita ya Ebola.
Alisema kampeni za elimu ya afya ya umma "zinatoa taarifa kuhusu jinsi ya kushughulikia mazishi" pamoja na umuhimu wa usafi wa msingi na mazingira safi, huku pia zikitoa hatua za kujikinga kwa wahudumu wa afya.
Kamba alisema mlipuko huo ulichelewa kuripotiwa kwa sababu baadhi ya jamii zilizoathirika ziliamini kuwa ni "uchawi" au "ugonjwa wa kimiujiza", hali iliyowafanya watu kutafuta matibabu katika vituo vya maombi na kwa waganga wa kienyeji badala ya hospitali.
Ugonjwa huu umeripotiwa maeneo gani?
Visa vya kwanza vilivyoripotiwa vilikuwa katika miji ya Mongwalu na Rwampara katika jimbo la Ituri, pamoja na Bunia.
Pia kumekuwa na kisa katika mji wa Goma, mji mkubwa zaidi mashariki mwa DRC, wenye idadi ya watu wapatao 850,000 na ambao uko chini ya udhibiti wa waasi.
Katika mji wa Goma, kisa kilichothibitishwa kilimhusu mwanamke aliyesafiri kwenda mjini humo baada ya mume wake kufariki kwa Ebola mjini Bunia, kulingana na Jean-Jacques Muyembe, mkurugenzi wa Institut National de Recherche Biomédicale, aliyeliambia shirika la habari la AFP.
Mtu mmoja pia amefariki jijini Kampala nchini Uganda, huku mwingine akiendelea kupatiwa matibabu. Wote wawili walikuwa raia wa Congo waliokuwa wamesafiri hivi karibuni kwenda nchini humo.
Hatua gani zimechukuliwa kupambana na Ebola?
Serikali imetuma timu za afya mjini Bunia zikiwa na vifaa vya kujikinga.
World Health Organization pamoja na shirika la madaktari wasio na mipaka, Médecins Sans Frontières (MSF) pia wako eneo hilo. Wanajenga vituo vya matibabu na kuandaa mpango wa kukabiliana na mlipuko huo.
Namba ya bure ya simu, 151, imetolewa kwa ajili ya kuripoti dalili za ugonjwa.
Wakazi wamehimizwa kuchukua tahadhari kama vile:
- Kupiga simu mara moja dalili zinapoanza kujitokeza
- Kuepuka kugusana na miili ya watu waliokufa wakiwa na dalili za ugonjwa huo au wanyama waliokufa
- Kuepuka kula nyama mbichi, kwani chakula kisichopikwa vizuri kinaweza kusambaza virusi
- Kufuatilia na kuzingatia umbali baina ya watu
Waasi wamesema nini?
Goma, mji mkuu wa jimbo la Kivu Kaskazini, kwa sasa unadhibitiwa na waasi wa kundi la AFC-M23, ambao wanasema wanaunda timu ya kukabiliana na Ebola.
Siku ya Jumapili, msemaji wa AFC-M23, Lawrence Kanyuka, alisema kuwa walikuwa "wameanzisha mara moja" mifumo ya kukabiliana na mlipuko huo kwa kushirikiana na huduma za afya pamoja na vituo vya tiba vya eneo hilo, ili kuzuia kuenea kwa Ebola katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wao.
Si serikali wala waasi waliosema kama wako tayari kuweka pembeni tofauti zao ili kushirikiana katika kudhibiti mlipuko huo.
Hata hivyo, kisa cha Ebola mjini Goma kilithibitishwa na Institut National de Recherche Biomédicale (INRB), taasisi ya serikali, jambo ambalo linatoa matumaini fulani kwamba ushirikiano unaweza kufanyika.
Rwanda na nchi nyingine jirani zinachukua hatua gani?
Africa Centres for Disease Control and Prevention imeonya kuhusu hatari kubwa ya Ebola kuenea katika nchi zinazopakana na DRC, hasa Uganda, Rwanda na Sudani Kusini.
Shirika hilo limesema linatarajia kufanya mazungumzo na nchi hizo nne kuhusu "jinsi ya kuimarisha mwitikio" wa kukabiliana na mlipuko huo.
Mamlaka za Rwanda zimesema zinaimarisha uchunguzi wa watu wanaoingia nchini humo baada ya kuthibitishwa kwa kisa cha Ebola mjini Goma, ambao uko mpakani mwa Rwanda.
Mwanaume mmoja kutoka Congo aliiambia BBC kwamba alikuwa amezuiwa kuvuka kutoka Goma kwenda Rwanda.
Hata hivyo, alisema aliambiwa kuwa raia wa Rwanda walikuwa wakiruhusiwa kurejea nyumbani, pamoja na raia wa Congo wanaoishi Rwanda.
Nchini Uganda, Yoweri Museveni ameahirisha hija, sikukuu ya Kikristo inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 3 Juni, ambayo kwa kawaida huvutia maelfu ya raia wa Congo kushiriki katika sherehe hizo.













