Je, Ureno imeanza kuchoshwa na Ronaldo?

.
Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Cristiano Ronaldo alijikuta akiwa kwenye benchi wakati Ureno ikishinda 2-1 dhidi ya Norway katika michuano ya UEFA Nations League siku ya Jumapili, tarehe 27 Septemba 2026.

Ronaldo hakushiriki kabisa katika mechi hiyo licha ya kuwa sehemu ya kikosi, na hii ilikuwa mara ya tatu jambo kama hilo kumtokea.

Hii ni mara ya kwanza katika kipindi cha zaidi ya miaka 18 kwa Ronaldo kukaa benchi kwa dakika 90 katika mechi ya Ureno bila kucheza.

Mara ya kwanza jambo hili kutokea ilikuwa katika mechi ya Euro 2008 ambapo Ureno ilifungwa na Uswisi.

Kwa nini kocha Jorge Jesus alimuacha Ronaldo kwenye benchi?

Kocha wa Ureno, Jorge Jesus, amefichua kuwa mchezaji huyo wa zamani wa Manchester United, Real Madrid na Juventus bado yumo katika mipango yake.

Kwa mujibu wa Jesus, Ronaldo alicheza kwa takriban dakika 70 katika ushindi wa Ureno wa bao 1-0 dhidi ya Wales siku ya Alhamisi, Septemba 24.

Hivyo, siku tatu tu baada ya mchezo huo, Jesus aliona haifai kwa Ronaldo kuanza katika mechi mbili mfululizo, na hivyo akampumzisha.

"Ronaldo alicheza kwa takriban dakika 70 katika mchezo dhidi ya Wales, na sidhani kama ilikuwa sahihi kwake kucheza michezo miwili mfululizo kwa ajili yetu."

Jesus pia alisema kuwa awali alipanga kumjumuisha Ronaldo kwenye mchezo huo, lakini baadaye aligundua kuwa hakuhitaji kushiriki.

Ronaldo
Hauhitaji Whatsapp
BBC Swahili WhatsApp bofya kutufuatilia
BBC Swahili sasa kwenye WhatsApp

Pata habari za kina kutoka BBC News Swahili, moja kwa moja kupitia WhatsApp.

Bonyeza hapa kujiunga

Mwisho wa Whatsapp

Ureno ilianza michuano ya Nations League ikiwa na Gonçalo Ramos kama mshambuliaji, akicheza sambamba na João Félix. Ramos alifunga bao, na hilo lilikuwa miongoni mwa mabao machache yaliyoisaidia Ureno kushinda mechi hiyo.

Jesus alisema kuwa alizungumza na Ronaldo kuhusu kumuingiza uwanjani wakati zikiwa zimesalia takriban dakika 30 za mchezo, lakini kutokana na jinsi mchezo ulivyokuwa ukiendelea kulingana na mpango wake, hakuona sababu ya kumtoa Ramos, kwani alikuwa akionyesha juhudi kubwa wakati huo.

Jorge Jesus amewahi kusema kuwa uteuzi wake wa wachezaji utategemea kiwango chao au majukumu yao uwanjani, na hatatumia nafasi au jina la mchezaji kama kigezo cha kumuanzisha katika kikosi.

Hata hivyo, alimjumuisha Ronaldo katika kikosi chake baada ya kuteuliwa kuwa kocha wa Ureno.

Kwa hivyo, kilichotokea katika mechi dhidi ya Norway ni zaidi suala la usimamizi wa muda wa kucheza na mbinu za kocha, na si tangazo kwamba Ronaldo si mchezaji muhimu tena.

Ni mara ngapi Ronaldo ameanza mchezo akiwa na timu ya Ureno?

Ronaldo ameichezea timu ya taifa ya wakubwa ya Ureno mara 234, jambo linalomfanya kuwa mchezaji aliyeichezea timu hiyo mara nyingi zaidi katika historia ya soka ya nchi hiyo.

Kati ya mechi hizo, takwimu za timu za taifa zinaonyesha kuwa Ronaldo alianza katika mechi 215, huku akiingia akitokea benchi mara 16.

Hii inaonyesha jinsi Ronaldo anavyoendelea kuwa mchezaji wa Ureno aliyeichezea timu hiyo mara nyingi zaidi licha ya umri wake mkubwa.

Mwaka 2026, kabla ya mechi dhidi ya Norway, takwimu za Opta zilionyesha kuwa alikuwa ameanza katika mechi zote nane za Ureno mwaka huo. Alikuwa amefunga mabao matatu mwaka huo kufikia wakati takwimu hizo zilipopatikana

Ureno imemweka Ronaldo benchi mara ngapi?

.

Katika kipindi chote cha taaluma yake ya kimataifa, Cristiano Ronaldo amekaa kwenye benchi bila kucheza hata mechi moja mara tatu.

Hali hii hutokea mara chache sana kwake, kwa sababu karibu kila anapowekwa benchi, huingizwa uwanjani kama mchezaji wa akiba.

Hizi hapa ni nyakati ambazo Ronaldo alikaa benchi na hakuchezea Ureno:

Mechi dhidi ya Uswisi mnamo Juni 2008: Katika michuano ya Euro 2008, Ureno ilikuwa tayari imefuzu kwa hatua inayofuata, hivyo kocha wa wakati huo aliwapumzisha wachezaji wake muhimu, huku Ronaldo akitazama mechi nzima akiwa benchi.

Mechi dhidi ya Croatia mnamo Juni 2024: Kabla ya kuanza kwa michuano ya Euro 2024, Ronaldo aliwekwa benchi katika mechi ya kirafiki dhidi ya Croatia na hakushiriki katika mchezo huo.

Mechi dhidi ya Norway mnamo Septemba 2026: Tukio la hivi karibuni lilitokea hivi karibuni katika michuano ya UEFA Nations League, ambapo kocha wa Ureno, Jorge Jesus, alimuacha Ronaldo benchi kwa dakika 90 bila kumchezesha.

Hii ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 18 hali hii kumtokea katika mechi ya mashindano makubwa rasmi.

Pia mnamo Septemba 8, 2024, Ronaldo alikuwa benchi katika mechi ya Ureno dhidi ya Scotland, lakini aliingia uwanjani baadaye na kufunga bao katika dakika ya 88. Hizi hapa ni baadhi ya mechi nyingine ambazo alianza akiwa benchi.

Ronaldo amefunga mabao mangapi akiichezea Ureno?

Cristiano Ronaldo amefunga mabao 146 akiichezea Ureno katika mechi 234.

Hii ndiyo rekodi ya juu zaidi ya ufungaji mabao kwa timu ya taifa duniani katika soka.

UEFA imethibitisha kuwa Ronaldo ana mabao 146 katika mechi 234, huku Lionel Messi akishika nafasi ya pili akiwa na mabao 125 katika mechi 207.

Katika mwaka wa 2026 pekee, Ronaldo alifunga mabao matatu akiichezea Ureno kabla ya kushiriki michuano ya Nations League.

Kilichotokea Oslo kiliashiria kuanza kwa zama mpya kwa timu ya Ureno.

Jorge Jesus ndiye kocha mpya wa timu hiyo, na anajaribu kuchanganya uzoefu wa Ronaldo na wachezaji vijana wa timu hiyo kama vile Gonçalo Ramos na João Félix.

Katika mechi dhidi ya Norway, Ureno ilishinda bila Ronaldo kucheza. Ramos alianza mechi hiyo kuchukua nafasi ya Ronaldo, na akafunga bao lililoipa Ureno ushindi wa mabao 2-1.

Lakini hilo halifuti mchango ambao Ronaldo ameutoa kwa Ureno.

Ronaldo tayari amecheza mechi 234 akiichezea Ureno na kufunga mabao 146 — yeye ndiye mfungaji bora duniani katika ngazi ya timu ya taifa, na nchi hiyo itakumbuka kwa muda mrefu mchango wa mchezaji huyo, huku kukiwa bado na hamu ya kujua ni lini atastaafu.

Imetafsiriwa na Seif Abdalla na kuhaririwa na Ambia Hirsi