Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Matatizo ya kifedha ya muda mrefu yanaweza kuathiri ubongo - Utafiti
- Author, Mariam Mjahid
- Nafasi, Mwandishi BBC Swahili
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 6
Unafungua simu yako asubuhi na kukuta ujumbe wa deni, huku kodi ya nyumba ikikaribia, ada za watoto zinasubiri na gharama za chakula zinaendelea kupanda. Badala ya kuanza siku ukiwa na utulivu, mawazo yanatawaliwa na swali moja, nitatoa wapi fedha?
Kwa Watu wengi barani Afrika hasa wanaoishi Afrika Mashariki, hali hii si jambo la muda mfupi. Ni sehemu ya maisha ya kila siku. Lakini sasa utafiti mpya unaonyesha kuwa shinikizo la kifedha la muda mrefu linaweza kuathiri zaidi ya akaunti ya benki. Linaweza pia kuathiri afya ya ubongo.
Utafiti uliofanywa na wanasayansi wa Uingereza umebaini kuwa watu wanaoishi na matatizo ya kifedha kwa muda mrefu wana uwezekano mkubwa wa kupungua uwezo wa kukumbuka, kufikiri na kuchakata taarifa wanapofikia umri wa kati.
Watafiti waliwafuatilia zaidi ya watu 2,700 waliozaliwa mwezi Machi mwaka 1946 kwa miongo kadhaa, wakichunguza jinsi hali zao za kifedha zilivyoathiri afya ya ubongo walipofikia umri wa kati.
Hizi ni baadhi ya athari kuu zinazoweza kujitokeza.
Matatizo ya fedha na afya ya akili vina uhusiano gani?
Matokeo ya utafiti yanaonyesha kuwa washiriki waliotumia sehemu kubwa ya maisha yao ya utu uzima, kuanzia miaka ya ishirini hadi mwanzoni mwa miaka ya hamsini, wakiwa miongoni mwa watu wenye kipato cha chini zaidi, walifanya vibaya zaidi katika vipimo vya kumbukumbu na uwezo wa kufikiri.
Aidha, watu walioripoti kushindwa kulipa bili zao mara mbili au zaidi walipokuwa katika miaka ya thelathini na arobaini walionekana kuwa na uwezekano mkubwa wa kuwa na kumbukumbu hafifu na kasi ndogo ya kuchakata taarifa walipofikia umri wa kati.
Hata baada ya kuzingatia sababu nyingine kama mazingira ya utotoni, kiwango cha elimu na uwezo wa kufikiri waliokuwa nao mapema maishani, watafiti walibaini kuwa uhusiano kati ya msongo wa kifedha na kudhoofika kwa afya ya ubongo uliendelea kuwepo.
Kwa mujibu wa watafiti, shinikizo la kifedha la muda mrefu linaweza kuacha athari zinazoonekana hata kwenye viashiria vya kibayolojia vya ubongo. Vipimo vya kasi ya kusoma, uwezo wa kufanya mahesabu pamoja na uchunguzi wa picha za ubongo vilionyesha dalili za mabadiliko yanayohusishwa na msongo wa kifedha uliodumu kwa miaka mingi.
Mmoja wa waandishi wa utafiti huo, Jacques Wels, alisema ushahidi walioupata unaonyesha kuwa matatizo ya kifedha yanaweza kuwa na mchango wa moja kwa moja katika afya ya ubongo.
"Tulibaini uhusiano wa kisababishi kati ya shinikizo la kifedha na afya ya ubongo. Viashiria kama kasi ya kusoma, uwezo wa kufanya mahesabu na picha za ubongo vinaonyesha kuwa matatizo ya fedha ya muda mrefu unaweza kuacha athari za kudumu," alisema.
Watafiti pia waligundua kuwa watu waliokuwa wamepitia shinikizo kubwa la kifedha walionyesha kasi ndogo ya kuzorota kwa uwezo wa kufikiri walipozeeka. Hata hivyo, walieleza kuwa huenda hali hiyo ilitokana na ukweli kwamba sehemu kubwa ya athari ilikuwa tayari imetokea mapema katika maisha yao.
Madeni yanavyovuruga akili na kuwa hatari kwa afya
Wataalamu wanaeleza kuwa matatizo ya fedha na afya ya akili huweza kuingia katika mzunguko unaojirudia.
Mtu anapokuwa na wasiwasi au sonona, uwezo wake wa kufanya maamuzi sahihi kuhusu fedha hupungua. Wengine huanza kuepuka kufungua bili, kuangalia salio la akaunti au kujibu simu kutoka kwa wadai.
Matokeo yake ni kuongezeka kwa ada za kuchelewa kulipa, riba na madeni, hali inayoongeza zaidi msongo wa mawazo.
Wataalamu wanaonya kuwa msongo wa kifedha usipodhibitiwa unaweza kusababisha:
- Wasiwasi wa kudumu kuhusu bili, madeni na mahitaji ya kila siku.
- Sonona kutokana na kukosa matumaini ya kuona suluhisho la matatizo ya kifedha.
- Kukosa usingizi au kupata usingizi usio na utulivu.
- Migogoro katika ndoa, familia na mahusiano mengine.
- Dalili za kimwili kama maumivu ya kichwa, misuli kukaza na hata shinikizo la damu.
Lakini kwa nini fedha zinaweza kuathiri ubongo kwa kiwango hicho?
Wataalamu wa afya ya akili wanaeleza kuwa mwili wa binadamu haukutengenezwa kuishi katika hali ya tahadhari kwa muda mrefu. Unapokuwa na hofu ya kila siku kuhusu namna ya kulipa kodi, kupata chakula, kulipia matibabu au kusomesha watoto, mwili huzalisha homoni za msongo kama cortisol kwa kiwango kikubwa.
Kwa muda mfupi, homoni hiyo husaidia mwili kukabiliana na changamoto. Lakini msongo unapodumu kwa miezi au hata miaka, kiwango kikubwa cha homoni hiyo kinaweza kuanza kuathiri sehemu za ubongo zinazohusika na kumbukumbu, kujifunza na kufanya maamuzi.
Hali hiyo inaweza kumfanya mtu ashindwe kuzingatia jambo kwa muda mrefu, asahau mambo kwa urahisi au apate ugumu wa kufanya maamuzi muhimu. Ndiyo maana wataalamu wanasema matatizo ya kifedha na afya ya akili mara nyingi hujikuta yakichocheana.
Kwa mfano, mtu anayesongwa na madeni anaweza kuanza kuepuka kufungua ujumbe wa benki au bili kwa sababu ya hofu. Kadiri anavyoendelea kuahirisha, ndivyo madeni yanavyoongezeka, riba inavyokusanyika na msongo wa mawazo kuongezeka zaidi.
Hata hivyo, watafiti wanasisitiza kuwa msongo wa kifedha haupaswi kuchukuliwa kama hukumu ya mwisho kuhusu afya ya mtu. Ubongo una uwezo wa kujifunza na kubadilika katika hatua mbalimbali za maisha, na hatua za mapema za kupunguza msongo zinaweza kusaidia kulinda afya ya akili.
Hatua zinazoweza kusaidia kupunguza msongo wa kifedha
1. Tathmini hali yako ya kifedha
Wataalamu wanasema hofu huongezeka pale mtu anapokosa kujua hali halisi ya fedha zake.
Anza kwa kuandika: Vyanzo vyote vya mapato, matumizi yako ya kila mwezi, madeni yote, viwango vya riba na tarehe za malipo.
Hatua hii inaweza kukusaidia kuona picha halisi ya hali yako ya kifedha na kupanga njia ya kutoka.
2. Tengeneza bajeti
Bajeti ni moja ya nyenzo muhimu za kudhibiti matumizi.
Kanuni inayopendekezwa mara nyingi ni ile ya 50, 30 na 20:
- Asilimia 50 ya mapato kwa mahitaji muhimu kama chakula, kodi na bili.
- Asilimia 30 kwa matumizi ya hiari kama burudani.
- Asilimia 20 kwa akiba na ulipaji wa madeni.
Iwapo una madeni makubwa, unaweza kuongeza sehemu ya fedha zinazokwenda katika ulipaji wa madeni hadi hali itakapokuwa nafuu.
3. Panga namna ya kulipa madeni
Madeni ni miongoni mwa vyanzo vikubwa vya msongo wa kifedha.
Baadhi ya wataalamu wanashauri kuanza kulipa deni dogo zaidi kwanza ili kupata hamasa ya kuendelea, huku wengine wakipendekeza kuanza na deni lenye riba kubwa zaidi ili kupunguza gharama kwa muda mrefu.
Jambo muhimu ni kuwa na mpango unaotekelezeka.
4. Weka akiba ya dharura
Hata akiba ndogo inaweza kupunguza hofu ya kukabili gharama zisizotarajiwa.
Wataalamu wanashauri kuanza kwa kuweka kiasi kidogo kila mwezi na kukiongeza kadiri uwezo unavyoruhusu.
5. Punguza matumizi yasiyo ya lazima
Mabadiliko madogo yanaweza kuleta tofauti kubwa bila kuathiri ubora wa maisha.
Miongoni mwa hatua zinazopendekezwa ni:
Kupika nyumbani badala ya kununua chakula mara kwa mara.
Kusitisha huduma za usajili ambazo huzitumii.
Kutumia usafiri wa pamoja pale inapowezekana.
Kununua bidhaa kwa kutumia punguzo na ofa.
6. Tafuta msaada unapouhitaji
Wataalamu wanasema hakuna aibu kutafuta msaada wakati wa changamoto za kifedha.
Katika nchi nyingi, serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali hutoa huduma za kusaidia familia zinazokabiliwa na ugumu wa maisha, ikiwemo msaada wa chakula, makazi, bili za huduma muhimu na ushauri wa kusimamia madeni.
Katika nchi za Afrika Mashariki pia, baadhi ya taasisi za serikali, mashirika ya kijamii na taasisi za kifedha hutoa programu za ushauri wa fedha na huduma za kusaidia watu wanaopitia changamoto za kiuchumi.
7. Linda afya yako ya akili
Wataalamu wanasisitiza kuwa afya ya akili ni muhimu sawa na hali ya kifedha.
Kupunguza msongo wa mawazo kupitia mazoezi ya mwili, usingizi wa kutosha, kuzungumza na watu unaowaamini au kutafuta ushauri wa mtaalamu wa afya ya akili kunaweza kuboresha uwezo wa mtu kufanya maamuzi sahihi kuhusu fedha na kukabiliana vyema na changamoto za maisha.
Kwao, hatua ndogo zinazochukuliwa leo zinaweza kusaidia kuvunja mzunguko wa hofu na kurejesha utulivu wa kifedha pamoja na ustawi wa maisha kwa ujumla.
Viwango vya umaskini Afrika
Wakati nchini China na India idadi jumla ya watu bilioni moja sio masikini tena, idadi ya watu walio masikini sana Afrika, kusini mwa jangwa la sahara ipo juu kuliko ilivyoshuhudiwa miaka 25 iliyopita.
"Katika muongo mmoja uliopita, tumeona dunia ikisogea kwa kasi mbili," anasema Carolina Sánchez-Páramo, mkurugenzi wa kimatiafa wa mpango wa Poverty and Equity Global Practice katika benki ya Dunia.
Zaidi ya waafrika milioni 460 bado wanaishi katika umaskini uliokithiri, wakiwa na kipato kisichozidi dola 2.15 kwa siku, kiwango kilicho juu kuliko ilivyokuwa miaka 15 iliyopita licha ya ukuaji.