Jason Arday, Profesa wa zamani wa Cambridge aliyekabiliwa na tuhuma za wizi wa kazi za kitaaluma, apatikana amefariki dunia
Jason Arday, profesa wa zamani wa Chuo Kikuu cha Cambridge aliyekuwa akikabiliwa na tuhuma za wizi wa kazi za kitaaluma, amefariki dunia.
Huduma za dharura zimesema mwanaume mmoja alipatikana akiwa hajitambui katika eneo la Battersea, kusini mwa London, Ijumaa alasiri.
Arday alijiuzulu wiki iliyopita kutoka nafasi yake ya profesa wa sosholojia ya elimu katika Chuo Kikuu cha Cambridge, kufuatia tuhuma za wizi wa kazi za kitaaluma pamoja na maswali kuhusu baadhi ya mafanikio yake. Arday alikuwa amekanusha tuhuma hizo.
Familia yake imesema katika taarifa kwamba ilikuwa "katika mshtuko" baada ya kumpoteza baba, mwenza, kaka, mjomba na mwana wao waliyemuelezea kuwa wa kipekee.
Familia hiyo iliongeza: "Kampeni ya taarifa za kupotosha ilikuwa imemlemea Jason, ambaye alikuwa mtu mpole na ambaye daima alitaka kuona mazuri kwa kila mtu."
Mapema Ijumaa, maafisa wa polisi waliitwa katika anwani hiyo iliyoko Battersea na Huduma ya Ambulance ya London.
Katika taarifa, Polisi wa Metropolitan walisema: "Kwa wakati huu, kifo chake kinachukuliwa kuwa kisichotarajiwa, lakini haiaminiki kuwa kilitokana na mazingira ya kutatanisha."
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Cambridge, Profesa Deborah Prentice, amesema: "Tumehuzunishwa sana kusikia habari hizi za kusikitisha."
Soma Zaidi: