Je, Elon Musk na Jeff Bezos hufadhili vipi mashindano yao ya kwenda anga za juu?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 7

Zaidi ya miongo miwili iliyopita, mabilionea wawili tajiri zaidi duniani walianza kutimiza ndoto yao ya kupeleka watu angani kupitia safari za kibiashara za kibinafsi. Hata hivyo, ndoto hiyo iligeuka kuwa shindano kati ya bilionea Elon Musk kupitia kampuni yake ya SpaceX na bilionea Jeff Bezos kupitia kampuni yake ya Blue Origin.

Shindano hili limepamba moto hivi karibuni baada ya kampuni ya kibiashara ya anga ya Elon Musk, SpaceX, kuanza kuuza hisa zake hadharani katika Soko la Hisa la New York na kuwa mojawapo ya kampuni kubwa zaidi duniani kwa thamani ya soko.

Wakati huo huo, bilionea na mwanzilishi wa Amazon, Jeff Bezos, alitangaza kuwa anauza hisa za Amazon zenye thamani ya dola bilioni 1 kila mwaka ili kufadhili kampuni yake, Blue Origin.

Ndoto ya "anga mpya"ni neno linalotumiwa na baadhi ya watu kurejelea uendeshaji wa safari za kibiashara za gharama nafuu kwenda angani, ilianza mwaka wa 2000 wakati bilionea Jeff Bezos alipoanzisha kampuni ya Blue Origin.

Miaka miwili baadaye, bilionea Elon Musk, mwanzilishi wa kampuni kubwa ya magari ya umeme ya Tesla, alianzisha SpaceX ili kuwa mshindani mkuu wa Blue Origin.

Kasi kubwa ya ukuaji

Sekta hii inayoibukia inashuhudia ukuaji mkubwa kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya kile kinachojulikana kama "utalii wa anga za juu" miongoni mwa matajiri duniani, sambamba na maendeleo ya haraka ya kiteknolojia ya hivi karibuni kuhusu roketi zinazoweza kutumika tena.

Sekta hiyo pia inapata msukumo kutokana na ongezeko la hivi karibuni la safari za kibiashara kwenda anga za juu.

Thamani ya soko la sekta hii inayoibukia ilikadiriwa kuwa takriban dola bilioni 1.95 mwaka 2025, kulingana na kampuni ya utafiti wa soko ya SNS Insider.

Tovuti hiyo ilitabiri kuwa thamani ya soko la utalii wa anga za juu ingepanda hadi kufikia dola bilioni 87.32 ifikapo mwaka wa 2035.

Thamani ya jumla ya makampuni yanayofanya kazi katika sekta hii mwaka wa 2023 ilikadiriwa kuwa takriban dola milioni 888.3, jambo linaloashiria kasi kubwa ya ukuaji inayoonekana wazi kutokana na thamani hiyo kuongezeka maradufu ndani ya takriban miaka mitatu.

Kushindwa mara kwa mara

Licha ya ukuaji huu, njia inayowakabili Elon Musk, Jeff Bezos, na washindani wao katika kufanikisha ndoto ya utalii wa anga za juu na kuenea kwa aina hii ya usafiri haionekani kuwa nyepesi, wanakabiliwa na changamoto kubwa inayotokana na kufeli kwa majaribio ya kurusha roketi zinazowezesha safari hizo.

Roketi ya Starship V3, iliyorushwa na SpaceX mnamo Mei 22, ilishindwa kutua kwa njia iliyodhibitiwa kama ilivyopangwa na kuangukia Bahari ya Hindi. Roketi nyingine ya Starship ililipuka mnamo Aprili 2023, dakika chache tu baada ya kurushwa.

Roketi nyingine ya SpaceX ililipuka mnamo Septemba 2016 wakati wa jaribio la kurushwa kutoka Kituo cha Jeshi la Anga cha Cape Canaveral huko Florida, Marekani, kabla ya kurushwa rasmi kulikokuwa kumepangwa.

Mnamo Juni 2015, roketi iliyorushwa na SpaceX ilishindwa kukamilisha safari ya kusafirisha mizigo kwa ajili ya shirika la NASA.

Mwezi Mei mwaka jana, roketi ya New Glenn, iliyorushwa na kampuni ya Blue Origin inayomilikiwa na Jeff Bezos, ililipuka wakati wa jaribio la injini katika Kituo cha Jeshi la Anga cha Cape Canaveral huko Florida, Marekani.

Roketi hiyo, ambayo ilikuwa na urefu wa takriban mita 100, ililipuka wakati wa jaribio la injini ikiwa katika maandalizi ya safari ya kupeleka satelaiti 49 angani ili kuimarisha huduma za intaneti za Amazon. Safari hiyo ilipangwa kuanza kwa kurushwa kwa roketi hiyo mnamo tarehe 4 Juni.

Hii ilikuwa safari ya nne ya New Glenn, ikitanguliwa na safari nyingine ambayo nayo ilishindwa kufikia malengo yake baada ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Marekani (FAA) kusimamisha matumizi ya roketi hiyo.

Hatua hiyo ilichukuliwa baada ya roketi hiyo kushindwa kuweka katika njia ya setilaiti yani obiti satelaiti ya mawasiliano ya Bluebird 7 mnamo Aprili 19, kulingana na tovuti ya Space.com inayoshughulikia masuala ya anga za juu.

Ufadhili na mtu wa kwanza duniani kuwa na utajiri wa trilioni moja

Awali, Elon Musk na Jeff Bezos walitumia utajiri wao binafsi kufadhili kampuni za SpaceX na Blue Origin.

Hata hivyo, Elon Musk alibadilisha hadhi ya kisheria ya kampuni yake, akiibadilisha kutoka kampuni binafsi na kuwa kampuni inayouza hisa kwa umma kwenye Soko la Hisa la New York mwaka huu, hatua hiyo ilivutia umakini mkubwa kutoka kwa wadau wa masoko ya fedha duniani kutokana na thamani kubwa ya soko ya kampuni hiyo baada ya kuanza kuuza hisa kwa umma (IPO).

Hivyo, chanzo cha fedha kwa ajili ya SpaceX kikawa ni mapato yanayotokana na ununuzi wa hisa, jambo lililoipa kampuni hiyo fursa zaidi za kupanua majaribio, tafiti, na shughuli zake za kibiashara.

Tangazo la kuanza kuuzwa kwa hisa za SpaceX kwa umma (IPO) lilitolewa tarehe 15 Julai. Wiki hii, bei ya hisa ya kampuni hiyo ilivuka bei yake ya awali ya IPO kwa mara ya kwanza, ikipanda kwa karibu asilimia 4 na kufikia dola 135.

Kupanda huko kulitokana na kutolewa kwa ripoti ya kwanza kabisa ya mapato ya kampuni hiyo, iliyoonyesha mapato ya dola bilioni 7.81 katika robo ya pili ya mwaka huu,kiasi kilichozidi makadirio ya soko ya dola bilioni 6.93.

Kampuni hiyo iliorodheshwa kwenye soko la hisa la Marekani baada ya kujumuishwa katika fahirisi ya Nasdaq 100 inayohusisha makampuni makubwa ya teknolojia mwezi Julai mwaka jana, hatua hiyo iliongeza thamani ya soko ya kampuni kwa dola bilioni 75 na kufikisha thamani yake jumla kuwa dola trilioni 2.

Kulingana na Bloomberg, Elon Musk anamiliki takriban asilimia 42 ya hisa, zenye thamani ya takriban dola bilioni 767.1, jambo linalomfanya kuwa mtu mwenye ushawishi mkubwa katika bodi ya wakurugenzi na kuathiri maamuzi yake. Musk pia aliweka historia kwa kuwa bilionea wa kwanza kuwahi kutokea baada ya kuongeza kiasi hicho kikubwa cha fedha kwenye utajiri wake binafsi.

Wakati huo huo, Jeff Bezos, mmiliki wa kampuni ya Blue Origin, alitoa maelezo kuhusu vyanzo vya fedha vya kampuni yake kwa ajili ya shughuli za utalii wa anga za juu. Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, Bezos alieleza kuwa huuza hisa za Amazon zenye thamani ya takriban dola bilioni 1 kila mwaka ili kufadhili majaribio na utafiti unaolenga kuanzisha safari za kibiashara za gharama nafuu kwenda anga za juu. Hatua hii ni sehemu ya juhudi zake za kutekeleza mpango wa kuanza safari za anga za juu za dakika 11 kufikia mwaka ujao.

Bezos alielezea biashara ya kampuni yake ya safari za kibiashara za anga za juu kama "kazi muhimu zaidi" aliyowahi kuifanya, akisisitiza kuwa anaiona kwa "mtazamo wa muda mrefu" na kwamba anajikita katika "mustakabali wa wanadamu nje ya sayari ya Dunia."

Mnamo tarehe 4 Agosti, Bezos alitangaza nia yake ya kuuza hisa milioni 15 kati ya zile anazomiliki katika kampuni ya Amazon kwa thamani ya dola bilioni 4.1. Hatua hiyo ilifuatia kupanda kwa kasi kwa bei ya hisa za kampuni hiyo kubwa ya Marekani inayojihusisha na biashara ya rejareja, jambo lililosababisha thamani yake ya soko kuvuka dola trilioni 3.

Washindani wengine

Ushindani hauko kwa SpaceX na Blue Origin pekee, kuna makampuni mengine yanayofanyia kazi lengo hilo hilo. Kufanya safari za kibiashara za gharama nafuu kwenda anga za juu.

Mmoja wa washindani wakuu wa Musk ni bilionea wa Uingereza, Richard Branson, kupitia kampuni yake ya Virgin Galactic. Hadi sasa, kampuni hiyo imesafirisha watu watano kwenda anga za juu katika safari mbili za majaribio.

Abiria wote walikuwa wafanyakazi wa kampuni hiyo, marubani wanne waliendesha chombo hicho cha anga, huku mkufunzi mkuu wa wanaanga, Beth Moses, akishiriki kama abiria wa majaribio katika safari ya pili.

Kampuni hiyo inatarajia kufanya safari nyingine mbili za majaribio kwenda anga za juu kabla ya kumbeba mwanzilishi wake, Richard Branson.

Thamani ya soko ya Virgin inakadiriwa kuwa dola milioni 498.02, na hisa zake tayari zimeorodheshwa katika masoko ya hisa ya Marekani.

Kwa mujibu wa Fortune Bens Insight, Axiom Space pia inaendelea kutengeneza moduli binafsi za anga zilizoundwa kuhudumia wanaanga wa kibiashara na safari za utalii wa anga, hatua inayozidi kuimarisha msingi wa baadaye wa utalii wa anga unaofanyika kupitia vituo vya anga vya kibinafsi.

Boeing imepanua ushirikiano wake katika mifumo ya anga inayobeba binadamu na teknolojia za makazi ya anga, ikiunga mkono mipango ya muda mrefu ya utalii wa anga na safari za kibiashara za binadamu kwenda anga za juu.