Je, Tanzania inaweza kufikia maridhiano ya kisiasa bila CHADEMA na Lissu?

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 5

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amekutana na viongozi wa vyama 18 kati ya 19 vyenye usajili wa kudumu nchini humo kujadili masuala mbalimbali ya kisiasa, yakiwemo maridhiano na mchakato wa Katiba.

Lakini chama kikuu cha upinzani nchini, CHADEMA, hakikushiriki mkutano huo licha ya kudaiwa kualikwa.

Kutokuwepo kwa CHADEMA kunafungua mjadala mpana zaidi ya mkutano wenyewe, kwamba Je, Tanzania inaweza kufikia maridhiano ya kisiasa bila ushiriki wa chama kikuu cha upinzani, huku mwenyekiti wake Tundu Lissu akiwa gerezani kwa tuhuma za uhaini?

Hili ni swali ambalo linagusa historia ya siasa za Tanzania, kwa sababu baadhi ya hatua kubwa za maridhiano nchini humo zimewahi kufikiwa baada ya vyama vyenye nguvu kisiasa kukubali kukaa meza moja na kukubaliana, hata kama makubaliano hayo yanaonekana na wengine kuwa na 'ukungu'.

Historia ya Zanzibar na somo la Muafaka

Mfano unaotajwa mara nyingi ni Zanzibar. Baada ya uchaguzi wa mwaka 2000 uliogubikwa na mvutano mkubwa wa kisiasa na vurugu za Januari 2001, hasa Pemba, na kusababisha vifo vya watu takriban 30 hadi zaidi ya 40 kulingana na ripoti rasmi na za mashirika ya haki za binadam

Vyama vya CCM na CUF vilianza mchakato wa mazungumzo kuweka sawa mambo. Wakati huo, CUF kilikuwa chama kikuu cha upinzani Zanzibar na kilikuwa mshindani mkubwa wa CCM.

Mazungumzo hayo yalipelekea makubaliano yaliyofahamika kama Muafaka, yaliyolenga kupunguza mvutano wa kisiasa na baadaye yakachangia katika mazingira yaliyowezesha kuundwa kwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar mwaka 2010.

Somo kubwa kutoka katika historia hiyo ni kwamba maridhiano yalihusisha pande mbili zenye ushawishi mkubwa katika mgogoro wa kisiasa wa wakati huo.

Miaka imepita na mazingira ya kisiasa Zanzibar yamebadilika. CUF si tena chama kikuu cha upinzani visiwani. Nafasi hiyo sasa inashikiliwa na ACT-Wazalendo, ambayo wafuasi na viongozi wengi wa CUF walijiunga na chama hiki kufufuatia mgogoro wa ndani wa chama uliogubika CUF.

Mazungumzo yanayoendelea kati ya CCM na ACT-Wazalendo yamekuwa yakitajwa kama hatua muhimu katika kujenga mazingira mapya ya kisiasa Zanzibar.

Hata katika kikao chake na vyama vya siasa Alhamisi Julai 30, 2026 Rais Samia amesifia hatua iliyofikiwa katika mazungumzo hayo, ambayo yamekuwa yakiongozwa na marais wastaafu, akisema ni mfano wa namna tofauti za kisiasa zinavyoweza kushughulikiwa kupitia mazungumzo.

Lakini kwa upande wa Tanzania Bara ina tofauti kubwa, chama kikuu cha upinzani, CHADEMA, hakipo kwenye meza ya mazungumzo, ambayo yanaanza kushika kazi kidogokidogo kuelekea kwenye mazungumzo ya maridhiano halisi.

"Hakuna maridhiano bila Lissu" - CHADEMA

CHADEMA inasema haikatai mazungumzo, lakini inaamini mazingira ya kuanza mchakato huo wa mazungumzo ya maridhiano bado hayajatimia.

Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, John Heche, amesema hakuna mazungumzo yatakayofanyika bila Mwenyekiti wa CHADEMA, Tundu Lissu, kuachiwa huru. Lissu yuko ndani kwa zaidi ya mwaka sasa akituhumiwa kwa kosa la uhaini, ambalo halina dhamana.

Heche pia amesema chama kinataka uwepo wa mpatanishi wa kimataifa au kikanda na uwajibikaji kama sehemu ya mchakato wa maridhiano.

"Hakuna mazungumzo yoyote yatakayoongozwa na mtu yoyote isipokuwa mwenyekiti mwenyewe akiwa nje. Kama kuna njia zozote za kuanza kuzungumza ni lazima kwanza mwenyekiti wetu awe nje. Cha pili, hakuna mazungumzo tutakayozungumza bila mpatanishi. Na hakuna mazungumzo yatakayofanyika bila watu kuwajibika."

Kwa msimamo huo, CHADEMA inaona suala la maridhiano haliwezi kutenganishwa na mazingira ya kisiasa yaliyopo sasa.

Kwa upande wake, Rais Samia amesema mlango wa mazungumzo bado uko wazi na Serikali bado inaendelea kupokea maoni, masharti na matakwa ya CHADEMA. Akizungumza baada ya kukutana na viongozi wa vyama vya siasa, Rais amesema:

"Kisiasa kama mnavyoona tuko vizuri, lakini mwenzetu mmoja bado anaendelea kutafakari. Tunaendelea kupokea misukumo yake, conditions zake (masharti yake), matakwa yake. Tunaendelea na ndiyo mambo yanavyoendeshwa kwenye nchi."

Rais pia amesema Serikali inalenga kuunda Tume ya Maridhiano ili kuharakisha mwenendo wa Katiba. Kauli hiyo inatafsiri kwamba Serikali inaamini mchakato unaweza kuendelea huku ikiacha nafasi wazi kwa CHADEMA kutafakari na hata kushiriki baadaye.

Maridhiano yanahusisha jamii nzima, si chama kimoja- CCM

Kwa upande wa CCM, maridhiano hayatazamwi kama mazungumzo kati ya vyama viwili pekee, bali kama mchakato unaohusisha wadau mbalimbali wa kijamii na kisiasa.

Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Stephen Wasira, amehojiwa na kusema chama hicho kinaona maridhiano yanapaswa kuwahusisha wadau wote, akisema si suala la chama kimoja cha siasa pekee.

"Unapozungumza juu ya kuridhiana, sisi CCM tunasema tunataka kuridhiana kwa kuleta wadau wote pamoja. Sio chama kimoja cha siasa. Kuna vyama vingi, kuna viongozi wa dini na wadau wengine."

Wasira amesema CCM haitaki kuangalia suala hilo kama mazungumzo yanayolenga chama kimoja pekee.

"Sitaki kuwasema CHADEMA, lakini wao wanasema hawataki maridhiano na wanafikiri wao ndiyo tunataka kuridhiana nao. Sisi tunataka kuridhiana na jamii yote."

Kwa wachambuzi, bado kunaonekana utofauti wa mitazamo kuhusu maana ya maridhiano na namna ya kuridhiana. Wakati CHADEMA ikisisitiza umuhimu wa kushughulikia masharti yake kabla ya kushiriki, CCM inaona mchakato huo kama jambo pana linalohusisha vyama vyote na makundi mbalimbali katika jamii.

"Kama anakualika, hutaki kwenda, utafanywaje?"

Mwenyekiti wa Baraza la Vyama vya Siasa Tanzania, Ali Khatib, anaona changamoto kubwa iko kwenye utayari wa vyama kushiriki mazungumzo. Akizungumza na Sauti Digital, alihoji uamuzi wa CHADEMA kutoshiriki: "Kama kiongozi wa nchi anakualika, njoo tuzungumze, wewe hutaki kwenda, sasa utafanywaje?"

Kwa wachambuzi wa siasa na viongozi wengine, changamoto kubwa katika mchakato wa maridhiano mara nyingi huwa ni suala la kuaminiana.

Aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Nigeria, Dkt. Benson Bana, amesema maridhiano hayawezi kufanikiwa ikiwa upande mmoja bado unaona haujaridhika au hauamini mazingira yaliyopo.

Katika mahojiano yake na Sauti Digital, Bana alisema: "Hamuwezi kuridhiana kama kuna upande haujaridhika. Hamuwezi kuridhiana kama bado mnahasimiana, hamuaminiani."

Kauli hiyo inachochea zaidi mjadala kwamba je pande zinazotofautiana zinapaswa kwanza kujenga mazingira ya kuaminiana kabla ya mazungumzo, au ni kupitia mazungumzo yenyewe ndipo uaminifu huanza kujengwa?

Je, maridhiano yanaweza kufanikiwa bila CHADEMA?

Kwa upande mmoja, Serikali imeonyesha kuwa mchakato wa mazungumzo unaweza kuendelea kupitia vyama vinavyoshiriki na imeonyesha nia ya kuanzisha Tume ya Maridhiano.

Kwa upande mwingine, historia ya Tanzania inaonyesha kuwa makubaliano makubwa ya kisiasa yamekuwa na nguvu zaidi pale ambapo vyama vyenye ushawishi mkubwa vimehusika moja kwa moja.

CCM ilizungumza na CUF wakati CUF ilikuwa nguvu kubwa ya upinzani Zanzibar. Leo, mazungumzo ya CCM na ACT-Wazalendo yanahusisha chama chenye ushawishi mkubwa visiwani.

Tanzania Bara ina hali tofauti. CHADEMA, ambacho ni chama kikuu cha upinzani, hakipo kwenye mchakato wala muelekeo huo kwa sasa, kinaonekana 'kususia' huku kikisisitiza kuwa masharti yake lazima yazingatiwe kwanza.

Hapo ndipo wengi wanajiuliza kama Tanzania inaweza kujenga maridhiano ya kudumu bila ushiriki wa CHADEMA na Lissu ambaye ni kiongozi wa chama hicho mwenye misimamo, au kama mafanikio ya mchakato huo yatategemea kwanza namna ya kuwaleta wadau hao wakuu kwenye meza ya mazungumzo.

Kadiri uchaguzi unavyokaribia, jibu la swali hilo linaweza kuwa na mchango mkubwa katika mwelekeo wa siasa za Tanzania.