Sekta 7 zinazotarajiwa kuzalisha ajira nyingi zaidi ifikapo 2030

    • Author, Mamadou Faye
    • Nafasi, BBC News Afrique
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 7

Mabadiliko makubwa yanayoendelea duniani yanaifanya ajira ya leo isitofautiane tu na ya kesho, bali pia kubadili ujuzi unaohitajika ili mtu aweze kupata kazi. Teknolojia mpya, mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la idadi ya watu na mabadiliko ya mifumo ya uzalishaji vinatarajiwa kuunda taswira mpya ya soko la ajira ifikapo mwaka 2030.

Kwa mujibu wa ripoti ya Future of Jobs 2025 iliyochapishwa na World Economic Forum (WEF) mwezi Januari 2025, dunia inatarajiwa kuunda ajira mpya milioni 170 kati ya mwaka 2025 na 2030. Wakati huohuo, ajira milioni 92 zinatarajiwa kutoweka kutokana na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya soko. Hii itaacha ongezeko halisi la ajira milioni 78, sawa na ukuaji wa asilimia saba ya ajira rasmi duniani, kwa kuzingatia uchambuzi wa ajira bilioni 1.2.

Lakini ongezeko hilo halitakuwa sawa katika sekta zote. Wakati baadhi ya taaluma zitapungua kutokana na matumizi ya akili mnemba (AI) na mashine, sekta nyingine zinatarajiwa kushuhudia mahitaji makubwa ya wafanyakazi kutokana na ongezeko la watu, mahitaji ya chakula, huduma za afya, mabadiliko ya nishati na kasi ya mageuzi ya kidijitali.

Ni muhimu pia kufahamu kuwa WEF haijatoa orodha rasmi ya "sekta zinazotengeneza ajira nyingi zaidi". Badala yake, ripoti imechambua taaluma zinazokua kwa kasi, sekta 22 za biashara na kiwango cha mabadiliko ya soko la ajira. BBC imeunganisha vigezo hivyo ili kubaini sekta zenye matarajio makubwa zaidi ya kuzalisha ajira kufikia mwaka 2030.

Kwa Afrika Mashariki, taarifa hizi zinaweza kuwa mwongozo muhimu kwa vijana wanaochagua taaluma, wafanyakazi wanaotaka kubadili kazi na wawekezaji wanaotafuta sekta zenye ukuaji wa muda mrefu. Ingawa mazingira ya uchumi hutofautiana kati ya nchi, sekta nyingi zinazotajwa kwenye ripoti zinaonyesha dalili za ukuaji pia katika nchi za Tanzania, Kenya, Uganda na Rwanda. sekta hizi 7 kati ya 22 zilizochambuliwa zinatajwa kuzalisha ajira nyingi ifikapo 2030.

1. Kilimo na rasilimali asili

Kilimo kinaendelea kuwa sekta yenye nafasi kubwa zaidi ya kuzalisha ajira duniani. WEF inakadiria kuwa zaidi ya ajira milioni 35 zitaongezeka katika shughuli zinazohusiana na kilimo ifikapo mwaka 2030, idadi ambayo ni kubwa kuliko sekta nyingine yoyote iliyochambuliwa kwenye ripoti.

Kwa sasa, sekta hii tayari inaajiri zaidi ya watu milioni 200 duniani. Ukuaji unaotarajiwa unasukumwa na sababu kadhaa, ikiwemo mpito kuelekea uchumi wa kijani, juhudi za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, kuongezeka kwa matumizi ya teknolojia za kidijitali katika kilimo na kupanda kwa gharama za maisha kunakoongeza shinikizo la uzalishaji wa chakula.

Kwa Afrika Mashariki, ambako kilimo bado kinatoa ajira kwa sehemu kubwa ya wananchi, mwelekeo huu unaweza kuongeza mahitaji ya wataalamu wa teknolojia za kilimo, umwagiliaji, kilimo biashara, usimamizi wa mashamba, pamoja na huduma za ushauri wa kilimo. Kadri teknolojia inavyoingia mashambani, ndivyo nafasi za ajira zenye ujuzi maalumu zinavyoweza kuongezeka.

2. Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT)

Teknolojia imekuwa injini ya mabadiliko katika karibu kila sekta ya uchumi. Kutoka benki hadi afya na elimu, mahitaji ya wataalamu wa kidijitali yanaendelea kuongezeka kwa kasi.

Ripoti ya WEF inaonyesha kuwa watengenezaji wa programu (software and application developers) ni miongoni mwa taaluma zinazokua kwa kasi zaidi na pia ni miongoni mwa zinazochangia ongezeko kubwa la ajira. Sekta ya ICT ina kiwango cha mabadiliko ya ajira cha asilimia 34, ikiwa ni moja ya sekta zinazokua kwa kasi zaidi. Pia ndiyo inayokusanya baadhi ya taaluma zinazotafutwa zaidi duniani, zikiwemo wataalamu wa Big Data, Artificial Intelligence (AI), Machine Learning, Cybersecurity, Internet of Things (IoT) na DevOps.

Katika nchi za Afrika Mashariki, ukuaji wa huduma za kifedha za kidijitali, biashara mtandaoni na matumizi ya akili mnemba unaweza kuongeza mahitaji ya wabunifu wa programu, wachambuzi wa data, wataalamu wa usalama wa mifumo ya kidijitali na wahandisi wa programu. Hii ni moja ya sekta ambazo zinaweza kuwapa vijana nafasi kubwa zaidi za ajira zenye mishahara mizuri katika miaka ijayo.

3. Afya na huduma za matibabu

Mahitaji ya huduma za afya yanatarajiwa kuendelea kuongezeka kadri idadi ya watu inavyoongezeka na watu wengi zaidi duniani kuishi kwa umri mkubwa.

Kwa mujibu wa WEF, wauguzi ni miongoni mwa taaluma 15 zitakazoongeza ajira kwa kiwango kikubwa zaidi duniani ifikapo mwaka 2030. Ripoti inaeleza kuwa sababu kuu ya ukuaji huo ni kuongezeka kwa idadi ya wazee katika nchi nyingi, jambo linaloongeza mahitaji ya huduma za afya na matunzo ya muda mrefu. Sekta ya afya ina kiwango cha mabadiliko ya ajira cha asilimia 19.

Kwa Afrika Mashariki, ambako bado kuna upungufu wa wataalamu wa afya katika maeneo mengi, mahitaji yanaweza kuongezeka kwa madaktari, wauguzi, wataalamu wa maabara, wahudumu wa afya ya jamii na wataalamu wa afya ya akili. Kadri uwekezaji katika sekta ya afya unavyoongezeka, ndivyo fursa mpya za ajira zinavyoweza kuendelea kuibuka.

4. Elimu na mafunzo

Wakati akili mnemba (AI) na teknolojia nyingine zikiendelea kubadilisha mazingira ya kazi, sekta ya elimu nayo inatarajiwa kuwa miongoni mwa maeneo yatakayozalisha ajira nyingi zaidi katika miaka ijayo. Sababu kubwa ni kwamba watu wengi zaidi watahitaji kujifunza ujuzi mpya ili kuendana na mahitaji ya soko la ajira.

Kwa mujibu wa ripoti ya WEF, walimu wa elimu ya sekondari na wahadhiri wa vyuo vikuu na elimu ya juu ni miongoni mwa taaluma 15 zitakazoongeza ajira kwa kiwango kikubwa zaidi duniani ifikapo mwaka 2030. Sekta ya elimu pia ina kiwango cha mabadiliko ya ajira (labour-market churn) cha asilimia 22, karibu na wastani wa sekta zote zilizochambuliwa.

Kwa Afrika Mashariki, ambako idadi ya vijana inaendelea kuongezeka kwa kasi, mahitaji ya walimu, wakufunzi wa vyuo vya ufundi, wataalamu wa mafunzo ya kidijitali na wabunifu wa maudhui ya kujifunzia yanatarajiwa kuendelea kuongezeka. Kadri kampuni zinavyowekeza katika kuongeza ujuzi wa wafanyakazi wao, ndivyo sekta hii itakavyopata umuhimu zaidi.

5. Usafirishaji na ugavi

Biashara ya mtandaoni, ukuaji wa miji na kuongezeka kwa biashara za kimataifa vinaifanya sekta ya usafirishaji na ugavi kuwa moja ya nguzo muhimu za uchumi wa kisasa. Bidhaa zinahitaji kufikishwa kwa wateja kwa haraka zaidi kuliko ilivyokuwa miaka michache iliyopita.

Ripoti ya WEF inaonyesha kuwa madereva wa magari ya kusafirisha bidhaa ni miongoni mwa taaluma 15 zitakazoongeza ajira kwa kiwango kikubwa zaidi duniani ifikapo mwaka 2030. Aidha, sekta ya usafiri, na ugavu ina kiwango cha mabadiliko ya ajira cha asilimia 35, ikiwa ni moja ya sekta zenye kasi kubwa ya kuunda na kubadili nafasi za kazi. Ukuaji huo unachangiwa na kuongezeka kwa biashara mtandaoni, mahitaji ya huduma za usafirishaji wa bidhaa hadi kwa mteja, pamoja na mabadiliko ya teknolojia ya usafirishaji.

Katika nchi za Afrika Mashariki, uwekezaji unaoendelea kwenye reli za kisasa, upanuzi wa bandari kama Dar es Salaam na Mombasa, pamoja na ukuaji wa biashara mtandaoni, unaweza kuongeza mahitaji ya wasimamizi wa ugavi, wataalamu wa minyororo ya usambazaji (supply chain), madereva wenye ujuzi na wasimamizi wa maghala.

6. Ujenzi na miundombinu

Ukuaji wa miji, ongezeko la watu na uwekezaji katika miundombinu vinatarajiwa kuifanya sekta ya ujenzi kuendelea kuwa chanzo kikubwa cha ajira katika miaka ijayo.

Kwa mujibu wa WEF, mafundi wa ujenzi, wanaofunga miundombinu ya majengo na taaluma nyingine za ujenzi ni miongoni mwa taaluma 15 zitakazoongeza ajira kwa kiwango kikubwa zaidi duniani ifikapo mwaka 2030. Ripoti inaeleza kuwa ukuaji huo unasukumwa na ongezeko la watu, kasi ya ukuaji wa miji pamoja na uwekezaji katika majengo na miundombinu inayokidhi malengo ya uchumi wa kijani.

Kwa nchi za Afrika Mashariki, ambazo zinaendelea kuwekeza katika barabara, reli, viwanja vya ndege, bandari na nyumba, mahitaji ya wahandisi, wasanifu majengo, wapima ardhi, wasimamizi wa miradi na mafundi wenye ujuzi yanatarajiwa kuendelea kuongezeka.

7. Viwanda na uzalishaji

Kazi za usindikaji wa chakula na wafanyakazi wa usindikaji wa chakula na wafanyakazi wa biashara zinazohusiana na usindikaji wa chakula ni miongoni mwa wachangiaji wakubwa wa jumla kwenye sekta ya ajira.

Kundi kubwa la utengenezaji wa hali ya juu wa vifaa vya elektroniki, bidhaa za watumiaji linaonyesha viwango tofauti vya mauzo, na kufikia hadi 50% kwa utengenezaji wa hali ya juu, moja ya viwango vya juu zaidi katika ripoti nzima. Hii inaonyesha mabadiliko ya haraka ya kiteknolojia (roboti, otomatiki).

Sekta nyingine zenye fursa kubwa za ajira

Mbali na sekta 7 zilizotajwa hapo juu, ripoti ya World Economic Forum inaonyesha kuwa sekta nyingine kadhaa pia zinatarajiwa kuendelea kuzalisha ajira nyingi katika miaka ijayo kutokana na uwekezaji, ukuaji wa miji na mabadiliko ya uchumi.

Moja ya sekta hizo ni ujenzi na miundombinu, ambapo mahitaji ya mafundi wa ujenzi, wahandisi, wasanifu majengo na wasimamizi wa miradi yanatarajiwa kuendelea kuongezeka kadri nchi zinavyojenga barabara, reli, nyumba na miundombinu mingine. Ukuaji wa miji na ongezeko la idadi ya watu ni miongoni mwa sababu kuu zinazochochea mahitaji hayo.

Ripoti hiyo pia inaonyesha kuwa nishati mbadala na teknolojia za kijani ni miongoni mwa sekta zinazokua kwa kasi zaidi. Mahitaji ya wahandisi wa nishati jadidifu, wataalamu wa mazingira na mafundi wa kufunga mifumo ya umeme wa jua yanatarajiwa kuongezeka huku dunia ikiendelea kuwekeza katika vyanzo vya nishati visivyochafua mazingira. Katika sekta ya nishati na huduma za matumizi, kiwango cha mabadiliko ya ajira kinakadiriwa kufikia asilimia 46, mojawapo ya viwango vya juu zaidi kwenye ripoti.

Aidha, biashara za jumla na rejareja zitaendelea kuwa chanzo muhimu cha ajira, hasa kutokana na ukuaji wa biashara mtandaoni, mabadiliko ya tabia za walaji na kupanuka kwa masoko ya bidhaa na huduma. Ingawa baadhi ya kazi za kawaida zinatarajiwa kubadilishwa na teknolojia, mahitaji ya wataalamu wa usimamizi wa biashara, ugavi na huduma kwa wateja yanatarajiwa kuendelea kuwepo.

Kwa Afrika Mashariki, sekta hizi zinaweza kuwa miongoni mwa maeneo muhimu ya uwekezaji na uundaji wa ajira, hasa kutokana na miradi mikubwa ya miundombinu, ongezeko la matumizi ya nishati safi na ukuaji wa biashara na miji. Hata hivyo, kama ilivyo kwa sekta nyingine, mafanikio yatahitaji wafanyakazi wenye ujuzi unaoendana na mabadiliko ya teknolojia na mahitaji ya soko la ajira.