Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Marekani yasema inaweza kuendelea na zuio la majini dhidi ya Iran bila ukomo

Kauli hiyo inakuja wakati mazungumzo ya kusitisha vita yakikwama, huku usafirishaji wa mafuta duniani ukiathiriwa na mzozo unaoendelea katika eneo la Mlango wa Hormuz.

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid

  1. Wabunge wa Marekani waeleza wasiwasi kuhusu hali ya meli ya kivita ya USS Abraham

    Wabunge wa chama cha Democratic nchini Marekani wameeleza wasiwasi mkubwa kuhusu hali ya meli ya kubeba ndege za kivita ya Marekani, USS Abraham Lincoln, ambayo imekuwa ikifanya shughuli katika Mashariki ya Kati kwa muda mrefu.

    Wamesema taarifa za upungufu wa mahitaji muhimu, hitilafu katika mabomba ya maji na matatizo mengine ndani ya meli hiyo hazikubaliki.

    Aidha, wameeleza wasiwasi kuhusu uchovu uliokithiri na msongo wa mawazo miongoni mwa wanajeshi, huku kukiwa na taarifa kwamba baadhi yao walijaribu kujirusha baharini.

    Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth, hata hivyo amesema taarifa kuhusu hali ya USS Abraham Lincoln zimewasilishwa kwa njia isiyo sahihi.

    Meli hiyo imekuwa baharini tangu Novemba mwaka jana.

    Soma Pia:

  2. Watu wanne wafariki dunia huku mvua kubwa ikisababisha maporomoko Japan

    Mvua kubwa isiyokuwa ya kawaida katika Mkoa wa Chiba nchini Japan imesababisha vifo vya watu wanne na kuwaacha maelfu ya wasafiri wakikwama usiku kucha katika Uwanja wa Ndege wa Narita jijini Tokyo.

    Mkoa huo, unaopakana na jiji la Tokyo, umerekodi zaidi ya milimita 100 za mvua kwa saa tangu Alhamisi alasiri, kwa mujibu wa mamlaka.

    Kiasi hicho ni takriban mara tatu ya wastani wa mvua inayonyesha nchini Japan mwezi Agosti na ndicho kikubwa zaidi kuwahi kurekodiwa nchini humo.

    Mvua hiyo kubwa ilisababisha kusitishwa kwa huduma za treni, mabasi na teksi, huku zaidi ya kaya 20,000 katika Chiba zikikosa umeme.

    Mamlaka za Japan zimeeleza mvua hiyo kuwa tukio lisilo na mfano.

    Gavana wa Chiba, Toshihito Kumagai, amesema tukio hilo lilikuwa la kipekee hata kwa viwango vya hali ya hewa vya kihistoria nchini Japan.

    “Nimekabiliana na majanga mengi hapo awali, lakini sijawahi kukumbana na hali kama hii,” amesema.

    Ameongeza kuwa serikali itaweka kipaumbele katika kuokoa maisha na kuendelea na shughuli za uokoaji na kurejesha hali ya kawaida.

    Mkazi mmoja wa jiji la Ichikawa, Chiba, ameiambia NHK kuwa mvua hiyo ilianza ghafla na kumshangaza.

    Mvua hiyo ilisababisha Shirika la Hali ya Hewa la Japan kutoa onyo la dharura la kiwango cha tano, ambacho ndicho kiwango cha juu zaidi.

    Onyo hilo lilishushwa hadi kiwango cha nne Ijumaa asubuhi, lakini mamlaka zimeendelea kuwaonya wakazi kuwa waangalifu kutokana na hatari ya maporomoko ya ardhi, mafuriko na kujaa kwa mito.

    Takriban watu 7,000 walikwama usiku kucha katika Uwanja wa Ndege wa Narita, mmoja wa viwanja viwili vikuu vya ndege vya Tokyo, baada ya mvua kusababisha kukatika kwa huduma za usafiri zinazounganisha uwanja huo na maeneo mengine.

    Soma Pia:

  3. Trump atangaza ushuru wa hadi asilimia 100 kwa ndege zisizo na rubani zinazoagizwa kutoka nje

    Rais wa Marekani Donald Trump ametangaza ushuru wa hadi asilimia 100 kwa ndege zisizo na rubani zinazoagizwa kutoka nje pamoja na baadhi ya vipuri vyake.

    Kwa mujibu wa tangazo hilo, ndege kubwa zisizo na rubani zenye uzito wa zaidi ya kilo 25 na zilizo na teknolojia zinazohusishwa na usalama wa taifa, ikiwemo kamera za joto na vituo vya kuziendeshea, zitatozwa ushuru wa asilimia 100.

    Ndege ndogo zisizo na rubani zitatozwa ushuru wa asilimia 25, huku ushuru huo ukitarajiwa kuanza kutekelezwa Septemba 3.

    Utawala wa Trump unasema hatua hiyo inalenga kuhamasisha uzalishaji wa ndege hizo na vipuri vyake nchini Marekani, pamoja na kupunguza utegemezi wa minyororo ya ugavi ya nje, hususan China.

    Mamlaka za Marekani zimeeleza kuwa ndege zisizo na rubani zina matumizi ya kibiashara, lakini pia zinaweza kutumika katika shughuli za kijeshi na kiusalama, ikiwemo ufuatiliaji, ukusanyaji wa taarifa nyeti na mashambulizi.

    Hatua hiyo huenda ikaongeza gharama kwa waagizaji, watumiaji na kampuni zinazotegemea ndege hizo pamoja na vipuri vinavyotengenezwa nje ya Marekani.

    Soma Zaidi;

  4. Marekani yasema inaweza kuendelea na zuio la majini dhidi ya Iran bila ukomo

    Marekani imesema inaweza kuendelea na mzingiro wake wa kijeshi dhidi ya Iran kwa muda usiojulikana, huku ikiendelea kuongeza shinikizo la kiuchumi kwa Tehran.

    Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth, amesema jeshi la Marekani lina uwezo wa kuendeleza mzingiro huo kwa muda wowote unaohitajika kwa kubadilisha meli za kivita zinazopelekwa katika eneo hilo.

    Kauli hiyo inakuja wakati mazungumzo ya kusitisha vita yakikwama, huku usafirishaji wa mafuta duniani ukiathiriwa na mzozo unaoendelea katika eneo la Mlango wa Hormuz.

    Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, amesema malengo makuu ya Washington katika mzozo huo ni kuhakikisha bei za nishati zinabaki katika viwango vinavyoweza kumudu Wamarekani, kuzuia Iran kupata silaha za nyuklia na kuhakikisha Marekani inakuwa katika nafasi imara zaidi kimkakati.

    Rais Donald Trump amekuwa akisisitiza kuwa Marekani inadhibiti kikamilifu Mlango wa Hormuz, wakati Iran ikisema njia hiyo itaendelea kufungwa hadi masharti yake yatimizwe.

    Waziri wa Hazina wa Marekani, Scott Bessent, amesema Washington iko tayari kuchukua hatua za kiuchumi dhidi ya Iran ambazo hazijawahi kutekelezwa katika historia ya kuitenga nchi kiuchumi.

    Bessent amesema Marekani itatangaza hatua zaidi wiki ijayo, huku ikilenga kuongeza shinikizo la kiuchumi kwa Tehran.

    Soma Zaidi Hapa:

  5. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya tarehe 14/08/2026.