Dunia yashuhudia kupatwa kwa Jua

.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 2

Mamilioni ya watu duniani kote walitazama angani Jumatano wakati Mwezi ulipopita moja kwa moja kati ya Dunia na Jua, na kwa muda mfupi kugeuza mchana kuwa giza katika eneo finyu lililoshuhudia kupatwa kabisa kwa Jua.

Kupatwa huko kulionekana katika baadhi ya maeneo ya Afrika Kaskazini, pamoja na Hispania, Iceland, Greenland na kaskazini mwa Urusi, huku maeneo mengi zaidi ya Ulaya, Afrika na sehemu nyingine za dunia yakishuhudia kupatwa kwa Jua kwa kiasi.

Makundi ya watu yalikusanyika katika maeneo mbalimbali kutazama tukio hilo adimu, wengi wakiwa wamevalia miwani maalumu ya kutazamia kupatwa kwa Jua huku Mwezi ukizidi kulifunika Jua. Kwa waliokuwa kwenye njia ya kupatwa kabisa, wakati Mwezi ulipolifunika Jua kikamilifu uliunda giza la kuvutia katikati ya mchana.

Tukio hilo lilikuwa muhimu zaidi barani Ulaya, ambako ilikuwa mara ya kwanza tangu mwaka 1999 kwa kupatwa kabisa kwa Jua kuonekana kutoka bara hilo. Nchini Hispania, kupatwa kabisa kulitokea muda mfupi kabla ya machweo, na kuunda mandhari ya kuvutia angani ambayo watazamaji waliielezea kuwa ya kipekee.

.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Maelezo ya picha, Watu wakikusanyika kushuhudia kupata kwa jua huko Greenwich Park London, Uingereza, Agostt 12, 2026
.

Chanzo cha picha, Getty Images

Maelezo ya picha, Uholanzi walishuhudia pia kupatwa kwa jua
.

Chanzo cha picha, AFP via Getty Images

Maelezo ya picha, Senegal walishuhudia pia

Kupatwa kabisa kwa Jua kutatokea lini tena?

Kwa watazamaji wa anga barani Afrika, fursa kubwa ijayo itakuwa Agosti 2, 2027, wakati kupatwa kabisa kwa Jua kutapita katika baadhi ya maeneo ya Afrika Kaskazini, yakiwemo Morocco, Algeria, Tunisia, Libya na Misri, kwa mujibu wa NASA.

Kupatwa kwa Jua mwaka 2027 pia kutaonekana katika njia inayopita kusini mwa Hispania, Saudi Arabia na Yemen. Sehemu kubwa ya Afrika itashuhudia kupatwa kwa Jua kwa kiasi, ambapo Mwezi utalifunika Jua kwa sehemu tu.

Hilo linaifanya shughuli hiyo ya mwaka 2027 kuwa muhimu hasa kwa watazamaji wa anga barani Afrika, huku nchi kadhaa za Afrika Kaskazini zikitarajiwa kuwa moja kwa moja kwenye njia ya kupatwa kabisa kwa Jua.

Kupatwa kwa Jua kwa kiasi pia kutaonekana katika maeneo makubwa ya Afrika, Ulaya, Mashariki ya Kati na baadhi ya maeneo ya Asia, na hivyo kuwapa mamilioni ya watu fursa ya kushuhudia Mwezi ukipita mbele ya Jua.

.

Chanzo cha picha, Getty Images