Dunia kushuhudia kupatwa kwa jua leo

h

Chanzo cha picha, Nasa/Bill Ingalls (2021)

    • Author, Daisy Stephens
    • Nafasi, BBC World Service
  • Iliyochapishwa
  • Muda wa kusoma: Dakika 4

Siku ya Jumatano, tarehe 12 Agosti, baadhi ya maeneo duniani yatashuhudia kupatwa kwa jua. Katika baadhi ya maeneo kupatwa huko kutakuwa kwa ukamilifu, na katika maeneo mengine kutakuwa kwa sehemu tu.

Hata kama hutaliona moja kwa moja, jiandae kuona picha za kuvutia kutoka sehemu mbalimbali duniani.

Kupatwa kwa jua ni nini?

Tukio hili la angani hutokea wakati Mwezi unapopita katikati ya Dunia na Jua, na kuzuia sehemu au mwanga wote wa Jua usitufikie.

Kuna aina mbalimbali za kupatwa kwa Jua. Aina utakayoweza kuiona inategemea mambo kadhaa, kama vile mahali ulipo duniani na umbali wa Mwezi

m

Kupatwa kwa jua kwa ukamilifu hutokea wakati Mwezi unapojipanga kikamilifu na Jua pamoja na Dunia, na kuufunika kabisa uso wa Jua; hali hii husababisha anga kuwa na giza, kama ilivyo wakati wa mapambazuko au machweo.

Wakati mwingine unaweza kuona mzunguko wa mwanga mkali ukizunguka Jua lililopatwa. Hii ni sehemu ya nje kabisa ya angahewa ya Jua, inayojulikana kama corona, ambayo kwa kawaida hufunikwa na mwangaza mkali wa uso wa Jua.

Utaona kupatwa kwa jua kwa sehemu iwapo utakuwa katika eneo la kivuli cha nje cha Mwezi, kinachoitwa penumbra.

Hali hii hutokea wakati Mwezi unapofunika sehemu tu ya Jua.

n

Chanzo cha picha, Space Frontiers/Hulton Archive/Getty Images (left); Rebecca Harding/Getty Images (right)

Maelezo ya picha, Tabaka la nje kabisa la angahewa ya Jua wakati mwingine huonekana wakati wa kupatwa kwa Jua kwa ukamilifu (kushoto), huku diski angavu ya Jua ikionekana wakati wa kupatwa kwa Jua kwa umbo la pete (kulia).

Kupatwa kwa Jua kwa aina ya 'annular' (ambapo Jua huonekana kama pete) hutokea wakati Mwezi unapokuwa mbele ya Jua lakini ukiwa mbali sana na Dunia kiasi cha kushindwa kulifunika kabisa. Njia ya mzunguko wa Mwezi ina umbo la duaradufu—yaani si duara kamilifu—na iwapo Mwezi utapita mbele ya Jua ukiwa katika sehemu ya mbali zaidi na Dunia au karibu na sehemu hiyo, huonekana mdogo zaidi kwetu.

Katika aina hii ya kupatwa kwa Jua, bado unaweza kuona sehemu angavu ya Jua ikizunguka Mwezi.

Aina hizi za kupatwa kwa Jua ni tofauti kabisa na kupatwa kwa Mwezi, ambapo Dunia ndiyo inayokaa katikati ya Jua na Mwezi na kutupa kivuli chake juu ya Mwezi.

Kupatwa kwa jua kutatokea lini na wapi?

Kupatwa kwa jua kutatokea siku ya Jumatano, tarehe 12 Agosti.

Itakuwa ni kupatwa kwa jua kamili katika maeneo ya kaskazini mwa Urusi, Greenland, Iceland, Uhispania na Ureno.

A graphic of the globe showing which areas will see 100%, 90%, 75%, 50%, 30% and 10% of the Sun during the August 2026 eclipse; a red arrow shows the path of totality moving eastwards.
Maelezo ya picha, To request:Complete the translations here: https://tinyurl.com/36hj3my5Fill-in the commissioning form https://bit.ly/ws_design_form with this title in English: Solar eclipse - 2026080304

Kulingana na NASA, tukio la kufunikwa kabisa kwa Jua litatokea wakati wa mchana katika eneo dogo na la mbali kaskazini mwa Urusi.

Kisha, kivuli hicho kitasonga kuelekea mashariki kuzunguka dunia, na kufika Uhispania jioni kabla ya jua kuzama.

Tukio hilo litakuwa la muda mfupi, huku hatua ya kufunikwa kabisa kwa Jua ikichukua muda usiozidi dakika mbili na nusu.

Maeneo ya kaskazini mwa Marekani, Canada, kaskazini-magharibi mwa Afrika na Ulaya yatashuhudia kupatwa kwa Jua kwa sehemu, ambapo katika baadhi ya maeneo zaidi ya asilimia 90 ya Jua litafunikwa.

Tukio hilo litakuwa la kipekee zaidi katika baadhi ya maeneo ya Afrika na bara la Ulaya kwani kutakuwa na kupatwa kwa Jua wakati wa machweo, yaani Jua litazama likiwa bado limefunikwa kwa sehemu.

Ninawezaje kutazama kupatwa kwa jua?

Ni muhimu usijaribu kutazama moja kwa moja tukio la kupatwa kwa jua, hata iwapo umevaa miwani ya kawaida ya jua; kwani miwani hiyo haitoi kinga ya kutosha.

Kufanya hivyo kunaweza kusababisha uharibifu wa kudumu kwenye sehemu ya nyuma ya jicho (retina).

Tazama jua tu ikiwa umevaa miwani maalum ya kutazama kupatwa kwa jua, ambayo ni myeusi zaidi mara elfu kadhaa kuliko miwani ya kawaida ya jua. Tafuta miwani inayokidhi viwango vya kimataifa vya ISO 12312-2.

Pia, usitazame kupitia lenzi ya kamera, darubini, miwani ya mbali (binoculars) au kifaa chochote kingine cha macho—hata kama umevaa miwani hiyo maalum ya kupatwa kwa jua.

Shirika la NASA linasema kuwa miale ya jua iliyojikita sehemu moja inaweza kutoboa kichujio cha miwani na kujeruhi jicho lako.

Unaweza pia kutumia njia zisizo za moja kwa moja kutazama taswira ya jua iliyokadiriwa (projected) kwenye uso fulani.

n

Chanzo cha picha, Steve Russell/Toronto Star/Getty Images

Maelezo ya picha, Unaweza kutumia chujio, au kipande cha kadibodi chenye tundu ndogo, kutengeneza kifaa cha kuonyesha picha kwa kutumia tundu hiyo..

Njia moja ni kuchukua vipande viwili vya kadibodi. Ukiwa umelipa Jua mgongo , viinue mbele yako juu ya mabega yako, kimoja kikiwa nyuma ya kingine, ili kadibodi iliyo karibu nawe itupie kivuli kwenye ile kadibodi nyingine.

Ukiunda tundu ndogo kwenye kadibodi iliyo karibu nawe, miale ya Jua itapita humo na kuunda umbo la duara dogo kwenye kadibodi iliyo nyuma. Unaweza pia kutumia kifaa chenye matundu, kama vile chujio, badala ya ile kadibodi ya mbele.

Kisha utaweza kuona Mwezi ukiziba taratibu duara hilo la mwanga kadiri tukio la kupatwa kwa Jua linavyoendelea.

Na ikiwa njia hizo hazitafanikiwa au hali ya hewa itakuwa kikwazo, kutakuwa na matangazo kadhaa ya moja kwa moja mtandaoni, likiwemo lile la NASA.