Wanasayansi waja na nguo ya ndani inayotambua mara ngapi unatoa ushuzi

Iliyochapishwa
Muda wa kusoma: Dakika 6

Sensa mpya inayovaliwa ndani ya nguo za ndani hukaa kwenye nguo yako na kunusa gesi unazotoa, kwa matumaini ya kubaini dalili zinazoweza kueleza afya ya utumbo wako.

Swali la binafsi: Je, unajiona kuwa mtu anayetoa gesi mara nyingi? Kwa wastani wa siku moja, unatoa gesi mara ngapi, tano? 20? Zaidi?

Hakuna jibu la kijinga kwa swali hilo, kwa sababu wanasayansi wamegundua hivi karibuni kwamba vitabu vyetu vya elimu vina taarifa chache sana kuhusu gesi za tumboni za binadamu.

Machapisho mengi ya kitabibu mara nyingi hudai kwamba mtu wa kawaida hutoa gesi kati ya mara 5 hadi 15 kwa siku, lakini makadirio hayo yanatokana na tafiti chache zilizofanywa miaka ya 1980, anasema Profesa Brantley Hall, ambaye anachunguza microbiome ya utumbo wa binadamu katika Chuo Kikuu cha Maryland nchini Marekani.

"Kuna tafiti kadhaa, lakini zilikuwa za undani. Zilihusisha matumizi ya mirija iliyowekwa kwenye puru (rektamu)," anasema. "Kwa kweli, hatujafanya maendeleo makubwa katika kuongeza uelewa wetu kuhusu jambo hili tangu wakati huo."

Mpaka sasa, hali imekuwa hivyo. Hall na timu yake wanaunda kile wanachokiita Atlasi ya Gesi za Binadamu (Human Flatus Atlas) ili kubainisha kiwango cha kawaida cha kutoa gesi tumboni katika jamii ya binadamu.

Kiini cha mradi huu ni nguo za ndani mpya za kisasa zenye vihisi (smart underwear) zinazoweza kutambua gesi zinazotolewa na mwili wa binadamu.

Kihisi chenye ukubwa wa sarafu ndogo hufungwa kwa siri ndani ya nguo ya ndani ya kawaida. Kikiwa hapo, hutambua utolewaji wa gesi mchana na usiku na kutuma taarifa husika kwenye programu ya simu, ambapo watumiaji au watafiti wanaweza kufuatilia mara na viwango vya utoaji wa gesi.

Katika utafiti uliochapishwa mwezi Desemba 2025 katika jarida la Biosensors and Bioelectronics: X, washiriki 38 walivaa nguo hizo za ndani za kisasa kwa zaidi ya saa 11 kwa siku kwa angalau siku tatu. Vihisi hivyo vilionesha kwamba watu hutoa gesi mara nyingi zaidi kuliko ilivyodhaniwa hapo awali.

Watu wazima wenye afya njema hutoa gesi tumboni wastani wa mara 32 kwa siku, ingawa idadi hiyo ya wastani pekee haielezi picha nzima.

Inaonekana kwamba kuna tofauti kubwa sana kutoka kwa mtu mmoja hadi mwingine linapokuja suala la kutoa hewa tumboni. Katika utafiti huo, washiriki walikuwa na viwango vilivyotofautiana kutoka kutoa gesi mara nne kwa siku hadi mara 59 kwa siku. Takwimu ambazo bado hazijachapishwa kutoka kwa tafiti zinazoendelea zinaonesha tofauti kubwa zaidi.

"Tulikuwa na mtu mmoja aliyekuwa akitoa gesi mara 175 kwa siku," Hall anasema. "Kisha kulikuwa na mtu mwingine, akiwa kwenye lishe ileile, ambaye alitoa gesi mara nne tu."

Kilicho nyuma ya nguo yako

Ufahamu huu wa kuvutia kuhusu gesi za tumboni unatokana na teknolojia ambayo timu hiyo imekuwa ikiiboresha kwa miaka mitano.

Hall anacheka anaposimulia chanzo cha ugunduzi huo.

"Mimi ni mtaalamu wa mikrobiolojia, na siku moja tulikuwa tukichunguza jinsi vijiumbe vidogo vinavyotekeleza michakato yao ya kimetaboliki ndani ya chumba kisicho na oksijeni," anasema.

"Mambo hayakuwa yanaenda vizuri. hatukufurahia, tukatoa kihisi (sensor) kutoka kwenye chumba hicho, halafu mmoja wetu akaachia gesi juu yake, na ghafla tukapata ishara ya ajabu sana!"

Tangu siku hiyo muhimu, kihisi hicho kimefika mahali ambapo vifaa vingi vya kuvaliwa havijawahi kufika hapo awali, yaani ndani ya suruali yako. Kifaa hicho hugundua haidrojeni, mojawapo ya gesi zinazozalishwa wakati bakteria waliomo kwenye utumbo wetu wanapovunjavunja chakula kupitia michakato ya kimetaboliki.

Kuna pia gesi nyingine zinazohusika katika mchanganyiko huo, na Hall anatumaini kwamba matoleo yajayo ya teknolojia hiyo yataweza kuzitambua pia. Hata hivyo, teknolojia ya sasa inaweza kugundua tu kile anachokiita H-bombs, akimaanisha gesi ya haidrojeni.

"Hiyo inatosha kwa watafiti kupima mzunguko wa utoaji wa gesi tumboni na kuanza kukusanya taarifa za Atlasi ya Gesi za Binadamu. Hall anasema kuwa idadi ya watu wanaojitolea kushiriki katika tafiti za timu yake imezidi nafasi zilizopo, jambo linalothibitisha mafanikio yao katika kubuni kifaa ambacho ni rahisi na chenye starehe kuvaliwa."

"Jambo lililotushangaza zaidi ni kwamba kuna nafasi katika eneo hilo," anasema. "Hutaihisi kabisa. Tulijaribu maumbo mengi na vifaa vya aina mbalimbali. Mwishowe tuligundua kwamba umbo la duara ndilo linalofaa zaidi, kwa sababu hakuna njia isiyo sahihi ya kuivaa."

Wakati wa mazungumzo yetu kwa video, anainua mfano wa kile anachokiita "sanamu ya makalio" kuonesha mahali kihisi hicho huwekwa.

"Huenda hapo," anasema huku akionesha kwa kidole, "karibu na eneo la msamba (perineum). Kuna nafasi hapo. Unapokaa chini, kifaa hicho hakigusani moja kwa moja na mwili wako."

"Na, unajua, wanawake huweka pedi za hedhi kwenye nguo zao za ndani na hawapati shida yoyote. Kifaa chetu ni kidogo zaidi kuliko pedi ya kawaida ya hedhi."

Jaribio la kunusa

Kadiri watu wengi zaidi wanavyovaa nguo za ndani mahiri za Hall, ndivyo tutakavyojifunza zaidi kuhusu kazi hii ya kawaida ya mwili ambayo, licha ya vicheko na mzaha unaoambatana nayo, inaweza kutuambia mengi kuhusu afya ya mfumo wetu wa mmeng'enyo wa chakula.

Kwa kiasi kikubwa, kutoa gesi tumboni ni jambo la kawaida kabisa na ni ishara ya afya njema. Kwa hakika, watu wanaokula lishe bora yenye nyuzinyuzi nyingi ni miongoni mwa wanaotoa gesi mara nyingi zaidi, kwa sababu gesi nyingi huzalishwa wakati vyakula vyenye nyuzinyuzi nyingi kama vile jamii ya kunde na mboga vinapochachushwa ndani ya utumbo.

Kutoa gesi ni kiashiria muhimu cha afya ya utumbo kwa ujumla. Kunaweza kuwa dalili ya ugonjwa wa utumbo (irritable bowel syndrome - IBS) au kutovumilia aina fulani za vyakula.

Mabadiliko katika tabia au mara ngapi mtu hutoa gesi yanaweza kuashiria mabadiliko katika mikrobiomu ya utumbo, ambayo yanaweza kuhusishwa na kuongezeka kwa msongo wa mawazo au matatizo yanayohusiana na lishe. Gesi nyingi kupita kiasi, au zenye harufu kali isiyo ya kawaida, zinaweza kuwa ishara kwamba mwili wako hauvumilii lactose au gluteni.

Na ikiwa mara kwa mara kutoa gesi kunaambatana na dalili nyingine kama kuhara, maumivu au kuvimbiwa kwa tumbo kutokana na gesi, ni vyema kumwona daktari wako kwa ushauri na uchunguzi zaidi.

Hall anasema kuwa tofauti za jinsi watu wanavyotoa gesi zinaweza kusababishwa na mambo kadhaa.

"Vinasaba vya binadamu, lishe na mikrobiomu ya utumbo vyote vinaathiri jinsi tunavyotoa gesi na mara ngapi tunatoa gesi," anasema.

"Kwa mfano, ikiwa mwili wako hauvumilii lactose, hiyo ni sababu ya kinasaba. Lakini ikiwa una tatizo hilo, basi lishe nayo ina nafasi kubwa, kwa sababu ukinywa maziwa utatoa gesi nyingi zaidi."

Hall anaamini kwamba teknolojia ya nguo za ndani mahiri inaweza kuwa njia nyingine inayowapa watu uwezo wa kufuatilia afya zao wenyewe, huku pia ikiwapatia madaktari taarifa zaidi za kuwasaidia wagonjwa wao.

"Kwa sasa hatuna kibali cha matumizi ya kimatibabu kwa kifaa hiki, hivyo kinatumika kwa ajili ya utafiti pekee. Lakini katika siku zijazo, tungependa madaktari na wataalamu wa magonjwa ya utumbo waweze kutumia taarifa hizi kusaidia kufanya maamuzi yao ya kitabibu. Ili kujua nini si cha kawaida, lazima kwanza uelewe ni nini kilicho cha kawaida," anasema.

Hall anatumaini kwamba siku moja tutafikia hatua ambapo kila mtu atakuwa na aina ya "alama ya gesi tumboni", ambayo inaweza kutoa taarifa kuhusu afya yake, sawa na jinsi viwango vya mafuta au shinikizo la damu vinavyotumika leo kutathmini afya.

Mojawapo ya hatua zinazofuata ni kuongeza uwezo wa kugundua gesi ya methane, ambayo kitabibu imehusishwa na tatizo la kufunga choo au kupata choo kigumu. Baadaye, timu hiyo inatarajia kupanua utafiti wake kimataifa ili kubaini jinsi tabia za watu kutoa gesi katika nchi nyingine zinavyolingana au kutofautiana na zile za Marekani.