Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
"Sikujua mpenzi wangu alikuwa akinibaka ninapolala "
- Author, Caroline Lowbridge
- Nafasi, BBC News
- Iliyochapishwa
- Muda wa kusoma: Dakika 7
"Kwangu mimi, hadi siku moja kabla hajakiri alichokuwa amefanya, huu ulikuwa uhusiano bora zaidi kuwahi kuwa nao maishani."
Adelle Overton alikuwa katika uhusiano wa miaka 13 na Steven Uden, ambaye alionekana kuwa mwenzi kamili kwake.
Walikutana wakati wa utengenezaji wa filamu ya watu waliogeuka kuwa mizuka, na walikuwa na mambo mengi waliyopenda kwa pamoja.
Anasema Uden alikuwa mtu mwenye upendo na anayejali, na hata aliacha kazi yake ili kuwa mlezi wake baada ya Overton kuwa na ulemavu.
"Alikuwa mtu mzuri sana. Nilimpenda sana, na nadhani bado ninampenda kidogo," anasema Overton akiwa ameketi kwenye sofa nyumbani kwake Derby, Uingereza.
Overton alimwamini Uden, lakini imani hiyo ilivunjika baada ya Uden kukiri kuwa alikuwa amembaka alipokuwa amelala.
"Nilihisi kusalitiwa mara moja. Sijawahi kujisikia salama kiasi hicho katika uhusiano wowote hapo kabla," anaeleza Overton.
Uden alikuwa amemtunza wakati alipokuwa akipokea matibabu ya saratani ya matiti, lakini baadaye aliiambia polisi kuwa alimbaka akiwa chini ya athari za dawa.
"Nilihisi kusalitiwa, kwa sababu nilidhani namfahamu, kumbe sikujua yeye ni nani hasa," anasema Overton.
"Na kufikiria kwamba alikuwa ameishi nami kwa miaka 13. Alisaidia kuwalea watoto wangu. Nilidhani niko salama nikiwa naye, kumbe sikuwa salama."
Uden sasa yuko gerezani na Overton ameamua kusimulia yaliyompata kwa matumaini kwamba uzoefu wake unaweza kuwasaidia watu wengine.
Penzi lililoanza kwa furaha
Overton na Uden walikutana mwaka 2009 wakati wa utengenezaji wa filamu ya watu waliogeuka kuwa mizuka mjini Nottingham, wakati Overton akiwa na miaka 29 na Uden akiwa na miaka 27.
Uden alikuwa msanii wa vipodozi na mwigizaji, huku Overton pia akiwa miongoni mwa waigizaji. Wote walikuwa katika mahusiano na watu wengine, lakini waliendelea kuwa marafiki.
Hatimaye walianza uhusiano wa kimapenzi Januari 13, 2012. Overton anakumbuka tarehe hiyo kwa sababu waliadhimisha kwa kutazama kwa mfululizo filamu za "Friday the 13th".
Kwa mujibu wake, kuwa na Uden kulikuwa tofauti na mahusiano aliyowahi kuwa nayo awali.
"Alikuwa mcheshi, mwenye kujali na alinifanya nijisikie kupendwa," anasema.
Walikutana kwa njia isiyo ya kawaida na pia waliishi maisha yasiyo ya kawaida.
Wote walifanya kazi kama "mizuka wa kitaalamu" katika kampuni iliyokuwa ikiandaa matukio ya kujinusuru dhidi ya watu waliogeuka kuwa mizuka, yaliyochochewa na filamu za kutisha kuhusu mizuka.
Kazi hiyo ilihitaji shughuli nyingi za kimwili, lakini Overton alilazimika kuiacha mwaka 2017 baada ya kugundulika kuwa na ugonjwa wa Ehlers-Danlos.
Mwanzoni mwa mwaka 2018, Uden akawa mlezi wake.
"Alikuwa akinifanyia karibu kila kitu," anakumbuka.
Kwa mtazamo alionao sasa, Overton, ambaye marafiki zake humuita Dell, anaamini Uden alianza kuonyesha tabia za kumdhibiti.
"Alipenda kuwaambia watu kile nilichokuwa na uwezo wa kufanya na kile ambacho sikuwa na uwezo wa kufanya," anaeleza.
"Kama mtu angependekeza tufanye shughuli fulani, alifurahia kujibu, 'Sidhani kama Dell anaweza kufanya hivyo; hebu tufikirie jambo lingine.''
Matatizo ya usingizi
Lakini sasa Overton anajua kuwa tabia ya Uden ilikuwa na upande wa kutisha zaidi kuliko alivyowahi kufikiria.
Alianza kuwa na mashaka mwaka 2020, alipokuwa akipokea chemotherapy kwa ajili ya saratani ya matiti.
"Sijui kama usumbufu wa mwili ulikuwa umeongezeka, lakini niliamka wakati akiwa anafanya hivyo. Alitoa visingizio vingi, kama vile, 'Nilidhani ulikuwa umeamka na ulikuwa ukitoa sauti hizo,'" anasema.
"Nilifikiria kuhusu msongo wote tuliokuwa tukipitia, na yeye akasema lilikuwa kosa," anaongeza.
Hivyo Overton aliweka kando mashaka yake.
"Nadhani ilikuwa rahisi zaidi kuamini uongo huo kuliko kukabiliana na maana ya ukweli," anasema.
Overton alianza kupata matatizo ya usingizi.
"Nadhani mahali fulani ndani ya akili yangu, ubongo wangu haukujisikia tena salama nilipokuwa nimelala," anasema.
Pia anasema alianza kupata ugumu wa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Uden na akaanza kuota ndoto mbaya zaidi zinazohusiana na unyanyasaji wa kingono aliowahi kufanyiwa hapo awali.
"Wakati huo nilidhani nilikuwa nahusisha jambo hilo na majeraha yangu ya zamani, na kwamba nilikuwa nikimhukumu yeye na alichokuwa amefanya kwa ukali zaidi kwa sababu ya majeraha hayo," anaeleza.
"Nilianza kujisikia mwenye hatia na kujilaumu kwa kila kitu," anasema.
Kukiri kwa Uden
Uden hakukiri hadi miaka mitano baadaye, mwaka 2025, wakati yeye mwenyewe alipokuwa akipokea matibabu ya saratani, katika kesi yake akiwa na uvimbe kwenye utumbo.
"Nadhani kuna kitu kilikuwa kinamsumbua, kwa sababu sasa aliona, kwa upande mwingine, kile nilichokuwa nimepitia," anasema Overton.
"Alisisitiza sana kwamba sikuwa nimejitunza vizuri wakati wa matibabu yangu."
Jambo hilo lilimkumbusha Overton tukio la miaka mitano iliyopita, wakati alipoamka na kumkuta Uden akifanya naye ngono.
Anasimulia: "Nilimsukuma. 'Unamaanisha nini? Unamaanisha nini kwamba sikukutunza vizuri? Kwa namna gani?'"
Wakati fulani katika mazungumzo hayo, ambayo Overton anasema yalidumu kwa siku mbili, Uden alimpigia simu rafiki yake na kukiri alichokuwa amefanya.
Kisha alirejea nyumbani na kukiri kwake.
Overton alihisi kusalitiwa na kushtuka, lakini hakumaliza uhusiano huo mara moja. Alimtegemea kwa mambo mengi na, zaidi ya yote, bado alimpenda.
Wakati huo Overton alikuwa tayari akishiriki katika tiba ya kikundi kwa ajili ya unyanyasaji wa kingono aliowahi kupitia hapo awali, na alieleza kuhusu tukio hilo katika kikao chake kilichofuata.
"Mmoja wa wataalamu wa tiba ndiye aliyenifanya nichukue hatua," anakumbuka.
"Nilikuwa nimevunjika moyo, nikilia bila kukoma na kuuliza, 'Nifanye nini? Nifanyeje aache?' Naye akajibu, 'Mtoe nyumbani na upige simu polisi.'"
Anaendelea: "Baadaye siku hiyo hiyo aliniambia kwamba walifanya kikao na kuamua kuwa wao ndio wangewasiliana na polisi. Wakati huo nilielewa kuwa hali hiyo haikuwa tena inategemea mimi pekee."
Uchunguzi
Kesi hiyo ilipelekwa kwa Mkuu wa Upelelezi, Eleanor Kirton wa Kituo cha Polisi cha Derbyshire.
"Jambo la kwanza nililofanya lilikuwa kuwasiliana na Adelle. Kwa kueleweka, alikuwa ameathirika sana na kilichokuwa kimetokea," anaeleza mpelelezi huyo.
Baada ya kumhoji Overton, polisi walimkamata Uden.
"Nilipomhoji, alikiri mara moja," anasema Kirton.
"Kuanzia mwanzo alikiri kwamba alikuwa amembaka, jambo ambalo ni nadra sana katika aina hii ya uchunguzi," anaongeza.
Uden alishtakiwa kwa makosa mawili ya ubakaji. Baadaye alikiri mashtaka hayo mahakamani na kuhukumiwa kifungo cha miaka sita na miezi minane jela.
Kirton anasema hatua zilizochukuliwa na Overton zimesaidia kuwalinda wanawake wengine.
"Ujasiri na uthabiti wake umewezesha kuwalinda watu wengine wengi ambao huenda wangekuwa waathirika wa mwanaume huyu," anasema.
"Kama kuna mtu anayefikiri huenda jambo kama hili linamtokea, ningemhimiza sana aje azungumze nasi. Kuna mambo tunayoweza kufanya, na kesi hii imethibitisha hilo."
Hata hivyo, Overton bado haelewi kwa nini mwanaume ambaye alionekana kuwa mwenzi mwenye upendo kwa miaka 13 alimvamia kingono alipokuwa amelala.
"Sielewi jinsi mtu anaweza kupata raha kutokana na mtu ambaye hajibu. Hilo ndilo ambalo halikuwa na maana kwangu," anasema.
"Nilikuwa na upendeleo fulani, sijui nielezeje, wa wanawake waliolala. Nilitaka awe amelala na asiwe anajua nilichokuwa nikifanya," alikiri Uden.
Overton anashuku kuwa Uden alimtumia dawa zake mwenyewe za kumfanya alale, ambazo alikuwa na udhibiti kamili juu yake.
"Nilikuwa na vijisanduku vya kuhifadhia vidonge na yeye ndiye aliyekuwa akiandaa dawa zangu zote," anaeleza.
"Sasa nina dawa chache sana za usingizi kuliko nilivyokuwa nazo awali, na nina mashaka makubwa kwamba alikuwa akinipa dozi kubwa kupita kiasi ili niendelee kulala."
Kirton anasema hilo ndilo polisi waliloliita "kesi ya zamani", hivyo uchunguzi wa kitaalamu na vipimo vya sumu mwilini havikuweza tena kubaini kama jambo hilo lilikuwa limetokea.
Aidha, hakuna ushahidi uliowasilishwa kuhusu tuhuma hiyo mahususi wakati wa kesi.
Hata hivyo, Uden alikiri kwa polisi kwamba alimbaka Overton mara moja wakati alipokuwa akipokea chemotherapy, matibabu ambayo husababisha uchovu.
"Yeye mwenyewe ndiye aliyelitaja jambo hilo," anaeleza Kirton.
Anaongeza: "Alikiri kwamba alikuwa akipokea chemotherapy na alikubali kuwa alikuwa chini ya athari za dawa wakati tukio hilo lilipotokea."
Ingawa Uden alishtakiwa rasmi kwa makosa mawili ya ubakaji, Overton anaamini unyanyasaji huo ulitokea mara nyingi zaidi.
"Aliniambia alikuwa amefanya hivyo mara saba au nane," anasema.
Binti yake, Shari Overton, anasema imekuwa vigumu kushuhudia madhara ambayo uhalifu wa Uden umemsababishia mama yake.
"Sasa amekuwa mtu tofauti sana. Naweza kuona kwamba kujiamini kwake kumepungua sana," Shari anaeleza.
"Lakini pia ninajivunia sana kwa kuchukua hatua, kuzungumza na polisi, kufika mahakamani na kujitetea," anaongeza.
Overton anatumaini simulizi yake itasaidia kuwaonyesha watu wengine walio katika mazingira ya utegemezi kwamba hawalazimiki kuvumilia unyanyasaji kutoka kwa watu wanaopaswa kuwahudumia.
"Ninahisi ninapaswa kuzungumza kuhusu hili kwa sababu limenifanya nifikirie ni watu wangapi wenye ulemavu wanaweza kujikuta katika hali ambayo mtu mwingine ana mamlaka na udhibiti juu yao," anasema.
"Kwa miezi michache baada ya kugundua kila kitu, hata nilifikiria labda ilikuwa aina fulani ya malipo kwa huduma alizonipa. Kwamba nilikuwa namdaiwa kumpa ukaribu huo wa kimapenzi. Lakini haikuwa hivyo. Na hakuna mtu mwingine anayemdai hilo pia," anahitimisha.