Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.

Bofya kuelekea tovuti kuu

Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data

Moja kwa moja, Iran: Hormuz kufunguliwa ndani ya siku saba iwapo Marekani itakubali masharti yake

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, amesema katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwamba Tehran, kupitia wapatanishi, imewasilisha mpango wa kufungua tena Mlango wa Bahari wa Hormuz.

Moja kwa moja

Na Mariam Mjahid & Ambia Hirsi

  1. Watu 41 wafariki katika ajali ya boti ziwa Tanganyika

    Takriban watu 41 wameripotiwa kufariki dunia baada ya boti waliyokuwa wakisafiri kutoka Kigoma, Tanzania, kuelekea Kalemie katika Mkoa wa Tanganyika, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, kupinduka katika Ziwa Tanganyika siku ya Alhamisi.

    Waziri wa Uchukuzi wa Mkoa wa Tanganyika, Norris Mulongoyi, amesema boti hiyo ilikuwa imebeba takriban watu 100 pamoja na mizigo ilipopata ajali karibu na kijiji cha Mapera.

    Kwa mujibu wa Mulongoyi, watu 49 wameokolewa huku juhudi za kuwatafuta manusura na miili ya waliokufa maji zikiendelea.

    Chanzo cha ajali hiyo hakijajulikana, lakini matukio ya vyombo vya majini kukumbwa majini yamekuwa yakiripotiwa mara kwa mara nchini Kongo.

    Wataalamu wamekuwa wakihusisha baadhi ya ajali hizo na upakiaji wa kupita kiasi wa abiria au mizigo pamoja na ukosefu wa vifaa muhimu vya usalama, ikiwemo jaketi za kuokoa maisha.

    Ziwa Tanganyika ni mojawapo ya maziwa makubwa ya maji baridi duniani na ni njia muhimu ya usafiri na biashara kwa maelfu ya wakazi wa eneo hilo.

    Katika sehemu nyingi za vijijini nchini Kongo, usafiri wa majini hubaki kuwa tegemeo kuu kutokana na changamoto za miundombinu ya barabara.

  2. NECTA yabadilisha ratiba ya mitihani kutokana na tahadhari ya El Nino

    Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limebadilisha ratiba ya mitihani na upimaji wa kitaifa wa mwaka 2026 kutokana na tahadhari ya uwezekano wa mvua kubwa za El Niño.

    Kwa ratiba mpya, Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Nne utafanyika Oktoba 5 na 6, badala ya Oktoba 21 na 22.

    Upimaji wa Kitaifa wa Darasa la Pili sasa utafanyika Oktoba 7 na 8, badala ya Novemba 17 na 18, huku Upimaji wa Kitaifa wa Kidato cha Pili ukifanyika Oktoba 12 hadi 23, badala ya Novemba 2 hadi 13.

    Kwa upande wa Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne, ambao awali ulipangwa kufanyika Novemba 9 hadi 27, sasa utafanyika kuanzia Oktoba 19 hadi Novemba 6, 2026.

    Mabadiliko hayo yametangazwa Ijumaa, Septemba 25, 2026, na Naibu Waziri wa Elimu, Wanu Hafidh Ameir, ambaye amesema yanalenga kuhakikisha usalama wa wanafunzi na wasimamizi pamoja na kulinda vifaa na nyaraka za mitihani.

    Amesema wizara imefanya uamuzi huo baada ya kupokea taarifa kutoka mikoa mbalimbali kuhusu maandalizi ya kukabiliana na athari zinazoweza kusababishwa na mvua hizo.

    “Lengo la marekebisho ya ratiba ni kuhakikisha usalama wa wanafunzi, walimu, wasimamizi na maofisa wengine wanaohusika na uendeshaji wa mitihani, pamoja na kulinda mitihani, vifaa na nyaraka za mitihani iwapo mvua kubwa zitatokea mwezi Novemba 2026,” amesema.

    Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa NECTA, Profesa Said Mohamed, mabadiliko hayo yamefanywa katika ratiba ya upimaji na mitihani ya kitaifa iliyokuwa imepangwa kufanyika Oktoba na Novemba mwaka huu.

    Wizara imesema usalama wa wanafunzi, walimu, wasimamizi na maofisa wengine pamoja na ulinzi wa mitihani na vifaa vyake ni miongoni mwa mambo yaliyozingatiwa katika kufanya marekebisho hayo.

  3. Saudi Arabia, Uturuki na Pakistan zakutana kujadili mashambulizi ya Houthi

    Saudi Arabia, Uturuki na Pakistan zimefanya kikao cha dharura cha ngazi ya juu kujadili namna ya kuisaidia Saudi Arabia, wakati mashambulizi ya WaHouthi kutoka Yemen yakiongezeka.

    Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi hizo tatu wamejadili hali hiyo na kulaani mashambulizi yanayolenga Makka na maeneo mengine ya raia. Pia wamethibitisha kuwa Saudi Arabia ina haki ya kujilinda.

    Nchi hizo zinapanga pia kukutana kwa makamanda wao wa kijeshi ili kujadili namna ya kuisaidia Saudi Arabia, kwa kutumia makubaliano yao ya ulinzi wa pamoja. Makubaliano hayo yanaeleza kuwa shambulio dhidi ya nchi moja linachukuliwa kuwa shambulio dhidi ya nchi zote.

    WaHouthi wamesema Alhamisi walifanya mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani dhidi ya maeneo ya Saudi Arabia. Kwa upande wake, Saudi Arabia imesema imefanikiwa kuyadungua makombora sita ya balestiki yaliyofyatuliwa na WaHouthi.

    Saudi Arabia pia imetoa tahadhari za dharura katika maeneo kadhaa, yakiwemo Makka, Jeddah na Yanbu, ambayo ni bandari muhimu kwa usafirishaji wa mafuta.

    Wakati huohuo, Mufti Mkuu wa Saudi Arabia ameitaka jeshi kuwa tayari kutoa maisha yao katika mapambano dhidi ya WaHouthi hadi kundi hilo liondolewe madarakani.

    Kikao hicho kinafanyika wakati Rais wa Iran, Masoud Pezeshkian, akisema WaHouthi wanapaswa kuwajibika kwa matendo yao, kauli inayotafsiriwa kama juhudi za kuitenga serikali ya Iran na mashambulizi hayo.

    Wakati huohuo, Iran na Marekani zinaendelea na mazungumzo ya kidiplomasia ya kupunguza mvutano. Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, amesema Tehran imependekeza kufunguliwa tena kwa Mlango wa Bahari wa Hormuz iwapo Marekani itapunguza shinikizo la kijeshi na vikwazo dhidi ya Iran.

    Vita na mvutano katika eneo hilo umeathiri usafirishaji wa mafuta na bidhaa, hasa kupitia Mlango wa Bahari wa Hormuz, njia muhimu inayotumika kusafirisha mafuta duniani.

  4. Rais wa China Xi Jiping amuonya Trump awe makini kuhusu Taiwan

    Rais wa China, Xi Jinping, amemtaka Rais wa Marekani, Donald Trump, kuwa makini katika kushughulikia suala la Taiwan.

    Kwa mujibu wa shirika la habari la China, Xinhua, Xi amesema China inatarajia Marekani kusimamia msimamo unaopinga Taiwan kujitenga na China.

    Xi ameitaka Washington “kushughulikia kwa umakini suala la Taiwan”, akisema hatua hiyo ni muhimu kwa kuimarisha ushirikiano kati ya China na Marekani.

    China inaiona Taiwan kuwa sehemu ya eneo lake, lakini Taiwan imekuwa ikijitawala yenyewe kwa miongo kadhaa.

    Katika miaka ya hivi karibuni, serikali ya Xi imeongeza shinikizo na vitisho dhidi ya Taiwan, ikitaka kuzuia hatua zozote za kujitenga na China.

    Kwa upande mwingine, Marekani haina uhusiano rasmi wa kidiplomasia na Taiwan, lakini ina wajibu wa kisheria kuisaidia Taiwan kujilinda.

    Hata hivyo, Washington imekuwa ikijaribu kusawazisha uhusiano wake na Taiwan huku ikiendelea kudumisha uhusiano wa kidiplomasia na Beijing.

  5. Ikulu ya Marekani yawaruhusu tena CNN, MS NOW na Politico

    Ikulu ya Marekani imeruhusu tena waandishi wa CNN, MS NOW na Politico kuingia katika eneo la Ikulu baada ya jaji kuamuru warejeshewe ruhusa hiyo.

    Jaji wa Marekani, Tim Kelly, alisema uamuzi wa Rais Donald Trump kuwazuia waandishi wa vyombo hivyo huenda ulikuwa kinyume na Katiba ya Marekani.

    Jaji huyo aliamuru zuio hilo lisitishwe kwa siku 14 wakati kesi hiyo ikiendelea.

    Hata baada ya amri hiyo kutolewa, waandishi hao walizuiwa kuingia Ikulu kwa muda siku ya Alhamisi. Hali hiyo ilisababisha vyombo hivyo vitatu kuomba jaji asikilize suala hilo haraka.

    Baadaye Ikulu ilianza kurejesha vitambulisho na ruhusa za waandishi hao.

    CNN, MS NOW na Politico zilifungua kesi dhidi ya utawala wa Trump baada ya kuzuiwa kuingia Ikulu. Vyombo hivyo vilisema hatua hiyo ilikiuka uhuru wa vyombo vya habari.

    Jaji Kelly pia alitilia shaka hoja ya serikali kwamba zuio hilo lilikuwa kwa sababu za usalama wa taifa.

    Alisema Trump mwenyewe alikuwa ameeleza kuwa hatua hiyo ilichukuliwa kutokana na taarifa ambazo rais huyo alidai zilikuwa za uongo au za kumkosoa.

    Maelezo zaidi:

  6. Jeshi la Ethiopia laonya: 'Mapigano hayataishia mipakani'

    Mkuu wa Majeshi ya Ethiopia, Field Marshal Berhanu Jula, amesema muungano mpya unaoitwa “Friendship for Survival”, unaolenga kuiondoa serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed, hautafanikiwa.

    Akizungumza na kituo cha televisheni cha serikali, ETV, Berhanu alisema Eritrea inatumia kundi la TPLF kutoka Tigray kama jeshi la wakala, huku ikitoa rasilimali na kuhamasisha nguvu kwa ajili ya kuiunga mkono.

    Alidai pia kuwa Misri, Sudan na vikundi vingine vinaunga mkono TPLF na Eritrea katika juhudi hizo.

    Mkuu huyo wa jeshi alionya kwamba Jeshi la Anga la Ethiopia halitazuia operesheni zake katika maeneo ya mipakani pekee.

    Hata hivyo, Berhanu hakuzungumzia mapigano yaliyoanza jana. Vyombo vya habari vya serikali pia vimekuwa vikitoa taarifa chache kuhusu matukio mapya yanayoendelea katika maeneo ya Tigray, Afar na Amhara.

  7. Netanyahu aituhumu Qatar kushawishi maoni ya Waisraeli

    Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ameishutumu Qatar kwa kujaribu kubadili maoni na mitazamo ya wananchi wa Israel.

    Netanyahu alitoa madai hayo katika hotuba yake kwenye Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN).

    Hata hivyo, Qatar imekataa madai hayo na kusema haijawahi kuendesha kampeni ya kuwashawishi watu waichukie Israel.

    Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar, Majed al-Ansari, alisema kupitia ukurasa wake wa X kwamba Qatar “inapinga kabisa” tuhuma za Netanyahu.

    Alisema kauli hizo za Netanyahu dhidi ya Qatar zinalenga kuondoa macho ya dunia kwenye kile kinachoendelea katika maeneo ya Palestina yanayokaliwa na Israel, pamoja na hali mbaya ya kibinadamu inayowakabili wananchi huko.

    Al-Ansari alisema Netanyahu na viongozi wengine wa Israel wanapaswa kubadili sera zao, kuacha kukiuka sheria za kimataifa na kuziheshimu, badala ya kutafuta mtu wa kulaumiwa.

    Pia alisema viongozi hao wanapaswa kuwajibika kwa wananchi waliowachagua, badala ya kumtafuta mtu wa kulaumiwa kwa kupungua kwa heshima ya Israel kimataifa.

  8. Vita Ethiopia: Wakazi wa Tigray waanza kuhifadhi chakula wakihofia mapigano kuongezeka

    Wakazi wa Tigray, nchini Ethiopia, wameanza kununua chakula na bidhaa muhimu kwa wingi kutokana na hofu kwamba mapigano yaliyoanza Jumatano yanaweza kuongezeka.

    Katika mji mkuu wa Tigray, Mekelle, wakazi wameripotiwa kununua kwa wingi chakula na mahitaji muhimu ya kila siku, huku wakihofia kurejea kwa hali kama ile iliyoshuhudiwa wakati wa vita vilivyopita, Reuters imeripoti.

    Jana, vikosi vya Tigray viliteka viwanja vitatu vya ndege na kusema vimewaamuru wanajeshi wao “kuchukua hatua” kukabiliana na kile walichodai kuwa ni “mashambulizi yanayofanywa dhidi yao.”

    Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya wamezitaka pande zinazopigana kusitisha mapigano na kurejea kwenye Makubaliano ya Pretoria, yaliyosaidia kumaliza vita vya miaka miwili vya Tigray.

    Getachew Radda, mshauri wa Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, kuhusu masuala ya Afrika Mashariki na aliyewahi kuongoza Serikali ya Mpito ya Tigray, alisema kupitia mtandao wa X kwamba vikosi vya TPLF “vimeanzisha vita.”

    “Tunanunua kile tunachoona tunahitaji,” wakazi waliiambia Reuters kwa njia ya simu.

    Wakazi hao, ambao waliomba majina yao yasitajwe, walisema hali ya usalama imekuwa ngumu na imekuwa “vigumu kununua au kupata mahitaji ya msingi.”

    Mmoja wao alisema: “Iwapo hali itakuwa kama vita vya awali, huenda mji ukazingirwa.”

    Wakazi pia wamesema vikosi vya usalama vimeanza kupelekwa mitaani katika mji wa Mekelle, huku sauti za ndege zisizo na rubani zikisikika na hofu ikiongezeka kwamba upatikanaji wa chakula unaweza kuvurugika.

    Mkazi mwingine wa Adigrat alisema maduka yameanza kuwa matupu baada ya wananchi kununua chakula kwa wingi kwa wakati mmoja.

    Wakazi hao wawili pia walisema walishuhudia vijana wakilazimishwa kujiunga na jeshi, hali iliyozua hofu miongoni mwa wananchi.

    “Nilimwona kijana mwenye umri wa miaka 18, ambaye alipoteza baba yake katika vita vilivyopita, akichukuliwa kwa lazima,” alisema mkazi mmoja wa Adigrat.

    Vita vya awali vilivyodumu kwa miaka miwili vilisababisha uhaba mkubwa wa chakula, fedha na dawa.

    Mapigano katika eneo la Tigray yalianza tena Februari 13, baada ya vita vya miaka miwili kumalizika kupitia Makubaliano ya Pretoria.

  9. Balozi wa Israel UN ajaribu kumpa mwakilishi wa Iran kifaa cha Starlink

    Baada ya hotuba ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, Balozi wa Israel katika Umoja wa Mataifa, Danny Danon, alijaribu kumpa mwakilishi wa Iran katika Umoja wa Mataifa kifaa cha intaneti cha Starlink.

    Mwakilishi huyo wa Iran, ambaye vyombo vya habari vya Iran vimemtaja kuwa Nasser Asadi, mkwe wa aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Manouchehr Mottaki, alipuuzia kitendo hicho cha balozi wa Israel.

    Danon alisema: “Mmesikia maneno ya Waziri Mkuu; kifaa hiki kinaweza kuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa Iran, na kuwasaidia kupata uhuru, baada ya kile mlichowafanyia.”

    Danon pia alimwambia mwakilishi huyo wa Iran: “Tunawapenda wananchi wa Iran, na tunaomba mabadiliko ya serikali nchini humo. Siku hiyo itafika.”

  10. UAE yasitisha safari zote za ndege za mashirika ya Iran

    Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) umetangaza kusitisha safari zote za ndege zinazoendeshwa na mashirika ya ndege ya Iran, kwenda na kutoka nchini humo.

    Shirika rasmi la habari la UAE, Emirates News Agency, limeripoti Alhamisi kwamba Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya UAE imesitisha safari zote za mashirika ya ndege ya Iran kwenda na kutoka UAE.

    Mamlaka hiyo imesema uamuzi huo umechukuliwa kutokana na vikwazo vilivyowekwa na Marekani dhidi ya mashirika ya ndege ya Iran, ambavyo vinayazuia kutumia huduma za viwanja vya ndege katika maeneo mbalimbali duniani.

    Vyombo vya habari vya Iran pia viliripoti Alhamisi kwamba UAE imesitisha safari hizo.

    Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, Dubai, ambayo ni kitovu cha biashara cha UAE, ni kituo muhimu kwa mashirika ya ndege ya Iran, huku kukiwa na safari kadhaa za kila siku kati ya Iran na Dubai. Dubai pia ina jamii kubwa ya Wairan, huku Iran na Dubai zikiwa na uhusiano wa karibu kibiashara.

    UAE imekuwa ikilengwa na maelfu ya makombora na ndege zisizo na rubani za Iran tangu kuanza kwa vita. Mwezi uliopita, UAE ilisimamisha shughuli za biashara na miamala ya kifedha na Iran.

    Siku mbili zilizopita, Benki Kuu ya UAE ilizuia miamala ya kifedha katika matawi ya National Bank of Iran nchini humo, ambayo huhamisha fedha kwenda na kutoka Iran.

    UAE iliishutumu benki hiyo kwa kukwepa sheria zinazohusu utakatishaji fedha, ufadhili wa ugaidi na usambazaji wa silaha.

    Haya yanajiri baada ya Iran kuonya nchi jirani kuwa zitavuruga viwanja vya ndege wakikubali kutekeleza vikwazo vya Marekani vya kuwafungia anga.

    Soma pia:

  11. Tetesi za soka Ijumaa: Chelsea yamfukuzia kumpata Scott

    Chelsea itakuwa mstari wa mbele iwapo kiungo wa Bournemouth, Alex Scott, mwenye miaka 23, atawekwa sokoni katika dirisha la usajili la Januari. (Mail)

    Bayern Munich inamfuatilia mshambuliaji wa Barcelona, Dani Olmo, mwenye miaka 28, huku klabu hiyo ikikadiria thamani ya mchezaji huyo wa Hispania, bingwa wa Kombe la Dunia, kuwa karibu pauni milioni 60. (Sky Sports)

    Kiungo wa England, Jude Bellingham, mwenye miaka 23, anatarajiwa kuongeza mkataba wake na Real Madrid na hana mpango wa kuhamia Manchester City. (Fichajes)

    Beki wa Atalanta na timu ya taifa ya Italia, Giorgio Scalvini, mwenye miaka 22, amevutia Tottenham, Newcastle na Chelsea. (Caught Offside)

    Chelsea na Aston Villa hazijaweka kipengele kinachomruhusu Alejandro Garnacho kuondoka mwezi Januari katika mkataba wake wa mkopo wa msimu mzima kwenda Aston Villa. Winga huyo wa Argentina ana miaka 22. (Telegraph)

    Liverpool inafikiria kumrudisha klabuni kiungo wa England mwenye miaka 23, Tyler Morton, kutoka Lyon. Hata hivyo, Nottingham Forest, Crystal Palace na Brighton pia zinamfuatilia. (Teamtalk)

    Chelsea ni miongoni mwa klabu nne za Premier League zinazomfuatilia kwa karibu beki wa Manchester City na Uzbekistan, Abdukodir Khusanov, mwenye miaka 22. (Caught Offside)

    Juventus huenda ikafufua tena nia yake ya kumsajili kipa wa Brazil, Alisson, mwenye miaka 33, ambaye mustakabali wake Liverpool bado haujawa wazi. (Football Italia)

    Barcelona italazimika kuuza baadhi ya wachezaji mwezi Januari ili kupata fedha za kufanya usajili mpya. Beki wa Inter Milan na timu ya taifa ya Italia, Alessandro Bastoni, mwenye miaka 27, ni miongoni mwa wachezaji waliopo kwenye orodha yao ya wanaowataka. (Fichajes)

    Pia unaweza kusoma:

  12. Iran: Hormuz kufunguliwa ndani ya siku saba iwapo Marekani itakubali masharti yake

    Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Abbas Araqchi, amesema katika mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwamba Tehran, kupitia wapatanishi, imewasilisha mpango wa kufungua tena Mlango wa Bahari wa Hormuz.

    Araqchi, ambaye Alhamisi alikutana na kundi la waandishi wa habari pamoja na wanachama wa taasisi za utafiti na uchambuzi wa sera za Marekani, alisema iwapo Marekani itatimiza masharti maalum yaliyowekwa na Iran, Mlango wa Bahari wa Hormuz utafunguliwa tena ndani ya siku saba.

    Aliongeza: “Masharti haya si mapya; ni yale yale yaliyowasilishwa awali katika makubaliano ya Islamabad.”

    Abbas Araqchi pia alisema Iran inaamini kuwa “ni vyema makubaliano hayo yatekelezwe kabla ya uchaguzi wa katikati ya muhula wa Marekani,” huku Rais wa Marekani, Donald Trump, akisema kuwa makubaliano yanaweza kufikiwa baada ya uchaguzi wa Novemba.

    Akijibu suala hilo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran alisema muda wa kufikiwa kwa makubaliano hayo “unategemea Marekani,” huku akisisitiza tena kwamba masharti yaliyopendekezwa hayana tofauti na masharti yaliyokuwamo katika makubaliano ya awali.

    Soma zaidi:

  13. Hujambo na karibu kwa matangazo ya moja kwa moja ya tarehe 25/09/2026.