Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Mambo 3 ambayo familia yako inapaswa kufanya sasa kuhusu El Nino
El Nino ya mwaka huu si suala la mvua pekee. Ni hali ya hewa inayoweza kuathiri chakula, usafiri, afya na kipato cha familia, huku athari zake zikitarajiwa kuendelea hadi mwaka 2027.
Shirika la chakula duniani (WFP) linakadiria kuwa El Nino ya mwaka huu (2026-27) inaweza kusababisha njaa kwa watu wasiopungua milioni 49 ifikapo mwisho wa 2027. Katika nchi 45 ambazo tayari zinakabiliwa na changamoto ya usalama wa chakula, idadi ya watu walio katika hali hiyo inaweza kuongezeka kutoka takriban milioni 225 hadi milioni 274.
Afrika Mashariki Kusini mwa Afrika, ni miongoni mwa maeneo yanayotajwa kuwa katika hatari kubwa. WFP inasema zaidi ya watu milioni 18 katika ukanda huo wanaweza kukumbwa na uhaba wa chakula, ikiwa ni ongezeko la asilimia 26. Hii ni muhimu kwa familia za Afrika Mashariki kwa sababu mvua kubwa inaweza kuathiri uzalishaji wa chakula, barabara zinazotumika kusafirisha chakula na kipato cha watu wanaotegemea kazi za kila siku.
Nchini Tanzania, Kenya na Uganda, Mamlaka zimekwishatoa tahadhari kuhusu mvua za El nino ambazo zitakuwa kubwa kuliko kawaida, lakini na kueleza mikakati yao ya namna ya kukabiliana na athari zozote zitakazoambatana na mvua hizo.
Lakini maandalizi hayo hayaishii kwenye serikali. Kwa familia, zinapaswa kuchukua hatua ikiwa mvua zitavuruga usafiri, huduma au upatikanaji wa chakula kwa siku kadhaa. Swali muhimu hapa, je mna maandalizi gani nyumbani kwenu na familia yenu?
1. Utunzaji wa chakula
Kwa familia nyingi, hatari kubwa inaweza isiwe maji kuingia ndani ya nyumba, bali ugumu wa kupata chakula endapo barabara zitafungwa au usafirishaji ukaathirika.
Dk Charles Makai, mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), anasema maandalizi yanapaswa kuanzia ngazi ya familia, hasa kwa watu ambao lazima waondoke nyumbani kila siku kutafuta kipato.
Anataja waendesha bodaboda, madereva, makondakta wa daladala na vibarua wa ujenzi miongoni mwa watu ambao wanaweza kushindwa kufika kazini endapo barabara au miundombinu itaathiriwa na mvua kubwa.
Kwa Dar es Salaam, anatoa mfano wa utegemezi wa jiji kwa chakula kinachotoka nje ya jiji. Kwa mujibu wa Makai, mahitaji ya chakula jijini ni takriban tani milioni 1.3 kwa mwaka, wakati uzalishaji wa ndani ni karibu tani 10,000 pekee. Hivyo sehemu kubwa ya chakula hutegemea usafirishaji kutoka maeneo mengine, yakiwemo Kanda ya Ziwa na Nyanda za Juu Kaskazini.
Ndiyo maana anashauri familia kuwa na akiba ya chakula nyumbani inayoweza kuwasaidia kwa angalau miezi miwili endapo usafirishaji au upatikanaji wa chakula utavurugika.
Mchele, mahindi na maharage ni miongoni mwa vyakula vinavyoweza kuhifadhiwa kwa muda mrefu zaidi ikiwa vimekauka vizuri na kuhifadhiwa katika vyombo vilivyofungwa, sehemu kavu na iliyoinuliwa mbali na maji. Vyakula hivyo pia vinapaswa kukaguliwa mara kwa mara ili kuzuia unyevu, wadudu au kuoza.
"Inapaswa ndani ya kaya tuchukue tahadhari. Endapo itatokea sintofahamu ya miundombinu kuharibiwa, basi tuwe na chakula cha akiba ambacho kinaweza kuwa maharage, mchele, mahindi, ambavyo vinaweza kuisaidia familia ikae angalau miezi miwili," anasema Makai.
Hata hivyo, akiba hiyo haipaswi kuhifadhiwa chini sakafuni ikiwa nyumba iko katika eneo linaloweza kufurika. Shirika la Afya Duniani (WHO) linashauri chakula kinachogusana na maji ya mafuriko kitupwe, kwa sababu maji hayo yanaweza kuwa na uchafu unaoweza kusababisha magonjwa.
Na suala si chakula pekee. Familia zinapaswa pia kufikiria kuhusu kuhifadhi maji ya kunywa.
2. Huduma ya kwanza -First Aid Kit
Mafuriko yanaweza kufanya safari ya kwenda kituo cha afya kuwa ngumu, hasa pale barabara zinapokatika au maji yanapozuia usafiri.
Ndiyo maana kuwa na 'First Aid Kit' nyumbani kunaweza kusaidia katika kushughulikia majeraha madogo wakati familia ikisubiri msaada au huduma za afya zipatikane.
Kifaa hicho kinaweza kuwa na vifaa vya msingi kama pamba, mkasi, bandeji, gozi, plasta, glavu za matumizi ya mara moja, kipima jotovifaa vya kusafishia majeraha na dawa za kawaida ambazo familia imeelekezwa kutumia na mtaalamu wa afya.
Pia ni muhimu kuweka dawa za mtu binafsi zinazotumiwa mara kwa mara na kuhakikisha hazijaisha muda wake. Kama kuna wagonjwa wenye kuhitaji dawa za kila siku, nunua ama zichukue na zihifadhiwe nyumbani za kutosha.
WHO inapendekeza pia familia zilizo katika maeneo ya mafuriko kuwa na vifaa vingine vya huduma ya kwanza, dawa muhimu, maji, chakula kisichoharibika, tochi, betri, vifaa vya usafi na simu iliyochajiwa.
Nyaraka muhimu kama vitambulisho, vyeti na taarifa za matibabu nazo zinapaswa kuwekwa katika mfuko usiopitisha maji. Hii inaweza kuwa muhimu iwapo familia italazimika kuondoka nyumbani kwa haraka.
3. Tahadhari ya wakati wote
Maandalizi ya El Nino hayamaanishi kusubiri mafuriko yatokee ndipo uchukue hatua. Familia zinapaswa kufuatilia utabiri na tahadhari zinazotolewa na mamlaka za hali ya hewa na viongozi wa maeneo yao.
TMA imesema mvua za vuli 2026 zinaweza kuanza katika maeneo ya Ukanda wa Ziwa Viktoria kuanzia wiki ya nne ya Septemba hadi wiki ya kwanza ya Oktoba, kabla ya kusambaa katika maeneo mengine. Mvua zinaweza pia kuendelea hadi Januari 2027 katika baadhi ya maeneo.
Kwa hiyo, kabla ya mvua kuanza, familia inaweza kutambua eneo salama la kukimbilia, njia ya kutoka nyumbani iwapo eneo litafurika, mahali pa kuweka nyaraka na dawa, na namna ya kuwasiliana na ndugu iwapo mawasiliano au usafiri utaathirika.
Maji yakianza kujaa, usijaribu kutembea, kuogelea au kuendesha gari katika maji yanayotiririka. Maji ya mafuriko yanaweza kuwa na nguvu kubwa, nyaya za umeme zilizoanguka, mashimo au vitu vingine hatari visivyoonekana. Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu na Hilali Nyekundu (IFRC) linashauri watu kuhamia maeneo ya juu na kufuata maelekezo ya mamlaka kuhusu uokoaji.
WHO pia inashauri watu wasitumie maji ya mafuriko kunywa, kupikia au kuosha vyombo, na chakula kilichogusana na maji hayo kitupwe. Baada ya mafuriko, watu wasirudi kwenye nyumba zao hadi mamlaka ithibitishe kuwa ni salama.
Kwa Tanzania, Kenya na Uganda, maandalizi ya serikali yanaonyesha kwamba El Nino si jambo la kusubiri mpaka athari zionekane. Lakini maandalizi ya kitaifa yanaweza kuwa na maana zaidi pale yanapofikia hatua ya mwisho kwa maana ya kwenye familia na mtu mmoja mmoja.
Kwa upande wa WFP, mantiki ya kuchukua hatua mapema ni hiyo hiyo: Fedha na maandalizi yanayowekezwa kabla ya janga yanaweza kupunguza hasara na gharama za kukabiliana nalo baadaye. WFP inakadiria kuwa kwa kila dola moja inayowekezwa katika hatua za mapema, kati ya dola tatu na saba zinaweza kuokolewa katika hasara na gharama za hatua za baada ya janga.