Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
Jezi za Taifa Stars: Makonda anaishia wapi, Serikali inaanzia wapi na TFF inaingia wapi?
Kama Taifa Stars ni timu ya taifa, je, Waziri mwenye dhamana ya michezo ana haki ya kusema jezi yake haifai?
Na kama TFF ndiyo yenye jukumu la kuendesha soka, Waziri anaweza kuingilia mkataba wake na kampuni inayotengeneza jezi?
Hapo ndipo sakata la jezi mpya ya Taifa Stars linapoleta hoja ya mipaka kati ya Serikali na uendeshaji wa soka.
Kwa upande mmoja, Serikali inasema Taifa Stars si timu ya mtu binafsi, bali ni timu inayowakilisha nchi na ambayo Serikali ina wajibu wa kuihudumia. Kwa upande mwingine, TFF ndiyo iliyokabidhiwa jukumu la kusimamia soka nchini na imeingia mkataba na kampuni ya kutengeneza na kusambaza jezi.
Kampuni iliyopewa mkataba inasema mkataba ni halali na itamfikisha Mahakamani waziri kwa kuathiri biashara yake kupitia kauli yake kwamba jezi ni mbaya na hazina viwango.
Lakini mstari kati ya majukumu ya pande hizi tatu umeanza kuwa mwembamba zaidi baada ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, kuhoji hadharani kupitia maswali yake 22 zaidi akigusia ubora wa jezi mpya na mchakato uliopelekea 'kuzinduliwa' kwake.
Kwanza, nini hasa kimezua mgogoro?
Mzozo ulianza baada ya picha za Naibu Waziri wa Michezo, Hamis Mwinjuma, akiwa amevaa jezi mpya ya Taifa Stars kusambaa mtandaoni.
Makonda, kupitia akaunti yake binafsi ya Instagram, aliikosoa jezi hiyo akisema:
"Hii sio jezi ya Taifa Stars, Taifa Stars kwa ubora wake hatuwezi kuwa na jezi za kiwango chini hivi. Acheni kutumia picha za Naibu wangu huku ofisi yangu haina taarifa. Tuheshimiane."
Kauli hiyo ilifungua mjadala ambao haukuishia kwenye muonekano wa jezi. Kampuni ya Sandaland Fashion Wear, inayohusishwa na utengenezaji na usambazaji wa jezi hizo, ilisema kauli ya Waziri imeathiri jina, biashara na uhalali wa kampuni na kutishia kuchukua hatua za kisheria. Kampuni hiyo ikasisitiza kuwa ina mkataba halali na TFF wa kutengeneza na kusambaza jezi za Taifa Stars.
Sakata hilo lilipanuka zaidi Serikali ilipotangaza kuunda kamati maalumu ya kuchunguza mikataba ya wazalishaji wa jezi za timu za taifa, manufaa kwa timu hizo pamoja na mapato yatokanayo na mauzo ya jezi. Serikali ilisema lengo ni kuangalia kama mikataba hiyo inanufaisha timu za taifa kulingana na fedha za umma zinazotumika kuziendesha.
Kisha Makonda akaibua maswali 22 kuhusu mkataba huo, akisisitiza kwamba suala kwake si muonekano pekee wa jezi, bali pia uwezo wa kampuni kuhakikisha jezi hizo zinapatikana na kuuzwa kwa kiwango kinachotarajiwa.
Hapo ndipo suala la jezi likaanza kubadilika na kuwa mjadala wa nani ana mamlaka ya kufanya nini.
Mstari mwembamba kati ya Serikali, TFF, Waziri na Makonda
Kisheria na kiutawala, hoja hii inaonekana kuwa na pande mbili zinazokutana katika eneo moja.
Serikali ina jukumu la kusimamia sera, miongozo na kanuni za michezo. Lakini usimamizi wa moja kwa moja wa soka umekabidhiwa TFF.
Ndiyo sababu mjadala muhimu si tu kama Waziri anaweza kusema jezi ni mbaya. Hoja ni kwamba anaposema hivyo, anazungumza kama Paul Makonda binafsi, au kama Waziri? Na mipaka ya kauli hiyo inaishia wapi?
Mdau wa michezi Zitto Kabwe amehoji kama hatua za Waziri wa Michezo katika suala la jezi zinaweza kukiuka Ibara ya 19 ya Katiba ya FIFA, inayotaka vyama wanachama kuendesha mambo yao kwa uhuru bila ushawishi wa watu au taasisi za nje.
Zitto ameandika kwenye mtandao wake wa Instagram: "Swali la dola milioni ni hili: Je, Mheshimiwa PCM hajakiuka Ibara ya 19 ya Katiba ya FIFA?" Kwa uelewa wake, Waziri wa Michezo hawezi kuingilia moja kwa moja masuala ya kiutawala au kibiashara ya shirikisho la soka, ikiwamo zabuni za jezi za timu ya Taifa.
Aliyewahi kuwa mwanasheria wa TFF, Emanuel Muga, anasema serikali inapaswa kubaki katika nafasi ya mwangalizi kuhakikisha TFF inatimiza majukumu yake kwa kuzingatia sera ya Serikali, lakini si kushuka kwenye uendeshaji wa kila siku wa shirikisho.
"Mamlaka ya Serikali yanaishia kwenye uangalizi, iwe muangalizi tu kama shirikisho la soka kama TFF linatimiza majukumu yake na majukumu yanayoendana na sera ya jumla ya Serikali."
Kwa mantiki hiyo, Serikali inaweza kusaidia timu za taifa kwa sababu zinaiwakilisha Tanzania, lakini hilo halimaanishi Serikali iwe sehemu ya kila uamuzi wa kiutendaji unaofanywa na TFF.
Muga anaweka tofauti hiyo wazi zaidi kwa kusema: "Ni jukumu la Serikali kusaidia timu za taifa kwa sababu zinapeperusha bendera ya taifa, lakini haipaswi kujiingiza."
Kwa mtazamo wake, ubora wa jezi ni suala la kiutendaji, si sera ya Serikali. Ikiwa kuna tatizo katika mkataba, ubora wa bidhaa au utekelezaji wa makubaliano, anasema kuna njia za kisheria na kiutawala za kulishughulikia badala ya Serikali kuingia moja kwa moja kwenye uamuzi huo.
Lakini hoja ya Makonda inaanzia sehemu nyingine. Makonda anasema, Taifa Stars si timu ya kawaida ya michezo. Ni timu inayobeba jina na nembo ya nchi, huku Serikali ikiwa inatumia fedha za umma kugharamia mishahara, posho, usafiri na mahitaji mengine ya timu.
"Timu ya taifa ni mali ya nchi na sisi kwa mamlaka tuliyonayo tumeikasimu TFF itusaidie kusimamia huku tukihudumia, mishahara, posho, usafiri na mambo kadha wa kadha kufanya timu ya taifa ifanye vizuri."
Makonda anasema haiwezekani Waziri mwenye dhamana ya michezo asiwe na taarifa kuhusu jambo analoliona kuwa sehemu ya utambulisho wa taifa.
"Itakuwa Waziri wa ajabu hajui kinachoendelea timu ya taifa, lakini akienda Bungeni anaomba bajeti ya kupitishiwa kwa ajili ya kuhudumia timu ya taifa."
Makonda pia anasema Serikali ilikuwa imeanza kushirikishwa kuhusu suala la jezi tangu Februari 2026 na kwamba kwa kuwa jezi ya Taifa Stars ni sehemu ya utambulisho wa nchi, haipaswi kushughulikiwa kama bidhaa ya kawaida ya kibiashara.
Hapo ndipo mipaka miwili inapokutana. Kwa upande wa Mwanasheria Muga, anaona kusaidia timu ya taifa na kusimamia sera hakumpi Serikali mamlaka ya kuingia katika mikataba na maamuzi ya kiutendaji ya TFF.
Kwa upande wa Waziri Makonda anaona, kutumia fedha za umma na kuwa na jukumu la kisera hakumruhusu Waziri kubaki hajui kinachoendelea kwenye timu inayoiwakilisha nchi.
Kwa hiyo, mjadala wa msingi haubaki tena kwenye swali la kama jezi ni nzuri au mbaya. Unaendelea zaidi mpaka kwenye swali la nani anapaswa kuwa na sauti, wakati uamuzi wa TFF unahusu kitu kinachobeba utambulisho wa taifa na kinachounganishwa na matumizi ya fedha za umma.
Na hapo ndipo kuna mstari mwembamba kati ya ushirikishwaji na uingiliaji.
Mstari huu mwembamba wanauvukaje?
Hata ndani ya mjadala huu, kuna nafasi ya kutoka. Aliyewahi kuwa Waziri wa Michezo, Damas Ndumbaro, ambaye pia ni mwanasheria na anayeujua mkataba huo kutoka utawala wake, anasema baada ya kuusoma mkataba kati ya TFF na Sandaland, kwa upande wa kisheria anaona mambo yako sawa, ingawa hakuhusika katika mchakato wa manunuzi.
Kwa upande wa Serikali, hata hivyo, Ndumbaro haoni kwamba kutoa maoni kuhusu kuboresha jezi ni sawa na kuingilia mkataba moja kwa moja.
"Serikali haiwezi kukosa fursa ya kutoa maoni juu ya uboreshwaji wa jezi pasipo kuwa na ulazima wa kuingilia mkataba, wanaweza kukaa pande zote zikasema jezi hii hapa viwango hivi viko chini, kwanini hapa tusiongeze hiki, ni ushirikishwaji na sio uingiliaji." Anasema alipozungumza na Wasafi fm.
Hili na kutoia maoni, baada ya Sandaland kutishia kuchukua hatua za kisheria, Makonda alizungumza na wanahabari na kusema:
"Tukisema jezi mbaya mnatupeleka mahakamani, kwamba hatuna uhuru wa kujieleza? Hatuwezi kutoa maoni, hiyo ni jezi ya nchi au ya kwako na familia yako."
Hata hivyo baada ya mvutano huu, ni njia gani inatumika kutatua tofauti inapojitokeza kati ya Serikali, TFF na mdau wa kibiashara. Ndiyo maana kauli ya Zitto Kabwe inaingia katika mjadala huu kwa namna tofauti.
Akiangalia kuelekea mashindano AFCON 2027, ambayo Tanzania atakuwa mwenyeji pamoja na Kenya na Uganda, Zitto anasema mabishano ya hadharani kuhusu jezi hayapaswi kuwa njia ya kushughulikia tofauti hizo. Anaeleza kuwa TFF tayari ina mkataba wa jezi na kwamba suala hilo linapaswa kumalizwa kwenye vikao.
"Makonda weka mawe mfukoni tafadhali. Elekeza nguvu kwenye kuboresha tufanye vizuri. Sandaland achana na mambo ya mahakamani. Kaeni chini na Waziri kupata jawabu".
Pendekezo lake ni rahisi anasema pande zote zishushe jazba na zitafute suluhu inayoweza kuwanufaisha TFF, Serikali na kampuni inayohusika. Pendekezo ambalo hata Mwanasheria Muga analiona ni jema, kukaa na kuzungumza.
TFF yenyewe haijatoa msimamo mpana hadharani kuhusu nani yuko na haki gani na wao wanafanya nini katika 'mgogoro' huo. Msemaji wake Cliford Ndimbo amesisitiza kwamba suala hilo linafanyiwa kazi na "Mamlaka za juu".
"Kuhusu mavazi, Timu ya Taifa haijawahi kukosa mavazi, sikuzote tumekuwa tunatumia jezi ambazo zinatumika mara zote, kwahiyo suala hilo lipo mtandaoni tusingependa kulizungumza sana kwa sababu linafanyiwa kazi na Mamlaka za Juu."
Kwa maana hiyo, suluhu iliyotajwa na Makonda mwenyewe ni moja ya njia ambazo zinaweza kuondoa mvutano huo kwenye hadhara. Suluhu ni Baraza la michezo (BMT), TFF na kampuni inayohusika kukaa pamoja na kutafuta maelewano.
Kwa sababu mwisho wa siku, jezi ni ndogo, lakini suala lililo nyuma yake ni kubwa. Ni suala la kitaifa na ni suala la namna Serikali inavyoshirikiana na taasisi yenye mamlaka ya kuendesha soka. Pia ni suala la kama ushirikishwaji wa Serikali unaweza kufanyika bila kugeuka kuwa uingiliaji. Unalitofautishaje? akupe bajeti ya mabilioni ya fedha, aendeshe timu za taifa, zinazovaa jezi zenye kuipaisha taifa, lakini kwa hadhi yenye mashaka?
Mstari huu hauwezwi kuwekwa wazi kwa rangi au muundo wa jezi, bali unaweza kuwekwa wazi kwa mipaka ya mamlaka, namna taasisi zinavyoshirikiana na mahali zinapochagua kutatua tofauti zao.