Hii ni tovuti ya maandishi pekee ambayo inatumia data kidogo. Tazama toleo kuu la tovuti likijumuisha picha na video zote.
Pata maelezo zaidi kuhusu toleo hili la linalotumia kiasi kidogo cha data
'Wanasema najifanya mkulima kwa sababu ya umbo langu' – Valentina, 24
Ukimwona Valentina Moi akiwa shambani, akiwa amevaa nguo za kazi na mikono ikiwa na udongo, huenda usifikirie kwamba ni mtu yuleyule anayevuta macho ya maelfu ya watu kwenye mitandao ya kijamii.
Mwonekano wake umekuwa sababu ya kuvutia watu wengi kwenye kurasa zake za mitandao ya kijamii, lakini nyuma ya picha hizo kuna binti mwenye miaka 24 aliyeamua kujenga maisha yake kupitia kilimo na biashara ya mazao.
Na kwa sababu ya mwonekano huo, anasema amekutana pia na maneno makali.
Baadhi ya watu humshutumu kuwa hafanyi kilimo, huku wengine wakidai anatumia mwonekano wake kujitangaza na kujiuza kingono.
"Watu wasinitukane kutokana na umbo langu, sijajiumba," anasema.
"Wengine wanasema sifanyi kilimo, najiuza."
Lakini Valentina anasema kilimo kwake si maigizo ya mitandaoni.
Ni biashara aliyoianza kwa pesa yake mwenyewe, baada ya kukataa kusubiri miaka kadhaa hadi amalize masomo na kupewa mtaji na wazazi wake. Akisisiza "Nilianza kilimo kwa pesa yangu, sio mwanaume," anasema.
Alikataa kusubiri mtaji wa wazazi
Valentina alizaliwa katika mazingira ambayo shughuli za kilimo zilikuwa sehemu ya maisha ya jamii yake, ingawa wazazi wake wote ni waajiriwa. Tangu akiwa mdogo, alikuwa na hamu ya kufanya biashara.
Baada ya kumaliza kidato cha nne, alipata nafasi ya kusimamia ghala la mazao kwa miezi kadhaa. Uzoefu huo ulimpa nafasi ya kujifunza mambo ambayo baadaye yamekuwa msingi wa biashara yake. Masuaa kama aina za mazao, misimu, bei na namna biashara ya mazao inavyofanyika kutoka maeneo ya uzalishaji hadi sokoni.
Wakati huo, hata hivyo, hakukuwa na mpango wa kuingia moja kwa moja kwenye kilimo. Baadaye alipoendelea na masomo ya chuo, alianza kufikiria zaidi kuhusu biashara. Alikuwa amewaomba wazazi wake mara kadhaa aache shule ili aanze biashara, lakini mama yake alimshauri amalize elimu kwanza.
"Mama mara zote aliniambia, 'soma kwanza umalize elimu yako. Ukimaliza mimi na baba yako tunakuahidi kukupa mtaji wa biashara.'"
Valentina alikubali. Lakini moyoni aliona miaka mitatu au minne ya kusubiri hadi amalize chuo ni mingi sana.
"Mimi ni mtu ambaye huwa nina uthubutu. Nipo tayari kwa chochote na siogopi kujaribu."
Akiwa mwaka wa kwanza chuoni, alianza kufanya biashara ndogo ndogo bila kuwaambia wazazi wake. Biashara hizo hazikudumu. Baadhi zilianza vizuri lakini baadaye zikafa.
Hapo ndipo alipoanza kujiuliza kwa nini asitumie ujuzi aliokuwa ameupata kwenye biashara ya mazao baada ya kumaliza kidato cha nne?
Alianza kuangalia zaidi kilimo na nafaka. "Nilipowaza miaka mitatu mpaka minne ya chuo niliona siwezi kusubiri."
Uamuzi huo ukampeleka Tandale, Dar es Salaam. Hapo ndipo safari yake ya biashara ya mazao na masuala ya kilimo ilipoanza rasmi.
Magunia manne ya maharage yakaanzisha safari
Valentina alianza kama dalali wa mazao katika soko la Tandale.
Hakuwa anajulikana sokoni. Lakini alikutana na dalali mwingine aliyemwamini na kumpa nafasi ya kuanza biashara. Kwa mtaji wake mdogo, alinunua takribani magunia manne ya maharage.
Akayauza. Huo ndio ukawa mwanzo wa biashara ambayo baadaye ingempeleka katika maeneo mbalimbali ya Tanzania.
"Nilipouza yale magunia ndio ulikuwa mwanzo wa biashara ya mazao. Nikawa napanda kidogo kidogo na muda ulivyosogea nikaanza kuaminika pale sokoni."
Anasema alijijengea uaminifu kwa kupeleka mazao yenye ubora. Wateja wakaanza kuongezeka. Baadhi yao walihitaji mizigo mikubwa kuliko uwezo wake wa kifedha.
Na hakuwa na mtaji mkubwa. Lakini mmoja wa madalali sokoni alimwamini na kumpa mtaji kwa mkopo ili aende kutafuta ngano.
Valentina tayari alikuwa anajua maeneo ambayo ngano nzuri ilipatikana. Aliunganisha mtaji wake na ule aliopata kwa mkopo na kuanza safari ya kutafuta mazao moja kwa moja kutoka maeneo ya uzalishaji.
Kadiri biashara ilivyokua, alianza kusafiri zaidi. Alikutana na wakulima. Akajifunza zaidi kuhusu uzalishaji. Na hatimaye, hakutaka tena kuwa mtu anayenunua na kuuza mazao pekee.
Akaingia shambani.
Anasema sasa anakodisha mashamba na kulima mwenyewe, akijikita zaidi kwenye mpunga na vitunguu katika maeneo ya Nyanda za Juu Kusini mwa Tanzania na Kaskazini, hasa Manyara.
Lakini safari yake haikuishia kwenye shamba. Alianza kujifunza pia kuhusu mnyororo mzima wa thamani; kuanzia shambani, kwenye ghala, sokoni hadi kwa mlaji.
Anasema aligundua kuwa watu wengi wanaingia kwenye kilimo bila taarifa za kutosha kuhusu biashara wanayoingia.
"Watu wengi wanakosea kuingia kwenye kilimo kutokana na kutokuwa na taarifa sahihi. Wengi hawafanyi utafiti na wala hawakutani na wataalamu ili kupata elimu stahiki kuhusu kilimo biashara na biashara ya mazao na nafaka."
Kwa hiyo akaanza kutumia mitandao ya kijamii kutoa maudhui kuhusu kilimo na biashara ya mazao. Mwanzo alitoa elimu bure.
Baadaye aliamua kuanzisha madarasa ambayo washiriki wanalipia ili kupata mafunzo. Hivyo ndivyo Nafaka Master Class ilivyoanza. Kupitia mpango huo, anasema huwaunganisha vijana na wataalamu wa kilimo na biashara ya mazao.
Si yeye pekee anayefundisha. Anawaalika wataalamu wenye ujuzi katika maeneo mbalimbali ya kilimo kutoa elimu kwa washiriki.
Anasema baadhi ya vijana wanaofika kwenye mafunzo hayo huwa wamekata tamaa kuhusu maisha, na anajivunia kuona baadhi yao wakibadilika baada ya kupata maarifa na mwelekeo mpya.
"Kwa hiyo nimeweza kubadilisha maisha ya baadhi ya vijana Tanzania."
Shamba la miaka 24 na ndoto ya trekta
Kwa sasa, baada ya takribani miaka mitano tangu aanze safari yake katika biashara ya mazao na baadaye kilimo, Valentina anasema amefikia hatua ya kuwa na maeneo anayolima na kuendelea kukuza biashara yake.
Moja ya mambo anayojivunia zaidi ni shamba alilojipa kama zawadi alipofikisha umri wa miaka 24 hivi karibuni.
Kwa mtu mwingine, anasema, huenda shamba likawa zawadi ya kawaida. Kwake ni jambo kubwa.
"Mwaka jana nilipokuwa natimiza miaka 24 nilijipa zawadi ya shamba."
"Kwa wengine wanaweza kuona ni kitu kidogo au cha kawaida, lakini kwangu ni mafanikio makubwa sana kumiliki ardhi ambayo ndio nyenzo muhimu katika kilimo."
Lakini pamoja na mafanikio hayo, safari haijawa ya faida pekee. Kuna nyakati amepata hasara kubwa.
Anakumbuka wakati mmoja alipokwenda Manyara kuchukua ngano na kuileta Dar es Salaam baada ya kuona kulikuwa na uhitaji mkubwa sokoni.
Mzigo huo uliuzwa vizuri. Wateja wakaongezeka.
Akaona fursa na kurudi tena kuchukua ngano. Lakini alipofika sokoni safari hiyo, hali ilikuwa imebadilika.
"Nilifika sokoni nikakuta magari zaidi ya matano yameleta ngano pale pale sokoni."
Ghafla ushindani ukaongezeka. Wafanyabiashara wengine walikuwa wameleta ngano nzuri na waliweza kuuza kwa bei ya chini.
Mzigo wake haukuweza kuuzwa kwa wakati. Hasara ikawa kubwa.
Changamoto nyingine ilimkuta alipolima ekari 100 za maharage. Mvua hazikunyesha kwa wakati. Mavuno yakawa madogo sana ukilinganisha na matarajio yake.
Lakini Valentina anasema matukio hayo hayajamfanya kuacha kilimo.
"Ni changamoto. Hukatai tamaa, unaendelea na kujipanga zaidi kwa msimu wa kilimo unaofuata."
Sasa anaangalia hatua inayofuata. Anataka kufikia wakati ambapo hatategemea nguvu kazi pekee katika shughuli zake za kilimo.
Ana ndoto ya kumiliki trekta pamoja na mashine za kupanda, kuvuna na kuchakata mazao.
Lakini ndoto yake kubwa zaidi ni kuanzisha taasisi ambayo itawasaidia vijana wa Tanzania kupata elimu kuhusu kilimo biashara bila kulipia.
Anaamini kilimo kinaweza kuwa biashara yenye tija kwa vijana ikiwa wataingia wakiwa na taarifa sahihi.
"Sikupenda kuwa na mwili huu"
Hata hivyo, si changamoto za kilimo pekee ambazo Valentina amekutana nazo.
Kuna vita nyingine amekuwa akipambana nayo kwenye mitandao ya kijamii.
Ni kuhusu mwili wake. Anasema picha na video zake zinapowekwa mitandaoni, baadhi ya watu huzungumzia zaidi umbo lake kuliko kazi anayofanya.
Matusi na tuhuma zimekuwa sehemu ya maisha yake ya mtandaoni. Wengine humwambia hawezi kuwa mkulima kwa sababu ya mwonekano wake.
Wengine humshutumu kuwa anatumia mwili wake kupata fedha. Maneno hayo yamewahi kumfanya ajifungie ndani na kulia.
"Wakati mwingine nakaa ndani nalia najiuliza, kwani mimi ndio nimejiumba?"
Anasema hakuchagua kuwa na mwili alionao. "Mimi sikupenda kuwa na mwili huu wa kibantu, lakini sasa hivi nimezoea."
Hata hivyo, anasema amejifunza kuendelea na maisha licha ya maneno hayo.
Kwa sasa anataka watu wazingatie zaidi kile anachokifanya kuliko mwonekano wake.
Kwa upande wake Valentina, kilimo si shughuli ya mtu mwenye umri mkubwa pekee.
Wala si kazi ya mtu anayekosa kitu kingine cha kufanya. Anasema kilimo ni kazi na biashara.
Na ni biashara ambayo yeye ameamua kuijenga hatua kwa hatua, kuanzia magunia manne ya maharage katika soko la Tandale, hadi mashamba anayolima leo.
Kwake safari bado ni ndefu. Trekta bado ni ndoto. Mashine za kilimo bado ni mpango wake. Na taasisi yake ya kuwasaidia vijana bado haijaanza, anaisubiria.
Lakini jambo moja analosema halijabadilika tangu alipoanza safari hii ni muonekano wake akisisitza wakati wote kwamba; alichagua kilimo kwa hiari yake mwenyewe, na hataki mwonekano wake uwe sababu ya watu kupuuza kazi anayofanya.